Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tatizo la Kidini Wakati Brazili Ilipokuwa Koloni

Tatizo la Kidini Wakati Brazili Ilipokuwa Koloni

Tatizo la Kidini Wakati Brazili Ilipokuwa Koloni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

MNAMO Novemba 30, 1996, wajumbe wa Kongamano Kuhusu Umishonari na Kueneza Injili Ulimwenguni, ambalo lilipangwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni, walikutana karibu na bandari moja huko Salvador, Brazili. Mahali hapo pana umaana mkubwa. Karne nyingi zilizopita, mamilioni ya Waafrika waliuzwa utumwani kwenye bandari hiyo. Kasisi mmoja, alisema hivi alipozungumzia safari ngumu ya watumwa hao: “Machozi yao yalikusanyika katika bahari hii.” Katika siku hiyo ya pekee ya kumbukumbu, watu walihuzunikia jinsi Ukristo ulivyohusika katika kile ambacho msemaji mmoja alikitaja kuwa biashara mbovu ya watumwa. Dini ilihusikaje katika biashara ya watumwa wakati Brazili ilipokuwa koloni?

“Kuwaokoa Wenye Dhambi”

Katika mwaka wa 1441, miaka 60 hivi kabla ya nchi ya Brazili kuvumbuliwa rasmi, baharia Mreno Antão Gonçalves aliwateka watumwa Waafrika na kuwasafirisha kwa mara ya kwanza hadi Ureno. Ni watu wachache tu katika zama za kati ambao hawakukubali wazo la kuwatumikisha mateka wa vita, hasa wale ambao kanisa liliwaita “makafiri.” Hata hivyo, katika miaka 20 iliyofuata, biashara ya watumwa yenye ufanisi iliyotukia wakati ambapo hakukuwa na vita ilihitaji kuthibitishwa kuwa halali. Watu fulani walidai kwamba kuwatumikisha Waafrika ni “kuwaokoa wenye dhambi,” kwani walikuwa wanawaokoa kutoka katika maisha yao ya kipagani.

Tangazo la Romanus Pontifex, ambalo lilitolewa na Papa Nicholas wa Tano mnamo Januari 8, 1455, liliunga mkono rasmi biashara ya watumwa iliyokuwa ikisitawi. Hivyo, kanisa halikupinga utumwa. Badala yake, kama anavyosema mwanahistoria Mbrazili João Dornas Filho, baadhi ya makasisi walikuwa “watetezi shupavu” wa utumwa. Basi msingi ulikuwa umekwisha kuwekwa ili wakoloni Wareno waeneze utumwa huko Brazili wakati walipohamia huko.

“Suluhisho Pekee”

Mnamo mwaka wa 1549, wamishonari Wajesuti waliokuwa wametoka tu kuwasili nchini Brazili walifadhaika walipogundua kwamba wafanyakazi wengi nchini walikuwa watumwa ambao walikuwa wametekwa kiharamu. Wenye mashamba walikuwa wamewateka kwa nguvu na kuwalazimisha wafanye kazi katika mashamba yao ya miwa. Mkuu wa Wajesuti Manuel de Nóbrega aliandika hivi mwaka wa 1550: “Watu wengi wanasumbuliwa na dhamiri zao kwa sababu wanamiliki watumwa.” Licha ya hayo, wenye mashamba waliendelea kuwatumikisha watumwa wao, hata ingawa jambo hilo lingewazuia kusamehewa makosa yao kanisani.

Lakini punde si punde tatizo fulani liliwakumba Wajesuti wa Brazili. Hawakuwa na pesa za kutosha kuendeleza kazi yao ya ufadhili. Suluhisho moja lilikuwa kugharimia shughuli za kidini kwa kulima mashamba waliyopewa na serikali na kutumia faida iliyopatikana kutokana na mazao. Lakini ni nani ambao wangefanya kazi katika mashamba hayo? Mwanahistoria Mreno, Jorge Couto, anasema hivi: “Suluhisho pekee lilikuwa kuwatumia watumwa Waafrika—suluhisho ambalo lilisababisha watu watilie shaka kanuni za maadili, lakini mkuu wa Wajesuti nchini Brazili alipuuza jambo hilo.”

Wajesuti waliwaunga mkono wenye mashamba ambao walisisitiza kwamba wanataka watumwa zaidi Waafrika. Ilikuwa vigumu kwa watumwa Wahindi kuzoea kazi ngumu ya kulima, na mara nyingi waliasi au kutorokea misituni. * Kwa upande mwingine, Waafrika walikuwa wametumikishwa kwenye mashamba ya miwa katika koloni za Ureno kwenye visiwa vya Atlantiki na wakaonekana kuwa wanafaa. “Hawakutoroka, wala hawakuwa na pa kutorokea,” akasema mwandishi mmoja wakati huo.

Hivyo, biashara ya kuwauza watumwa Waafrika ilikubaliwa na makasisi na ikaongezeka hatua kwa hatua. Brazili ilitegemea sana biashara ya watumwa waliosafirishwa kupitia Bahari ya Atlantiki. Kufikia mwaka wa 1768, shamba la Wajesuti la Santa Cruz lilikuwa na watumwa 1,205. Watawa waliofuata kanuni ya Mtakatifu Benedict na watawa wengine pia walinunua mashamba na watumwa wengi. Joaquim Nabuco, Mbrazili aliyepinga sana utumwa katika karne ya 19, alilalamika hivi: “Makao ya watawa yamejaa watumwa.”

Kwa kuwa wakulima walishindana kuuza mazao, mara nyingi watu waliomiliki watumwa kwenye mashamba ya makanisa waliwatumikisha kwa ukatili. Stuart Schwartz, ambaye ni profesa wa historia, anasema kwamba hata wengi wa wale makasisi waliopinga ukatili uliotendwa dhidi ya watumwa “waliwadharau Waafrika” na “kuamini kwamba nidhamu, adhabu, na kazi zilikuwa njia pekee za kuwafanya watumwa wawe na adabu na kuacha ushirikina na uvivu.”

“Theolojia ya Utumwa”

Makasisi walipojaribu kupatanisha maadili ya Kikristo na mfumo uliosababisha dhuluma nyingi, walifanya utumwa uonekane kuwa jambo lililo sawa kimaadili. Mwanatheolojia mmoja alitaja hali hiyo kuwa theolojia ya utumwa. Kwa kuwa meli zilizowasafirisha watumwa zilijaa sana na kusababisha magonjwa na vifo vingi, kanisa lilisisitiza kwamba Waafrika wabatizwe kabla ya kuelekea kwenye Ulimwengu Mpya. * Kwa wazi, watu waliolazimishwa kuwa waumini mara nyingi walibatizwa bila kufundishwa mambo ya dini.—Ona sanduku lenye kichwa “Kuwa Wakristo kwa Ghafula?”

Kwa vyovyote, watumwa hao hawangeweza kutumia imani yao mpya kwani walifanya kazi kwa muda mrefu na maisha yao yalikuwa mafupi sana. Hata hivyo, mafundisho ya kanisa kwamba “mwili na nafsi zimetengana” yalisuluhisha tatizo hilo kwa kadiri fulani. Makasisi walionelea hivi: ‘Ni kweli kwamba Waafrika wanaumia kwa sababu ya utumwa wenye ukatili, lakini nafsi zao ziko huru. Basi watumwa wanapaswa kufurahi wanapodhalilishwa, kwani hivyo ndivyo Mungu alivyopanga kuwatayarisha kwa ajili ya utukufu.’

Wakati huohuo, kanisa liliwakumbusha watu waliomiliki watumwa kuhusu wajibu wao wa kimaadili wa kuwaruhusu kwenda kanisani, kuadhimisha sherehe za kidini, na kuoa. Makasisi walikashifu matendo yenye ukatili mwingi, lakini, kwa busara, walikazia pia hatari za kuwaendekeza watumwa. Kasisi mmoja Mjesuti alitoa shauri hili: “Wachapeni, wafungeni kwa minyororo, wafungeni pingu miguuni, fanyeni mambo yote hayo kwa wakati unaofaa na kwa kiasi, na mtaona jinsi uasi wa watumishi unavyodhibitiwa mara moja.”

Ni watu wachache tu ambao hawakutumia mbinu za ukatili ili kubadili imani ya Waafrika. Watetezi shupavu wa utumwa, kutia ndani Azeredo Coutinho, aliyekuwa Askofu wa Brazili, walidokeza kwamba wafanyabiashara waliowauza watumwa walikuwa wamewatendea Waafrika hao tendo la fadhili! Coutinho aliuliza hivi katika utetezi wake wa utumwa ambao ulichapishwa mwaka wa 1796: “Je, ingekuwa afadhali zaidi ikiwa Wakristo wangewaacha [Waafrika] kufa wakiwa wapagani na wakiabudu sanamu kuliko kufia katika dini yetu takatifu?” Vivyo hivyo, António Vieira, mishonari Mjesuti, aliwahimiza Waafrika hivi: “Mshukuruni Mungu sana kwa . . . kuwaleta katika [nchi] hii, ambako, baada ya kufundishwa mafundisho ya dini, mnaishi maisha ya Kikristo na mmeokolewa.”

Hasara za Utumwa

Kwa kukubali utumwa, kanisa lilikuwa limetarajia “kuwaokoa wenye dhambi.” Badala yake, utumwa ulisababisha mgawanyiko kwa sababu Waafrika walikataa katakata kuacha imani na desturi zao za kidini. Ndiyo sababu Wabrazili wengi leo wanachanganya Ukatoliki na dini ya Kiafrika.

Ijapokuwa watu fulani walioishi nyakati za ukoloni huko Brazili waliona kwamba kuna faida kwa kanisa kujihusisha na mambo ya kiuchumi, matokeo yalikuwa mabaya. Vifo na mateso yaliyosababishwa na matendo hayo yamezusha mashaka kuhusu maadili ya kanisa, na mashaka hayo hayawezi kumalizwa kabisa. Mwanahistoria mmoja alisema kwamba kukubali utumwa kulikuwa kufuata mtazamo wa watu ambao nabii Isaya aliwashutumu, kwa sababu walikuwa wakisema hivi: ‘Uovu ni wema, na wema ni uovu.’—Isaya 5:20.

Biblia Haiungi Mkono Kuwatumikisha Watu Kikatili

Biblia inaonyesha wazi kwamba Yehova Mungu hakubali ‘mtu mmoja awe na mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake,’ na hiyo inatia ndani kuwatumikisha watu kikatili. (Mhubiri 8:9) Kwa mfano, Sheria ya Mungu kwa Waisraeli ilisema kwamba mtu aliyemteka nyara mwanadamu na kumuuza alipaswa kuuawa. (Kutoka 21:16) Ni kweli kwamba watu wa Mungu walioishi kale walikuwa na watumwa, lakini utumwa huo haukuwa wa kimabavu kama ule unaozungumziwa katika makala hii. Kwa kuwa watumwa fulani Waisraeli waliamua kuendelea kuwatumikia mabwana zao hata wakati wao wa kuachiliwa ulipofika, hilo linaonyesha wazi kwamba utumwa uliokuwepo miongoni mwa watu wa Mungu haukuwa wa kikatili. (Kumbukumbu la Torati 15:12-17) Hivyo, kudai kwamba ule utumwa uliokuwepo miongoni mwa watu wa Mungu unahalalisha ukatili ambao umetokea katika historia yote ni kupotosha kabisa Maandiko. *

Katika Neno lake, Biblia Takatifu, Yehova Mungu anaahidi kwamba utumwa wote utakoma hivi punde. Tunafurahi kama nini kwamba katika ulimwengu mpya wa Mungu, watu hawataishi kwa hofu kwa sababu ya kukandamizwa na mabwana wakatili. Badala yake, “wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu.”—Mika 4:4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Kitabu The World Book Encyclopedia kinasema kwamba “Wahindi wengi sana walikufa kutokana na magonjwa ya Ulaya. Wengine wengi walipigana na Wareno na kuuawa.”

^ fu. 14 Nyakati nyingine ubatizo huo wa kidesturi ulirudiwa tena wakati watumwa hao walipowasili Brazili.

^ fu. 22 Kwa kuwa utumwa ulikuwa sehemu ya mfumo wa kiuchumi wa Milki ya Roma, Wakristo fulani walikuwa na watumwa. Haidhuru kile ambacho sheria za Roma ziliruhusu, Maandiko yanaonyesha kwamba Wakristo hawakuwadhulumu watumishi wao. Badala yake, walipaswa kumtendea kila mmoja kama “ndugu.”—Filemoni 10-17.

[Blabu katika ukurasa wa 15]

Yehova mungu anaahidi kwamba aina zote za utumwa zitakoma hivi Punde

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

Kumfaidi Mungu Au Kujifaidi?

Fernão de Oliveira, msomi Mreno wa karne ya 16, alisema kwamba pupa—wala si bidii kwa ajili ya dini—ndiyo iliyowachochea watu waliofanya biashara ya watumwa. Watu walibeba bidhaa kwa meli kutoka Ulaya ili kununua watumwa kwenye bandari za Afrika kwa bidhaa hizo. Kisha watumwa hao walisafirishwa hadi Amerika na kununuliwa kwa sukari, ambayo ilienda kuuzwa huko Ulaya. Safari hiyo ya biashara iliwapa faida kubwa wafanyabiashara na Serikali ya Ureno. Hata makasisi walifaidika, kwani walitoza kodi kwa ubatizo wa kila Mwafrika kabla ya kupelekwa Amerika.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

KUWA WAKRISTO KWA GHAFLA?

Katika kitabu chake The Slave Trade, mwanahistoria Hugh Thomas anaandika hivi: ‘Mwanzoni mwa karne ya kumi na saba, ilikuwa desturi kwa watumwa Waafrika kubatizwa kabla ya kuhamishwa. Kwa kawaida, watumwa hawakuwa wamefundishwa kamwe kabla ya tukio hilo, na wengi wao, hawakuwa wamejua kwamba kuna Mungu wa Ukristo kabla ya hapo. Kwa hiyo ubatizo huo ulikuwa wa kijuujuu tu.”

Profesa Thomas anaeleza kwamba kwa kawaida watumwa walipelekwa kanisani, ambako mwalimu wa mambo ya dini, ambaye mara nyingi alikuwa mtumwa, aliwajulisha watumwa hao katika lugha yao ya kienyeji kuhusu kubadili imani yao. “Kisha kasisi angepita miongoni mwa watumwa hao walioduwaa na kumpa kila mmoja wao jina la Kikristo, ambalo tayari lilikuwa limeandikwa kwenye karatasi. Pia, kasisi alinyunyiza chumvi kwanza kwenye ndimi za watumwa hao, kisha maji matakatifu. Halafu, kasisi angesema hivi, huku maneno yake yakitafsiriwa: ‘Sasa jioneni kuwa watoto wa Kristo. Mtafunga safari kwenda kwenye eneo la Wareno, ambako mtafundishwa mambo ya kidini. Sahauni kabisa mlikotoka. Msile mbwa, wala panya, wala farasi. Ridhikeni.’”

[Picha katika ukurasa wa 13]

Papa Nicholas wa Tano

[Hisani]

Culver Pictures

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kuchapwa hadharani, picha hii ilichorwa na Johann Rugendas wa karne ya 19 ambaye alijionea tukio hilo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Michoro ya watumwa kwenye ukurasa wa 13 na 15: De Malerische Reise in Brasilien de Johann Moritz Rugendas, cortesia da Biblioteca Mário de Andrade, São Paulo, Brasil