Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kuwapatia Ndege “Peremende”
Gazeti la Ujerumani linaloitwa GEO, linaripoti kwamba ‘mmea mmoja nchini Brazili unatumia njia ambayo haikujulikana ili kuongeza kiwango cha uchavushaji.’ Badala ya kutengeneza kinywaji kitamu, mmea wa Combretum lanceolatum huwapatia wageni wake “peremende.” Usiku, maua ya mmea huo hutoa vidonge vyenye sukari ambavyo huwa na vipenyo vya milimeta sita vinapokuwa vigumu. Glukosi na sukari inayopatikana katika matunda hutumiwa kuongeza utamu kwenye peremende, na wachunguzi wanasema zinakuwa kama “peremende zinazouzwa dukani.” Ripoti hiyo inaeleza kwamba “maua ya mmea huo yanapochanua wakati jua linapochomoza, peremende hizo zinazopitisha mwangaza, na zenye kumetameta huwa kama zilizopangwa kwenye sinia.” Peremende hizo huvuta angalau “aina 28 za ndege kutoka kwa makundi manane ya ndege.” Wakati ndege hao wanapotafuta chakula kutoka mmea mmoja hadi mwingine, wao hubeba chembe nyingi za chavua, na kwa njia hiyo kusaidia mmea huo kuenea kwa haraka katika sehemu nyingine.
Watoto Waitaliano Wenye Furaha
Likiripoti kuhusu uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Kitaifa cha Uchanganuzi wa Habari za Watoto na Wabalehe, gazeti la kila siku La Repubblica mjini Roma linasema kwamba ‘watoto Waitaliano ni wenye furaha zaidi barani Ulaya.’ Watafiti waligundua kuwa asilimia 96 ya watoto nchini Italia hulelewa katika nyumba zilizo na wazazi wote wawili. Hicho ni kiwango cha juu kuliko cha nchi nyinginezo barani Ulaya, ambako wazazi wengi wametengana ama kutalikiana. Kwa kuongezea, zaidi ya nusu ya jamaa zina babu na nyanya wanaokaa katika nyumba hiyohiyo au karibu na hapo. Kwa hiyo, babu au nyanya “8 hadi 10” huwaona wajukuu wao “zaidi ya mara moja kila juma.” Ripoti hiyo inasema kwamba jambo hilo humfanya mtoto “kuhisi kwamba yeye ni sehemu ya jamaa fulani” na hupunguza upweke. Mwanasaikolojia Alessandra Graziottin anasema: “Kama ilivyo na mtu mzima, mtoto hufurahi anapohisi kwamba anapendwa, lakini si kwa kupata mali au kuvalia mavazi ya hali ya juu.”
Kufurahia Kusafiri kwa Ndege
Ili kufurahia kusafiri kwa ndege, gazeti la El Universal la Mexico City linatoa madokezo yafuatayo: (1) Tumia vinywaji vingi, kwa sababu hewa ndani ya ndege huwa kavu sana. (2) Hewa kavu yaweza kufanya macho yawashe, kwa hiyo vaa miwani badala ya lenzi zinazoingizwa ndani ya macho. (3) Fanya mazoezi mepesi ukiwa kitini ili kulegeza misuli na kusaidia mzunguko wa damu miguuni. (4) Tembea kwenye kijia cha ndani ya ndege mara kwa mara. (5) Vaa viatu ambavyo ni rahisi kutoa, na utumie kikanyagio—pengine mfuko wako wa safari. (6) Ili kuruhusu ngozi yako ipate hewa ya kutosha, valia mavazi mororo yanayostarehesha yaliyotengenezwa kwa nyuzi asilia. (7) Tumia kileo kidogo tu au usinywe hata kidogo, kwani athari ya kileo huongezeka kadiri ndege inavyoendelea kupaa. (8) Rekebisha kisafisha-hewa ili kisielekee moja kwa moja shingoni au mgongoni. (9) Jaribu kulala. Labda itakuwa vizuri ufunike uso kuzuia mwangaza. (10) Tafuna kitu fulani wakati ndege inapopaa na wakati inapotua ili kupunguza mkazo masikioni. Watoto wanaweza kupewa mpira wa kunyonya.
Watoto Wanaoendekezwa Huko Ujerumani
“Tabia mpya ya kuwaendekeza” watoto imeonekana miongoni mwa wazazi, anasema Udo Beckmann, mwenyekiti wa chama cha walimu cha Ujerumani. Kulingana na gazeti la Südwest Presse, Beckmann alisema kwamba watoto zaidi na zaidi wanaendekezwa sana, na tokeo ni kwamba, hawataki kujitahidi sana shuleni. “Yeye alisema kuwa ni jambo la kawaida kwa wazazi kuwa na maoni ya kwamba migao ya shule inawapatia watoto wao ‘mfadhaiko mwingi sana’ na kwamba ‘si jambo la akili’ kuwataka watoto wasome kwa ajili ya mitihani ya shule.” Ripoti hiyo pia ilisema kwamba ikiwa wazazi wataendelea kuwaendekeza watoto ili kuepuka kuwakasirisha, watawanyima watoto “nafasi ya kuwa watu wenye kuwajibika maishani.” Beckmann anasema kwamba watoto walioendekezwa, huwa “watu wazima wenye ubinafsi” wanaotaka kupata kila kitu lakini hawataki kukitolea jasho.
Kwa Nini Ndege Hufanyiza Muundo wa V Wanaporuka?
Likizungumza kuhusu ripoti iliyochapishwa katika gazeti la Nature, gazeti la The Daily Telegraph la London lilisema kwamba watafiti wamechunguza na kubainisha kuwa ndege aina ya bata-bukini na mwari “hufanyiza muundo wa V wanaporuka ili kupunguza athari ya upepo na kupunguza nguvu wanayotumia wanaposafiri mbali sana.” Wanasayansi wa Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Kisayansi huko Villiers en Bois, Ufaransa, walipima mpigo wa moyo wa ndege wanane aina ya mwari walioruka kwa kufanyiza muundo wa V kisha wakalinganisha vipimo hivyo na “mara ambazo wao hupigapiga mabawa na jinsi wanavyoruka.” Watafiti hao walitambua kwamba mpigo wa moyo wa ndege hao ulipungua waliporuka pamoja na walipigapiga mabawa yao mara chache kuliko wakati kila mmoja aliporuka peke yake, ingawa mwendo haukubadilika. Gazeti la Nature linasema kwamba ‘wakati ndege wanaporuka pamoja, kila bawa huinuliwa kwa msukumo unaotokezwa na wale ndege wengine katika kikundi kile.’ Mbinu hii huwawezesha mwari weupe wakubwa kupunguza nguvu wanayotumia kwa asilimia 20 kuliko wakati kila mmoja anaporuka akiwa peke yake.
Usomaji wa Biblia Nchini Ufaransa
Kulingana na ripoti iliyochapwa na gazeti la Kikatoliki La Croix, ingawa asilimia 42 ya Wafaransa waliohojiwa katika uchunguzi mmoja walikuwa na Biblia, ni karibu asilimia 2 tu kati yao ndio waliosema kwamba waliisoma kila siku. Asilimia 72 walisema “hawaisomi Biblia hata kidogo.” Asilimia 54 ya wale waliohojiwa waliiona Biblia kuwa “kitabu cha kale” ambacho “hakipatani na ulimwengu wa kisasa.” Ripoti hiyo inaeleza kuwa “Wafaransa wanaiona Biblia kwanza kabisa kuwa kitabu cha kitamaduni,” cha kuelezea “chanzo cha dini ya Kiyahudi na ya Kikristo.” Gazeti la La Croix linasema kwamba “kila mwaka, karibu Biblia 250,000 na nakala 30,000 za Agano Jipya huuzwa nchini Ufaransa.”
Shule ya Unajimu Yakubaliwa Rasmi
Gazeti la The New York Times linasema kwamba shule moja huko Marekani “ambako wanafunzi hujifunza kutabiri kwa kutumia nyota na kushauri kuhusu wakati ujao . . . imepata kibali kutoka kwa shirika linalotambuliwa na serikali, na inaaminiwa kuwa hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa shule ya unajimu kupata kibali kama hicho.” Kulingana na mwanzilishi wa shule hiyo, “nyota zilionyesha” mwezi ambao kibali hicho kingetolewa. Shule hiyo inayoitwa Taasisi ya Unajimu, inafundisha masomo yanayotia ndani ‘somo linalofundishwa na mwalimu stadi kuhusu miungu ya kike ya anga,’ na jingine kuhusu “jinsi ya kuandika safu ya kinajimu katika magazeti.” Wengi wanaohitimu kutoka taasisi hiyo “huanzisha biashara zao wenyewe, ingawa wengine huajiriwa katika zahanati zinazohusika na magonjwa ya akili, ya mwili, na matatizo ya watu katika jamii, katika sehemu za kufanyia mazoezi ya kimwili, na katika meli zinazosafiri mbali.” Gazeti la Times lilitaarifu kuwa “taasisi hiyo ilipata kibali hicho . . . baada ya kuthibitisha kwamba walimu wake wanastahili kufundisha na kwamba wale wanaohitimu kutoka taasisi hiyo wanaweza kupata kazi za kuajiriwa.” Hata hivyo, kulingana na mkuu wa Baraza la Kutoa Vibali vya Elimu ya Juu, “kibali hicho hakidokezi kwamba habari za unajimu ni za kweli, bali kilitolewa kwa sababu taasisi hiyo inawatimizia wanafunzi ahadi zake.”
Kuusafisha Mlima Everest
Mlima Everest, ni mlima mrefu zaidi duniani (meta 8,850) nao ni mkubwa na wenye kuvutia sana. Hata hivyo, ripoti moja iliyoandikwa katika gazeti la Down to Earth la New Delhi inaonyesha kwamba Mlima Everest umekuwa mahali pa kutupa takataka nyingi. Mamia ya watu ambao wameupanda mlima huo kwa miaka michache iliyopita wametupa tani nyingi za takataka, kutia ndani “mitungi iliyofunuliwa ya oksijeni, ngazi kuukuu au magongo ya zamani na vijiti vya plastiki.” Kituo kilicho na takataka nyingi zaidi kinaitwa “South Col, ambapo wengi wanaopanda husimama ili kujitayarisha kuelekea kwenye kilele cha mlima.” Ofisa wa Muungano wa Wapanda-Milima wa Nepal Bhumi Lal Lama, alisema hivi: “Tunapanga kuwalipa [watu wa Sherpas] dola 13.50 za Marekani kwa kila kilogramu [ratili 2.2] ya takataka watakazoondoa.” Ripoti hiyo inasema kwamba watu wa Sherpas “huwaelekeza na kuwabebea mizigo watu” wanaopanda Mlima Everest.
“Mizungu” Yashindwa Kufanya Kazi
Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba “mwanamume mmoja Mghana alipigwa risasi na kuuawa na mwenzake kijijini alipokuwa akijaribu mizungu fulani iliyotazamiwa kufanya risasi isipenye mwilini mwake.” Watu kadhaa wanaoishi vijijini kaskazini-mashariki mwa Ghana walimwomba mganga wa miti-shamba wa kienyeji awagange ili wasiumizwe na risasi. “Baada ya kupaka mwili mzima dawa fulani iliyotengenezwa kwa miti-shamba kila siku kwa majuma mawili,” ripoti hiyo inasema mwanamume huyo “alijitolea kupigwa risasi ili aone ikiwa mizungu ilikuwa imefanya kazi.” Mwanamume huyo alikufa papo hapo alipopigwa risasi ya kwanza. Baadaye, majirani waliokuwa na hasira walimshika mganga huyo na kumpiga vibaya kwa sababu mizungu yake haikufaulu. Mara nyingi, watu wanaoishi sehemu ya kaskazini mwa Ghana hutafuta msaada kutoka kwa waganga wa miti-shamba wa kienyeji, ili kulindwa na maadui kutoka kwa makabila mengine.