Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Sherehe ya Vía Crucis Huko Mexico

Sherehe ya Vía Crucis Huko Mexico

Sherehe ya Vía Crucis Huko Mexico

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

ILI kuadhimisha kifo cha Yesu, sherehe 300 hivi za kidini hufanywa nchini Mexico kila mwaka. Sherehe moja kubwa inaitwa Vía Crucis, nayo inatia ndani misafara na michezo ya kuigiza kuhusu siku za mwishomwisho za maisha ya Yesu. Vía Crucis ni jina la Kilatini linalomaanisha “Njia ya Msalaba.” Mkurugenzi wa Nyumba ya Utamaduni katika wilaya ya Iztapalapa la Mexico City anaeleza jinsi sherehe hiyo ilivyoanza: “Watu wengi walikufa ugonjwa wa kipindupindu huku Iztapalapa mwaka wa 1833. Ili kupunguza huzuni iliyosababishwa na msiba huo, watu wa mahali hapo walianzisha mchezo wa kuigiza kuhusu mateso yaliyompata Yesu usiku wake wa mwisho.

Simulizi linalofuata linaeleza jinsi sherehe ya kawaida ya Vía Crucis inavyofanywa: Umati wa watu hukusanyika ili waone mchezo wa kuigiza unaoonyesha viongozi wa Wayahudi, maaskari, mitume wa Yesu, na wanawake waliomfuata, kutia ndani Maria. Mwanamume kijana humwigiza Yesu. Yeye hukariri maneno ya Biblia mchezo unapoendelea. Waigizaji hutumia nywele bandia, ndevu bandia, na masharubu bandia, nao huvalia kanzu nzito. “Wanazareti” wamfuata “Yesu” pia, baadhi yao wakitembea miguu mitupu na wengine wakiwa wamevalia makubadhi ya ngozi. Wote wana mataji ya miiba vichwani ili kuigiza mateso yaliyompata Yesu. Nyakati nyingine idadi yao inaweza kufikia 2,500. Siku hiyo wao hubeba misalaba hadi Cerro de la Estrella (Kilima cha Nyota), mahali ambapo Yesu “atasulubishwa.”

Wachuuzi huuza vitu kama vile kofia, vinywaji, picha za kidini zinazokusudiwa kuchorwa kwenye shavu au mikono, maputo, peremende kwa ajili ya watoto, na vitu vingine vingi. Hata michezo na burudani mbalimbali hupangwa katika sherehe hiyo.

Jijini Querétaro, watu wanaotubu dhambi hujaribu kutembea huku miguu yao ikiwa imefungwa minyororo. Huko Taxco, wanaume hubeba vifurushi vya miiba vyenye uzito wa kilogramu 40 hadi 50 mgongoni kwa muda wa saa tano hivi. Wengine wanafuata msafara huku wakijipiga wenyewe. Mara nyingi washiriki kadhaa hulazwa hospitalini.

Ibada ya aina hiyo hutukumbusha maneno ya Paulo ya kushutumu “ibada ya kujitwika na unyenyekevu wa dhihaka, kutendea mwili kwa ukali.” (Wakolosai 2:23) Wakristo wa kweli huadhimisha kifo cha Kristo, lakini wao huepuka desturi zisizo za kweli zinazopinga kanuni za Biblia.