Mazoea ya Kutupatupa Vitu
Mazoea ya Kutupatupa Vitu
WATU wanaoishi katika nchi zilizoendelea hutupa takataka nyingi sana. Kwa mfano, wazia kiasi cha takataka ambacho hutupwa huko Marekani kila mwaka. Inasemekana kwamba uzito wa takataka hizo ni ‘sawa na uzito wa maji yanayoweza kujaza madimbwi 68,000 ya kuogelea yenye urefu wa meta 50.’ Yapata miaka kumi iliyopita ilikadiriwa kwamba kila mwaka, wakazi wa New York City walitupa takataka nyingi hivi kwamba zingeweza kufunika bustani ya jiji hilo inayoitwa Central Park kwa tabaka ya meta nne za takataka! *
Si ajabu kwamba nchi ya Marekani imetajwa kuwa “onyo kwa nchi nyingine duniani” kwa habari ya “kununua na kutupa vitu ovyoovyo.” Lakini hali hiyo inakumba nchi nyingine pia. Imekadiriwa kwamba takataka ambazo hutupwa kila mwaka huko Ujerumani zingeweza kujaza gari-moshi la kubeba mizigo lenye urefu wa kilometa 1,800. Huo ni umbali wa kutoka Berlin, mji mkuu wa Ujerumani, hadi pwani ya Afrika. Na hapo nyuma ilikadiriwa kwamba kila mwaka familia ya kawaida yenye watu wanne nchini Uingereza hutupa kiasi cha karatasi ambacho kimetengenezwa kutokana na miti sita.
Hata nchi zinazoendelea zina tatizo la takataka. Gazeti moja maarufu linasema hivi: “Jambo baya hata zaidi ni kwamba hivi karibuni wengi wa wale watu bilioni 6 duniani wameanza kutupa vitu ovyoovyo wakifuata mfano wa Marekani na nchi nyingine zilizoendelea.” Naam, upende usipende, popote tulipo watu hupenda kutupatupa vitu siku hizi.
Bila shaka watu wamekuwa na vitu vya kutupa tangu zamani. Lakini vyakula vya mikebe na vyakula vilivyofungwa kwa karatasi za aina mbalimbali vyapatikana kwa wingi siku hizi kuliko miaka michache iliyopita. Kwa hiyo, mikebe na karatasi za vyakula hivyo ziko kila mahali. Vilevile, kiasi cha magazeti, karatasi za matangazo ya biashara, na vichapo vingine kimeongezeka kwa haraka.
Viwanda vingi na vitu vingi vilivyobuniwa na wanasayansi vimesababisha pia aina nyingine za takataka. Gazeti Die Welt la Ujerumani linasema kwamba “magari milioni tisa hivi hutupwa kila mwaka katika nchi za Muungano wa Ulaya.” Kuondosha magari hayo si jambo rahisi. Lakini kuondosha takataka za mitambo ya nyuklia na viwanda vya kemikali ni tatizo kubwa hata zaidi. Yasemekana kwamba katika mwaka wa 1991 huko Marekani kulikuwa na “takataka nyingi sana zenye mnururisho na hapakuwa na mahali pa kuziweka” Iliripotiwa kwamba mapipa milioni moja yenye kemikali zenye sumu ya kufisha yalikuwa yamewekwa katika ghala za muda. Na sikuzote ilihofiwa kwamba mapipa hayo “yangepotea, yangeibwa, au kusababisha uharibifu wa
mazingira kwa sababu ya kutoshughulikiwa ifaavyo.” Viwanda 20,000 hivi huko Marekani vilikuwa na zaidi ya tani milioni 40 za takataka zenye sumu katika mwaka wa 1999.Jambo jingine linalochangia tatizo hilo ni ongezeko kubwa la idadi ya watu katika karne iliyopita. Watu wanapoongezeka, takataka huongezeka pia. Na watu wengi wana mwelekeo wa kununua vitu ili kuzidisha mali. Hivi majuzi, Taasisi ya Worldwatch ilikata kauli hii: “Tumetumia bidhaa nyingi zaidi na kuhudumiwa kwa njia nyingi zaidi tangu mwaka wa 1950 kuliko wakati mwingine wowote.”
Bila shaka watu wengi wanaoishi katika nchi zilizoendelea hawataki kukosa ‘bidhaa na huduma’ hizo zote. Kwa mfano, fikiria jinsi ilivyo rahisi kwenda dukani na kununua vyakula ambavyo vimekwisha fungwa kwa njia mbalimbali na kuvipeleka nyumbani katika mifuko ya karatasi au plastiki inayopatikana dukani. Kama watu wangenyimwa huduma hiyo ghafula, labda wangegundua haraka kwamba wameizoea sana. Mbinu mbalimbali za kufunga vyakula huchangia afya nzuri, angalau kwa kadiri ambavyo zinazuia vyakula visichafuliwe.
Hata hivyo, licha ya faida hizo, je, vitu hutupwa kwa wingi hivi kwamba tunapaswa kuwa na wasiwasi? Bila shaka, kwa kuwa masuluhisho mbalimbali ambayo yamependekezwa ili kupunguza takataka hayajawa na matokeo mazuri. Jambo baya hata zaidi ni kwamba mielekeo ya kutupatupa vitu inaweza kuwa na matokeo mabaya zaidi.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Bustani hiyo ni yenye eneo la ekari 843.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Kuondosha takataka hatari za viwanda bila kusababisha madhara ni tatizo kubwa sana