Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Taraja Lenye Kuogofya”

“Taraja Lenye Kuogofya”

“Taraja Lenye Kuogofya”

WAZIA tukio lifuatalo. Magaidi wamesambaza kisiri viini vya ugonjwa wa ndui katika maduka matatu makubwa sana nchini Marekani. Viini hivyo vinawavamia wanunuzi wasiokuwa na habari. Juma moja hivi baadaye, madaktari wanagundua kwamba watu 20 wameambukizwa ndui. Siku zinazofuata, watu zaidi wanaambukizwa viini hivyo. Watu wanashikwa na hofu. Maandamano yapamba moto. Vituo na wahudumu wa afya wamelemewa. Mipaka inafungwa. Uchumi umezorota. Siku 21 baada ya shambulizi la kwanza, ugonjwa wa ndui umeenea katika majimbo 25 ya Marekani na katika nchi nyingine 10. Sasa, watu 16,000 wameambukizwa na 1,000 wamekufa. Madaktari wanakadiria kwamba baada ya majuma matatu, watu 300,000 watakuwa wameambukizwa. Asilimia 75 kati yao watakufa.

Hilo si tukio la kuwaziwa tu katika sinema ya kisayansi. Ni jaribio la kompyuta, lililoonyesha jinsi ambavyo mambo yangekuwa iwapo shambulizi la namna hiyo lingetokea. Jaribio hilo lilifanywa Juni 2001 na kikundi kinachochunguza matatizo ya kijamii.

Watu wengi waliona jaribio hilo likiwa halisi sana na lenye kuogofya baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Mashambulizi ya World Trade Center huko New York na makao makuu ya kijeshi ya Pentagon, huko Washington, D.C., yalionyesha wazi kuwa kuna watu wakatili na wenye chuki wanaoweza kuwaangamiza wanadamu wengi sana. Zaidi ya hilo, mashambulizi hayo yalidhihirisha kuwa Marekani na nchi nyingine yoyote inaweza kushambuliwa. Tunaishi katika ulimwengu ambamo magaidi walioazimia wanaweza kuangamiza maelfu ya watu kwa muda mfupi sana.

Kufuatia mashambulizi ya Septemba 11, wanasiasa na wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini Marekani walikuwa shabaha ya shambulizi la viini hatari vya ugonjwa wa kimeta vilivyotiwa ndani ya barua. Watu waliogopa sana. Vyombo vya habari na wataalamu walizidisha hofu hiyo waliposema kuwa huenda magaidi wangeshambulia kwa viini vya magonjwa hatari zaidi kuliko kimeta—kwa mfano tauni au tetekuwanga. Huenda “mataifa yanayounga mkono ugaidi” yalikuwa yakitengeneza viini hivyo katika maabara za siri. Fikiria baadhi ya mambo ambayo yameandikwa hivi majuzi:

“Shirika la Tiba Ulimwenguni linatambua hatari inayoongezeka iwapo silaha za kibiolojia zitatumiwa kushambulia watu kwa tauni inayoweza kusambaa ulimwenguni pote. Bila shaka, mataifa yote yamo hatarini. Shambulizi la viini vya ugonjwa wa ndui, tauni, na kimeta laweza kuwa hatari sana kwa sababu litaleta magonjwa na vifo, na hofu itakayowakumba watu itafanya tatizo liwe baya hata zaidi.”—Shirika la Tiba la Marekani.

“Tofauti na mabomu na gesi za neva, shambulizi la kibayolojia huwa la siri: ugonjwa huenea pasipo kugunduliwa. Mwanzoni ni watu wachache wanaoenda hospitalini. Dalili zake huwatatanisha madaktari au hufanana na zile za magonjwa ya kawaida. Kabla ya wataalamu wa tiba kujua kinachoendelea, majiji mazima-mazima huenda yakawa yameambukizwa.”—Gazeti Scientific American

“Iwapo watu wangeshambuliwa kwa viini vya ugonjwa wa ndui leo, wengi duniani hawangekuwa na kinga, na karibu bilioni mbili wangekufa, kwa sababu ugonjwa huo huua asilimia 30 ya wale walioambukizwa viini vyake.”—Gazeti Foreign Affairs.

‘Nchi zote ziko hatarini. Majiji mazima-mazima huenda yakaambukizwa. Watu bilioni mbili huenda wakafa.’ Hizo ni taarifa zenye kuogofya. Lakini je, shambulizi la kibayolojia linaweza kutokea? Wataalamu wanalifikiria swali hilo. Makala ifuatayo itakusaidia kuelewa masuala yanayohusika.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Wanajeshi wanapambana na shambulizi la kibiolojia la kuwaziwa

[Hisani]

DoD photo by Cpl. Branden P. O’Brien, U.S. Marine Corps