Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Faida na Hasara za Moto

Faida na Hasara za Moto

Faida na Hasara za Moto

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

MOTO unaweza kufaidi au kuleta hasara. Moto unaweza kuboresha au kuharibu mazingira. Mioto mikubwa inaweza kusababisha uharibifu mkubwa sana. Na si rahisi kuzima mioto hiyo.

Hali iliyotukia nchini Indonesia mwaka wa 1997 ni mfano mmoja unaoonyesha jinsi moto unavyoweza kusababisha hasara kubwa sana. Mwaka huo mioto iliteketeza vichaka nchini humo, iliharibu sana ardhi, ikadhuru afya, na kusababisha hasara ya kiuchumi. Na moshi mbaya sana wa mioto hiyo ulisambaa katika nchi jirani—jumla ya nchi nane—ukawaathiri watu wapatao milioni 75. Ripoti zinaonyesha kwamba watu milioni 20 waliugua ugonjwa wa pumu, ugonjwa wa kuvimba mapafu, magonjwa ya moyo, ya macho, na ya ngozi.

Katika nchi ya Singapore, uchafuzi wa hewa ulifikia kiwango cha juu sana. Jiji lilifunikwa na moshi. Mkazi mmoja aliyeogopa kutoka nje ya nyumba yake yenye hewa safi alilalamika hivi: “Sote tu wafungwa nyumbani mwetu.” Ukungu wa moshi ulikuwa mzito sana siku fulani hivi kwamba watu hawangeweza kuona miale ya jua.

Mwaka uliofuata wa 1998, wakazi 8,000 wa British Columbia, Kanada, walilazimika kuhama makwao kwa sababu ya moto mkubwa uliokuwa ukisambaa kwa kasi. Moto huo ulikuwa mojawapo ya mioto elfu moja hivi iliyoteketeza misitu nchini Kanada mwaka huo—mioto 115 kati yake haingeweza kuzimwa pindi fulani. Moto mmoja uliozuka kaskazini mwa Alberta, Kanada, uliteketeza msitu wenye ukubwa wa eka 90,000. Mkazi mmoja alisema hivi: “Ulikuwa kama mlipuko mkubwa wa kombora la nyuklia. Wingu kubwa jeusi la moshi lilitanda juu ya eneo lote.”

Hasara ya Moto

Moto ni moja ya vitu vya asili vyenye nguvu sana. Moto mkubwa wa msitu unaweza kubadili ardhi, kuathiri mimea na wanyama wa porini, kuhatarisha uhai na kuharibu mali.

Moto mkali sana unaweza kuchangia mmomonyoko wa udongo. Udongo usio na mimea humomonyolewa na mvua kubwa, ambayo mara nyingi hunyesha baada ya majira ya kiangazi. Mimea huathiriwa. Baadhi ya mimea myepesi hunyauka na kufa, lakini mimea mingine husitawi. Lakini kwa kawaida, magugu yasiyofaa ndiyo yanayositawi na kusambaa kotekote badala ya mimea ambayo kwa kawaida hukua katika maeneo hayo.

Wanyama wanaotegemea mimea fulani hususa inayokua kwenye maeneo hayo huwa hatarini pia. Wanyama wanaoishi Australia kama vile koala na possum wenye mikia yenye manyoya mengi ni wachache na huenda wakaangamia wote ikiwa makao yao yatateketezwa. Asilimia 75 ya misitu ya mvua, asilimia 66 ya pori, jamii 19 za wanyama, na jamii 68 za mimea ya asili katika bara la Australia zimetoweka katika muda wa miaka 200 iliyopita. Jamii nyingi kati ya hizo hazipatikani kwingineko ulimwenguni.

Majiji yamejengwa katika maeneo yenye misitu na hivyo watu wamekabili hatari kubwa ya kuathiriwa na moto wa msitu. Mnamo Desemba 1997, eneo lenye ukubwa wa zaidi ya eka 600,000 liliteketezwa wakati mioto mingi iliposambaa katika vitongoji vya Sydney, Australia, na katika miji kadhaa midogo karibu na milima ya Blue Mountains. Karibu nusu ya mioto hiyo haikuweza kuzimwa. Msimamizi wa idara ya wazima-moto alisema kwamba hajawahi kamwe kuona mioto mibaya hivyo katika muda wa miaka 30. Mamia ya watu walilazimika kuhama, na baadhi ya nyumba ziliteketea. Watu wawili walikufa. Kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Desemba 2001, mioto ya msitu ambayo yasemekana iliwashwa kimakusudi iliharibu misitu yenye ukubwa wa eka milioni 1.9.

Hatari ya Moto

Mioto inaweza kusambaa kwa sababu ya hali mbalimbali. Hali moja ya asili inayosababisha mioto ni mabadiliko ya hali ya hewa yanayohusiana na mkondo wa El Niño. Mara kwa mara, mkondo huo husababisha joto kali na ukame ulimwenguni pote. Eneo lolote lililokauka kwa sababu ya mkondo wa El Niño linaweza kuteketea mara moja.

Mara nyingi wanadamu husababisha mioto mikubwa kwa sababu ya kutojali. Katika nchi nyingi, ni uhalifu kuteketeza msitu kimakusudi. Imekadiriwa kwamba nusu ya mioto inayoteketeza misitu ya serikali huko New South Wales, Australia, huwashwa na watu kimakusudi au bila kutarajia.

Kuharibu mazingira kunaweza pia kusababisha mioto mikubwa. Kukata miti kunazidisha hatari ya misitu kushika moto. Mara nyingi majani makavu na vijiti hurundamana wakati miti inapokatwa na inaweza kuchochea moto mkubwa. Miti inapokatwa, miale ya jua hupenya misitu na kukausha majani hayo na vijiti hivyo. Cheche ya moto inapoanguka kwenye majani hayo na vijiti hivyo vikavu, moto huzuka na unaweza kusambaa kwa urahisi.

Matatizo ya kiuchumi yanaweza pia kuzidisha visa vya mioto mikubwa. Kwa mamia ya miaka, wakulima nchini Indonesia wamekuwa wakikata na kuteketeza vichaka ili kuboresha ardhi yao, bila kuharibu mazingira. Wakulima wanapotumia moto kwa njia nzuri, wanaboresha ardhi kama mioto ya asili inavyofanya. Hata hivyo, mbinu ya kale ya kukata na kuteketeza vichaka kwa ajili ya kilimo imeenea sana siku hizi. Kwa sababu ya uhitaji mkubwa sana ulimwenguni pote wa bidhaa kama vile mawese, watu wameteketeza misitu na kupanda mimea inayokua upesi na inayowaletea pesa. Njia rahisi na isiyogharimu ya kutayarisha ardhi ni kuteketeza misitu. Kwa hiyo, watu huteketeza maeneo yenye ukubwa wa maelfu ya eka bila kujali faida za muda mrefu za kuhifadhi misitu.

Faida za Moto

Ijapokuwa moto unaweza kusababisha uharibifu mkubwa sana na hasara, unaweza pia kufaidi mimea mingi na wanyama wengi. Kwa kweli, moto unaweza kuboresha mazingira. Namna gani?

Moto ni moja ya vitu ambavyo vimemsaidia mwanadamu kwa miaka mingi sana. Mwanadamu ameutumia kujipasha joto, kwa ajili ya mwangaza na kupika chakula. Makabila ya asili ya Australia yametumia moto kwa mamia ya miaka katika shughuli mbalimbali za kila siku. Kabila la Yanyuwa linathamini sana moto hivi kwamba lina zaidi ya majina kumi na mbili kwa ajili ya mioto mbalimbali na athari zake. Kwa mfano, wao huuita moto wa vichakani au wa porini kambambarra. Sehemu iliyoteketezwa na inayofaa uwindaji huitwa warrman. Moshi unaopaa angani na kufanyiza wingu huitwa rrumarri.

Wakazi hao wa asili huteketeza vichaka ili mimea mipya ichipuke. Wao hutumia mioto midogo kuteketeza majani makavu yaliyorundamana mashambani, ambayo mara nyingi huchochea mioto ya misitu. Kutumia moto kwa njia hiyo kumewawezesha wakazi wa asili wa Australia wajiruzuku kwa kilimo huku wakihifadhi misitu na wanyama. Kumepunguza pia hatari ya watu kuteketezwa na mioto hatari ya misitu.

Umuhimu wa Kudhibiti Moto

Wazungu walipowasili Australia zaidi ya miaka 200 hivi iliyopita, walianza kuvuruga uhusiano kati ya wanadamu, mazingira, na moto. Kwa maoni ya Wazungu, mioto ya misitu ilihitaji kukomeshwa. Kwa hiyo visa vya moto vilipungua, lakini kwa sababu majani makavu na vijiti viliongezeka, mioto iliyozuka ilikuwa mikali zaidi na haikuzimika kwa urahisi. Hata hivyo, hivi karibuni serikali zimeona umuhimu wa mbinu za wakazi wa asili wa Australia na wameanzisha mbinu ya kuteketeza majani ya msituni kwa mpango. Kwa kutumia mbinu hiyo moto hudhibitiwa ili usisababishe hasara. Mioto midogo huwashwa kabla ya majira ya kiangazi. Mioto hiyo husambaa polepole, si mikali sana, na huteketeza majani yote bila kuharibu miti. Kwa kawaida, umande huzima mioto hiyo wakati wa jioni.

Kusudi la mbinu hiyo ya kuteketeza majani msituni kwa moto uliodhibitiwa ni kulinda viumbe na mali na kudumisha aina mbalimbali za mimea na wanyama. Mbinu hiyo huzuia magugu fulani mapya yasienee upesi. Inasaidia pia kuhifadhi mazingira mbalimbali ili kulinda wanyama wanaopatikana kwenye sehemu hizo.

Yaonekana mbegu za mimea fulani hutegemea moto ili ziote. Baadhi ya mbegu hizo zina maganda magumu sana ambayo yanahitaji kuteketezwa na moto kuwezesha unyevunyevu upenye ndani. Utafiti unaonyesha kwamba moshi unasaidia pia mbegu kuota. Yadhaniwa kwamba moshi una kemikali 70 hivi ambazo zinachangia ukuzi wa mbegu. Kemikali moja muhimu ni nitrojeni-dioksidi.

Ardhi iliyoteketezwa karibuni huwa na udongo wenye virutubisho vingi kama vile nitrojeni na fosforasi. Moto hutokeza virutubishi kutokana na majani, huruhusu mwangaza wa jua kupenya ardhini, na huboresha ardhi ili miche isitawi. Kwa mfano, mbegu za migunga, huchipuka baada ya kuteketezwa na moto na miti hiyo husitawi katika mazingira hayo.

Yaonekana kwamba wanyama wengi hupenda maeneo yaliyoteketezwa na moto, hasa wanapokula mimea iliyochipuka ambayo mara nyingi huwa laini na yenye umajimaji. Jamii fulani za kangaruu na wallaby hupendelea misitu inayoteketezwa mara kwa mara. Yasemekana kwamba wanyama hao wanategemea moto kwa sababu mimea wanayokula na mahali wanakoishi husitawi sana baada ya kuteketezwa.

Kuna Mengi ya Kujifunza

Watu wanazidi kuelewa faida na hasara ya moto, lakini athari ya moto katika mazingira ni tata, na bado kuna mengi ya kujifunza. Utafiti zaidi unahitaji kufanywa kuhusu athari za moto kwa mimea na wanyama fulani hususa. Utafiti zaidi unahitaji pia kufanywa kuhusu faida na athari za moto kwa viumbe na mazingira. Baadhi ya maswali yanayohitaji kujibiwa ni: Je, mioto huchangia kuongezeka kwa joto duniani? Moshi unaathirije hali ya hewa? Mioto huathiriwaje na hali fulani-fulani?

Siku hizi kuna programu za kompyuta zinazoigiza hali halisi za mazingira, ambazo zimebuniwa ili kutabiri hali ya moto. Programu hizo hufasiri vipimo vya joto, vitu vinavyochochea moto, mwendo wa upepo, na hali nyingine za hewa. Lakini programu zilizopo sasa si sahihi nyakati zote, na haziwezi kutabiri matukio ya pekee kama mlipuko wa moto au kuongezeka ghafula kwa moto. Wazima-moto wawili wenye uzoefu waliteketea wakati moto wa msituni ulipolipuka ghafula huko Sydney mwaka wa 1997. Milipuko hiyo ya ghafula huwa hatari sana.

Ni vigumu sana kutabiri kuzuka kwa mioto mikubwa kwa sababu inaweza kutokeza hali za pekee za hewa, kutia ndani pepo kali, mawingu, na hata dhoruba za radi. Pepo zinaweza kubadili mwelekeo au mwendo ghafula, basi inakuwa vigumu kuudhibiti moto huo. Watafiti wanatumaini kuboresha programu zilizopo kwa kuongeza habari nyingine kama vile mwinamo na umbo la ardhi na kiasi cha vitu vinavyochochea moto.

Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Hali ya Hewa (NCAR) huko Colorado, Marekani, kinajitahidi kufikia lengo hilo. Watafiti hao wametia vifaa vya kisasa vya kisayansi pamoja na kompyuta saba zilizohifadhiwa kwenye vifuniko vizito ndani ya ndege maalumu aina ya C-130. Ndege hiyo imebuniwa ili iweze kupaa juu ya moto unaoenea na kukusanya habari fulani kwa kutumia vifaa maalumu vilivyo kwenye mabawa yake. Habari hizo huingizwa kwenye kompyuta ili zichunguzwe. Ndege hiyo ina kamera inayoitwa Thermacam inayotumia miale isiyoonekana ambayo inaweza kuonyesha ukali wa kila sehemu ya moto. Kwa njia hiyo wanasayansi wa NCAR wanajifunza kuboresha programu zinazopima hali ya moto.

Programu hizo bora zinatarajiwa kuwasaidia wataalamu kudhibiti mioto kwa njia salama zaidi. Uwezo wa kutabiri kwa usahihi athari za moto unaweza kupunguza pia hatari ambazo wazima-moto wanakabili wanapowalinda watu.

Naam, moto unapokosa kudhibitiwa unaweza kusababisha hasara kubwa sana, lakini unaweza pia kufaidi sana. Moto ni muhimu sana katika kudumisha mizunguko ya asili ambayo Muumba alibuni ili isitawishe dunia na kuhifadhi aina mbalimbali za mimea na wanyama.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kongoni walioduwaa wakimbia moto kwenye Bonde la Ufa la Bitterroot huko Montana

[Hisani]

John McColgan, BLM, Alaska Fire Service

[Picha katika ukurasa wa 26]

Moto uliodhibitiwa nchini Australia

[Hisani]

Photo provided courtesy of Queensland Rural Fire Service