Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Fumbo la Mawimbi ya Evripos

Fumbo la Mawimbi ya Evripos

Fumbo la Mawimbi ya Evripos

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UGIRIKI

MLANGO mwembamba wa bahari hutenganisha kisiwa cha Évvoia na sehemu nyingine ya nchi karibu na jiji la Khalkís, mashariki mwa Ugiriki. Mlango huo unaitwa mlangobahari wa Evripos. Una urefu wa kilometa nane na una upana unaotofautiana kuanzia kilometa 1.6 hadi meta 40. Sehemu yenye kina kifupi zaidi ya mlango huo ni meta sita tu. Jina Evripos, lamaanisha “Mkondo uendao kasi.” Jina hilo huelezea vizuri mwendo wa kasi wa maji katika mlango huo, wakati mwingine maji huenda kwa mwendo wa kilometa 20 hivi kwa saa. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kwamba nyakati nyingine mkondo huyumba-yumba polepole, na hata kutulia kabisa! Wageni wengi ambao hutembelea Khalkís husimama kwenye daraja dogo lililojengwa juu ya mlango huo ili kutazama mawimbi hayo yasiyo ya kawaida.

Mawimbi husababishwa na uvutano wa jua na mwezi juu ya uso wa bahari. Hivyo, mawimbi hubadilika kwa kutegemea mahali dunia ilipo ikilinganishwa na jua na mwezi. Wakati wa mwezi mpya, jua na mwezi huwa upande mmoja wa dunia. Wakati wa mwezi mpevu, jua na mwezi huwa pande tofauti za dunia. Nyakati zote hizo, jua na mwezi hufanya maji yajae kabisa.

Maji katika mlango wa Evripos hujaa kabisa mara mbili na hupungua mara mbili karibu kila saa 24. Mawimbi huelekea upande mmoja kwa muda wa saa 6 na dakika 13, kisha hutulia kidogo, na kuelekea upande wa pili. Mawimbi hayo hubadilika hivyo kwa siku 23 au 24 za mwezi-mwandamo. Lakini siku nne au tano za mwisho wa mwezi, mambo yasiyo ya kawaida hutukia. Siku fulani mawimbi huelekea upande mmoja peke yake. Siku nyingine mkondo hubadilika mara 14!

Jitihada za Kufumbua Fumbo

Kugeuka kwa mkondo wa mlango wa Evripos kumekuwa fumbo kwa watazamaji kwa maelfu ya miaka. Hekaya zinazojulikana vizuri husema kwamba Aristotle, wa karne ya nne K.W.K., alijitupa humo na kufa maji aliposhindwa kufumbua fumbo la mawimbi hayo. Lakini uhakika ni kwamba, badala ya kujitupa, alijaribu kulifumbua fumbo hilo kwa kuandika kitabu chake kinachoitwa Meteorologica. Aliandika hivi katika kitabu hicho: “Inaonekana bahari hupita katika mlango huo mwembamba kwa sababu ya ardhi iliyo kando yake. Maji ya bahari hutoka kwa ziwa dogo hadi kwa ziwa kubwa kwa sababu ardhi inayumbayumba.” Aristotle alidhani kimakosa kwamba ardhi iliyumbayumba kwa sababu ya mawimbi ya bahari na kwa sababu ya matetemeko ya ardhi ambayo ni ya kawaida katika eneo hilo. Karne moja hivi baadaye, mtaalamu wa nyota Mgiriki, Eratosthenes alitambua kwamba “pande zote [za mlango huo] zilikuwa na kina tofauti cha maji.” Alifikiri kwamba mawimbi hayo yalisababishwa na tofauti katika kingo za mlango huo.

Hata leo haijulikani vizuri ni kwa nini mawimbi ya Evripos hubadilika-badilika. Lakini ni wazi kuwa kwa kawaida mawimbi hutegemea tofauti ya kiwango cha maji kwenye pande mbili za mlango huo. Hiyo hufanya maji yateremke kutoka juu yakielekea chini. Tofauti hiyo hufikia kina cha sentimeta 40, na mtu anaweza kuiona akiwa katika daraja la Khalkís.

Tofauti Hiyo Husababishwa na Nini?

Tofauti katika kiwango cha maji husababishwa na nini? Wimbi litokalo Mediterania mashariki hugawanyika pande mbili lifikapo katika Kisiwa cha Évvoia. Wimbi la magharibi huelekea hadi upande wa kusini wa mlango huo. Wimbi la mashariki huzunguka kisiwani kote kabla ya kuingia upande wa kaskazini wa mlango huo. Wimbi hilo huchelewa kuingia kwenye mlango huo kwa muda wa saa moja na robo. Chini ya hali hizo, kiwango cha maji hutofautiana katika pande tofauti za mlango na kusababisha tofauti katika msukumo wa maji. Msukumo huo hufanya mawimbi ya kawaida yawe na nguvu zaidi yanapopita kwenye mlango wa Evripos.

Vipi kuhusu mawimbi yanayobadilika-badilika? Wakati wa robo ya kwanza na ya mwisho ya mwezi, uvutano wa jua hutenda kinyume cha uvutano wa mwezi. Uvutano wa mwezi husababisha maji kupungua, na uvutano wa jua hujaribu kuyafanya yajae. Hiyo hutokeza tofauti ndogo katika kina cha maji upande wa kaskazini na upande wa kusini wa mlango huo. Hivyo, nguvu za mawimbi hupungua. Wakati kuna upepo, wimbi hufifia na kutoweka kabisa.

Ni mengi yanayoweza kusemwa kuhusu tabia hiyo yenye kutatanisha na kupendeza ya mawimbi. Wakati wowote utakapotembelea Ugiriki, njoo Évvoia ujionee mwenyewe fumbo lenye kusisimua la mawimbi ya Evripos!

[Ramani katika ukurasa wa 12, 13]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI YA MEDITERRANIA

BAHARI YA AEGEA

ÉVVOIA

Khalkís

Mlango wa Evripos

UGIRIKI

ATHENS

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Picha ya Mlango wa Evripos iliyopigiwa angani