Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Ua Haba la Okidi Lalindwa Lisiangamie
Ua la okidi aina ya lady’s-slipper (Cypripedium calceolus) linaloota lenyewe nchini Uingereza limekuwa likilindwa saa 24 kwa muda wa miaka 50 ili lisiangamizwe. Ua hilo maridadi sana lenye rangi nyekundu iliyokoza na manjano lilipendwa mno na watu walioishi wakati wa utawala wa Malkia Viktoria na katika miaka iliyofuata hivi kwamba kufikia miaka ya 1950, lilikuwa “limechumwa kwa wingi karibu litoweke,” na ni mmea mmoja tu uliosalia. Wataalamu wa mimea walijaribu kuzalisha mmea huo unaotoka jimbo la North Yorkshire, lakini uchavushaji wa asili haukufaulu kwa sababu ua hilo huchanua maua mara chache sana. Hata hivyo, katika miaka ya mapema ya 1990, wanasayansi wa Bustani ya Kew, huko London, walivumbua mbinu ya kukuza mimea mipya kutokana na mbegu za maua yaliyochavushwa na wakulima. Kisha mimea hiyo ilihamishwa hadi kwenye mazingira yake ya asili yenye mawe ya chokaa. Hivyo, kwa sasa okidi za lady’s-slipper zipatazo 200 hadi 300 zinakua kaskazini mwa Uingereza. Gazeti la The Independent la London linaripoti kwamba watu wanaweza kutembelea bustani moja tu lakini bustani nyinginezo zimefichwa ili kulinda maua hayo, huku “wanasayansi wakijaribu kuyaimarisha ili yaweze kukinza wadudu na kuvu.”
Wanadamu Huwaletea Wanyama Mizio
Gazeti la Ujerumani Leipziger Volkszeitung linasema kwamba “wanadamu huwaletea wanyama wengi mizio.” Shirika la Ujerumani la Mizio na Pumu (DAAB) lilitangaza hivi majuzi kwamba “mnyama-kipenzi 1 kati ya 20 hupatwa na dalili za mizio kama vile upele au kupiga chafya mara nyingi anapokuwa na wanadamu.” Inasemekana kwamba tatizo hilo husababishwa mara nyingi na magamba ya ngozi ya mwanadamu na kinyesi cha utitiri wanaokula magamba hayo. Mtu akimwona mnyama wake akijikunakuna, akijiramba au kujinyonyoa na hana viroboto mwilini, anapaswa kutambua kwamba ana mzio wa wanadamu. Jambo hilo laweza kubainika hata zaidi mnyama huyo anapokosa kuonyesha dalili hizo anapokuwa mahali pengine au anapokuwa peke yake. Vyakula na chavuo vilitajwa pia kuwa visababishi vya mizio katika wanyama. Kwa mfano, shirika la DAAB lilisema kwamba katika miaka ya karibuni, farasi wengi wamekuwa wakiugua homa ya mafua iletwayo na vumbi.
Ni Nini Humfanya Mtu Awe “Mwanamume Halisi”?
Gazeti la Independent la London linaripoti kwamba “wavulana . . . wangali wanaamini kwamba ‘mwanamume halisi’ ni yule aliye hodari michezoni, anayevaa mavazi maarufu na asiye na marafiki wa karibu, lakini hawaoni kufanya kazi kwa bidii kuwa sifa ya ‘kiume.’” “Wavulana huwaheshimu wanafunzi wenzao wanaotumia mabavu na kuwatukana wengine. Vijana wasiofanya hivyo wanaweza kuteswa au kuitwa mabasha.” Gazeti hilo lasema kwamba katika uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Birkbeck, London, wavulana wenye umri wa miaka 11 hadi 14 wa shule 12 huko London, “walikubali kwamba ‘kuwa wakatili’ kuliwafanya wawe wapweke na waogope kujieleza.” Profesa Stephen Frosh, aliyesimamia uchunguzi huo alisema hivi: “Wavulana wanahitaji kusadikishiwa kwamba kuwa mwanamume hakumaanishi kutoonyesha hisia.”
Chama cha Msalaba Mwekundu Chashutumiwa
Chama cha Msalaba Mwekundu cha Marekani kilianza kukusanya michango na damu baada tu ya mashambulizi ya magaidi ya Septemba 11. Kilikusanya dola milioni 850 taslimu za Marekani na lita 180,000 za damu. Chama hicho kilikawia kuwapa wenye uhitaji misaada hiyo ijapokuwa ilikusanywa haraka. Gazeti la The Washington Times lasema hivi: ‘Chama cha Msalaba Mwekundu cha Marekani kilikawia sana kuzipa familia za watu walioathiriwa na msiba pesa za msaada. Pesa hizo za misaada zilikuwa zikitumiwa kwa miradi mingine isiyohusiana na shambulizi la Septemba 11,’ na kiasi kikubwa cha pesa hizo kilitengwa ili kushughulikia “mahitaji ya muda mrefu, kama vile mradi [mmoja] wa kugandisha damu, kutoa ushauri, na kwa ajili ya mashambulizi wakati ujao.” Makala hiyo yasema kwamba damu iliyokusanywa “haiwezi kutumiwa na ni lazima ichomwe” kwa sababu haihitajiwi na haiwezi kutumiwa baada ya siku 42 kupita. Vyombo vya habari viliripoti kwamba baada ya kushutumiwa vikali, wakurugenzi wa Chama cha Msalaba Mwekundu walilazimika kumfuta kazi msimamizi wa chama hicho kisha wakatangaza mwishoni mwa mwezi wa Januari 2002 kwamba wale walioathiriwa na shambulizi hilo watapewa asilimia 90 ya pesa zilizokusanywa kufikia Septemba 11, 2002.
Misiba Mibaya Zaidi ya Asili
Ripoti ya shirika la habari la Reuters yasema kwamba “angalau watu 25,000 walikufa kutokana na misiba ya asili ulimwenguni pote mwaka wa 2001. Idadi hiyo ni maradufu ya idadi ya watu waliokufa mwaka uliotangulia.” Kampuni kubwa zaidi ya bima ulimwenguni, Munich Re, inasema kwamba misiba hiyo ilileta hasara ya dola bilioni 36 za Marekani—hasara kubwa kuliko ile iliyosababishwa na mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani. Karibu asilimia 70 ya misiba mikubwa 700 iliyotukia ilihusiana na dhoruba na mafuriko. Inadaiwa kwamba hali hiyo mbaya sana ya hewa inasababishwa na mabadiliko yanayoendelea ya tabia ya nchi ulimwenguni pote. Kampuni hiyo ilisema kwamba “mioto ya msitu iliyotukia nchini Australia, mafuriko yaliyotukia nchini Brazili na Uturuki, maanguko makubwa mno ya theluji yaliyotukia katikati na kusini mwa Ulaya na kimbunga kilichotukia nchini Singapore, ambacho watabiri wa hali ya hewa walidhani hakiwezi kuikumba nchi hiyo, yanaonyesha uhusiano uliopo kati ya mabadiliko ya tabia ya nchi na ongezeko la misiba ya asili.” Ilisema kwamba mwaka wa 2001 ulikuwa mwaka wa pili wenye joto kali zaidi kwa muda wa miaka 160 iliyopita. Matetemeko ya ardhi yalisababisha vifo vingi zaidi—zaidi ya watu 14,000 walikufa mwezi wa Januari peke yake katika tetemeko la ardhi huko India. Kwa ujumla, matetemeko makubwa ya ardhi 80 yalitukia mwaka huo.
Mikanda ya Viti vya Nyuma Huokoa Uhai
Gazeti la The Guardian la London laripoti kwamba “abiria wasiojifunga mikanda ya usalama katika viti vya nyuma huhatarisha kwa zaidi ya mara tano uhai wa abiria waliojifunga mikanda wanaoketi kwenye viti vya mbele.” Watafiti wa Chuo Kikuu cha Tokyo waliochunguza rekodi za misiba ya magari zaidi ya 100,000 iliyotukia katika muda wa miaka mitano huko Japan, waligundua kwamba asilimia 80 hivi ya abiria walioketi mbele wakiwa wamejifunga mikanda hawangekufa kama abiria walioketi nyuma wangejifunga mikanda ya usalama. Magari yanapogongana, abiria wasiojifunga mikanda hurushwa mbele kwa nguvu sana hivi kwamba wanaweza kuwajeruhi vibaya au hata kuwaua abiria wanaoketi mbele. Ingawa kujifunga mikanda ya viti vya nyuma ni takwa la kisheria nchini Uingereza tangu mwaka wa 1991, uchunguzi unaonyesha kwamba asilimia 40 hivi ya watu wazima nchini humo bado hawajifungi mikanda hiyo.
Hatari ya Uchafuzi wa Hewa Huko Asia
Gazeti la kimazingira Down to Earth linasema kwamba “huko India, zaidi ya watu 40,000 hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa.” Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia na Taasisi ya Mazingira ya Stockholm ulionyesha kwamba uchafuzi wa hewa huko Asia ni mkubwa sana kuliko huko Ulaya na Amerika kwa ujumla, na umesababisha maelfu ya vifo huko Seoul, Beijing, Bangkok, Jakarta, na Manila. Kwa mfano, zaidi ya watu 4,000 hufa kila mwaka katika jiji la Manila kutokana na magonjwa yanayohusiana na kupumua, na watu 90,000 wanaugua ugonjwa sugu wa mkamba. Kiwango cha vifo ni kikubwa zaidi huko Beijing na Jakarta. Gazeti hilo linasema kwamba “kutumia petroli isiyofaa, uzalishaji mbaya wa nguvu za umeme, uendeshaji wa magari mabovu na msongamano wa magari,” husababisha tatizo hilo.
Kupata Faida Kutokana na Pesa Mpya za Euro
Gazeti la Corriere della Sera linasema kwamba tangu pesa za euro zianze kutumiwa, Kanisa Katoliki la Italia “limepata njia ya kujipatia faida kubwa pesa za lira zilipofutiliwa mbali ‘kwa kupandisha malipo ya huduma zake,’ kwa sababu ya upungufu wa michango.” Padri wa Rome alituma barua kwa parokia zote ili “zirekebishe ‘orodha ya malipo.’ Malipo kwa ajili ya misa yaliyokuwa lira 15,000 tu yamepanda hadi euro 10 (lira 19,363). Malipo ya juu zaidi kwa ajili ya arusi yaliyokuwa lira 450,000, yamepanda hadi euro 270 (lira 523,000).” Hata hivyo, barua hiyo yasema wazi kwamba “malipo hayo yanahusu hasa ndoa za ‘watu wasio waumini,’ lakini waumini wataamua wenyewe mchango wanaotaka kutoa, kama ilivyo pia kwa habari ya ubatizo na mazishi.” Hata hivyo, makasisi wa parokia huko Rome bado hawapati michango yoyote masandukuni. Gazeti hilo lasema kwamba labda ni kwa sababu “idadi ya waumini imepungua na wanapenda pesa kwa kadiri fulani.”