Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Chumvi Ni Bidhaa Muhimu

Chumvi Ni Bidhaa Muhimu

Chumvi Ni Bidhaa Muhimu

YESU aliwaambia wanafunzi wake hivi: “Nyinyi ndio chumvi ya dunia.” (Mathayo 5:13) Nao Waarabu husema kwamba, “Kuna chumvi kati yetu,” na Waajemi husema kuhusu “asiye wa kweli kwa chumvi” (asiye mwaminifu au asiye na shukrani). Kwa kuwa chumvi inaweza kuhifadhi vitu, neno “chumvi” limeheshimiwa na kustahiwa katika lugha za kale na hata za leo.

Chumvi pia imekuwa alama ya uthabiti na udumifu. Hiyo ndiyo sababu, katika Biblia agano muhimu liliitwa “agano la chumvi,” na wale waliokubaliana mara nyingi walikula mlo pamoja, uliotiwa chumvi ili kuidhinisha agano hilo. (Hesabu 18:19) Chini ya Sheria ya Musa, chumvi ilitiwa kwenye matoleo madhabahuni, bila shaka ikionyesha hali ya kutokuwa na ufisadi au uharibifu wowote.

Historia ya Chumvi Yenye Kupendeza

Tangu zamani, chumvi (sodiamu kloridi) imeonwa kuwa bidhaa muhimu na hata watu walipigana vita kwa sababu yake. Kodi ya juu iliyoongezwa na Louis wa 16 na iliyofanya bei ya chumvi ipande, ilikuwa mojawapo ya visababishi vya Mapinduzi ya Ufaransa. Chumvi pia ilibadilishwa na bidhaa nyingine katika biashara. Wafanya-biashara wa Moor walibadilisha chumvi na dhahabu, gramu moja ya chumvi ilibadilishwa kwa gramu moja ya dhahabu, na makabila fulani huko Afrika ya kati yalitumia chumvi ya mawe kama pesa. Wagiriki walinunua watumwa kwa chumvi, hivyo usemi “hana thamani ya chumvi yake” ukaanzishwa.

Katika Enzi za Kati, watu walianza kuwa na ushirikina kuhusiana na chumvi. Kumwaga chumvi kulionwa kuwa hatari. Kwa mfano, katika mchoro wa “Chakula cha Mwisho” uliochorwa na Leonardo da Vinci, Yuda Iskariote anaonekana akiwa na chombo cha kuwekea chumvi kilichopinduliwa mbele yake. Kwa upande mwingine, kufikia karne ya 18, kuketi katika nafasi iliyo karibu na chombo cha kuwekea chumvi katika sherehe kulionyesha cheo cha mtu katika jamii. Nafasi iliyoheshimiwa zaidi ilikuwa karibu na chombo hicho, karibu na msimamizi wa meza.

Tangu zamani binadamu amejifunza kuzoa chumvi kutokana na maji ya kiasili yenye chumvi, maji ya bahari, na mawe ya chumvi. Rekodi ya kale ya Kichina inayohusu sayansi ya madawa imeorodhesha zaidi ya aina 40 za chumvi na inaeleza kuhusu njia mbili za kuzoa chumvi ambazo zinafanana sana na zile zinazotumiwa leo. Kwa mfano, nguvu za miali ya jua hutumiwa kuzoa chumvi kutokana na maji ya bahari katika kiwanda kikubwa zaidi cha kutengeneza chumvi duniani kinachoendeshwa na nguvu ya jua, kilichoko ufuoni mwa Bahía Sebastián Vizcaíno huko Baja California Sur, Mexico.

Kwa kupendeza kichapo Encyclopædia Britannica kinasema kuhusu makadirio yanayoonyesha kwamba kama bahari zote duniani zingekaushwa maji, “zingetoa angalau jiwe la chumvi la kilometa milioni 19 za mraba. Hilo ni mara 14.5 ya ukubwa wa bara lote la Ulaya.” Nayo Bahari ya Chumvi ina kiasi cha chumvi kinachozidi bahari za kawaida karibu mara tisa!

Matumizi ya Chumvi Siku Hizi

Leo chumvi bado ni bidhaa muhimu inayotumiwa kukoleza vyakula, kuhifadhi nyama, na kutengeneza sabuni na vioo, yakiwa baadhi ya matumizi mengine. Chumvi pia hutumiwa kuboresha afya ya umma. Kwa mfano, katika mataifa mengi duniani, chumvi huongezwa aidini ili kuzuia upungufu wa madini hayo. Ugonjwa wa tezi na kupungukiwa akili ni magonjwa yanayotokana na ukosefu wa madini ya aidini mwilini. Pia, katika mataifa fulani floraidi huongezwa kwenye chumvi ili kuzuia kuoza kwa meno.

Chumvi ni muhimu kwa afya—hiyo husaidia kudumisha kiasi na shinikizo la damu. Lakini vipi kuhusu dai la kwamba chumvi husababisha shinikizo la juu la damu? Ni kweli kwamba madaktari wamewakataza watu wenye ugonjwa wa shinikizo la damu wasile vyakula vyenye chumvi. Thuluthi moja hadi nusu ya watu walio na shinikizo la juu la damu wanaathiriwa vibaya wanapokula vyakula vyenye chumvi. Kwa watu kama hao kupunguza kiasi cha chumvi wanachotumia huelekea kupunguza shinikizo lao la damu.

Bila shaka chumvi huongeza ladha kwenye chakula, kama tu vile Ayubu alivyodokeza kwa kuuliza hivi: “Je! kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi?” (Ayubu 6:6) Tunapaswa kumshukuru Muumba wetu, “ambaye hututolea sisi vitu vyote kwa utajiri kwa ajili ya ufurahio wetu,” kutia ndani ile bidhaa muhimu, yaani chumvi.—1 Timotheo 6:17.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Aina za chumvi (kuanzia juu kuelekea kulia): (1) chumvi ya Alaea kutoka baharini, Hawaii; (2) fleur de sel, Ufaransa; (3) chumvi inayotokana na viumbe wa bahari; (4) sel gris (chumvi ya rangi ya majivu), Ufaransa; (5) chumvi yenye chembe kubwa-kubwa; (6) chumvi nyeusi ya ardhini, India