Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Tutawahitaji Polisi Sikuzote?

Je, Tutawahitaji Polisi Sikuzote?

Je, Tutawahitaji Polisi Sikuzote?

IWAPO hakungekuwa na polisi, huenda kungekuwa na vurugu. Lakini hata tukiwa na polisi, je, kuna usalama ulimwenguni? Siku hizi, hakuna usalama katika majiji mengi na maeneo mengi ya mashambani. Je, twaweza kutazamia kwamba polisi watatulinda dhidi ya mashirika ya wahalifu na wahalifu sugu? Je, twaweza kutazamia kwamba polisi wataleta usalama mitaani mwetu? Je, watakomesha uhalifu?

David Bayley anaeleza maoni yake katika kitabu chake Police for the Future: ‘Polisi hawazuii uhalifu. Wanaweza kulinganishwa na bendeji ambayo inafunika kidonda cha kansa. Hatuwezi kuwategemea polisi, hata ikiwa wanajitahidi sana kuzuia uhalifu, kulinda jamii dhidi ya uhalifu.’ Uchunguzi umeonyesha kwamba kazi tatu kuu za polisi, yaani, kulinda mitaa, kuitikia miito ya dharura, na kufanya uchunguzi, hazizuii uhalifu. Kwa nini?

Kujaribu kuzuia uhalifu kwa kuongeza idadi ya polisi ni jambo linaloweza kugharimu pesa nyingi sana. Hata ikiwa inawezekana kugharimia shughuli hiyo, hilo haliwezi kuwazuia wahalifu. Hata polisi wakifika haraka mahali palipoibiwa, bado hilo haliwezi kuzuia uhalifu sana. Polisi wamesema kwamba hawawezi kumkamata mhalifu isipokuwa tu wafike mahali palipoibiwa kwa muda usiozidi dakika moja. Wahalifu wanajua kuwa polisi hawawezi kufika haraka hivyo. Wala uchunguzi hausaidii. Hata majasusi wanapofaulu kuwashtaki na kuwafunga wahalifu yaonekana hilo halizuii uhalifu. Katika nchi ya Marekani, wahalifu wengi zaidi hufungwa gerezani kuliko katika nchi nyingine yoyote, lakini bado kuna uhalifu mwingi sana huko; kwa upande mwingine, nchini Japani wahalifu wachache hufungwa gerezani, na ni kati ya nchi ambazo hazina uhalifu mwingi sana. Hata mipango ya kuzuia uhalifu kama vile ushirikiano kati ya majirani haikomeshi uhalifu sana, hasa katika maeneo yenye uhalifu mwingi. Hatua kali zinazochukuliwa ili kukomesha uhalifu mbalimbali, kama vile uuzaji wa dawa za kulevya na wizi, hufua dafu kwa muda mfupi, lakini hazidumu kwa muda mrefu.

Kitabu Police for the Future kinasema hivi: “Watu wenye akili wanafahamu kwamba polisi hawawezi kuzuia uhalifu. Inaeleweka kwamba hali za kijamii zisizoweza kudhibitiwa na polisi wala mfumo wa sheria, ndizo zinazosababisha uhalifu katika jumuiya.”

Ni Nini Kingetukia Iwapo Hakungekuwa na Polisi?

Wewe hutendaje wakati ambapo hakuna polisi wanaokutazama? Je, wewe hutumia nafasi hiyo kuvunja sheria? Ni jambo la kushangaza kwamba watu wengi wanaoishi maisha ya kawaida na ya hali ya juu huharibu sifa yao na maisha yao kwa kuiba pesa kazini kwa kutumia udanganyifu. Hivi karibuni gazeti la The New York Times liliripoti kuhusu ‘watu 112 ambao walishtakiwa kwa kujaribu kulaghai kampuni za bima ya magari. Wale walioshtakiwa walitia ndani mawakili, madaktari, na msaidizi mmoja katika ofisi ya Idara ya Polisi.’

Hivi majuzi matajiri wanaodhamini sanaa walishtushwa na kisa cha ulaghai mkubwa wakati wale waliokuwa wasimamizi-wakuu wa mnada wa Sotheby huko New York na mnada wa Christie huko Uingereza walipopatikana na hatia ya kupanga bei za bidhaa zao. Watu hao na minada hiyo imetozwa dola milioni 843 za Marekani ili kulipa faini na fidia! Hivyo, watu wa matabaka yote wanatamani sana pesa.

Kisa kilichotukia mwaka wa 1997 huko Recife, Brazili, wakati polisi walipogoma, kinaonyesha kwamba watu wengi hufanya matendo ya uhalifu wakati ambapo hakuna kizuizi chochote. Imani yao ya kidini haiongozi mwenendo wao. Wanaweza kupotosha na kupuuza maadili kwa urahisi. Basi haishangazi kwamba polisi katika nchi nyingi hawawezi kukomesha uhalifu kwa sababu watu ulimwenguni hupenda kuvunja sheria, iwe ni kwa kadiri ndogo au kubwa.

Kwa upande mwingine, watu fulani hutii sheria kwa sababu wanaheshimu mamlaka. Mtume Paulo aliwaambia Wakristo huko Roma kwamba wanapaswa kunyenyekea mamlaka ambazo Mungu ameruhusu ziwepo kwa kuwa zinadumisha utaratibu wa kadiri fulani katika jamii. Aliandika hivi kuhusu mamlaka hiyo: “Hiyo ni mhudumu wa Mungu, mlipiza-kisasi ili kuonyesha hasira ya kisasi juu ya yeye anayezoea kufanya lililo baya. Kwa hiyo kuna sababu yenye kushurutisha nyinyi watu kuwa katika ujitiisho, si kwa sababu ya hasira hiyo ya kisasi tu, bali pia kwa sababu ya dhamiri yenu.”—Waroma 13:4, 5.

Kubadili Hali Katika Jamii

Ni wazi kwamba kazi ya polisi huboresha hali za kijamii kwa kadiri fulani. Wakati dawa za kulevya na ujeuri unapokomeshwa mitaani kwa kiwango kikubwa, watu hubadili maisha yao kulingana na mabadiliko hayo. Lakini, hakuna jeshi lolote la polisi ambalo linaweza kuboresha kabisa hali katika jamii.

Hebu wazia jamii yenye watu wanaoheshimu sana sheria hivi kwamba hawahitaji polisi. Hebu wazia ulimwengu ulio na watu wanaojali wenzao, ulimwengu ulio na watu ambao wanapenda kusaidiana kila wakati hivi kwamba hakuna yeyote anayehitaji msaada wa polisi. Huenda hilo likaonekana kuwa ndoto za mchana. Hata hivyo, ijapokuwa maneno haya ya Yesu yalisemwa katika kisa kingine, bado yanafaa hali hiyo. Alisema hivi: “Kwa wanadamu hilo haliwezekani, bali kwa Mungu mambo yote yawezekana.”—Mathayo 19:26.

Biblia inazungumza juu ya kipindi fulani cha wakati ujao ambapo wanadamu wote watakuwa raia wa serikali iliyosimamishwa na Yehova Mungu. “Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu.” (Danieli 2:44) Serikali hiyo itabadili hali za kijamii zinazosababisha uhalifu kwa kuwafundisha watu wote wenye moyo mweupe njia ya Mungu ya upendo. “Dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:9) Yesu Kristo, Mfalme aliyewekwa na Yehova, ataweza kuzuia aina zote za uhalifu. “Hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili.”—Isaya 11:3, 4.

Hakutakuwa na wahalifu wala uhalifu. Polisi hawatahitajiwa. “Kila mtu atakaa kwa amani chini ya mitini na mizabibu yake, bila kutishwa na mtu yeyote.” (Mika 4:4, Biblia Habari Njema) Iwapo ungependa kuishi katika “dunia mpya” inayotajwa katika Biblia, sasa ndio wakati wa kuchunguza yale ambayo Mungu ameahidi katika Neno lake.—2 Petro 3:13.

[Blabu katika ukurasa wa 12]

Hebu wazia jamii yenye watu wanaoheshimu sana sheria hivi kwamba hawahitaji polisi

[Blabu Picha katika ukurasa wa 12]

Hakutakuwa na wahalifu wala uhalifu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 11]

Polisi Dhidi ya Magaidi

Kama vile matukio ya Septemba 11, 2001, huko New York City na Washington, D.C., yanavyoonyesha, wateka-nyara na magaidi hufanya iwe vigumu sana kwa polisi kuwalinda watu. Vikosi maalumu vya polisi katika sehemu nyingi za ulimwengu wamezoezwa kuingia mara moja katika ndege na kudhibiti hali. Pia, wamejifunza kuingia kwa ghafula katika majengo—kwa kuteremka kupitia kwenye paa, kuingilia kwenye madirisha, na kutupa makombora yanayofanya watu wapoteze fahamu na gesi ya machozi. Maafisa hao waliozoezwa wamefaulu mara nyingi kuwashtua na kuwashinda magaidi bila kuwahatarisha mateka.

[Hisani]

James R. Tourtellotte/U.S. Customs Service

[Picha katika ukurasa wa 12]

Vitu ambavyo havitahitajiwa tena katika ulimwengu mpya wa Mungu