Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hazina za Oaxaca

Hazina za Oaxaca

Hazina za Oaxaca

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

KULINGANA na Taasisi ya Kitaifa ya Elimu ya Wanadamu na Historia huko Mexico, vitu vya kale vimepatikana kwenye sehemu 4,000 kotekote katika jimbo la Oaxaca, kusini-mashariki mwa Mexico. Katika maeneo hayo, wachimbaji wa vitu vya kale wamefukua vitu vya kale vyenye thamani sana, na vingi vya vitu hivyo vimehifadhiwa katika Jumba la Makumbusho la Tamaduni za Oaxaca. Jiunge nasi tunapotembelea jumba hilo zuri la makumbusho.

Jumba la Makumbusho la Tamaduni za Oaxaca * liko katika nyumba iliyokuwa ya watawa wa Santo Domingo de Guzmán katika jiji la Oaxaca, umbali wa kilometa 430 hivi kusini-mashariki mwa Mexico City. Jumba hilo lina vyumba 14 vyenye vito, sanamu, vyombo vya udongo, na vitu vingine vya sanaa vyenye thamani.

Katika chumba cha kwanza kuna ncha za mishale. Hizo zinaonyesha kwamba maelfu ya miaka iliyopita kulikuwapo wawindaji waliohama-hama kotekote katika maeneo ya Oaxaca. Tunapoingia katika chumba cha pili, tunajifunza juu ya Monte Albán, jiji lililokuwa kwenye kilele cha mlima katikati ya bonde la Oaxaca. Jiji hilo linajulikana kuwa “jiji kuu la kwanza katika nchi za Amerika.” Yaelekea Monte Albán lilisitawi sana kati ya mwaka wa 300 W.K. na 900 W.K. Hata hivyo, huenda lilianzishwa katika miaka ya 700 K.W.K.

Magofu ya Monte Albán yanaonyesha kwamba watu wake walijua mengi kuhusu nyota, ufuaji wa dhahabu, na maandishi ya kuchorwa. Baadhi ya majengo yake na vitu vingine vya kale vingalipo. Kwa mfano, kuna piramidi kadhaa zinazoonekana wazi katika bonde hilo. Isitoshe, nyua kubwa za jijini, vijia vya chini ya ardhi, uwanja wa kuchezea mchezo wa mpira uliohusianishwa na dini ulioitwa ollama, na makaburi 170 ya chini ya ardhi yamefukuliwa.

Mnamo Januari 9, 1932, Dakt. Alfonso Caso, ambaye ni mchimbaji wa vitu vya kale, aligundua Kaburi la 7, ambalo ni kaburi la watu wa Zapotec, lililokuwa na mifupa ya mtu mashuhuri na vitu vingi vyenye thamani. Katika kaburi hilo, kulikuwa na mapambo yaliyotengenezwa kwa dhahabu, fedha, na shaba-nyekundu, na vilevile mapambo yenye johari aina ya jade, feruzi, johari zinazofanana na kioo, lulu, na marijani. Vingi kati ya vitu hivyo na vilevile kilogramu nne hivi za vitu vingine vya dhahabu vimehifadhiwa katika jumba hilo la makumbusho.

Mbali na mapambo na vito vinavyometa-meta, vyombo maridadi vya udongo na mifupa iliyochongwa vizuri ilipatikana katika Kaburi la 7. Kitu kimoja kilichovutia kilikuwa gudulia lenye rangi nyingi na michoro. Jiji la Monte Albán lilipoanguka, mtindo wa kuchonga maandishi kwenye mawe ulikoma, na watu walianza kutumia vitabu vyenye maandishi ya lugha ya Mixtec.

Kufikia mwaka wa 900 W.K., majiji yote ya eneo la kusini la Amerika Kaskazini, kutia ndani Monte Albán, yakawa mahame. Kwa miaka 600 iliyofuata, vikosi vya majeshi na wapiganaji walitawala. Kati ya watu wote waliokaa huko Oaxaca katika pindi hiyo, yamkini watu wa Mixtec ndio walioacha vitu vingi vya thamani kuliko wale wengine. Kitabu cha The Encyclopedia Americana kinasema hivi: “Watu wa Mixtec walikuwa mafundi na wasanii stadi waliotengeneza vito na vitabu vyenye picha maridadi.”

Tunatumaini kwamba tutaweza kurudi ili kujifunza jinsi watu wa Mexico walivyopigania uhuru na kuwafukuza Wahispania. Tunakukaribisha ujionee mwenyewe hazina za kale za Mexico. Kwa hakika utafurahia ukifanya hivyo!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Hapo awali jumba hilo liliitwa Jumba la Makumbusho la Regional.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Jiji la Monte Albán lilisitawi sana kati ya mwaka wa 300 W.K. na 900 W.K.

Chini: Picha iliyochongwa na vitu vingine kutoka katika Kaburi la 7, na vyombo vya kipindi hicho

[Hisani]

Picha zote: Reproducción Autorizada por el Instituto Nacional de Antropología e Historia CONACULTA-INAH-MEX