Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nyasi Si Mmea wa Kijani Tu Unaokua Katika Udongo

Nyasi Si Mmea wa Kijani Tu Unaokua Katika Udongo

Nyasi Si Mmea wa Kijani Tu Unaokua Katika Udongo

KWA watu fulani huo ni mmea wa kijani tu unaokua nje ya nyumba yao ambao itawapasa kuufyeka. Mmea huo ni muhimu kwa wakulima na wacheza-soka, katika shughuli zao. Na kwa watoto, ni mahali pazuri pa kuchezea. Lakini, je, neno nyasi linamaanisha tu mmea unaokua katika ua wa nyumba, mashambani, na kwenye viwanja vya michezo?

Ikiwa unaishi mjini katika orofa ndefu, labda utasema kwamba nyasi haihusiani kwa vyovyote na maisha yako. Hata hivyo, kwa njia fulani sote tunaona aina fulani za nyasi kila siku au kutumia bidhaa zinazotokana nazo. Je, ni mimea ipi inayoweza kuitwa nyasi? Nasi huitumiaje?

Mmea wa Nyasi Ni Upi?

Acha tuchunguze mmea huu wa hali ya chini kwa makini zaidi. Kwa kawaida, mimea yote mifupi ya kijani husemwa kuwa nyasi. Zaidi ya mimea ambayo sayansi imeainisha kuwa nyasi (makundi ya Gramineae, au Poaceae), wengine huona tete na mafunjo kuwa nyasi pia. Hata hivyo, ni aina fulani tu zinazofaa kuitwa nyasi. Aina hizo zina mambo yanayozitambulisha. Hebu litazame kwa makini shina la mmea ambao unafikiri kuwa nyasi.

Je, shina hilo lina umbo la mviringo wenye shimo katikati, na je, lina viungo? Je, majani yake ni marefu, laini na membamba, yenye mistari inayoenda sambamba na majani hayo yanachipuka kutoka kwa ala zinazozunguka shina la mmea? Je, jani moja linachipuka upande huu wa shina na lile linalofuata upande ule mwingine, yote yakifanyiza mistari miwili ya majani iliyo wima? Je, ina mizizi mingi myembamba isiyo na mpangilio wowote hususa bali si mzizi mmoja mkubwa? Je, maua yake—yakiwepo—ni madogo, yasiyovutia, yaliyopangwa kama suke la mahindi, au yana matawi na hayasongamani sana, ama ni maua mengi yaliyorundamana pamoja? Iwapo unajibu ndiyo kwa maswali hayo yote, mmea uliochunguza huenda ukawa aina ya nyasi.

Ingawa nyasi zote zinafanana kwa njia fulani, kuna aina 8,000 hadi 10,000 tofauti-tofauti. Nyasi fupi zina urefu wa sentimeta mbili, na zile ndefu, aina fulani ya mianzi ina urefu wa meta 40. Nyasi ndiyo aina ya mmea ambao hupatikana kwa wingi kuliko mimea mingine duniani. Na si ajabu, kwa sababu huo ndio aina ya mmea ambao unaweza kusitawi katika sehemu nyingi za dunia, kama vile katika ncha ya kaskazini na kusini ya dunia, jangwani, katika misitu ya mvua ya sehemu zenye joto, na kwenye mabonde ya milima ambapo upepo huvuma daima. Nyika zilizojaa nyasi zinapatikana kusini-mashariki mwa Ulaya na Asia; kaskazini mwa Amerika Kusini, hasa; Marekani, na Kanada, hasa sehemu ya magharibi; na sehemu zenye joto.

Nyasi ni mmea wenye nguvu na hilo linaeleza kwa nini unasitawi sana. Tofauti na mimea mingine ambayo hukua kuelekea ncha, nyasi hukua kwenye sehemu iliyo juu ya viungo vyake. Machipukizi mapya huanza kukua kwenye shina na kutambaa kwenye ardhi au chini yake. Inapofyekwa au kuliwa na ng’ombe, nyasi huendelea kukua, jambo ambalo mimea mingine haiwezi kufanya. Kwa hiyo, unapofyeka mara nyingi, nyasi pekee ndiyo huendelea kukua na kuongezeka na kufanya uwanja wako uwe maridadi, huku mimea mingine ikitoweka.

Zaidi ya hilo, mashina ya nyasi aina nyingi yanapojikunja kwa sababu ya kupigwa na upepo au kukanyagwa, upande unaoelekea ardhi unaweza kuchipuka na kusimama tena. Sababu hizo hufanya nyasi kusitawi tena inapokatwa au kukanyagwa, na kuiwezesha kupata mwangaza mwingi kuliko mimea mingine. Kusitawi hivyo kwa nyasi ni kwenye manufaa kwa kuwa sote tunaitegemea.

Mmea Wenye Manufaa Nyingi

Nyasi ndiyo mimea inayopatikana kwa wingi zaidi, na vilevile ina manufaa nyingi zaidi kati ya mimea yote inayochanua maua duniani. Mtaalamu mmoja wa mimea alisema kwamba nyasi ndiyo chanzo cha chakula chetu. Hiyo ‘huzuia wanadamu wasife njaa.’ Jaribu kukumbuka chakula ulichokula leo. Je, ulianza siku kwa bakuli la uji wa wimbi, wali, oat, au mtama? Ikiwa ndivyo, ulikula mbegu ya nyasi aina fulani. Ama pengine ulikula aina fulani ya mkate. Unga uliotumiwa kutengeneza mkate huo ulitokana na mbegu za ngano, shayiri, au mbegu nyingine za nafaka, na zote ni aina za nyasi. Vilevile vyakula vyote vinavyotengenezwa kwa unga wa mahindi kama vile ugali au sima, chapati, na vitinda-mlo mbalimbali. Ndiyo, mahindi ni aina ya nyasi pia. Je, uliongeza sukari katika kahawa au chai yako? Zaidi ya nusu ya sukari yote hutokana na miwa ambayo ni aina ya nyasi. Hata maziwa na jibini ni bidhaa zinazotokana na nyasi kwa njia fulani, kwani ng’ombe, kondoo, na mbuzi ambao hutoa maziwa hula nyasi.

Namna gani chakula chako cha mchana? Tambi na piza zinatengenezwa kwa unga wa ngano. Kuku na ndege wengine hula nafaka. Ng’ombe hulishwa aina nyingi za nyasi. Kwa hiyo, mayai, nyama ya ndege, na ya ng’ombe, hutokana kwa kadiri kubwa na nyasi ambazo mnyama hula. Pia, vinywaji vingi vinatokana na nyasi. Mbali na maziwa, vileo vya aina nyingi hutengenezwa kutokana na nyasi: pombe, wiski, rum, sake, kvass, na aina fulani za vodka.

Ikiwa chakula unachokipenda hakikutajwa hapo juu, usijali kwa kuwa haiwezekani kutaja vyakula vyote vinavyotokana na nyasi. Kulingana na makadirio fulani, zaidi ya nusu ya nishati zinazotokana na kula chakula ulimwenguni pote hupatikana kutoka kwa aina fulani ya nyasi. Na si ajabu, kwa kuwa nyasi inakua kwenye asilimia 70 ya eneo lote la dunia iliyolimwa!

Hata hivyo, nyasi ina matumizi mengine mbali na chakula. Iwapo nyumba yako ina kuta za udongo, na kuezekwa kwa mabua, basi imetengenezwa kwa nyasi. Katika sehemu mbalimbali za ulimwengu, paa huezekwa kwa nyasi. Huko Kusini-Mashariki mwa Asia mianzi hutumiwa kujenga nguzo za kukanyagia wakati wa ujenzi, mabomba ya maji, fanicha, kuta na matumizi mengine mengi. Mikeka na vikapu hushonwa kwa nyasi, na hutumiwa kutengeneza gundi na karatasi. Na usisahau mavazi unayovalia. Wanyama wengi wanaotoa manyoya na ngozi hula nyasi. Aina ya nyasi inayoitwa Arundo donax inatumiwa kutengeneza ala za muziki zinazopulizwa, kama zumari. Hakuna vifaa vingine ambavyo vimepatikana vinavyotumiwa kwa kazi hiyo kama nyuzi hizo za asili.

Nyasi hupamba na kuremba sehemu kubwa ya dunia yetu. Na inafurahisha kama nini kuona konde lenye nyasi msituni au uwanja maridadi uliofyekwa vizuri! Kwa kuwa nyasi zinatoa majani mengi sana, zinatoa kiasi kikubwa cha oksijeni. Mizizi yake iliyo kama nyuzi huzuia mmomonyoko wa udongo. Tunapofikiria manufaa zake nyingi, hatushangai kwamba matumizi na kilimo cha nyasi kina historia ndefu.

Historia ya Nyasi

Nyasi imetajwa kwa mara ya kwanza katika masimulizi ya uumbaji ya Biblia. Katika siku ya tatu ya uumbaji, Mungu alisema hivi: “Nchi na itoe majani.” (Mwanzo 1:11) * Katika lugha ya awali neno lililotafsiriwa ‘majani’ hapa linamaanisha ‘nyasi.’ Jamii zote zimetegemea aina fulani ya nyasi. Kwa mfano, chakula muhimu cha Wamisri, Wagiriki, na Waroma kilikuwa ngano na shayiri; Wachina walikula wimbi na wali; watu wa Indus walikula ngano, shayiri, na wimbi; na Wamaya, Waazteki, na Wainka, walikula mahindi. Maeneo makubwa ambako aina za nyasi zilikua yalitumiwa kulisha farasi za kivita za Wamongoli. Ndiyo, tangu zamani nyasi zimekuwa na manufaa nyingi kwa wanadamu.

Wakati utakapoona shamba la mahindi, uwanja ulio na nyasi nzuri, ama majani machache tu ya nyasi yakikua katikati ya mawe katika kijia, tua na uifikirie mimea hii ya ajabu yenye manufaa nyingi. Hata huenda ukachochewa kumshukuru Mbuni wake Mkuu, Yehova Mungu, kama alivyofanya mtunga-zaburi alipoimba hivi: “Wewe, BWANA Mungu wangu, umejifanya mkuu sana. . . . Huyameesha majani [“nyasi,” NW] kwa makundi, na maboga kwa matumizi ya mwanadamu, ili atoe chakula katika nchi. . . umhimidi Bwana.”—Zaburi 104:1, 14, 31-35.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 17 Huenda mwandishi wa awali wa andiko hili hakutambua tofauti iliyopo kati ya mimea inayofanana na nyasi na ile inayoonwa kwa kweli leo kuwa nyasi.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Muundo wa mimea ya nyasi

Aina kuu za maua ya nyasi

Maua yaliyojipanga kama suke la mahindi

Maua yenye matawi na yasiyosongamana sana

Maua mengi yaliyorundamana pamoja

Mizizi iliyo kama nyuzi

Shina

Jani

Kiungo

Ala

[Picha katika ukurasa wa 18]

Je, ulikula chakula kilichotokana na nyasi leo?

[Picha katika ukurasa wa 18]

Au ulikunywa kutokana nayo?

[Picha katika ukurasa wa 18]

Unaweza pia kuishi katika nyumba iliyotengenezwa nayo

[Picha katika ukurasa wa 18]

Hawa pia hula nyasi