Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Watu Husisimuliwa na Michezo Hatari?

Kwa Nini Watu Husisimuliwa na Michezo Hatari?

Kwa Nini Watu Husisimuliwa na Michezo Hatari?

KATIKA uwanja wa Roma ya kale, watu 50,000 walisubiri kwa hamu nyingi. Kwa siku kadhaa wamekuwa wakingojea kwa hamu sana tukio hili kwa sababu ya matangazo yaliyoonyesha kutakuwa na “burudani tosha la kusisimua ajabu.”

Ingawa watu walipenda kutazama kiini-macho, maigizo yasiyotumia maneno, sarakasi, na vichekesho, matukio ya uwanjani yalikuwa tofauti kabisa. Hatimaye, watazamaji wangesahau ugumu wa viti vyao na mahangaiko ya siku wakati wangeona maonyesho hayo.

Waimbaji walianza, halafu walifuatwa na kuhani aliyevalia joho. Kisha wengine walifukiza uvumba kwa sanamu mbalimbali zilizowakilisha miungu ya kiume na ya kike, iliyoinuliwa juu ili watu wote waione. Hilo liliashiria baraka za miungu katika tamasha hizo.

Uchinjaji wa Wanyama

Sasa maonyesho makuu ya tamasha yalikaribia kuanza. Mwanzoni, mbuni na twiga, ambao watazamaji wengi hawakuwahi kuwaona maishani, waliruhusiwa kuingia uwanjani bila kuwa na njia ya kutorokea. Kisha walengaji hodari waliwapiga mishale viumbe hao maskini, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho. Jambo hilo liliwafurahisha sana watazamaji hao waliopenda tamasha za kusisimua.

Kisha, watazamaji hao wenye vifijo na nderemo walitazama pigano kati ya tembo wawili wakubwa sana ambao pembe zao ziliongezewa vyuma vikali virefu. Kulikuwa na nderemo mnyama mmoja alipoangushwa kwenye mchanga uliolowa damu akifa. Matukio hayo yamekuwa kionjo tu cha tamasha kuu itakayoanza hivi punde.

Tukio Kuu

Wapiganaji wawili wanapojitokeza uwanjani, watazamaji wainuka kwa shangwe na vigelegele. Wapiganaji wengine wamebeba mapanga na ngao na kuvaa kofia za chuma, na wengine hawana silaha sana na hawana kinga nzuri. Watazamaji washangilia wapiganaji hao wanaposhambuliana, hadi mmoja wao au wote wawili wanapokufa. Rekodi zaonyesha kwamba katika tukio moja wanyama 5,000 waliuawa katika siku 100. Kwenye tukio jingine wapiganaji 10,000 waliuawa kikatili. Na bado watazamaji walitaka machinjo zaidi.

Wafungwa na wale walioshikwa vitani walitumiwa kwenye michezo hiyo. Hata hivyo, kitabu kimoja kinasema, “hao ni tofauti na wapiganaji hodari waliopigana kwa silaha, na kupewa pesa nyingi, na ambao hawakuwa wamehukumiwa kuwa wapiganaji maishani mwao mwote.” Kwingineko wapiganaji walihudhuria shule maalumu ili kufundishwa utaalamu wa kupigana kwa mikono. Wakiwa na msisimuko, wapiganaji walivutiwa na michezo hiyo hatari. Walichochewa sana na tamaa ya kupigana tena na tena. Kitabu kimoja kinasema kwamba “mpiganaji aliyefanikiwa zaidi ni yule aliyeshiriki mapigano hamsini na kustaafu.”

Kupigana na Mafahali

Ulimwengu sasa umeingia kwenye milenia mpya. Lakini ni dhahiri kwamba bado watu wanapenda sana michezo hatari, hasa ile inayoweza kuua. Kwa mfano, kupigana na mafahali kumekuwa maarufu huko Amerika Kusini na Mexico kwa karne nyingi. Leo michezo hiyo huchezwa katika Amerika ya Latini, Ureno, na Hispania.

Inaripotiwa kwamba nchini Mexico kuna viwanja 200 hivi na zaidi ya 400 huko Hispania. Uwanja mmoja nchini Mexico unatoshea watu 50,000. Viwanja vingi hujaa watu wanaokuja kuwatazama watu wanaoonyesha ujasiri kwa kupigana na mafahali. Mpiganaji anayeonyesha dalili yoyote ya woga huzomewa sana na watazamaji.

Wanawake hawajaachwa nyuma, wengine hupata mamilioni ya dola kwa kuua mafahali. Mwanamke mmoja anayepigana na fahali aliyehojiwa katika televisheni alisema kwamba hakuna kitu kiwezacho kumsisimua kama kupigana na fahali mwenye ghadhabu, licha ya hatari ya kuuawa.

Kukimbizwa na Mafahali

Ripoti moja inasema kwamba kuna “makelele yasiyokoma ya watazamaji waliojipanga katika mistari minne kando ya barabara ya Estafeta karibu na mkahawa wa Sixto huko Pamplona, Hispania. Watu wanazungumza lugha tofauti-tofauti kama vile Basque, Castilian, Catalan, na Kiingereza.” Umati unakusanyika mapema kulitazama tukio hilo. Mafahali hufungiwa mazizini kilometa moja hivi kutoka uwanjani.

Katika asubuhi ya mapigano, milango ya mazizi hufunguliwa, na mafahali sita hutoka, na yule atakayepigana usiku huo hubaki. Barabara hiyo yenye majengo huwekewa vizuizi kila upande ili kuziba barabara ndogo-ndogo zinazoungana nayo ili mafahali waende moja kwa moja hadi uwanjani, ambako mafahali hao hufika baada ya dakika mbili mambo yakienda vizuri.

Miaka iliyopita, watu fulani walihatarisha uhai wao kwa kujaribu kushinda mafahali hao kwa mbio. Na bado wengine hufanya hivyo kila mwaka. Hatimaye kujaribu kushindana mbio na mafahali kumekuwa mashindano ya kimataifa. Wengi wamejeruhiwa vibaya na mafahali, na wengine kuuawa kwa kupigwa kwa pembe. Mkimbiaji mmoja alisema: “Ukifikiri unaweza kushinda fahali kwa mbio, umekosea sana.” Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Hispania, katika kipindi cha miaka 20, “kwa wastani, mtu mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa pembe kila siku.” Wengine 20 hadi 25 walijeruhiwa na kutibiwa kila siku.

Mbona watu huvutiwa na michezo hiyo hatari? Mkimbiaji mmoja ajibu: “Zile sekunde chache unapokuwa na mafahali, ukiwa mbele yao, na kuwanusa, na kusikia kwato zao zikipiga chini, na kutazama pembe zake zikikukosa tu kidogo zikienda juu na chini—huo ndio uvutio mkubwa sana.” Wakimbiaji hushangiliwa sana na umati. Je, kuna wengine ambao huudhika iwapo hawaoni mmoja akiuawa au kurushwa na fahali mwenye uzani wa karibu kilogramu 700? Je, wengine wanapenda kuona umwagikaji wa damu kama Waroma wa kale?

Kucheza na Kifo

Kuna wale wanaopenda kucheza na kifo katika njia nyinginezo. Waendeshaji fulani wa pikipiki huhatarisha uhai wao kwa kuruka juu ya magari 50 yaliyoegeshwa karibu-karibu au kuruka juu ya mabasi makubwa ya abiria au juu ya bonde pana. Mwendeshaji mmoja kama huyo alisema kwamba amevunjika mifupa 37 na kuzirai kwa jumla ya siku 30. Alisema: “Kuvunjika mifupa au mikono si kitu kwangu. . . . Nimefanyiwa upasuaji mkubwa mara kumi na mbili wa kurekebisha mifupa yangu iliyovunjika. Katika upasuaji huo, mtu anapasuliwa na kuwekewa kipande fulani cha kushikilia mifupa au anawekewa skurubu. Nafikiri nina skurubu 35 hadi 40 mwilini mwangu zinazoshikilia mifupa yangu. Mimi huenda hospitalini kila wakati.” Wakati fulani alijeruhiwa alipokuwa akifanya mazoezi ya kuruka juu ya magari kadhaa na kushindwa, watazamaji walimzomea.

Watu wengi husisimukia michezo hatari—kutia ndani michezo inayoweza kuua kama kupanda majengo marefu jijini bila kutumia vifaa vya usalama, kuteleza kwenye theluji kutoka juu ya mlima wenye urefu wa meta 6,000, kuruka kutoka juu ya majengo marefu na katika daraja wakiwa wamejifunga kwa kamba, kuruka kutoka kwa ndege wakiwa wamening’inia mgongoni mwa mtu mwingine kwa mwavuli, au kupanda majabali yenye theluji kwa kutumia shoka ndogo za mkononi. Mpandaji mmoja wa milima ya theluji anaomboleza hivi: “Mimi hupoteza marafiki watatu au wanne kila mwaka.” Hiyo ni baadhi tu ya michezo hatari ambayo imepata umaarufu ulimwenguni. Mwandishi mmoja anasema: “Uwezekano wa kupatwa na msiba ndilo jambo linalowavutia watu kushiriki katika michezo hiyo.”

Gazeti la U.S.News & World Report linasema: “Hata mchezo ulio hatari kati ya michezo hatari zaidi inazidi kupendwa na watu wengi.” “Mchezo ambao mrukaji hodari wa miavuli huachiliwa kutoka kwa ndege urefu wa meta 4,000 juu angani na kupinduka-pinduka akitumia ubao, haukujulikana katika mwaka wa 1990; lakini sasa unapendwa na maelfu ya watu. Mchezo wa kuruka uitwao BASE, ulianzishwa rasmi katika mwaka wa 1980, na sasa umevutia mamia ya watu, ambao huruka kwa miavuli—mara nyingi usiku na kinyume cha sheria—kutoka kwenye minara ya vituo vya redio au kutoka juu ya daraja.” Tayari mchezo huo umeua watu wengi. Mrukaji mmoja mashuhuri anasema: “Hakuna majeruhi wengi katika mchezo wa BASE. Unakufa au unaishi.”

Kupanda milima iliyoinuka sana kwa kutumia tu vifaa vidogo vya kujishikilia kwa vidole vya mikono na vya miguu huwavutia maelfu ya watu. Hata matangazo ya bidhaa za kila aina kuanzia malori ya mizigo hadi dawa za kuumwa na kichwa katika televisheni na magazetini huonyesha wapandaji wakiwa wamening’inia vibaya katika milima mirefu sana, wakishikiliwa na kamba nyembamba tu. Imeripotiwa kwamba mnamo mwaka wa 1989 karibu watu 50,000 nchini Marekani walishiriki michezo hiyo, na inakadiriwa kwamba hivi karibuni zaidi ya nusu milioni wanashiriki katika mchezo huo hatari. Idadi hiyo inazidi kuongezeka ulimwenguni pote.

Nchini Marekani, “idadi inayoongezeka ya wavulana na wasichana ‘wa kawaida’ wanakufa au kulemazwa wakicheza michezo mipya ya ajabu iliyo hatari,” laripoti gazeti Family Circle. Vijana wengi wamekufa wakijaribu kutokea kwenye dirisha la gari linaloenda kasi na kusimama juu yake, au kusimama juu ya lifti inayotumika, au juu ya gari-moshi la chini ya ardhi linaloenda kasi.

Sasa kuliko wakati mwingine wowote, watu wengi wanapanda Mlima Everest ulio mrefu sana. Wapandaji wasiokuwa na ujuzi wa kutosha hulipa hata dola 65,000 za Marekani ili waongozwe hadi kwenye kilele na kisha kushuka. Tangu mwaka wa 1953, zaidi ya wapandaji 700 wamefika katika kilele hicho. Wengi hawakufanikiwa kushuka chini wakiwa hai. Baadhi ya miili ingali huko juu. Mwandishi mmoja wa habari aliandika: “Wapandaji wanataka kuweka rekodi za kuwa wapandaji wachanga zaidi, wazee zaidi, wenye kasi zaidi kuwahi kupanda Mlima Everest.” Mwingine aliandika: “Tofauti na michezo mingine, anayepanda mlima ni lazima awe tayari kufa.” Je, ni lazima mtu ahatarishe uhai wake ili aonyeshe ujasiri wake? “Kuwa jasiri hakumaanishi kufanya mambo ya kijinga,” aonya mpandaji mmoja mashuhuri. Baadhi ya “mambo ya kijinga” anayoorodhesha ni “kupanda Mlima Everest bila kuwa mtaalamu ‘ili kujifurahisha tu.’”

Basi hali ya kufuatia michezo hatari inaendelea tu. Sasa watu wanaendelea kubuni na kufuatia mambo mengi zaidi hatari ya aina tofauti-tofauti. Mwanasaikolojia mmoja anatabiri kwamba michezo hatari, ambayo wale wanayoishiriki huhatarisha uhai katika pindi fulani, “itapendwa na watazamaji na washiriki wengi zaidi katika karne ya 21.”

Kwa Nini Watu Huvutiwa Nayo?

Wengi wanaoshiriki michezo hatari husema kwamba wanafanya hivyo kwa sababu ya kukosa mambo ya kufanya. Wakiwa wamechoshwa na kazi za kawaida, wengine huacha kazi zao na kufuatia michezo hiyo hatari. “Nilianza kuruka kutoka juu ya vitu kama daraja ili nipate kutulia, ili nisahau matatizo yangu na kuanza upya,” asema mtu mmoja. “Ningeruka na kuhisi sina matatizo yoyote.” “Sasa ameruka mara 456, kutia ndani kuruka kutoka juu ya jabali linaloitwa El Capitan katika Yosemite, kutoka juu ya Daraja la San Francisco, na kutoka juu ya gari linalotumia kamba linalopitia juu angani na ambalo liko juu zaidi ulimwenguni huko Ufaransa,” gazeti moja liliripoti.

Mrukaji mwingine alisema: “Ni kana kwamba wakati husimama. Hujali yatakayotokea.” Mwingine alisema: “Yale tunayofanya ili tupate raha [kutia ndani pesa], wengi hawawezi kufanya hata wakitishwa kwa bunduki.” Gazeti la Newsweek lilisema: “Mambo yote hayo yanafanywa ili kusisimua.”

Wanasaikolojia fulani wamechunguza sana watu wanaopenda msisimuko. Mmoja ameorodhesha watu wanaopenda msisimuko katika kikundi fulani. ‘Watu waliomo katika kikundi hicho wanapenda kusisimuka—kufanya mambo hatari, kupenda kuchangamka, kupenda kusisimuka, na kupenda kuchachawa.’ Anasema: “Watu wengine hutafuta usalama maishani—kwa kufuata kanuni na desturi.” “Wale wanaopenda msisimuko huacha kushikilia kanuni na mapokeo hayo. Wao huishi kivyao.” Yeye anadai uchunguzi unaonyesha kwamba watu wa aina hiyo husababisha aksidenti mara mbili barabarani kuliko watu wengine. “Aksidenti ndiyo husababisha vifo vingi zaidi miongoni mwa vijana, nayo hutokea vijana wanapojihatarisha wakitafuta msisimuko.”

Wanasayansi na wanasaikolojia wanakubali kwamba si jambo la kawaida kwa mtu yeyote kushiriki katika michezo hatari inayoweza kuua kwa urahisi. Ukweli wa kwamba wengi hujeruhiwa vibaya sana na kupata nafuu baada ya kukaa hospitalini na vituo vya kuwasaidia kurudia hali yao ya kawaida, halafu kisha wanarudia michezo hiyo hatari, huonyesha kwamba wana kasoro fulani. Na mara nyingi huenda hao ni watu wenye akili sana.

Wataalamu hawafahamu ni kwa nini watu hao hutaka kuhatarisha uhai na miili yao. Wanadokeza kwamba huenda wakawa na kasoro ya akili. Wanasema: “Huwezi kumzuia asitafute msisimuko, labda ujaribu kumzuia asifanye mambo ambayo ni hatari sana. Angalau, utamzuia asihatarishe uhai wa watu wengine.”

Maoni ya Kikristo

Wakristo huona uhai ukiwa zawadi ya thamani kutoka kwa Yehova Mungu. Mtu anapohatarisha uhai wake kimakusudi kwa kufanya mambo ambayo ni hatari ili aonyeshe ujasiri wake—eti kwamba yeye ni mwanamume—ama kuwasisimua watazamaji au kutosheleza msisimuko wake mwenyewe, kwa hakika huyo anadharau zawadi ya ajabu ya uhai ambayo Mungu ametupatia. Kwa kweli, Yesu alistahi sana uhai wake na hakuuhatarisha bila sababu. Yeye alikataa kumjaribu Mungu.—Mathayo 4:5-7.

Wakristo vilevile, wanawajibika kustahi uhai. Mkristo mmoja aliandika: “Wakati mmoja nilipanda jabali refu sana na nikashindwa kusonga mbele wala nyuma. Hata leo mimi hushtuka nikikumbuka jinsi nilivyokaribia kufa. Ungekuwa upumbavu ulioje kama ningepoteza uhai wangu!”

Kijana Mkristo aliandika: ‘Mahali ninapoishi, watoto hushiriki katika michezo mingi hatari. Wakati wote wao hujaribu kunishawishi nijiunge nao. Hata hivyo, katika taarifa za habari, mimi hutazama watu waliokufa au kujeruhiwa vibaya kwa kushiriki katika michezo ambayo wenzangu husema eti inafurahisha. Halingekuwa jambo la hekima kuhatarisha uhai ambao Yehova Mungu alinipa, kwa sababu ya msisimuko kama huo wa muda mfupi.’ Na uwe na utimamu wa akili kama huo na ufanye maamuzi mazuri.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

© Reuters NewMedia Inc./CORBIS

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Steve Vidler/SuperStock