Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wadudu Wanaoondoa Takataka kwa Ustadi

Wadudu Wanaoondoa Takataka kwa Ustadi

Wadudu Wanaoondoa Takataka kwa Ustadi

YAPATA miaka 150 tu iliyopita, wanadamu walianza kutengeneza mabomba ya maji machafu na kuwa na njia maalumu ya kuondoa takataka. Hata hivyo, kabla ya hapo chungu mmoja huko sehemu za Amerika zenye joto alijua jinsi ya kuondoa takataka kwa ustadi sana.

Chungu wa kawaida wanaokusanya majani milioni moja hivi huishi katika kiota kikubwa cha chini ya ardhi. Chungu hao wanafanya kazi mbalimbali. Baadhi ya chungu hukusanya vipande vya majani, na chungu wengine huvitafuna viwe rojo. Chungu wanaotunza bustani hutumia rojo hiyo ili kukuza kuvu inayoweza kuliwa ndani ya vyumba mbalimbali kiotani. Wao pia huondoa chochote kile kinachoweza kusababisha ugonjwa, kama vile kuvu inayodhuru, chungu waliokufa au wanaoelekea kufa, na vitu vinavyooza. Lakini chungu hao huondoa takataka hiyo jinsi gani?

Gazeti la The Independent laripoti kwamba wanasayansi Waingereza wa Chuo Kikuu cha Sheffield wamegundua jinsi wanavyofanya. Karibu na vyumba vya bustani kuna vyumba vikubwa vya kuhifadhi takataka. Chungu wanaofanya kazi katika vyumba vya takataka huishi humo maisha yao yote. Wao hugeuza takataka ili zioze, na wakati zinapooza bakteria zinazoweza kusababisha ugonjwa huangamizwa. Chungu wanaofanya kazi bustanini hawaingii kamwe katika vyumba vya takataka. Wao hupeleka takataka hadi kwenye kijia fulani na chungu wanaoshughulikia takataka huzichukua hapo. Njia hiyo ya kuondoa takataka inazuia chungu wasiambukizwe magonjwa na kulinda afya yao.

Mbali na kuwaumba wadudu na kuwapa hekima ya kisilika, Yehova Mungu pia aliwapa Waisraeli miongozo kuhusu afya, zaidi ya miaka 3,500 iliyopita. Kufuata sheria hizo kungezuia chakula na maji yasichafuliwe, magonjwa ya kuambukizwa yasienee, na kuhakikisha kwamba uchafu uliondolewa kwa njia isiyodhuru. Magonjwa mengi na vifo vingi vingeweza kuepukwa ikiwa kanuni hizo zingefuatwa.—Mambo ya Walawi 11:32-38; Hesabu 19:11, 12; Kumbukumbu la Torati 23:9-14.