Watu Wanaopigapiga Vitambaa Huko Bamako
Watu Wanaopigapiga Vitambaa Huko Bamako
KULE Bamako, jiji kuu la nchi ya Mali huko Afrika Magharibi, sauti fulani husikika mchana kutwa. Lakini si sauti ya wanamuziki. Badala yake, sauti hiyo ni kama sauti ya ngoma na inatoka kwenye vibanda vya watu wanaopigapiga vitambaa. Lakini mbona wanapigapiga vitambaa?
Vitambaa hupigwa-pigwa baada ya kutiwa rangi katika ufundi usio wa kawaida. Kwanza, kitambaa cheupe au vazi fulani hutiwa rangi na mapambo mbalimbali. Kisha hutumbukizwa kwenye umajimaji mzito unaotokana na wanga wa mizizi ya mihogo au utomvu wa mikalitusi mbalimbali. Vitambaa au nguo hizo hukauka na kuwa ngumu kama ubao zinapoanikwa juani. Sasa vinakuwa tayari kwa ajili ya hatua ya mwisho—kupigwapigwa.
Kazi ya watu hao ni kupigapiga vitambaa au nguo hizo kavu mpaka zinyooke kabisa. Kwa kawaida, gogo la mti unaoitwa shea huwekwa katikati ya wanaume wawili vijana wanaoketi wakielekeana humo vibandani. Wanaume hao hupaka kitambaa nta na kukinyoosha kwenye gogo hilo. Kisha wao hupigapiga kitambaa hicho wakitumia nyundo kubwa zilizotengenezwa kutokana na mti aina ya shea. Kwa ustadi mkubwa wao hupigapiga kitambaa hicho mmoja baada ya mwingine, kila mmoja hupiga sehemu ambayo haikupigwa na mwenzake.
Mbona wasitumie pasi? Sababu moja ni kwamba joto la pasi hufanya kitambaa kichujuke upesi. Pia, kupiga kitambaa kwa nyundo hufanya rangi za kitambaa ziwe nyangavu zaidi kuliko kupiga pasi. Kila kipigo cha nyundo hufanya rangi za kitambaa zing’ae sana. Kitambaa kikiisha pigwapigwa kabisa, kinang’aa sana hivi kwamba unaweza kufikiri ndipo tu kimepakwa rangi.
Kwa hiyo, ukisikia sauti mfululizo kama ya ngoma kwenye mitaa ya jiji hili, tazama vibanda vilivyo karibu nawe. Huenda isiwe sauti ya ngoma; labda ni watu wanaopigapiga vitambaa jijini Bamako.