Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wasafiri Walioongozwa na Nyota Baharini

Wasafiri Walioongozwa na Nyota Baharini

Wasafiri Walioongozwa na Nyota Baharini

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HAWAII

KARNE nyingi kabla Christopher Columbus hajavuka Bahari ya Atlantiki, wasafiri Wapolinesia walikuwa wakisafiri maelfu ya kilometa katika Bahari ya Pasifiki kwa mitumbwi. Walifika kwenye visiwa vingi vya Polinesia. Wapolinesia hao wa kale walijuaje kwamba kuna visiwa vingi katika eneo hilo kubwa? Je, walifika huko pasipo kutarajia?

Ikiwa Wapolinesia walijua vizuri walikokuwa wakienda, walisafirije baharini bila ramani, dira, au vifaa vingine muhimu ambavyo vilitumiwa na wavumbuzi waliotoka nchi za Magharibi?

Jibu la swali hilo linaonyesha kwamba Wapolinesia walitumia mbinu zenye ustadi sana waliposafiri baharini na linatusaidia kuthamini zaidi utaratibu na muundo wa ulimwengu wetu.

Madai Mawili ya Kale

Baadhi ya wanasayansi na wasomi wanakataa wazo la kwamba Wapolinesia walikuwa wamepanga kusafiri kwa ustadi kutoka kisiwa kimoja hadi kingine. Mvumbuzi Thor Heyerdahl, ambaye ni mwenyeji wa Norway, alidai kwamba Wapolinesia walitoka Amerika Kusini na kwamba mitumbwi yao ilipeperushwa tu na upepo na mawimbi ya bahari hadi visiwa vya Pasifiki.

Ili kuthibitisha dai hilo, Heyerdahl na mabaharia watano Waskandinavia walisafiri kutoka pwani ya magharibi ya Peru kwa mashua iliyotengenezwa kwa magogo ya mti wa balsa. Walianza kusafiri katika Bahari ya Pasifiki kisha mashua yao ikapeperushwa na mawimbi yanayovuma kutoka upande wa magharibi. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku 101 umbali wa kilometa 7,000, Heyerdahl na mabaharia wenzake walifika kwenye kisiwa cha matumbawe cha Raroia ambacho kiko miongoni mwa visiwa vya Tuamotu. Kwa hiyo, Heyerdahl alionyesha kwa njia ya pekee kwamba Wapolinesia wangeweza kupeperushwa na mawimbi ya bahari kutoka Amerika Kusini. Lakini wasomi wengine hawakusadikishwa na uthibitisho wa Heyerdahl.

Mwanahistoria anayeitwa Andrew Sharp, kutoka New Zealand, alikuwa mmojawapo wa wasomi ambao walitilia shaka dai la Heyerdahl. Katika kitabu chake Ancient Voyagers in Polynesia, kilichoandikwa mwaka wa 1963, alitaja maoni ya kawaida ya wanahistoria na wataalamu ya kwamba Wapolinesia walitoka magharibi. Alitoa uthibitisho mwingi wa kiakiolojia na wa utafiti wa lugha. Hata hivyo, alipuuza maoni yoyote ambayo yaliwasifu Wapolinesia kuwa wasafiri stadi wa baharini.

Sharp alikubali kwamba wasafiri hao wangeweza kujua upande walikoelekea katika safari fupi, lakini alidai kwamba Wapolinesia hawangeweza kamwe kujua kwa hakika walikoelekea katika safari inayozidi kilometa 500. Aliamini kwamba waligundua visiwa vyote vya mbali bila kutarajia.

Safari za Uchunguzi

Dakt. David Lewis anayetoka New Zealand aliamua kuthibitisha usahihi wa mbinu za kale za kusafiri baharini, kwa sababu aliamini kwamba Heyerdahl na Sharp walipuuza ustadi wa Wapolinesia wa kusafiri baharini. Mnamo mwaka wa 1965, alisafiri umbali wa kilometa zaidi ya 3,000, kutoka Tahiti hadi New Zealand, kwa mashua ya kisasa akiongozwa na nyota, jua, na mawimbi mazito ya bahari bila kutumia dira. Safari ya Lewis iliwafanya wengi wapendezwe kujua mbinu za kale za kusafiri baharini na njia zilizofuatwa na wahamaji. Ben Finney ni mmojawapo wa watu waliopendezwa na safari ya Lewis.

Kwa miaka mingi, Finney ambaye ni profesa wa elimu ya binadamu katika Chuo Kikuu cha Hawaii alikuwa amechunguza jinsi ambavyo Wapolinesia wa kale walivyotengeneza mashua. Finney na baadhi ya wafanyakazi wenzake katika chuo cha Shirika la Polinesia la Usafiri wa Baharini walitengeneza mashua yenye urefu wa meta 20 yenye sehemu mbili. Waliiita mashua hiyo Hokule‛a, neno la Kihawaii linalomaanisha “Nyota ya Shangwe.” Ingawa mashua ya Hokule‛a ilitengenezwa kwa vifaa vya kisasa badala ya vifaa vya kale kama vile mbao za mti wa koa, ilikuwa na kiunzi na umbo kama la mashua za kale na hata ilisafiri kama mashua hizo.

Mashua ya Hokule‛a ilianza safari mnamo Mei 1, 1976, kutoka kwenye kisiwa cha Maui huko Hawaii kuelekea Tahiti. Kwa kuwa mbinu ya Wapolinesia ya kupata njia baharini kwa kutumia nyota haijulikani, ilibidi mtu mwenye ustadi huo atafutwe kwingineko mbali na Visiwa vya Hawaii. Kwa hiyo, Mau Piailug, baharia stadi kutoka Mikronesia, alichaguliwa kuongoza mashua ya Hokule‛a katika safari hiyo ya kwanza. Mashua hiyo ilifika Tahiti baada ya kusafiri umbali wa maelfu ya kilometa katika muda wa siku 31.

Safari hiyo yenye kufana iliwachochea wengi katika Polinesia kupendezwa na utamaduni, ustadi wa kusafiri baharini na utengenezaji wa mashua. Miaka iliyofuata, watu walifunga safari kama hizo hadi visiwa vinginevyo vya Polinesia, kama vile Hawaii, New Zealand (ambayo huitwa pia Aotearoa), Rarotonga (katika Visiwa vya Cook), na Kisiwa cha Easter (ambacho huitwa pia Rapa Nui). Idadi kubwa ya safari hizo ziliongozwa na Nainoa Thompson, baharia aliyezaliwa Hawaii ambaye alifunzwa na Piailug.

Mbinu za Kale za Kusafiri Baharini

Wapolinesia walisafirije umbali wa maelfu ya kilometa bila vifaa vinavyoongoza meli? Dennis Kawaharada wa Shirika la Polinesia la Usafiri wa Baharini asema kwamba waliongozwa hasa na jua. Walisafiri wakati wa mchana kwa kuzingatia upande hususa ambao jua huchomoza na kutua. Wakati wa usiku, baharia alielekeza mashua kulingana na upande ambao nyota zilichomoza na kutua.

Hata kama hakuna nyota inayochomoza au kutua upande ambao mashua inaelekea, nyota nyingine zilizo angani zinaweza kutumiwa. Mbali na nyota, mabaharia hutumia mwezi na sayari tano zinazoonekana angani ili kusafiri upande unaofaa.

Wakati wa adhuhuri na katika usiku wenye mawingu mengi wakati ambapo nyota hazionekani, baharia anaweza kuendesha mashua akitegemea upepo na mawimbi mazito ya bahari (akizingatia upande ambao jua huchomoza na kutua). Kawaharada anasema kwamba, “mawimbi mazito ni mawimbi ambayo yamefika mbali kuliko pepo au dhoruba zinazoyasababisha, au mawimbi yanayozidi kusonga baada ya upepo kupungua.”

Kwa hiyo, mawimbi mazito yanaweza kutegemeka kuliko mawimbi mepesi ambayo husababishwa na upepo mwepesi unaobadilika-badilika. Kwa kuwa mawimbi mazito huelekea upande mmoja tu, baharia anaweza kuendesha mashua yake kuelekea upande unaofaa. Baharia anaweza kujua iwapo mashua inaelekea upande unaofaa ikitegemea mwelekeo wake mawimbini.

Kuna uthibitisho unaodokeza kwamba Wapolinesia wa kale waliweza kuelekeza mashua zao upande ufaao na kusafiri maelfu ya kilometa wakiongozwa na nyota au sayari, pepo na mawimbi mazito ya bahari. Hata hivyo, ijapokuwa mabaharia hao walikuwa na ustadi, mbinu zao zote zingeambulia patupu iwapo vitu vya asili havingefuata utaratibu wenye kutegemeka, kama vile kuchomoza na kutua kwa nyota.

Zaidi ya miaka 2,700 iliyopita, nabii Isaya alimsifu Muumba Mtukufu, Yehova Mungu, kwa sababu ya utaratibu ulioko angani. Aliandika hivi: “Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.”—Isaya 40:26; Zaburi 19:1.

Roho takatifu ilimwongoza mtunga-zaburi kuandika kwamba Mungu “huihesabu idadi ya nyota, huzipa zote majina.” (Zaburi 147:4) Wapolinesia walitambua kwamba nyota zimepangwa kwa utaratibu angani na hivyo walizitumia walipofanya safari zao za uvumbuzi katika Bahari ya Pasifiki. Je, hilo halithibitishi kwamba ulimwengu wetu umeumbwa na Muumba mwenye akili nyingi na mwenye utaratibu?

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Fiji

VISIWA VYA POLINESIA

Hawaii

Samoa

Tonga

New Zealand

Visiwa vya Cook

Tahiti

Visiwa vya Marquesas

Visiwa vya Tuamotu

Visiwa vya Tubuaï

Kisiwa cha Easter

[Picha]

Mashua inayoitwa “Hawai‘iloa” yenye sehemu mbili ilitengenezwa mwaka wa 1993 kwa vifaa vingi vya kale kuliko mashua ya “Hokule‘a”

[Hisani]

Hawai‘iloa kwenye ukurasa wa 21 na 23: © Monte Costa