Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Namba Huathiri Maisha Yako?

Je, Namba Huathiri Maisha Yako?

Je, Namba Huathiri Maisha Yako?

JE, NAMBA zina ujumbe wa siri? “Bila shaka!” ndivyo wanavyojibu watu fulani, huku wakitaja mfano mmoja wenye kustaajabisha—shambulizi la magaidi lililotukia Septemba 11, 2001.

Mbashiri mmoja anayetumia namba asema hivi: “Punde tu niliposikia habari hizo, niliangalia tarehe: tarehe 11, mwezi wa 9, mwaka wa 2001.” Kwa kawaida 11 huonwa na wabashiri wanaotumia namba kuwa moja ya “namba kuu” za ubashiri. Kwa hiyo, baadhi ya watu wanaopenda ubashiri huo wameorodhesha mambo mbalimbali kuhusu shambulizi hilo la magaidi, ambayo yanahusiana na namba 11 ambayo wanaiona kuwa “namba kuu.” Yafuatayo ni baadhi ya mambo waliyogundua:

Msiba huo ulitukia tarehe 11, mwezi wa 9. . . . 9 + 1 + 1 = 11.

Septemba 11 ilikuwa siku ya 254 ya mwaka. . . . 2 + 5 + 4 = 11.

Namba ya ndege iliyogonga jengo la kaskazini ilikuwa 11.

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 92. . . . 9 + 2 = 11.

Ndege iliyogonga jengo la kusini ilikuwa na abiria 65. . . . 6 + 5 = 11.

Majengo Mawili yaliyogongwa yalikuwa na umbo la namba 11.

Jina la Kiingereza “New York City” lina herufi 11.

Kubashiri kwa kutumia namba kumeenea sana Afrika, Asia, na Amerika. Katika ubashiri huo, tarakimu na jumla ya namba mbalimbali huonwa kuwa na ujumbe wa pekee. Kwa nini watu huvutiwa na ubashiri huo? Kituo kimoja kwenye Internet kinasema kwamba kufumbua mafumbo ya herufi za alfabeti zilizotumiwa katika majina—aina maarufu ya ubashiri unaotumia namba—“hufunua habari sahihi kuhusu utu wa mtu, mwelekeo wake, sifa zake na udhaifu wake.” Kituo hicho kinasema kwamba kuchunguza “tarehe yetu ya kuzaliwa huonyesha jinsi maisha yetu yatakavyokuwa, shangwe na magumu tutakayopata.”

Je, madai hayo ni ya kweli? Au je, kuna hatari zisizoonekana katika kuchunguza ujumbe wa siri katika namba?