Idadi ya Familia za Mzazi Mmoja Inaongezeka
Idadi ya Familia za Mzazi Mmoja Inaongezeka
“Mara nyingi nilikuwa nikisali na kulia usiku nikimwambia Mungu: ‘Sijui nitafanya nini kesho.’”—GLORIA, MAMA ASIYE NA MUME, MWENYE WATOTO WATATU.
KUNA familia nyingi za mzazi mmoja katika jamii nyingi siku hizi, nazo zitaendelea kuwapo. * Wataalamu wanaochunguza idadi ya watu katika jamii mbalimbali wanajiuliza ni kwa nini watu huacha kuishi kama familia ya kawaida yenye mume, mke, na watoto na kupendelea aina nyingine za maisha ya jamaa.
Maprofesa wa taaluma ya jamii Simon Duncan na Rosalind Edwards wanasema kwamba “mabadiliko ya kudumu yanatokea katika familia na mitazamo ya wanaume kuwahusu wanawake na ya wanawake kuwahusu wanaume inabadilika.” Kwa nini? Baadhi ya wataalamu wanasema kwamba jambo hilo ni matokeo ya maamuzi ambayo watu hufanya maishani, kwa sababu ya mabadiliko katika uchumi, tamaduni, na jamii.
Ebu tuchunguze baadhi ya mabadiliko hayo, na maamuzi ambayo watu hufanya. Watu hulemewa sana na mambo mbalimbali maishani. Mambo yanayotukia ulimwenguni huwaathiri watu kuanzia wanapoamka hadi wanapokwenda kulala. Hapo awali watu walitumia wakati mwingi kufanya mambo pamoja na wengine katika familia, lakini sasa muda huo hutumiwa kuchunguza mambo kwenye Internet, kutazama televisheni, kupiga simu, kusafiri, na kufanya shughuli nyinginezo.
Watu hulemewa pia na hali ngumu ya uchumi. Vitu vya kisasa ni vya bei ghali, kwa hiyo wazazi wengi hufanya kazi ya kuajiriwa. Watu hukubali pia kuhama kwa sababu ya kazi, kwa hiyo wengi *
huishi mbali na kwao, na hawawezi kuwaomba watu wa ukoo msaada wanapouhitaji. Na hata wengine huishi mbali na wenzi wa ndoa. Katika nchi nyingi muziki wa kisasa, sinema, na vipindi vya televisheni, vinafanya hali kuwa mbaya hata zaidi kwa sababu vinaonyesha ndoa na familia kuwa mipango isiyo na maana.Mama Wasio na Waume
Hapo awali katika nchi zilizoendelea, mama wengi wasiokuwa na waume walikuwa wasichana wadogo ambao walisaidiwa na serikali kuruzuku watoto wao. Lakini hali hiyo imebadilika. Kuwa mama asiye na mume si jambo la kuaibikia siku hizi, na hata kunaonekana kuwa jambo la kuvutia kwa sababu hata wanawake wengine maarufu wana watoto ijapokuwa hawajaolewa. Isitoshe, wanawake wengi wana elimu nzuri zaidi siku hizi na wanaweza kujiruzuku, hivyo si lazima mwanamke awe na mume ili ajiruzuku mwenyewe na mtoto wake.
Baadhi ya akina mama wasio na waume, hasa wale wenye wazazi waliotalikiana, hubaki wakiwa waseja kwa sababu hawataki watoto wao wahuzunike kwa kumwona baba akiwaacha. Wanawake wengine wanakosa wenzi kwa sababu waume wao waliwaacha, wala si kwa kupenda kwao. Shirika la Joseph Rowntree huko Uingereza linasema hivi: “Kwa kawaida wanawake hawachagui kukaa bila mume kwa sababu ya ubinafsi, na watoto wanaolelewa na mzazi mmoja hutunzwa vizuri nao hutiwa nidhamu.”
Hata hivyo, ongezeko la familia za mzazi mmoja ni jambo linalotia wasiwasi kwa sababu wazazi hao na watoto wao wanaweza kupatwa na mfadhaiko, hali ngumu ya uchumi, na hasara nyinginezo. Watu wengine hujiuliza ikiwa inawezekana kwa mzazi asiye na mwenzi wa ndoa kulea watoto wake kwa mafanikio. Ni magumu gani hasa ambayo wazazi wasio na wenzi wa ndoa hukabili? Mkristo asiye na mwenzi wa ndoa anaweza kulea watoto wake kwa mafanikio jinsi gani?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Wataalamu wa jamii waonyesha kwamba akina mama wasio na waume ‘ni wengi sana kuliko akina baba wasio na wake.’ Kwa hiyo, makala hizi zinazungumzia hasa akina mama wasio na waume. Hata hivyo, kanuni zinazozungumziwa zinahusu vilevile baba wasio na wake.
^ fu. 6 Magumu ya akina mama yanazungumziwa kwa kindani katika makala ya “Je, Mama Wana Kazi Nyingi Mno?” katika toleo la Amkeni! la Aprili 8, 2002.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Semi Mbalimbali
Semi mbalimbali hutumiwa ulimwenguni kote kuzungumzia mama wanaolea watoto wakiwa peke yao. Katika makala hizi tunatumia semi “mzazi asiye na mwenzi wa ndoa,” na “mama asiye na mume” kumaanisha wazazi ambao wanawalea watoto wao peke yao bila msaada wa mume au mke au mwenzi iwe ni kwa sababu ya kifo, talaka, kutengana, au hawakupata kuoa au kuolewa, au sababu nyingine kama hiyo.
[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 4, 5]
IDADI YA FAMILIA ZA MZAZI MMOJA INAONGEZEKA KATIKA NCHI NYINGI
Marekani: “Idadi ya mama wasio na waume iliongezeka kati ya mwaka wa 1970 na 2000, kutoka milioni 3 hadi milioni 10; katika kipindi hicho, idadi ya akina baba wasio na wake iliongezeka kutoka 393,000 hadi milioni 2.”—Shirika la Marekani la Sensa.
Mexico: Kulingana na gazeti la La Jornada, karibu asilimia 27 ya mimba zote katika nchi hiyo ni za wasichana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 19.
Ireland: Idadi ya familia za mzazi mmoja iliongezeka kutoka asilimia 5.7 mwaka wa 1981 hadi asilimia 7.9 mwaka wa 1991. “Mama wengi wasio na waume hulea watoto wao wakiwa peke yao kwa sababu ndoa zao zimevunjika.”—Single Mothers in an International Context, 1997.
Uingereza: “Idadi ya familia za mzazi mmoja imepita asilimia 25 kwa mara ya kwanza. Jambo hilo linaonyesha kwamba idadi ya mama ambao hawajawahi kuolewa na talaka imeongezeka sana katika miaka 30 iliyopita.”—The Times, London, Machi 2, 2000.
Ufaransa: “Tangu mwishoni mwa miaka ya 1970, idadi ya familia za mzazi mmoja imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50.”—Single Mothers in an International Context, 1997.
Ujerumani: “Idadi ya wazazi wasio na wenzi wa ndoa imeongezeka maradufu katika miaka 20 iliyopita. Karibu familia zote za mzazi mmoja . . . zinatunzwa na mama.”—Single Mothers in an International Context, 1997.
Ugiriki: “Tangu mwaka wa 1980, idadi ya mama ambao hawajaolewa imeongezeka kwa asilimia 29.8 huku [Ugiriki]. Na kulingana na habari zilizotolewa na Muungano wa Ulaya, asilimia 3.3 ya watoto walizaliwa nje ya ndoa mwaka wa 1997, ikilinganishwa na asilimia 1.1 mwaka wa 1980.” —Gazeti la Ta Nea, Athens, Septemba 4, 1998.
Japan: ‘Idadi ya familia zinazotunzwa na akina mama wasio na waume imeongezeka tangu miaka ya 1970.’ Asilimia 17 ya familia zote zilitunzwa na akina mama wasio na waume katika mwaka wa 1997.—Single Mothers in an International Context, 1997; The World’s Women 2000: Trends and Statistics.
Australia: Karibu asilimia 25 ya watoto wanaishi na mzazi mmoja tu. Kwa kawaida jambo hilo lilisababishwa na kuvunjika kwa ndoa ya wazazi au wazazi walitengana. Imekadiriwa kwamba idadi ya familia za mzazi mmoja itaongezeka kwa asilimia 30 hadi 66 katika miaka 25 ijayo.—Shirika la Takwimu la Australia.