Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Njaa Kuu ya Ireland Iliyosababisha Vifo na Uhamaji Usio na Kifani

Njaa Kuu ya Ireland Iliyosababisha Vifo na Uhamaji Usio na Kifani

Njaa Kuu ya Ireland Iliyosababisha Vifo na Uhamaji Usio na Kifani

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND

CHINI ya mlima “mtakatifu” wa Ireland, Croagh Patrick, * kuna merikebu isiyo ya kawaida. Inafanana na zile merikebu zenye matanga zilizotengenezwa katika miaka ya 1800, na gubeti yake inaelekea Bahari ya Atlantiki upande wa magharibi. Lakini merikebu hiyo haitasafiri baharini kamwe. Imekazwa kikiki katika saruji. Katikati ya milingoti yake kuna sanamu zinazofanana kabisa na viunzi vya mifupa ya binadamu.

Merikebu hiyo ni sanamu iliyotengenezwa kwa metali. Ilizinduliwa rasmi mwaka wa 1997 kwa ukumbusho wa mojawapo ya misiba mikubwa zaidi iliyowahi kukumba Ireland, yaani, ile Njaa Kuu. Viunzi vya mifupa na merikebu hiyo ni mifano ya vifo na uhamaji mkuu uliotokea katika ile miaka ya huzuni kuanzia 1845 hadi 1850.

Ni kweli kwamba njaa imekumba nchi nyingi. Hata hivyo, ile Njaa Kuu ya Ireland ilikuwa mbaya zaidi kwa njia nyingi. Idadi ya watu huko Ireland ilikuwa milioni nane hivi mwaka wa 1845. Kufikia mwaka wa 1850, labda watu milioni moja na nusu walikuwa wamekufa njaa! Na watu milioni moja walikuwa wamehamia Uingereza au Marekani ili watafute maisha bora. Bila shaka hiyo ilikuwa njaa kuu.

Ni nini kilichosababisha njaa hiyo kuu? Watu walioathiriwa walisaidiwaje? Tunaweza kujifunza nini kutokana na msiba huo? Acha tuchunguze kifupi maisha ya watu wa Ireland katika miaka iliyotangulia njaa hiyo ili tupate majibu.

Kabla ya ile Njaa Kuu

Mapema katika miaka ya 1800 milki ya Uingereza ilikuwa ikitawala sehemu kubwa ya dunia. Ireland pia ilitawaliwa na Uingereza. Sehemu kubwa ya ardhi ya Ireland ilikuwa mali ya makabaila Waingereza, ambao wengi wao waliishi Uingereza. Wenye mashamba hao walitoza kodi za juu kutoka kwa wapangaji wao huko Ireland, nao waliwalipa mshahara wa chini kwa kazi yao.

Maelfu ya wakulima wenye mashamba madogo walikuwa maskini hohehahe. Kwa sababu hawakuweza kununua nyama au vyakula vingine, watu hao walipanda chakula kilichokuwa cha bei nafuu, rahisi kupanda, na kilichotoa mazao mengi, yaani, viazi.

Viazi Vilikuwa Muhimu Sana

Viazi vilianza kupandwa Ireland yapata mwaka wa 1590. Viazi vilifaa sana huko Ireland kwa sababu kulikuwa na mvua nyingi na joto la kiasi, na havihitaji udongo wenye rutuba. Viazi vilikuwa chakula cha wanadamu na pia wanyama. Kufikia katikati ya miaka ya 1800, viazi vilipandwa kwenye karibu thuluthi ya mashamba yote katika nchi hiyo. Thuluthi mbili hivi za viazi zilikuwa chakula cha wanadamu. Wanaume wa kawaida wa Ireland walikula viazi vitupu kila siku!

Kwa kuwa watu wengi hawakuwa na chakula kingine isipokuwa viazi, hali hiyo iliweza kusababisha msiba kwa urahisi. Wangefanya nini kama mazao yangeharibika?

Zao la Kwanza Lililoharibika

Mazao ya viazi yalikuwa yameharibika mara kwa mara hapo awali. Lakini njaa iliweza kuzuiwa msaada ulipotolewa nyakati hizo na mavuno ya mwaka uliofuata yalipokuwa mazuri. Kwa hiyo, mazao ya viazi yalipoharibika mwaka wa 1845, watu wenye mamlaka hawakuwa na wasiwasi wowote.

Lakini wakati huo hali ilikuwa mbaya zaidi. Siku hizi tunajua kwamba ugonjwa unaosababishwa na kuvu, phytophthora infestans, ndio uliosababisha kuharibika kwa mazao mwaka wa 1845. Kuvu hiyo inayosambazwa na upepo ilienea upesi kutoka shamba moja la viazi hadi shamba lingine. Viazi vyote vilivyoathiriwa vilioza, vile vilivyokuwa shambani na vilevile vilivyokuwa vimehifadhiwa. Kwa sababu ni aina moja tu ya kiazi iliyokuwa imepandwa, viazi vyote nchini viliathiriwa. Na kwa kuwa viazi hivyo ndivyo vilivyokuwa mbegu za mwaka uliofuata, kuvu hiyo iliathiri pia mazao ya miaka iliyofuata.

Mazao Yaharibika Mara ya Pili

Viazi hivyo vibovu vilivyohifadhiwa vikapandwa mwaka uliofuata, 1846, lakini kuvu iliharibu mazao ya mwaka huo pia. Kwa kuwa hakukuwa na viazi vyovyote vya kuvuna, wafanyakazi wengi walipoteza kazi zao. Makabaila hawakuweza kuwalipa mishahara.

Ili kuwasaidia watu maskini kulisha familia zao, serikali ilianzisha miradi mbalimbali na kuwaajiri. Wengi wao waliajiriwa kujenga barabara.

Wengine waliweza kupata kazi tu katika nyumba za serikali ambapo watu maskini waliweza kufanya kazi ili wapate chakula na mahali pa kulala. Kazi ilikuwa ngumu. Chakula kilikuwa kibovu mara nyingi, na makao yenyewe yalikuwa ya hali ya chini sana. Baadhi ya wafanyakazi walikufa.

Hatua hizo ziliwasaidia watu kidogo. Lakini hali ikawa mbaya zaidi. Kulikuwa na baridi kali sana katika majira ya baridi ya mwaka wa 1846-1847. Baridi hiyo ilizuia kazi zote za nje. Mashirika mbalimbali ya serikali yaliwagawia watu chakula bila malipo. Hata hivyo, baada ya miaka miwili, pesa za serikali zilianza kwisha, na hazikutosha kusaidia idadi iliyoongezeka ya watu waliokuwa wanyonge kwa sababu ya kukosa chakula. Kisha msiba mwingine mkubwa ulikumba Ireland.

Makabaila walioishi Uingereza, ambao wengi wao walikuwa na madeni makubwa, waliendelea kutoza kodi. Wapangaji wengi hawakuweza kulipa kodi hiyo, na kwa hiyo, maelfu wakafukuzwa kwenye mashamba yao. Baadhi ya wapangaji waliacha mashamba na kuhamia mjini wakitumaini kupata maisha bora. Lakini waende wapi? Hawakuwa na chakula, pesa, wala mahali pa kukaa. Wengi hawakuwa na namna nyingine isipokuwa kuhama nchi.

Wengi Walihama Nchi

Kuhama nchi hakukuwa jambo jipya. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 1700 watu walikuwa wamehamia Uingereza na Amerika kutoka Ireland, japo si kwa wingi sana. Baada ya majira ya baridi kali ya mwaka wa 1845, watu wengi sana wakahama nchi! Kufikia mwaka wa 1850, asilimia 26 ya wakazi wa New York ilikuwa watu waliozaliwa Ireland. Jiji hilo lilikuwa na watu wengi waliozaliwa Ireland kuliko jiji kuu la Ireland, Dublin.

Katika kile kipindi cha miaka sita ambacho njaa hiyo iliendelea, merikebu elfu tano zilifanya ile safari hatari ya kilometa 5,000 ya kuvuka Bahari ya Atlantiki. Merikebu nyingi zilikuwa kuukuu. Nyingine zilikuwa zimetumiwa kuwasafirisha watumwa hapo awali. Ziliendelea kutumiwa tu kwa sababu ya msiba huo mkubwa. Mahali pa kukaa katika merikebu hizo palikuwa finyu sana na hali ilikuwa mbaya kama wakati watumwa waliposafirishwa. Palikuwa pachafu, na chakula kilikuwa haba.

Maelfu ya abiria, ambao tayari walikuwa wanyonge kwa sababu ya njaa, wakawa wagonjwa. Wengi wakafa baharini. Mwaka wa 1847, merikebu zilizosafiri hadi Kanada zilianza kuitwa merikebu za jeneza. Hizo ziliwasafirisha wahamaji 100,000 hivi na zaidi ya 16,000 walikufa baharini au baada tu ya kuwasili kwenye bandari. Marafiki na watu wa ukoo huko Ireland walitumiwa barua na kuelezwa kuhusu hali hizo hatari, lakini bado watu walihama kwa wingi.

Makabaila wachache waliwasaidia wapangaji wao wa zamani. Kwa mfano, mmoja wao alikodi merikebu tatu na kuchangia nauli ya safari kwa wapangaji elfu moja. Hata hivyo, wahamaji wengi walihitaji kujilipia nauli. Mara nyingi ni mtu mmoja au wawili tu katika familia kubwa walioweza kulipa nauli ya safari hiyo. Wazia ile huzuni iliyokuwapo wakati maelfu ya watu walipoziaga familia zao kwenye bandari. Yamkini hawangeonana tena maishani.

Ugonjwa na Kuharibika kwa Mazao Mara ya Tatu

Baada ya mazao ya viazi kuharibika mara mbili na wengi kufukuzwa kutoka katika mashamba yao, watu waliobaki walikumbwa na msiba mwingine. Ugonjwa! Watu wengi walikufa kwa homa iletwayo na chawa, ugonjwa wa kuhara damu, na kiseyeye. Bila shaka wale walionusurika walifikiri kwamba hali haingeweza kamwe kuwa mbaya zaidi. Lakini walikosea.

Wakulima walipoona mazao mazuri ya viazi mwaka wa 1847 walitiwa moyo kuongeza eneo la mashamba ya viazi mara tatu mwaka wa 1848. Balaa! Kulikuwa na mvua nyingi sana katika majira ya joto mwaka huo. Kuvu ilirudi tena. Katika kipindi cha miaka minne mazao ya miaka mitatu yalikuwa yameharibika. Mashirika ya serikali na mashirika ya kutoa misaada hayakuweza kufanya zaidi. Na balaa nyingine ikatokea. Watu 36,000 walikufa kwa kipindupindu mwaka wa 1849.

Matokeo

Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya ugonjwa huo wa kipindupindu kwisha. Mazao yaliyofuata yalikuwa mazuri. Polepole mambo yakawa mazuri. Serikali ilitunga sheria mpya zilizofuta madeni yote yaliyosababishwa na njaa. Idadi ya watu ilianza kuongezeka tena. Ijapokuwa kuvu iliathiri mazao mara chache tena katika miaka iliyofuata, hakukutokea tena kamwe hali mbaya kama ya miaka ile ya njaa wakati Ireland ilipopoteza robo ya wakazi wake.

Leo, kuta na nyumba zilizoharibika hutapakaa kotekote Ireland, ambazo ni ukumbusho wa nyakati ngumu sana zilizofanya watu wengi wa nchi hiyo watawanyike. Babu za Wamarekani zaidi ya milioni 40 walitoka Ireland. Babu ya John F. Kennedy, aliyekuwa Rais wa Marekani, na vilevile babu ya Henry Ford, mbuni wa gari linaloitwa Ford, walihama Ireland wakati wa njaa hiyo kuu.

Bila shaka kuharibika kwa mazao kwa miaka kadhaa kulikuwa sababu kuu ya hali hiyo yenye kuhuzunisha ya uhamaji na vifo vingi. Mwandikaji mmoja wa Biblia alieleza jambo lingine lililochangia hali hiyo aliposema hivi: ‘Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.’ (Mhubiri 8:9) Tunathamini sana kwamba Neno la Mungu, Biblia, linatuhakikishia kwamba Muumba wa dunia na mazao yake yote ataleta ulimwengu mpya ulio paradiso. Wakati huo watu wote wataishi kwa amani na ufanisi. (2 Petro 3:13) Mtunga-zaburi wa kale pia alitabiri hivi: “Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima.”—Zaburi 72:16.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Ona Mnara wa Mlinzi, Aprili 15, 1995, ukurasa wa 26-28.

[Picha katika ukurasa wa 14]

Ukumbusho wa ile Njaa Kuu

[Picha katika ukurasa wa 15]

Watu wanaotafuta viazi. Picha iliyokuwa katika gazeti la “Illustrated London News,” Desemba 22, 1849

[Picha katika ukurasa wa 16]

Kuwapa familia maskini nguo

[Hisani]

na ukurasa wa 15: From the newspaper The Illustrated London News, December 22, 1849

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

“Meli ya Wahamaji” (Picha iliyochorwa na Charles J. Staniland, c. 1880)

[Hisani]

Bradford Art Galleries and Museums, West Yorkshire, UK/Bridgeman Art Library

[Picha katika ukurasa wa 17]

Magofu haya ya nyumba yanaonyesha wazi hali ngumu zilizosababishwa na ile miaka ya njaa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Mchoro ulio juu: Courtesy of the “Views of the Famine” Web site at http://vassun.vassar.edu/-sttaylor/FAMINE