Mbuga ya Kipekee ya Wanyama wa Mediterania
Mbuga ya Kipekee ya Wanyama wa Mediterania
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA
KWA maelfu ya miaka, watu wanaoishi karibu na Bahari ya Mediterania wamekuwa wakiharibu misitu, kutumia malisho kupita kiasi, na kuwinda wanyama fulani wa mwituni hadi karibu watoweke kabisa. Ni maeneo machache tu yaliyosalia bila kuharibiwa. Hata hivyo, katika sehemu moja ndogo ya Hispania, hali fulani zimefanya eneo dogo kuepuka uharibifu huo. Eneo hilo linaitwa Monfragüe, jina linalomaanisha “mlima wenye miamba.”
Ingawa sehemu hiyo ya Hispania haifikiki kwa urahisi, hilo pekee halikutosha kulihifadhi eneo hilo. Wakulima walioishi katika eneo la Monfragüe, walitumia njia ya ufugaji iliyosaidia kuhifadhi sehemu moja ya misitu mikubwa ya kiasili iliyofunika milima ya Mediterania wakati mmoja. Msitu huo uliohifadhiwa uliitwa dehesa au “malisho yenye miti.”
Aina ya Kilimo Inayohifadhi Mazingira
Karne nyingi zilizopita wakulima wa Extremadura (mahali lililoko eneo la Monfragüe huko Hispania) waligundua kwamba misitu ya mialoni iliyofunika eneo hilo ilitoa kivuli na malisho yaliyohitajika kwa ajili ya mifugo yao. * Kwa hiyo, badala ya kukata miti yote ili kupata malisho, wao walihifadhi mialoni ya kutosha ili kufanyiza msitu wenye nafasi katikati ya miti. Wao pia walipogoa miti ili matawi yake yaenee. Kivuli cha mialoni hiyo yenye kupendeza kilizuia jua kuharibu malisho, na njugu zake zilitumiwa kulisha ng’ombe na nguruwe. Kwa sababu miti mingi iliyokuwepo hapo awali ilihifadhiwa katika msitu huo, hilo lilisaidia kuokoa ndege na wanyama wengi wa kienyeji.
Mto wa Tagus na wa Tiétar hukatiza msitu huo wa dehesa na kufanyiza mabonde, halafu hukutana chini ya kilele cha milima ya Monfragüe. Hatimaye, katika mwaka wa 1979, eneo lenye milima linalopakana na mito hiyo miwili, ambalo ni eneo la pekee lenye msitu wa awali wa Mediterania, likawa hifadhi ya wanyama na mimea. Mbuga hiyo ilianzishwa kwa sababu eneo la Monfragüe sasa linaonwa kuwa mojawapo ya hifadhi bora zaidi za mfumo wa ikolojia wa Mediterania.
Ndege wa Biblia
Ingawa mbuga hiyo ni ndogo, hiyo ni makao ya kanu, mbawala mwekundu, nguruwe-mwitu, na simba-mangu wa Hispania ambaye haonekani sana na ambaye ni mmoja wa wanyama walio katika hatari kubwa ya kutoweka huko Ulaya. Kwa sababu wanyama walio wengi
hutembea usiku, ni rahisi kwa mgeni anayezuru mchana kuona tu ndege walao nyama wenye kuvutia ambao wanapatikana kwa wingi kuliko kuwaona wanyama hao. Wengi wa ndege hao pia walipatikana kwa wingi nyakati za Biblia.Katikati ya karne ya 19, mwanasayansi mmoja kwa jina H. B. Tristram aliwaona tumbusi aina ya griffon wenye madoadoa wakiruka angani aliposafiri huko Palestina. Ndege hao huonekana pia huko Monfragüe, ambapo ndege 800 wamejenga viota katika miamba inayoelekea mto wa Targus na Tiétar. Wakati wa jioni, tumbusi wengi huruka juu wakizunguka viota vyao vya pamoja, huku maumbo yao makubwa meusi yakionekana kama madoa yanayotapakaa kotekote angani. *
Korongo weupe wanaojenga viota katika nyumba nzee za sehemu nyingi za Ulaya, bado wanajenga viota katika mialoni ya Monfragüe ambapo wanasitawi. (Zaburi 104:17) Pamoja na korongo, ndege wengine wanaopaa bila kuchoka katika ukanda wenye joto ni tai-mfalme na tai-dhahabu ambao ‘huangalia toka mbali’ wakitafuta windo lao.—Ayubu 39:27-29.
Wakati wa kiangazi mwewe wekundu huongezeka, ambao ni wepesi na wengi kuliko tai. Pia, tai weusi ambao wana macho makali huruka wakitafuta daima kunasa samaki katika maji ya mito iliyomo katika hifadhi hiyo.—Ayubu 28:7
Aina nyingine za ndege walao nyama, kama bundi-tai na bundi babewatoto, huanza kuruka angani wakati wa usiku. Bundi tai hutengeneza kiota katika majabali yaliyo mbali ya Monfragüe, sawa tu na mahali penye magofu ya Babiloni ya kale ambapo nabii Isaya alitabiri kwamba bundi angekaa.—Isaya 13:21
Kuhifadhi na Kurekebisha Mbuga
Maua ya mwitu huiongezea umaridadi mbuga hiyo hasa katika majira yenye mvua nyingi. Machipukizi meupe na mororo ya waridi za miamba, pamoja na machanuo ya maua ya zambarau, hufunika kila mlima ambao hauna miti. Majira ya kiangazi yakaribiapo, mipopi ipatikanayo kila mahali huongezea wekundu kwenye malisho hayo ya kijani kibichi.
Kuhifadhi makao hayo ya wanyama sasa ni kazi inayohangaisha mamlaka ya mbuga. Ili kuyalinda, miti ya kienyeji inapandwa mahali pa misonobari na mikalitusi (eucalyptus) iliyopandwa hapo awali ambayo haifaidi wanyama katika mbuga hiyo. Wanashirikiana pia na wakulima wa eneo hilo kulinda misitu inayozunguka, wakiwahimiza kupanda tena mialoni inapohitajika. Inatumainiwa kuwa jitihada hizo zitaihifadhi mbuga hiyo ya kipekee ya wanyama wa Mediterania.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 6 Aina za mialoni ambayo inapatikana sana huko Hispania ni cork oak na holm oak. Aina hizo zilisitawi pia kwa wingi huko Palestina nyakati za Biblia.
^ fu. 10 Tumbusi aina ya griffon ana mabawa yenye urefu wa sentimeta 280 na ni mmoja kati ya ndege wakubwa zaidi katika mabara ya Ulaya na Asia.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Kutoka kushoto hadi kulia: Ng’ombe wanaolisha katika msitu wenye nafasi katikati ya miti, kanu, na mbawala mwekundu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Tumbusi mweusi
[Picha katika ukurasa wa 18]
Bundi-mwewe
[Picha katika ukurasa wa 18]
Tai-dhahabu
[Hisani]
Fotos: Cortesía de GREFA