Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Panya na Wanadamu Wanashindania Chakula

Kulingana na Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Australia (CSIRO), duniani pote panya kumi huzaliwa kwa kila mtoto wa binadamu anayezaliwa. Kila siku watoto 360,000 hivi waliozaliwa karibuni wanahitaji kulishwa, lakini panya 3,600,000 waliozaliwa karibuni pia wanataka chakula. Kwa mfano, nchi ya Indonesia ina wakazi milioni 230 hivi, na asilimia 60 hivi kati yao hula wali kila siku. Hata hivyo, katika nchi hiyo, panya hula asilimia 15 hivi ya mazao ya mpunga kila mwaka. Mwanasayansi Dakt. Grant Singleton, mfanyakazi wa shirika la CSIRO anasema hivi: “Jambo hilo linamaanisha kwamba panya hula kiasi cha mchele ambacho kingeweza kuwalisha Waindonesia zaidi ya milioni 20 kwa mwaka mmoja.”

Supu ya Kuku Ni Dawa ya Mafua

Supu ya kuku imetumiwa kwa muda mrefu kutibu magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vile mafua. Katika kitabu Food—Your Miracle Medicine, Dakt. Irwin Ziment, mtaalamu wa mapafu wa Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, anaeleza jinsi supu hiyo inavyosaidia kuponya magonjwa hayo: “Nyama ya kuku, kama vile vyakula vingi vyenye protini, ina asidi-amino inayoitwa cysteine, ambayo inapatikana wakati kuku anapochemshwa. Asidi-amino hiyo inafanana sana na dawa inayoitwa acetylcysteine ambayo hutumiwa na madaktari kutibu ugonjwa wa kifua na magonjwa mengine yanayohusiana na mfumo wa kupumua.” Dawa hiyo ilitengenezwa awali kwa manyoya na ngozi ya kuku, nayo inafanya makamasi ya pua, koo, na mapafu yasiwe mazito sana ili yatiririke kwa urahisi zaidi. Supu ya kuku ina matokeo hayohayo. Ili kuifanya iwe yenye manufaa hata zaidi Dakt. Ziment anapendekeza kuongeza vitunguu saumu, vitunguu, na pilipili katika supu hiyo.

Wafaransa na Mambo Ambayo Wanasayansi Hawawezi Kueleza

Ijapokuwa Wafaransa wanajulikana kuwa watu wanaoamini mambo yanayoweza kuthibitishwa na sayansi tu, bado wengi wao huamini mambo ambayo wanasayansi hawawezi kuyaeleza. Kulingana na gazeti la Le Monde la Ufaransa watafiti walipata kwamba “thuluthi moja ya wenyeji wanaamini ya kuwa utu wa mtu huamuliwa na nyota, na robo ya watu hao wanaamini matabiri ya nyota.” Yapata nusu ya Wafaransa wanaamini katika uponyaji wa imani na kwamba watu fulani wanaweza kuwasiliana kupitia mawazo. Jambo la kushangaza ni kwamba, hata watu wanaopendezwa na sayansi huamini mambo yasiyoweza kuelezwa kwa njia ya kisayansi. Wale waliokuwa na elimu nyingi kuhusu sayansi waliamini zaidi mambo yasiyothibitishwa kisayansi kuliko wale wasiokuwa na maarifa mengi kuhusu sayansi.

Joto Linaloua

Lilipozungumzia kifo cha mwana-michezo Korey Stringer aliyekufa kwa sababu ya joto, gazeti la Time lilieleza kwamba katika hali ya hewa yenye joto kali na unyevu mwingi, huenda jasho lisiweze kuvukizwa haraka vya kutosha ili kupunguza joto mwilini wakati mtu anapofanya kazi ngumu. Hivyo, huenda joto mwilini likaongezeka kiasi cha kusababisha kifo. Dalili zinazoonyesha kwamba joto limeongezeka kupita kiasi mwilini zinaweza kuwa kizunguzungu, maumivu ya kichwa, kichefuchefu, unyonge, kuchanganyikiwa akili, mpigo wa haraka wa moyo, na ngozi iliyo kavu na yenye joto. Ili kuokoa maisha ya mgonjwa ni lazima joto lipunguzwe mwilini kwa kutumia maji ya barafu, vipande vya barafu, au kwa njia nyinginezo. Lakini ni heri kuzuia kuliko kuponya. Gazeti la Time linapendekeza hivi: ‘Usifanye mazoezi wakati wa jua kali. Vaa nguo zisizobana zinazoruhusu hewa kuzunguka mwili wako. Na ni lazima unywe vinywaji vingi, hasa maji. Vileo, chai na vinywaji vya kola vinaweza kupunguza maji mwilini kwa sababu vinaongeza mkojo.’

Tabia Zinazotiliwa Shaka za Makampuni ya Tumbaku

Gazeti la New Scientist la Uingereza linaripoti kwamba hati za siri za makampuni ya tumbaku zinaonyesha kwamba makampuni hayo “yamewadanganya kimakusudi watu wanaovuta sigara kuamini kwamba sigara wanazovuta zina kiasi kidogo cha lami na nikotini.” Kwa mfano, mwaka wa 1990, Muungano wa Ulaya uliweka sheria kwamba kila sigara inaruhusiwa kuwa na miligramu 15 tu za lami na vilevile kiasi fulani cha nikotini. Hata hivyo, ili kutimiza matakwa hayo, hati za kampuni moja zilionyesha kwamba badala ya kupunguza kiasi cha lami na nikotini katika sigara, kampuni hiyo ilibadili njia ya kupima kiasi cha vitu hivyo. Kwa nini udanganyifu huo haukugunduliwa? Gazeti la New Scientist linaripoti kwamba “udanganyifu huo haukugunduliwa kwa sababu makampuni hayo ya sigara ndiyo yanayosimamia baraza [ambalo] linaagiza upimaji huo.” Stella Bialous wa Shirika la Afya Ulimwenguni anasema hivi: “Jambo hilo linaonyesha kwamba sheria hizo haziwezi kulinda watu hata kidogo.”

Matangazo ya Biashara ya Kale

Gazeti la Kila Siku la Watu wa China katika Internet linaripoti kwamba wachimbaji wa vitu vya kale huko China wamegundua matangazo ya biashara ya kale zaidi yaliyoandikwa kwenye karatasi. Sehemu mbili za karatasi ya kufungia vitu, iliyotengenezwa miaka 700 iliyopita na ambayo yaelekea ilitumiwa kufungia unga wa rangi ya mafuta, zilifukuliwa kwenye kaburi moja katika Mkoa wa Hunan, China. Ripoti hiyo inasema hivi: “Kuna herufi 70 za Kichina zinazotaja rangi mbalimbali zilizopatikana, ubora wake, na sifa nyingine, na anwani ya duka lililoziuza pia imeandikwa kwenye karatasi hiyo.” Maneno mengine kwenye karatasi hiyo yanafanana sana na matangazo ya biashara ya siku hizi zetu. Baadhi ya maandishi hayo yanasema: “Rangi zetu ni bora zikilinganishwa na rangi nyingine za mafuta.” Ripoti hiyo inaonyesha kwamba karatasi ilianza kupatikana Ulaya katika miaka ya 1100 na Gutenberg alivumbua uchapishaji baadaye katika miaka ya 1400. Kisha inasema hivi: ‘Mwanamume aliyeitwa Ts’ai Lun alitengeneza karatasi mara ya kwanza mwaka wa 105 A.D. huko China; na uchapishaji wa kutumia mbao ulikuwa ukiendelea huko China katika miaka ya 800.’

Biashara Katika Makanisa

Makanisa kotekote Marekani yanaanzisha biashara ili kulipa gharama kwa sababu michango imepungua na hata wahudhuriaji wamepungua. Stephen Munsey, padri mkuu wa Kituo cha Kikristo cha Familia huko Munster, Indiana, anasema hivi: ‘Itayabidi makanisa yote yenye bidii yaanzishe biashara.’ Kulingana na The Wall Street Journal, biashara hizo katika makanisa zinaweza kuhusisha shughuli kama vile kuuza kahawa na maandazi katika sebule ya kanisa au kuwa na mikahawa maalumu nje ya kanisa. Kanisa moja huko Jacksonville, Florida, lilifungua maduka mbalimbali karibu na jengo la kanisa. Maduka hayo yanatia ndani ofisi ya kuuzia tiketi za ndege, duka la kutengeneza nywele, na mkahawa unaoandaa vyakula vya watu wa kusini mwa nchi hiyo. Mwanzilishi na askofu wa kanisa hilo, Vaughn McLaughlin, anasema hivi: “Yesu alitaka tuzitumie zawadi alizotupatia ili kupata faida.” Anaongeza kwamba mwaka wa 2000, biashara za kanisa hilo zilileta faida ya zaidi ya dola milioni mbili za Marekani.

Je, Bangi Inadhuru?

Gazeti la The Independent la London linasema hivi: ‘Ripoti mpya inaonyesha kwamba bangi inadhuru afya, na inaonya kwamba nguvu ya bangi inazidi kuongezeka na inaweza kusababisha madhara mabaya ya afya yenye kudumu kwa muda mrefu.’ Profesa Heather Ashton wa Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza, anasema hivi: “Bangi inaathiri karibu mwili wote. Ina athari kama zile za kileo, dawa za kutuliza akili, afyuni, na dawa zenye kuleta njozi.” Inajulikana kwamba inapunguza sana uwezo wa kuendesha gari. Inaweza pia kusababisha ugonjwa wa akili, kutia ndani sizofrenia; inaharibu mapafu mara tano zaidi ya sigara; inaweza kusababisha aina mbalimbali za kansa za koo zisizo za kawaida; na inaweza kufanya wavutaji wasio na umri mkubwa wafe kwa mshtuko wa moyo. Katika miaka ya 1960, msokoto mmoja wa bangi ulikuwa na miligramu 10 za kemikali fulani inayoathiri ubongo. “Sasa, kwa sababu ya mbinu za kisasa za kilimo na uzalishaji, msokoto mmoja unaweza kuwa na miligramu 150 hadi miligramu 300 za kemikali hiyo wakati ambapo imeongezwa mafuta ya bangi,” gazeti hilo linasema.

Je, Unamwelewa Daktari Wako?

Gazeti la Brazili la Folha de S. Paulo linaripoti kwamba “madaktari na wagonjwa hawaelewani.” Uchunguzi mmoja uliofanywa kwenye idara ya matibabu ya dharura ya watoto kwenye hospitali moja huko São Paulo, ulionyesha kwamba asilimia 25 ya wazazi waliopeleka watoto hospitalini walitoka bila kujua watoto wao walikuwa na ugonjwa gani, asilimia 24 hawakuweza kusoma agizo la dawa la daktari kwa sababu ya maandishi yasiyosomeka, na asilimia 90 hawakukumbuka jina la daktari. Mambo mbalimbali yanasababisha kutoelewana huko. Baadhi yake ni mahojiano ya “haraka bila kujali hisia za mtu” ambayo huwafanya wagonjwa “wasimtumaini daktari na uchunguzi wake.” Isitoshe, madaktari hutumia maneno mengi yasiyoeleweka, na kwa sababu ya mbinu nzuri za uchunguzi wa magonjwa madaktari hawahitaji kuwauliza wagonjwa maswali mengi kuhusu dalili zao za ugonjwa kama walivyofanya zamani. Kulingana na ripoti hiyo, daktari mmoja wa akili anataja pia kwamba madaktari wengi ‘wanajaribu kuepuka maumivu, mateso, mfadhaiko, na woga wa kifo.’