Reli Inayoenea Kotekote India
Reli Inayoenea Kotekote India
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA
Zaidi ya miaka 4,000 iliyopita, wajenzi walikuwa wakichoma matofali kaskazini mwa India. Lakini hawakujua kamwe kwamba miaka mingi baadaye matofali hayo yangetumiwa katika ujenzi wa mfumo mkubwa sana wa reli huko India.
MFUMO wa Reli ya India ni mkubwa sana. Wengi wa wakazi zaidi ya bilioni moja wa nchi hiyo husafiri kwa gari-moshi kwa kawaida. Mbali na usafiri wa kila siku, Wahindi wanaoishi mbali na jamaa zao husafiri nyumbani wakati mtoto anapozaliwa, mtu anapokufa, wakati wa arusi au sherehe nyingine, au ili kumtembelea mgonjwa.
Kwa wastani, zaidi ya magari-moshi 8,350 husafiri jumla ya kilometa 80,000 hivi kila siku, yakisafirisha zaidi ya abiria milioni 12.5. Magari-moshi ya mizigo husafirisha zaidi ya tani milioni 1.3 ya bidhaa. Kila siku, magari-moshi ya mizigo na ya abiria husafiri umbali unaolingana na kusafiri hadi kwenye mwezi mara tatu na nusu!
Reli ya India ina vituo 6,867, vichwa 7,500 vya magari-moshi, mabehewa zaidi ya 280,000, kilometa 107,969 za reli kutia ndani reli fupi za kandokando, na wafanyakazi milioni 1.6. Hakuna kampuni nyingine ulimwenguni iliyo na waajiriwa wengi hivyo. Huo ni mfumo mkubwa mno wa reli!
Jinsi Reli Hiyo Ilivyoanza Kujengwa
Kwa nini kulikuwa na uhitaji wa reli huko India? Ujenzi ulianza lini? Na vipi yale matofali yaliyochomwa miaka 4,000 iliyopita?—Ona sanduku lililo hapo juu.
Katikati ya miaka 1800, pamba ilipandwa kwa wingi huko India, nayo ikasafirishwa kwa magari hadi kwenye bandari ili iuzwe katika nchi nyingine. Hata
hivyo, pamba nyingi iliyotumiwa kwenye viwanda vya nguo huko Uingereza haikutoka India, bali ilitoka katika majimbo ya kusini-mashariki mwa Marekani. Lakini, kukawa na upungufu wa pamba kwa sababu ya kuharibika kwa zao la pamba huko Marekani mwaka wa 1846, na kwa sababu ya Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe kati ya mwaka wa 1861 hadi 1865. Suluhisho lilikuwa kupata pamba kutoka India. Lakini usafirishaji ulihitaji kuharakishwa ili viwanda vya nguo huko Lancashire, Uingereza, visisimame kwa sababu ya kukosa pamba. Kampuni ya Reli ya India Mashariki (1845) na Reli Kuu ya Peninsula ya India (1849) zilianzishwa. Mikataba ilifanywa na kampuni ya East India Company ya Uingereza, iliyokuwa kampuni kuu ya biashara nchini India. Baada ya muda mfupi, gari-moshi la kwanza huko India lilianza kusafiri Aprili 16, 1853. Lilisafiri kilometa 34 kutoka eneo la bandari linaloitwa Bori Bunder jijini Bombay (ambalo siku hizi linaitwa Mumbai), hadi mji wa Thāne.Reli kutoka Bombay hadi sehemu ya mbali ya mashambani ambapo pamba ilipandwa ilihitaji kuvuka milima yenye miinuko mikali inayoitwa Western Ghats. Wahandisi na wafanyakazi Waingereza, pamoja na maelfu ya wafanyakazi Wahindi walifanya kazi hiyo ngumu bila tekinolojia ya siku zetu. Nyakati nyingine wafanyakazi walikuwa 30,000. Walijenga reli kwa njia ya kupindapinda kwenye miinuko mikali. Mbinu hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza ulimwenguni wakati huo. Katika sehemu moja, kilometa 24 za reli zilijengwa ili kupanda mlima wenye mwinuko wa meta 555. Reli hiyo inapita chini ya ardhi katika sehemu 25, kwa meta 3,658 kwa ujumla. Na ilipofikia uwanda wa juu wa Deccan, reli hiyo ilikuwa tayari kutumika. Kazi ya kujenga reli iliendelea kwa haraka kotekote nchini. Mbali na uhitaji wa kusafirisha bidhaa, kulikuwa na uhitaji wa kuhamisha wanajeshi na wafanyakazi kwa haraka kwa sababu Waingereza walizidi kupanua shughuli zao katika nchi hiyo.
Katika miaka ya 1800, watu wachache wenye mali waliweza kusafiri kwa starehe sana bila kusumbuliwa na joto na vumbi. Magari-moshi yalikuwa na behewa lenye kitanda kizuri, choo na bafu. Watumishi waliandaa viburudisho kuanzia chai ya asubuhi hadi chakula cha jioni. Feni iliyowekwa juu ya chombo chenye maji ya barafu ilipunguza joto. Kulikuwa na kinyozi, na vilevile vichapo vya hadithi kutoka Maktaba ya Reli ya Wheeler, kutia ndani hadithi mpya za mwandishi Rudyard Kipling, aliyezaliwa nchini India. Louis Rousselet, aliyekuwa akisafiri katika miaka ya 1860, alisema kwamba aliweza “kusafiri umbali huo wote bila kuchoka sana.”
Mfumo wa Reli Wapanuliwa
Kufikia mwaka wa 1900, mfumo wa reli wa India ulikuwa wa tano kwa ukubwa ulimwenguni. Vitu ambavyo hapo awali vilitengenezwa katika nchi za nje, vilianza kutengenezwa nchini India. Hivyo vinatia ndani vichwa vya magari-moshi, injini zinazoendeshwa kwa mvuke, mafuta, na umeme; na mabehewa na magari mengine yanayosafiri kwenye reli. Vichwa vingine vya magari-moshi vilifikia uzito wa tani 230. Baadhi ya vichwa vinavyoendeshwa kwa umeme vilikuwa na nguvufarasi 6,000, na kimoja kinachoendeshwa kwa mafuta kilikuwa chenye uzito wa tani 123 na chenye nguvufarasi 3,100. Gari-moshi la kwanza lenye ghorofa mbili lilianza kutumiwa mwaka wa 1862. Katika jiji la Kharagpur, huko Bengal Magharibi, kuna sehemu iliyoinuka kando ya reli yenye urefu wa meta 833, nayo ni ndefu kuliko zote ulimwenguni. Huko Sealdah, jijini Calcutta, kuna sehemu kama hizo zilizofunikwa zenye urefu wa meta
300 hivi, hizo pia ni ndefu kushinda zote ulimwenguni.Mwanzoni, reli zilijengwa zikiwa na nafasi ya zaidi ya meta moja kutoka chuma kimoja cha reli hadi kile kingine. Lakini baadaye, ili kuhifadhi fedha, zilijengwa zikiwa na nafasi ya meta moja kati ya vyuma vya reli, na hata zikiwa na nafasi ndogo zaidi kwenye milima. Kazi ya kufanya reli zote ziwe na nafasi sawa kati ya vyuma vya reli ilianza mwaka wa 1992, na hadi leo hii karibu kilometa 7,800 za reli zenye nafasi ya meta moja na zile zenye nafasi ndogo zimebadilishwa kuwa zenye nafasi inayozidi meta moja kati ya vyuma vya reli.
Kila siku magari-moshi ya jiji la Mumbai husafirisha mamilioni ya watu wanaoishi karibu na jiji hilo hadi jijini. Yaelekea, sikuzote, watu husongamana katika magari-moshi hayo. Magari-moshi ya chini ya ardhi jijini Calcutta yanaweza kusafirisha abiria milioni 1.7 kila siku. Reli ya kwanza ya India inayopita kwenye daraja inapatikana jijini Chennai (lililoitwa Madras hapo awali). Siku hizi kuna vibanda vya kuagiza tiketi kupitia kompyuta na vilevile vibanda vyenye vyombo vya habari vinavyotoa taarifa za usafiri. Kampuni hiyo ya reli ina shughuli nyingi na inafanya maendeleo daima.
Magari-Moshi Madogo Yanayopendeza
Waingereza walioishi India walipenda sana kwenda milimani ili waepuke joto. Ili wafike milimani kwa haraka zaidi, reli za magari-moshi madogo zilijengwa. Kusafiri kwa magari-moshi hayo kulichukua muda mfupi kuliko kusafiri kwa farasi au kubebwa kwa machela. Kwa mfano, gari-moshi moja dogo huku kusini mwa India huwasafirisha abiria hadi Milima ya Nilgiri, au Blue Mountains. Kwa wastani, gari-moshi hilo husafiri kwa mwendo wa kilometa 10.4 kwa saa, mwendo ambao huenda ni wa polepole kuliko mwendo wa magari-moshi yote mengine huko India. Lakini safari hiyo inapendeza sana kwa kuwa gari-moshi hilo hupitia mashamba ya chai na kahawa ya milimani hadi linapofika Coonoor kwenye mwinuko wa meta 1,712. Reli hiyo ilijengwa mwishoni mwa miaka ya 1800, na meta 12 za reli zilihitajika ili kupanda mwinuko wa meta 1 wa mlima. Reli hiyo inajipinda mara 208 na inapita chini ya ardhi katika sehemu 13. Kwenye reli hiyo kuna magurudumu yenye meno yanayosaidia kichwa cha gari-moshi kupanda mlima, huku kikisukuma mabehewa kutoka nyuma. Reli hiyo ndiyo ya zamani na yenye mwinuko mkali zaidi kati ya reli zote ulimwenguni zinazotumia mbinu hiyo ya kupanda mlima.
Reli ya Darjeeling ya Himalaya ina nafasi ya sentimeta 61 tu kati ya vyuma vya reli, na meta 22.5 za reli zilihitajika ili kupanda mwinuko wa meta 1 wa mlima. Reli hiyo inafika hadi kituo cha gari-moshi cha
Ghoom kilicho kwenye mwinuko wa meta 2,258. Kituo hicho kiko kwenye mwinuko wa juu kuliko vituo vingine huko India. Reli hiyo inajivuka katika sehemu tatu, na katika sehemu sita inajipinda hivi kwamba inaonekana inarudi mahali ilipoanzia. Mpindo wa Batasia ndio mpindo maarufu zaidi wa reli hiyo. Gari-moshi linapofika sehemu hiyo, abiria anaweza kutamani kushuka, kupanda mlima kwa mguu, na kupanda gari-moshi tena linapopita mahali alipo. Jambo linalopendeza sana kwenye safari hiyo yenye kusisimua ni kuuona mlima wa Kanchenjunga, mlima wa tatu kwa urefu ulimwenguni. Reli hiyo imelindwa na shirika la UNESCO tangu mwaka wa 1999, kwa hiyo inatumainiwa kwamba haitatokomea.Waingereza walipotawala, mji wa Simla, ulioko kwenye mwinuko wa meta 2,200, ndio uliokuwa mji mkuu wakati wa joto. Ili kufika mji huo gari-moshi husafiri kilometa 95, hupita chini ya ardhi katika sehemu 102, huvuka madaraja 869, na reli hiyo hujipinda mara 919. Abiria wanaweza kuona mandhari nzuri sana kupitia madirisha makubwa ya gari-moshi na paa linalopitisha mwangaza lililotengenezwa kwa mchanganyiko wa kioo na plastiki. Ndiyo, magari-moshi hayo madogo hupendeza sana. Hata hivyo, kwa sababu nauli ni ya bei nafuu, kampuni ya reli za milimani inapata hasara. Watu wanaopenda reli wanatumaini kwamba suluhisho litapatikana ili magari-moshi hayo yenye kusisimua yasikomeshwe.
Safari Ndefu
Inasemekana kwamba reli ya India “ilileta mwisho wa enzi moja na kuanzisha enzi nyingine” na kwamba “reli hiyo iliunganisha India kuliko mbinu yoyote ile ya kuunganisha tangu wakati huo.” Maneno hayo ni kweli kabisa. Ukitaka, unaweza kupanda gari-moshi Jammu, chini ya milima ya Himalaya, na kushuka Kanyakumari, sehemu ya kusini kabisa ya India, mahali ambapo Bahari ya Arabia, Bahari ya Hindi, na Ghuba ya Bengal zinakutana. Ukifanya hivyo, utakuwa umesafiri kilometa 3,751, utakuwa umepita majimbo 12, na utakuwa umesafiri kwa muda wa saa 66 hivi. Hata ukisafiri katika behewa lenye kitanda huenda ukalipa chini ya dola 15 za Marekani. Pia, utakuwa umekutana na watu wenye urafiki wa tamaduni mbalimbali wanaopenda mazungumzo na utakuwa umeona sehemu kubwa ya nchi hiyo inayovutia. Kata tiketi yako na uwe na safari njema!
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Yale Matofali ya Zamani
Waingereza walipotawala India (1757-1947), magari-moshi yalifaa sana kwa kuwahamisha wanajeshi. Kabla ya miaka mitatu kupita baada ya kulizindua gari-moshi la kwanza la India, wahandisi walikuwa wakijenga reli kati ya Karachi na Lahore. Eneo hilo ni la Pakistan siku hizi. Mawe hayakupatikana kwa ajili ya msingi wa reli, lakini karibu na kijiji cha Harappa, wafanyakazi waligundua matofali yaliyokuwa yamechomwa. Wahandisi John na William Brunton wa Scotland waliona kwamba matofali hayo yalifaa kwa ujenzi na kwamba gharama zingepunguka kama wangetumia hayo badala ya mawe. Wafanyakazi walipokuwa wakiendelea kufukua matofali hayo, walipata visanamu vya udongo na mihuri yenye maandishi ya lugha isiyojulikana, lakini jambo hilo halikuwazuia wasiendelee na kazi hiyo muhimu ya kujenga reli. Kilometa 160 za reli zilijengwa kwa kutumia matofali kutoka Harappa. Miaka 65 baadaye, wachimbaji wa vitu vya kale walichimbua kwa utaratibu eneo la Harappa, na wakapata vitu vya kale vya utamaduni wa hali ya juu wa Bonde la Indus, ulioanza zaidi ya miaka 4,000 iliyopita. Utamaduni huo ulikuwapo wakati uleule wa utamaduni wa kale wa Mesopotamia!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
Reli ya Pekee ya KONKAN
Eneo jembamba la Konkan lililoko kwenye pwani ya magharibi ya India, katikati ya Bahari ya Arabia na safu ya milima ya Sahyadri, lina upana usiozidi kilometa 75. Eneo hilo linafaa biashara kwa kuwa linaanzia Mumbai ambalo ni jiji kuu la biashara la India na kufika hadi bandari kubwa ya Mangalore upande wa kusini. Kwa karne nyingi bandari zilikuwa muhimu kwa ajili ya biashara za ndani ya nchi na za nchi nyinginezo. Lakini kusafiri baharini kulikuwa hatari, hasa wakati wa msimu wa pepo wakati mito pia ilipofurika. Na kusafiri kwenye barabara na reli kulichukua muda mrefu kwa sababu hizo zilizunguka mito na milima na vizuizi vingine. Watu wa eneo hilo walitamani sana kuwa na njia ya moja kwa moja hadi pwani ili waweze kupeleka bidhaa zao kwa haraka kwenye masoko makubwa, hasa bidhaa zilizoharibika upesi. Suluhisho lilikuwa nini?
Mradi wa kujenga Reli ya Konkan ulikuwa mradi mkubwa zaidi wa kujenga reli katika miaka ya 1900 huko India. Mradi huo ulihusisha kujenga kilometa 760 za reli zenye matuta na mitaro. Baadhi ya matuta yalikuwa na kimo cha meta 25, na mitaro mingine ilikuwa na kina cha meta 28. Pia ulitia ndani kujenga zaidi ya madaraja 2,000. Mojawapo ya madaraja hayo ni daraja la Panval Nadi lenye kimo cha meta 64 ambalo linavuka bonde lenye upana wa meta 500. Hilo ni daraja refu kushinda yote huko Asia. Daraja jingine ni lile linalovuka Mto Sharavati lenye urefu wa kilometa 2.065. Ili reli hiyo isizunguke milima, inapita chini ya ardhi katika sehemu 92, na sehemu 6 kati ya hizo ni zenye urefu wa kilometa 3.2 hivi kila moja. Reli ya chini ya ardhi inayoitwa Karbude ilichimbwa wakati huo. Hiyo ina urefu wa kilometa 6.5, nayo ndiyo ndefu zaidi huko India.
Vizuizi vilikuwa vingi—mvua kubwa, maporomoko ya ardhi, miamba migumu, na udongo laini sana. Wahandisi walihitaji kushinda vizuizi hivyo vyote kwa kutumia ustadi na mbinu za tekinolojia. Kuingiza hewa mahali ambapo reli zinapita chini ya ardhi na kuweka vifaa vingine vya kuzuia hatari kulikuwa kazi ngumu sana. Pia, ardhi ilipasa kununuliwa kutoka kwa zaidi ya wamilikaji 42,000 wa ardhi.
Hata hivyo, baada ya ujenzi wa miaka saba tu, huo ukiwa muda mfupi sana kwa kazi kubwa hivyo, gari-moshi la kwanza lilianza safari kwenye Reli ya Konkan, Januari 26, 1998. Safari kuanzia Mumbai hadi Mangalore ilifupishwa kwa kilometa 1,127, na muda wa kusafiri ulifupishwa kwa saa 26. Reli ya Konkan huwawezesha watu kuona mandhari maridadi sana, huwawezesha watalii kuona maeneo mapya ya matembezi, nayo imeboresha uchumi wa mamilioni ya watu.
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MUMBAI
Mangalore
[Picha]
Daraja la Panval Nadi ndilo daraja refu zaidi huko Asia
[Hisani]
Dipankar Banerjee/STSimages.com
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
FAIRY QUEEN
Kichwa cha gari-moshi cha kale zaidi kinachoendeshwa kwa mvuke, ambacho kingali kinatumika, kinaitwa Fairy Queen. Kilitengenezwa na kampuni ya Kitson, Thompson na Hewitson, huko Leeds, Uingereza, mwaka wa 1855, nacho kilivuta magari-moshi yaliyopeleka barua kutoka kwenye kituo cha Howrah, karibu na Calcutta, hadi Raniganj huko Bengal. Kiliwekwa kwenye Jumba la Makumbusho la Reli la Taifa, New Delhi, mwaka wa 1909, na watu wanaopenda magari-moshi walifurahia kwenda kukitazama. Ili kusherehekea miaka 50 ya uhuru huko India, kichwa hicho cha gari-moshi kilianza kutumika tena. Tangu mwaka wa 1997, kichwa hicho cha gari-moshi Fairy Queen Express kimekuwa kikiwasafirisha watalii kutoka Delhi hadi Alwar huko Rajasthan. Hiyo ni safari ya kilometa 143.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Magari-Moshi ya ANASA NA YA KASI!
ANASA Zamani za kale kulikuwa na anasa nyingi huko India. Inawezekana kufurahia anasa hiyo ya kale kwenye safari za kipekee za magari-moshi, ijapokuwa safari hizo hugharimu pesa nyingi. Gari-moshi la mvuke, linaloitwa Palace on Wheels, lilianza kusafiri mwaka wa 1982. Mabehewa yake yalitengenezwa ili yafanane kabisa na yale yaliyotumiwa zamani na wakuu na magavana Wahindi. Gari-moshi hilo lenye mabehewa meupe lina vitu vya anasa kama vile kuta za ndani zilizofunikwa kwa mbao ya msaji kutoka Burma, taa zenye vito aina ya kioo, na vitambaa maridadi vya hariri. Kila kitu kinastarehesha. Kuna vyumba vya kulala vya starehe, vyumba vya kulia, ukumbi na maktaba, chakula cha hali ya juu, na watumishi wanaovalia mavazi maalumu wanaowahudumia abiria.
Mnamo mwaka wa 1995, kwa sababu nafasi kati ya vyuma vya reli ilipanuliwa, gari-moshi jipya ambalo pia linaitwa Palace lilitengenezwa, na mabehewa ya zamani hayakutumiwa tena. Gari-moshi jipya la anasa, ambalo linaitwa The Royal Orient, husafiri kwenye reli ya zamani yenye nafasi ya meta moja kati ya vyuma vya reli katika majimbo ya Gujarat na Rajasthan upande wa magharibi. Kwa kawaida magari-moshi hayo husafiri usiku, na abiria hutalii sehemu mbalimbali mchana. Wasafiri hupitia jangwa kuu la Thar lenye ngome za kale na hekalu mbalimbali. Watalii wanaweza kupanda ngamia jangwani na kupanda ndovu hadi ngome maarufu ya Amber Fort. Jiji la Jaipur lenye majengo mekundu-hafifu liko karibu ambako matukio mengi ya maana yalitokea zamani. Jiji hilo linajulikana pia kwa vito na vitu vilivyotengenezwa kwa mkono. Matembezi hayo yanatia ndani kutembelea hifadhi za ndege na simbamarara, na makao ya simba wa Asia wanaoishi mwituni. Usikose kutembelea jumba la kifalme la Udaipur lililoko karibu na ziwa, na kaburi la Taj Mahal. Mambo hayo na mengi zaidi yatafanya safari yako iwe yenye kupendeza.
MWENDO WA KASI Magari-moshi ya India hayawezi kusafiri kwa kasi kama yale ya Ufaransa na Japani. Lakini unaweza kusafiri kwa kasi sana na kwa starehe kwa magari-moshi 212 mbalimbali ambayo husafiri katikati ya majiji. Magari-moshi ya Rajdhani na Shatabdi husafiri kwa karibu mwendo wa kilometa 160 kwa saa. Mabehewa yake yana vifaa vya kupunguza joto na viti vinavyoweza kurudishwa nyuma au vitanda vizuri. Msafiri ambaye amelipa nauli ya kusafiri kwa magari-moshi hayo hupata chakula, malazi, maji safi ya kunywa, na matibabu bila malipo ya ziada.
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Jaipur
Udaipur
[Picha]
Hawa Mahal, Jaipur
Kaburi la Taj Mahal, Agra
Gari-moshi la “The Royal Orient”
Ndani ya gari-moshi la “Palace on Wheels”
[Hisani]
Hira Punjabi/STSimages.com
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
NEW DELHI
[Picha]
Baadhi ya reli kuu
Mvuke, Zawar
Mvuke, Reli ya Darjeeling ya Himalaya (DHR)
Umeme, Agra
Umeme, Mumbai
Mafuta, Hyderabad
Mafuta, Simla
[Hisani]
Ramani: © www.MapsofIndia.com
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MUMBAI
[Picha]
Kituo cha Churchgate, Mumbai
[Hisani]
Sandeep Ruparel/STSimages.com
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Milima ya Nilgiri
[Picha]
Kichwa cha gari-moshi kinachoendeshwa kwa mvuke kinalisukuma gari-moshi dogo la Nilgiri juu ya mlima
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 18]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Darjeeling
[Picha]
Reli inajivuka huko Batasia
Jinsi Mlima wa Kanchenjunga unavyoonekana kutoka mahali reli inapojipinda huko Batasia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
Magari-moshi kwenye ukurasa wa 2, 13, 15 katikati, 16-18: Reproduced by permission of Richard Wallace