Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuokoa Uhai wa Watoto Waliozaliwa Karibuni

Kila mwaka, watoto milioni nne hufa kabla hawajafikisha umri wa mwezi mmoja. Gazeti la Bild der Wissenschaft la Ujerumani linaripoti kwamba “zaidi ya asilimia 40 ya watoto wote wanaokufa wakiwa chini ya umri wa miaka mitano,” hufa katika mwezi wa kwanza baada ya kuzaliwa. Tunawezaje kuokoa uhai wa watoto hao? Mbinu zisizogharimu sana kama vile kuhakikisha watoto wana joto na kuwanyonyesha mara tu baada ya kuzaliwa, zinapendekezwa katika uchunguzi mmoja wenye kichwa “Hali ya Watoto Waliozaliwa Karibuni Duniani.” Kumnyonyesha mtoto mara moja baada ya kuzaliwa humkinga na magonjwa. Vifo vinaweza kuzuiwa pia kwa kuboresha afya ya wanawake wajawazito, kwa sababu wengi wao hufanya kazi kupita kiasi, hawali chakula cha kutosha, na hawajapona tangu walipojifungua wakati uliopita. “Katika nchi zinazoendelea, ambako asilimia 98 ya vifo hivyo hutokea,” wenyeji wanaweza kuzoezwa kusaidia wanawake wanaojifungua. Kulingana na uchunguzi huo, “kazi yao hasa ingekuwa kuwafundisha wanawake wajawazito, kushughulikia usafi, na kuchanja.”

Minara ya Taa Haihitajiki Tena

Gazeti la Financial Post linasema hivi: “Kama vile taa ya umeme ilivyochukua mahali pa mshumaa, mnara wa taa ambao unaendeshwa na mitambo unatumiwa badala ya mwangalizi wa mnara wa taa. Sasa inaonekana kana kwamba mnara wa taa ambao unaendeshwa na mitambo utatoweka pia hivi karibuni.” Mnara wa taa wa kisasa unatoa nuru inayoonekana kwa umbali wa kilometa 32 baharini na una king’ora kinacholia wakati ambapo kuna ukungu ili kuonya mabaharia kwamba wanakaribia nchi kavu. Hata hivyo, tekinolojia ya setilaiti inawawezesha mabaharia kujua mahali walipo barabara. Sasa meli zina redio za setilaiti zinazowawezesha mabaharia kuongoza meli wasipoweza kuona kile kilicho mbele. Mike Clements, anayeratibu shughuli za Walinzi wa Pwani wa Kanada, huko St. John’s, Newfoundland, anasema kwamba redio hizo za setilaiti ‘huenda zikafanya minara ya taa isihitajike tena. Redio hizo hazina kifani. Mnara wa taa hauwezi kukuongoza ukafika unakotaka kwenda.’

Mawasiliano ya Watoto Wachanga

Gazeti la The Times la London linasema hivi: ‘Watoto walio na wazazi wasio viziwi huanza kutamka maneno yasiyoeleweka wakiwa na umri wa miezi saba hivi. Watoto wa umri huo wanaolelewa na wazazi walio viziwi huanza kufanya ishara za mikono zisizoeleweka, wakijaribu kuiga jinsi wazazi wao wanavyowasiliana kwa lugha ya ishara.’ Watoto hao hufanya hivyo hata ikiwa wao si viziwi. Matokeo ya uchunguzi uliosimamiwa na Profesa Laura Petitto kwenye Chuo Kikuu cha McGill, Montreal, Kanada, yanaonyesha kwamba watoto wanazaliwa wakiwa na kipawa cha kujifunza lugha zote, kutia ndani lugha ya ishara. Anasema kwamba watoto wachanga wasio viziwi, ambao wana wazazi viziwi ‘wanaowasiliana kwa kutumia lugha ya ishara, wanafanya ishara fulani ya kipekee kwa mikono yao, inayotofautiana na jinsi ambavyo mtoto husogeza mikono kwa kawaida. Ni wazi kwamba watoto hao wanajaribu kuwasiliana kupitia ishara za mikono.’ Watoto waliokuwa na wazazi walio viziwi wanaotumia lugha ya ishara walisogeza mikono kwa njia mbili, lakini watoto waliokuwa na wazazi walioongea kwa sauti walisogeza mikono kwa njia moja tu. Watafiti hao walitumia vifaa fulani ili kupima jinsi watoto hao walivyosogeza mikono yao walipokuwa na umri wa miezi 6, miezi 10, na miezi 12.

Hati za Kukunja za Bahari ya Chumvi Zimechapishwa

Gazeti la U.S. News & World Report linasema kwamba “zaidi ya miaka 50 baada ya Hati za Kukunja za Bahari ya Chumvi kupatikana katika mapango ya jangwa la Yudea, wataalamu wanafurahia kwamba sehemu ya mwisho ya maandishi hayo ya kidini yaliyoandikwa miaka 2,000 iliyopita imechapishwa.” Profesa Emanuel Tov, aliyewaongoza wasomi waliochunguza hati hizo za kukunja, alitangaza kwamba vitabu 37 vyenye maandishi hayo vimetolewa. Vifaa vya hali ya juu vya kisasa vilichangia kukamilisha kazi hiyo kwa kuwa viliwawezesha wasomi kusoma maandishi yaliyokuwa hafifu. Maandishi hayo, yaliyotafsiriwa kutoka lugha ya Kiebrania, Kiaramu, Kigiriki, na Kilatini, yaliandikwa kuanzia mwaka wa 250 K.W.K. hadi 70 W.K.

Jinsi Watu Wanavyotenda Nyakati za Wasiwasi

Gazeti la Globe and Mail la Kanada linaripoti kwamba washiriki wa Shirika la Wauza-Vitabu vya Kikristo nchini Kanada wameongeza mauzo yao ya Biblia kwa asilimia 30 tangu mashambulizi ya magaidi huko Marekani. Marlene Loghlin, mkurugenzi-mtendaji wa shirika hilo anasema hivi: “Watu wanajaribu kuelewa hali hiyo, nao wana wasiwasi. Kuna mambo mengi ambayo watu hawajaelewa yanayowafadhaisha.” Ripoti hiyo inasema pia kwamba hata katika maduka madogo ya vitabu “mauzo ya vitabu vya kidini vinavyoweza kuwasaidia watu kuelewa msiba huo wenye kuhuzunisha yameongezeka.” Profesa mmoja wa theolojia wa Chuo Kikuu cha Toronto alisema kwamba jambo hilo ni la kawaida. Alisema hivi: “Katika nyakati za wasiwasi mwingi, watu huanza kujiuliza maswali ya msingi ya kidini,” na “kutafuta majibu katika Biblia kunaweza kusaidia.”

UKIMWI—Kisababishi Kikuu cha Kifo Huko Afrika Kusini

Gazeti la The New York Times lilisema hivi lilipozungumzia uchunguzi uliofanywa na Baraza la Utafiti wa Kitiba la Afrika Kusini: “UKIMWI ndio kisababishi kikuu cha vifo huko Afrika Kusini, na watu wazima ndio wanaokufa hasa.” Watafiti wanakadiria kwamba katika miaka kumi ijayo, kati ya watu milioni tano na milioni saba watakufa kwa UKIMWI huko Afrika Kusini. Wanawake wengi wenye umri wa kati ya miaka 20 na 30 hufa kuliko wanawake wenye umri wa kati ya miaka 60 na 70. Makala hiyo inasema pia kwamba huko Afrika Kusini “kuna watu wengi wanaojulikana kuwa na virusi vinavyosababisha UKIMWI, kuliko katika nchi nyingine yoyote. Maafisa wa serikali wanasema kwamba mtu mmoja kati ya watu tisa, na mtu mmoja kati ya watu wazima wanne [wenye umri wa kati ya miaka 30-34], wanadhaniwa kuwa wameambukizwa virusi vinavyosababisha UKIMWI nchini Afrika Kusini.”

Kuishi Katika Majiji

Gazeti la The Sunday Times la London linasema kwamba “katika mwaka wa 1900 majiji makubwa yalikuwa London, New York, Paris, Berlin na Chicago.” Lakini kulingana na makadirio mapya, “kufikia mwaka wa 2015 majiji mengine yatakuwa yamepita majiji ya Magharibi kwa ukubwa. Ndipo, Tokyo, Bombay, Lagos, Dhaka nchini Bangladesh na Sao Paulo nchini Brazili yatapokuwa makubwa.” Kila moja ya majiji hayo na majiji 25 mengine yatakuwa na wakazi zaidi ya milioni 20. Hata hivyo, gazeti la Times linasema kwamba “makadirio yanaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2015, London halitakuwa kati ya majiji 30 yenye watu wengi, na kati ya majiji yale makubwa, idadi ya wakazi wa London pekee ndiyo itakuwa imepunguka.” Ongezeko la ghafula la wakazi linaleta matatizo mengi. Douglas Massey, profesa wa mambo ya jamii wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Marekani, alisema hivi: “Maskini watazidi kusongamana katika mitaa yao yenye uhalifu mwingi, ujeuri, na msukosuko wa kijamii.” Tokyo lina wakazi milioni 26, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 30 hivi karibuni. Hata hivyo, Tokyo halijapatwa na matatizo mengi sana kwa kuwa idadi ya wakazi imeongezeka polepole, na jiji hilo lina mifumo na huduma mbalimbali zinazohitajika kwa ajili ya ongezeko hilo. Kulingana na Massey, tangu siku za milki ya Roma kufikia utawala wa malkia Victoria wa Uingereza (1837-1901), asilimia 5 hivi tu ya watu wote ulimwenguni waliishi katika majiji, lakini inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2015 asilimia 53 watafanya hivyo.

Acha Kuvuta Sigara, na Usirudie Tena!

Profesa Bo Lundback wa Taasisi ya Taifa ya Watu Wanaofanya Kazi huko Stockholm, Sweden, anaonya hivi: “Wote wanaovuta sigara wanapaswa kujaribu kuacha tabia hiyo. Ukifaulu, hakikisha kwamba hutarudia kuvuta sigara kamwe.” Kwa nini? Kwa sababu huenda ikawa mapafu ya watu walioacha kuvuta sigara na wanaorudia tabia hiyo tena yanaharibika haraka zaidi kuliko ya wale wasioacha kuvuta kamwe. Uchunguzi wa wanaume na wanawake 1,116 walio na umri kati ya miaka 35 hadi 68 uliofanywa kwa muda wa miaka kumi, ulionyesha kwamba mapafu ya wale waliovuta sigara katika muda huo wote yaliharibika kwa asilimia 3, lakini mapafu ya wale walioacha kuvuta kwa mwaka mmoja au zaidi na kuanza tena yaliharibika kwa asilimia 5. Lundback alionya hivi: “Mapafu yanaharibika hasa katika miaka chache ya kwanza mtu anapoanza tena kuvuta sigara baada ya kuacha. Na mapafu yao hayatarudia hali ya kawaida kamwe.” Gazeti la The Times la London linasema kwamba mapafu ya wale walioacha kabisa kuvuta sigara wakati wa uchunguzi huo wa miaka kumi yaliharibika tu kwa asilimia moja.