Kwa Nini Ni Muhimu Kuwa na Polisi?
Kwa Nini Ni Muhimu Kuwa na Polisi?
HEBU wazia jinsi ambavyo hali zingekuwa iwapo hakungekuwa na polisi. Ni nini kilichotokea mwaka wa 1997 wakati polisi 18,000 walipogoma katika jiji la Recife huko Brazili lenye zaidi ya wakazi milioni moja?
Gazeti la The Washington Post liliripoti hivi: ‘Kwa kipindi cha siku tano zenye fujo, idadi ya mauaji ya kila siku imeongezeka mara tatu katika jiji hili la pwani. Mabenki manane yameibiwa. Magenge yamezusha fujo madukani na kufyatua risasi katika mitaa ya matajiri. Na hakuna mtu yeyote anayefuata sheria za barabarani. Uhalifu huo umesababisha vifo vingi sana hivi kwamba chumba cha kuhifadhia maiti kimejaa sisisi, na watu wengi sana waliojeruhiwa kwa risasi au kudungwa visu wamejaa katika hospitali kubwa ya serikali huku wakiwa wamelala sakafuni.’ Waziri wa sheria aliripotiwa akisema hivi: “Uvunjaji wa sheria wa aina hii haujawahi kamwe kutukia hapa.”
Uovu uko kila mahali hata ingawa umefichwa na ustaarabu. Tunahitaji ulinzi wa polisi. Kwa wazi, wengi wetu tumesikia kwamba baadhi ya maafisa wa polisi ni wakatili, wafisadi, wasiojali, na wanatumia mamlaka vibaya. Idadi ya visa hivyo hutofautiana katika nchi mbalimbali. Lakini hali zingekuwaje iwapo hakungekuwa na polisi? Je, hukubali kwamba mara nyingi polisi hutoa huduma muhimu? Gazeti la Amkeni! liliwaomba baadhi ya maafisa wa polisi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu waeleze ni kwa nini walichagua kazi hiyo.
Huduma kwa Jamii
Ivan, afisa mmoja wa polisi huko Uingereza, alisema hivi: ‘Ninapenda kuwasaidia watu. Nilivutiwa na kazi hii kwa
sababu inahusisha mambo mbalimbali. Kwa kawaida watu hawajui kwamba asilimia 20 hadi asilimia 30 tu ya kazi ya polisi ndiyo inayohusisha kushughulika na uhalifu. Kazi ya polisi inahusisha hasa kuhudumia jamii. Kazi yangu ya kila siku inaweza kuhusisha kushughulikia kifo cha ghafula, msiba wa barabarani, uhalifu, na hata kumsaidia mzee aliyechanganyikiwa. Unaweza kujihisi vizuri sana unapomrudisha mtoto aliyepotea kwa mzazi wake au kumfariji mtu aliyeathiriwa kwa sababu ya uhalifu.’Hapo zamani, Stephen alikuwa afisa wa polisi huko Marekani. Anasema hivi: ‘Nilitaka kuwa polisi kwa sababu polisi ana uwezo na wakati wa kuwasaidia watu kwa njia bora zaidi wakati wanapomwomba awasaidie. Nilitaka kujitolea kuwasaidia watu. Ninahisi kwamba nilisaidia kwa kiasi fulani kuwalinda watu dhidi ya uhalifu. Niliwakamata zaidi ya watu 1,000 kwa kipindi cha miaka mitano. Lakini nilifurahi sana nilipowapata watoto waliokuwa wamepotea, nilipowasaidia wagonjwa wa akili waliokuwa wametoroka makwao, na kupata magari yaliyokuwa yameibwa. Pia, nilisisimuka nilipowafuata na kuwakamata washukiwa.’
Roberto, afisa wa polisi huko Bolivia, anasema hivi: ‘Nilitaka kuwasaidia watu katika hali za dharura. Nilipokuwa kijana nilivutiwa na polisi kwa sababu waliwalinda watu na hatari. Muda mfupi baada ya kuanza kazi hiyo niliwasimamia askari wa doria jijini, mahali ambapo kuna ofisi za serikali. Karibu kila siku kulikuwa na maandamano ya kisiasa. Kazi yangu ilikuwa kuzuia ghasia. Nilitambua kwamba nikishughulika na viongozi wa maandamano hayo kwa urafiki na busara ningeweza kuzuia fujo ambazo zingeweza kusababisha watu wengi wajeruhiwe. Jambo hilo lilinifurahisha.’
Polisi hutoa huduma nyingi. Wao hufanya mambo kama vile kuokoa paka aliyekwama kwenye mti, kuwaokoa watu waliotekwa nyara na magaidi, na kukabili wezi wa benki. Hata hivyo, tangu majeshi ya polisi yalipoanzishwa katika siku za kisasa, watu wametarajia na kuhofia mambo fulani kuhusu polisi. Makala inayofuata inazungumzia sababu ya maoni hayo.
[Picha katika ukurasa wa 2, 3]
Ukurasa wa 2 na 3: Polisi wanaongoza magari huko Chengdu, China; polisi wa kutuliza ghasia huko Ugiriki; maafisa wa polisi huko Afrika Kusini
[Hisani]
Linda Enger/Index Stock Photography
[Picha katika ukurasa wa 3]
Duka ambalo liliporwa wakati wa mgomo wa polisi huko Salvador, Brazili, Julai 2001
[Hisani]
Manu Dias/Agência A Tarde
[Picha katika ukurasa wa 4]
Stephen, Marekani
[Picha katika ukurasa wa 4]
Roberto, Bolivia