Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Paka Rangi Mpya

Paka Rangi Mpya

Paka Rangi Mpya

INAVUTIA sana kuona mahali palipopakwa rangi. Kupaka rangi mpya kwenye chumba kisichopendeza kunaweza kukifanya kiwe maridadi sana. Je, unataka kufanya nyumba yako iwe maridadi? Iwapo hujawahi kupaka rangi, huenda utaona hiyo ikiwa kazi rahisi kuliko ulivyofikiri!

Hebu tumsaidie Fernando, mke wake, Dilma, na binti yao Vanessa, mwenye umri wa miaka minane, wanapopaka sehemu fulani ya nyumba yao rangi mpya. Hivyo, sisi pia tutajua kupaka rangi. Hata hivyo, kabla ya kuvaa mavazi ya kazi, kwanza tutajifunza jinsi ya kuchagua rangi.

Kuchagua Rangi

Ni muhimu kuchagua rangi kwa uangalifu. Zaidi ya kufanya nyumba yako ionekane maridadi, rangi pia inaweza kuathiri hali yako ya moyoni. Rangi nyangavu husisimua, lakini rangi ambayo si nyangavu huelekea kumtuliza mtu. Huenda rangi fulani isiangaze inapopakwa ndani ya kuta za jengo, lakini ikawa nyangavu zaidi inapopakwa nje ya jengo hilo. Fernando na Dilma wamechagua kupaka nyumba yao rangi ya manjano ya kidhahabu na “rangi nyeupe ya kijivu.” Baadaye tutaona mahali ambapo watapaka rangi hizo.

Tazama mpangilio wa rangi unaoonyeshwa hapa juu. Rangi zinazoangaliana zinaitwa rangi zenye kukamilishana, nazo huonekana ziking’aa zaidi zikiwa pamoja. Ikiwa kusudi lako si kusisimua, chagua aina mbalimbali za rangi moja.

Kabla ya kuanza kupaka rangi, Fernando na Vanessa wana maswali kadhaa. Fernando angependa kujua rangi ambazo watahitaji, na Vanessa anataka kujua jinsi rangi inavyotengenezwa. Kwa hiyo, itafaa tutembelee kiwanda cha kutengeneza rangi ili tujifunze mambo fulani.

Kutengeneza Rangi

Gerard, mwenye kiwanda hicho, amekubali kututembeza. Kitu cha kwanza kuona tunapoingia kiwandani ni mashine kubwa sana ikichanganya umajimaji wa unga wenye kunata katika bakuli kubwa linalochukua lita 800. Kwa kuwa kuna kelele, Gerard anapaaza sauti hivi: “Kutengeneza rangi ni kama kuoka keki—lazima viungo vyote vipimwe na kuchanganywa vizuri.”

“Ni viungo gani vinavyohitajiwa ili kutengeneza rangi ya kisasa?” tunauliza.

“Vitu vikuu vinne vinahitajika,” Gerard anajibu. “Rangi za asili, kiunganishi, umajimaji fulani, na bidhaa nyingine maalumu inayoongezwa ili kuboresha mchanganyiko huo. Kwenye mchanganyiko unaoona, dayoksaidi ya titani ndiyo kiungo kikuu. Rangi hii ya asili huchimbwa ardhini na hutumiwa badala ya risasi kutengeneza rangi za kisasa.” Mchanganyiko huo unafanana na unga unaotumiwa kuoka.

Gerard anaendelea: “Mchanganyiko huo unakorogwa-korogwa hadi unapokuwa laini na wenye kunata, na kuchanganywa na kiunganishi kidogo. Kiunganishi kinachotumiwa sasa ni utomvu wa akriliki. Mtengenezaji wa rangi anapoona mchanganyiko umekuwa laini, ataongeza utomvu uliobaki, kisha umajimaji fulani kama vile maji au umajimaji wenye madini na hatimaye bidhaa ya kuboresha.”

Tunataka kujua ni rangi gani tunayopaswa kutumia kupaka nyumba. Mwelekezi wetu anaeleza: “Kuna aina mbili za rangi ya nyumba. Rangi za mafuta hutumia kiunganishi cha mafuta ya kitani au soya, na rangi za maji hutumia utomvu wa plastiki au wa akriliki. Rangi za mafuta huwa ngumu sana zinapokauka, kwa hiyo zinafaa sana mahali panaposhikwa-shikwa mara nyingi, kama vile kwenye milango na kwenye ncha za mbao. Hata hivyo, rangi za mafuta huchujuka na kutoka baada ya muda. Kwa upande mwingine, rangi za maji, zilizotengenezwa kwa utomvu wa plastiki na wa akriliki wa hali ya juu, huhifadhi rangi yake na hazitoi harufu mbaya. Rangi zilizotengenezwa kwa akriliki pia huhimili vyema zaidi majira ya joto kali ya Australia au majira ya baridi kali ya Kanada.”

Tunatumaini tutakumbuka mambo tuliyofundishwa na Gerard. Lakini bado ana mambo machache ya kutuambia: “Aina zote mbili za rangi hung’aa kwa njia nne kuu. Aina ya kwanza inayoitwa gloss inafaa kutumiwa katika vifaa ambavyo vinatumiwa sana. Aina ya pili inayoitwa satin inafaa bafu na mahali pa kupitia. Aina ya tatu inayoitwa low sheen na ya nne inayoitwa flat inafaa chumba cha kupumzikia. Aina hiyo ya nne inafaa kutumiwa katika dari.” Tunamshukuru sana Gerard kwa kutufahamisha mengi katika matembezi yetu na tunarudi nyumbani ili kufanya sehemu ngumu ya kazi yetu—kutayarisha mahali ambapo rangi itapakwa.

Matayarisho Mengi Yanahitajika

Ili rangi ipendeze na kudumu, unahitaji kufanya matayarisho mengi. Kwa hiyo, jitayarishe kufanya kazi ngumu. Huenda tutajifunza mambo mengine muhimu kadiri tunavyoendelea na kazi. Fernando anataka kupaka rangi chumba cha kulia na ua wa mbele. Hebu tuanze chumbani.

Baada ya kuondoa fanicha, tunatandika mashuka yaliyozeeka sakafuni. Kwanza, tunahitaji kutoa rangi ya zamani iliyochakaa kutoka kwa fremu za madirisha, ncha za mbao, na dari. Tutamsaidia Fernando kufanya kazi hiyo. Yeye anaweka ngazi yake mahali palipo tambarare sakafuni. Kuongezea hilo, atakuwa mwangalifu kutosimama juu ya kikanyagio cha juu zaidi cha ngazi, ambapo anaweza kuanguka. Kuta zilizopigwa plasta ziko katika hali nzuri, lakini zinahitaji kuoshwa kwa maji na sabuni kabla ya kupakwa rangi.

Halafu, tutatumia kifaa maalumu kutoa uchafu katika mianya, kisha tutaiziba. Tutatumia kizibo cha akriliki kuziba mianya iliyo kwenye dirisha na ubao unaotenganisha sakafu na ukuta kwa sababu kizibo hiki kinaweza kuendelea kuziba hata mbao na plasta zinaposongezwa. Baadaye Vanessa anapoosha vifaa vya kupigia plasta, sisi tutapiga msasa sehemu za mbao na ukuta, tukitumia msasa wa kadiri. Hiyo italainisha sehemu itakayopakwa rangi na kufanya ukuta ushike rangi vizuri.

Huenda ukauliza, Kwa nini tuvae vichuja-hewa puani? Ili kuzuia rangi na vumbi ya plasta isiingie na kusababisha koo zetu kuwasha. Miwani yetu itazuia vipande vinavyoanguka kutoka juu visiingie katika macho yetu wakati tunapofanya kazi. Tunapaswa kuwa waangalifu sana tunapotumia rangi iliyotengenezwa kwa risasi. (Ona sanduku lenye kichwa, “Hatari ya Risasi” katika ukurasa huu.)

Hatimaye, tunafagia chumba chote. Mbao ambazo hazikupakwa rangi hapo awali zinahitaji kupakwa rangi kwanza na mashimo katika ukuta uliopigwa plasta yanahitaji kuzibwa kabla ya kupakwa rangi. Jambo hilo litaruhusu rangi inayopakwa iwe na mng’ao mzuri badala ya kuingia katika mashimo yanayotokana na msasa au rangi zilizopakwa awali. Tukiisha fanya mambo hayo, chumba chetu kitakuwa tayari kupakwa.

Ua umetengenezwa kwa mbao ambazo hazijapakwa rangi. Baada ya kuosha ua, tutahitaji kufunika misumari kwa rangi ya chuma. Hiyo itazuia kutu isipenye ndani. Kwa kuwa ua hautafunikwa, tutaupaka rangi ya akriliki mara mbili au tatu.

Naam, hayo yatosha kwa leo. Kwa kuwa tumefanya matayarisho yote, kesho tutaanza kazi yenyewe ya kupaka rangi.

Kutumia Burashi

Leo tutaanza kuona matokeo ya matayarisho tuliyofanya jana. Kwanza kabisa, tutakoroga rangi vizuri kabla hatujaanza kuipaka. Tayari tumeongeza maji kidogo kwenye rangi ya ukuta ya akriliki. Maji hayo yanafanyiza asilimia 5 hivi ya kiasi cha mchanganyiko. Hilo litasaidia burashi kupaka rangi kwa urahisi zaidi. Lakini lazima tuwe waangalifu tusiongeze maji mengi sana, kwani rangi itakuwa nyepesi sana na ile ya zamani itaonekana hata baada ya kupaka mara ya mwisho. Itafaa kutumia burashi pana kupaka miisho ya ukuta na dari. Kisha, tutatumia rola ya kupaka rangi kwenye sehemu kubwakubwa. Hiyo itaharakisha kazi. *

Lazima tukumbuke kutumia upande mmoja tu wa mkebe wa rangi ili kupangusa rangi iliyo kwenye burashi na kuwekelea burashi kwenye upande ule mwingine ulio safi ili kishikio na mikono yetu isishike rangi. Hatimaye, ni lazima tutumie kanuni hii, “Paka kuanzia juu ukielekea chini.” Hiyo inamaanisha kwanza tutapaka dari kisha ukuta. Baadaye, tutahitaji tu kupangusa madoa yoyote ya rangi kutoka kwa ncha ya mbao kwa kitambaa chenye maji na kupaka mbao hizo rangi nyangavu ya mafuta tuliyochagua. Sote twastahili pongezi! Kuta zetu zenye rangi ya manjano isiyong’aa na rangi nyeupe ya kijivu zinapendeza kwelikweli.

Sasa tuelekee kwenye ua wa mbele. Tutatumia burashi kubwa kupaka rangi ya maji kwenye nguzo za ua huo. Ua utapakwa rangi mara tatu. Tutangoja kwa saa moja hivi ili rangi ikauke kabla ya kupaka mara ya pili na pia kabla ya kupaka mara ya tatu, kwa hiyo tutamaliza kabla tu giza halijaingia. Hebu tuanze kazi.

Kwanza, tutasuza burashi katika maji na kuitikisa ili maji yatoke. Kufanya hivyo kunairuhusu burashi kufyonza rangi vizuri na kuzuia rangi isikauke kwenye burashi. Tutaweka rangi nyingi kwenye burashi na kupaka sehemu kubwakubwa ndefu. Badala ya kupaka juujuu, tutahakikisha “tunaifinyilia” rangi ndani ya mbao.

Aha! Tumemaliza kupaka rangi mara ya tatu mara jua linapoelekea tu kutua. Ua umeng’ara! Tuchunguze kazi yetu. Jasho letu halijatoka bure kwa siku hizo mbili. Kuna badiliko kubwa wee! Inapendeza kupaka rangi mpya nyumbani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 24 Watu wengi hutumia utepe wa kufunika mahali ambapo hapahitaji kupakwa rangi wakati wa kupaka miimo ya milango, fremu za madirisha, na kwenye ncha nyingine na kona.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 26]

Madokezo ya Kuzuia Matatizo ya Kawaida

KUVU: Osha sehemu itakayopakwa rangi kwa kutumia mchanganyiko wa kiasi kidogo cha dawa ya kuondoa madoa na maji mengi. Tumia glavu na miwani ya kujikinga. Paka rangi nzuri ya akriliki, kwani kuvu hukua sana katika sehemu iliyopakwa rangi ya mafuta. Ongeza dawa ya kuua kuvu, iwapo yapatikana.

MADOA YA MAJI NA MADOA MENGINE: Rekebisha mahali panapovuja au uondoe kisababishi cha madoa. Safisha madoa kwa sabuni na maji. Paka rangi ya kuzuia madoa, kisha upake rangi ya kwanza.

▪ SEHEMU ZILIZO NA UNGAUNGA: Pangusa vumbi yote. Ziba kwa rangi inayokauka polepole. Rangi za mafuta za kuzibia hupenya ndani na kuunganisha vipande vya ungaunga pamoja tofauti na zile za maji.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Hatari ya Risasi

Shirika la Kuzuia Uharibifu wa Mazingira la Australia linadokeza hivi katika kijitabu Lead Alert—Painting Your Home?

▪ Kiasi kidogo tu cha risasi katika damu kinaweza kuathiri tabia na maendeleo ya akili ya watoto wachanga.

▪ Watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano wanakabili hatari kubwa hata zaidi, kwa kuwa mfumo wao wa neva bado unaendelea kukua. Watoto wachanga hufyonza nusu ya risasi inayoingia mwilini mwao, huku watu wazima wakifyonza asilimia 10 hivi.

▪ Mtoto akila kipande cha rangi ya risasi chenye ukubwa wa kidole-gumba, kiasi cha risasi katika damu yake kitakuwa juu sana kwa majuma kadhaa.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mpangilio wa rangi mbalimbali

[Picha katika ukurasa wa 25]

“Jiko” la mtengenezaji wa rangi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Vaa mavazi ya kujikinga