Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Vanila Kiungo cha Tangu Zamani za Kale

Vanila Kiungo cha Tangu Zamani za Kale

Vanila Kiungo cha Tangu Zamani za Kale

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

WAAZTEKI waliiita tlilxochitl, yaani “ua jeusi,” jina ambalo linaonyesha rangi ya tunda lililohifadhiwa. Walitumia vanila kuongeza ladha ya kinywaji chao kilichotengenezwa kwa kakao kilichoitwa xocoatl, au chokoleti. Inasemekana kwamba mnamo mwaka wa 1520, Maliki wa Kiazteki wa Mexico, Montezuma, alimkaribisha mshambuliaji Mhispania Hernán Cortés kwa kinywaji hicho. Kisha Cortés alipeleka mbegu za kakao na vanila barani Ulaya. Kinywaji moto cha chokoleti kilichotiwa vanila kilipendwa sana kwenye makao mengi ya wafalme barani Ulaya. Lakini ilikuwa kuanzia mwaka wa 1602 ndipo daktari wa Malkia Elizabeth wa 1, Hugh Morgan, alipodokeza vanila itumiwe kuongeza ladha ya vyakula vingine. Halafu, katika miaka ya 1700, vanila ilianza kutumiwa kutengenezea pombe, tumbaku, na marashi.

Hata hivyo, muda mrefu kabla ya kuwapo kwa Miliki ya Kiazteki, Wahindi wa Totonak kutoka Veracruz, Mexico, walikuwa wakilima, kuvuna na kuhifadhi mbegu za vanila. * Lakini mapema katika miaka ya 1800 ndipo mmea wa vanila ulipopelekwa Ulaya ili ukuzwe na kutoka huko ulisambaa kwenye visiwa vya Bahari ya Hindi. Jitihada za wataalamu wa matunda na mboga za kuzalisha tunda la mmea huo hazikufaulu kwa sababu hakukuwa na nyuki aina ya melipona ambaye kiasili huchavusha mmea huo. Kwa hiyo, Mexico ikawa nchi pekee iliyouza vanila kuanzia karne ya 16 hadi ya 19. Mnamo mwaka wa 1841, Edmond Albius, aliyekuwa wakati mmoja mtumwa katika kisiwa cha Ufaransa cha Réunion, aligundua mbinu ya kuchavusha maua kwa mkono ili kuzalisha mbegu za vanila. Huo ulikuwa mwanzo wa biashara ya kukuza vanila nje ya Mexico. Leo, vanila hukuzwa kwa wingi katika visiwa vilivyomilikiwa na Ufaransa, kama Réunion, Visiwa vya Komoro, na Madagaska ambayo inatoa kiasi kikubwa zaidi.

Kukuza Vanila

Vanila ni mmea wa jamii ya okidi. Okidi ya vanila ndiyo okidi pekee inayoliwa kati ya mimea zaidi ya 20,000 ya okidi. Mmea huo ni namna ya mzabibu unaotambaa kwenye miti mingine na husitawi kivulini. Huo hukwea miti katika misitu ya kitropiki yenye mvua kwenye nyanda za chini. Kwenye mashamba makubwa ya kienyeji ya Mexico, miti kama pichoco hutumiwa kuitegemeza lakini hivi majuzi michungwa imeanza kutumiwa kwa mafanikio.

Okidi ya vanila huchanua maua kwenye vichala vingi vya rangi ya kijani-manjano. Kila ua hufunguka mara moja kwa saa chache kila mwaka. Inavutia sana kuwaona Wahindi wa Totonac wakifanya kazi inayohitaji uangalifu mkubwa ya kuchavusha maua. Wao huchavusha maua machache katika kila kichala ili mmea usipoteze nguvu nyingi na kushindwa na ugonjwa. Miezi sita hadi tisa baadaye, maganda marefu ya kijani yenye mbegu chache huvunwa kwa mkono, kabla hazijaiva kabisa.

Kutengeneza Vanila

Jambo la kushangaza ni kwamba mbegu za vanila si tamu na hazina harufu yoyote. Zinahitaji kupitia hatua nyingi ili kutokeza vinillin, bidhaa yenye harufu maalum na ladha nzuri. Hatua hizo nyingi na uchavushaji wa mikono hufanya vanila iwe kiungo ghali kupita viungo vyote. Nchini Mexico, walitumia njia ya kienyeji ya kuanika mbegu juu ya vyandarua vyeusi ili zikauke kwanza. Leo, mara nyingi mbegu hizo hukaushwa kwa joko. Kisha huwekwa katika masanduku maalum yaliyofunikwa kwa vyandarua na mikeka ili zikauke. Baadaye, vanila huanikwa juani na kukaushwa kwa siku kadhaa hadi mbegu zinapokuwa na rangi ya chokoleti-manjano. Kisha, mbegu hizo huwekwa ndani ya masanduku au kwenye vitanda vilivyofunikwa kwa karatasi iliyotiwa nta ili zikauke polepole kwa siku 45 kwa joto la kawaida. Kwa hiyo mbegu hizo huachwa kwa miezi mitatu zikiwa zimefunikwa ili ziwe na harufu kamili. Hivyo, kutengeneza vanila ni kazi kubwa sana.

Vanila ya Asili Au Isiyo ya Asili?

Vanila pia hutengenezwa kutokana na unga wa mbao. Huenda ukashangaa kusoma kibandiko cha bidhaa ambazo zinasemekana zimetengenezwa kwa vanila. Nchini Marekani, kwa mfano, aiskrimu yenye kibandiko kilichoandikwa “vanila” imetengenezwa kwa vanila pekee, mbegu za vanila au mchanganyiko wa vitu hivyo, ikiwa kimeandikwa “ina ladha ya vanila” huenda ikawa na karibu asilimia 42 ya viungo visivyo vya asili, na kama kimeandikwa “ina viungo visivyo vya asili,” bidhaa hiyo ina viungo visivyo vya asili peke yake. Wataalamu wa kuonja wamethibitisha kwamba ladha ya vanila halisi ni ya kipekee.

Ingawa Mexico haiongozi tena katika uzalishaji wa vanila—uzalishaji umeathiriwa na mambo kama vile ukataji wa misitu ya kitropiki iliyo pwani, na hivi majuzi, mafuriko—bado inachangia kwa njia muhimu, yaani ni kitovu cha uzalishaji wa okidi ya vanila. * Tangu zamani vanila ya Mexico inajulikana kwa harufu yake nzuri na ladha tamu sana. Ni kana kwamba watalii wamekubali jambo hilo kwa sababu mara nyingi wao humiminika kununua vanila kwenye maduka yaliyo katika mpaka wa Mexico na yale yasiyotozwa ushuru katika viwanja vya ndege vya Mexico ambapo bei ni nafuu kidogo. Wakati mwingine utakapokula aiskrimu iliyotengenezwa kwa vanila ya asili, fikiria kuhusu bidhaa hiyo ya tangu zamani za kale na kazi nyingi iliyofanywa wakati wa kuitengeneza, na ufurahie ladha yake!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Mbegu za vanila pia zilikuzwa Amerika ya Kati tangu zamani za kale.

^ fu. 12 Inasemekana kwamba vanila inayokuzwa katika mashamba makubwa huko Réunion, Madagaska, Mauritius na Shelisheli ilitokana na kipandikizi kimoja cha mmea kilicholetwa Réunion kutoka kwa shamba moja maarufu huko Paris liitwalo Jardin des Plantes.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mhindi wa Totonac akichavusha maua (kushoto) na akitenganisha mbegu za vanila baada ya kuzitayarisha (kulia). Okidi ya vanila (chini)

[Hisani]

Copyright Fulvio Eccardi/vsual.com