Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ninahitaji Simu ya Mkononi?

Je, Ninahitaji Simu ya Mkononi?

Vijana Huuliza . . .

Je, Ninahitaji Simu ya Mkononi?

“Mimi huwa na wasiwasi mwingi na huudhika wakati sina simu ya mkononi.”—Akiko. *

SIMU za mkononi zimeongezeka katika nchi nyingi. Simu hizo zimerahisisha mawasiliano. Sasa watu wanaweza kuwasiliana na marafiki na wazazi wao wakati wowote na mahali popote. Simu nyingine zina vifaa vya kutuma ujumbe mfupi ulioandikwa, na hiyo imekuwa “njia ya kisasa zaidi ambayo vijana wengi hutumia kutosheleza tamaa yao ya kuwasiliana,” kulingana na gazeti The Times la London. Simu nyingine za mkononi zinaweza kukuunganisha na mtandao wa Internet, na unaweza kusoma habari na kutuma barua-pepe.

Labda una simu ya mkononi tayari, au huenda unapanga kuinunua. Vyovyote vile, unapaswa kufahamu kwamba hakuna jema lisilokuwa na kasoro. Ni kweli simu ya mkononi ina faida fulani. Hata hivyo, fikiria pia hasara zake, kwa kuwa ikiwa umeamua kuinunua, utaitumia kwa hekima zaidi ikiwa unafahamu vizuri hasara hizo.

‘Hesabu Gharama’

Yesu alitoa kanuni muhimu aliposema kwamba mtu anapaswa “kupiga hesabu ya gharama” kabla ya kuanza kazi yoyote ya maana. (Luka 14:28) Je, kanuni hiyo inaweza kutumiwa kuhusiana na simu ya mkononi? Bila shaka inaweza. Huenda ukapata simu ya mkononi kwa bei nafuu, au bila malipo yoyote. Hata hivyo, kama Henna mwenye umri wa miaka 17 alivyotambua, “gharama ya kuitumia huenda ikaongezeka haraka sana.” Huenda pia ukashawishiwa kutumia huduma nyingine za simu na kununua simu za bei ya juu zaidi. Hiroshi asema: “Mimi hufanya kazi ya muda na kuweka pesa ili ninunue simu mpya kila mwaka.” Vijana wengi hufanya hivyo. *

Hata kama wazazi wako hukulipia gharama ya simu, bado ni muhimu kuzingatia gharama ya matumizi. Mhudumu Mkristo asafiriye huko Japan asema: “Akina mama wengine hufanya kazi ya ziada ili kulipia gharama za simu za mkononi za watoto wao, ambazo huenda si muhimu.” Bila shaka hungependa kuwatwika wazazi wako mzigo kama huo!

‘Mwizi wa Wakati’

Mwanzoni huenda wengi wakatumia simu kwa usawaziko, lakini baadaye wanaweza kujikuta wakitumia wakati mwingi kuliko walivyotarajia—na kukosa wakati wa kufanya mambo ya maana zaidi. Hapo awali Mika alitumia muda mwingi pamoja na familia yao wakati wa chakula cha jioni. Anaeleza: “Siku hizi, baada ya kula, kila mmoja wetu hurudi chumbani mwake kuzungumza [kwa simu za mkononi].”

“Thuluthi moja ya vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 20 wanapenda kuandika ujumbe katika simu badala ya kutumia namna nyinginezo za mawasiliano ya kuandika,” lasema gazeti The Guardian la London. Huenda kuandika ujumbe kukagharimu pesa kidogo kuliko kuzungumza kwa simu, lakini kuandika ujumbe huchukua wakati mrefu zaidi. Mieko asema: “Mtu anaponitumia ujumbe usemao ‘lala salama,’ mimi humjibu ‘lala salama.’ Halafu, mawasiliano huendelea kwa saa nzima. Ni mazungumzo ya kipuzi tu.”

Watu wengi wanaotumia simu za mkononi watashangaa wakihesabu wakati wanaotumia kuzungumza kwa simu kila mwezi. Teija, msichana mwenye umri wa miaka 19, asema: “Kwa watu wengi, badala ya kuwaokolea wakati, simu ya mkononi huwaibia wakati.” Hata kama hali zako zinakulazimu uwe na simu ya mkononi, ni muhimu kufikiria wakati unaotumia kuzungumza kwa simu.

Msichana Mkristo aitwaye Marja asema: “Katika makusanyiko ya Kikristo, vijana wengi huandikiana ujumbe usio na maana. Jambo hilo hutokea mara nyingi sana!” Tabia hiyo imeonekana pia wakati vijana wanapokuwa katika huduma ya Kikristo. Biblia huwahimiza Wakristo watafute wakati wa kufanya mambo ya kiroho. (Waefeso 5:16) Inahuzunisha kama nini ikiwa wakati huo unatumiwa kuzungumza kwa simu!

Mawasiliano ya Siri

Marie aeleza kuhusu mtego mwingine: “Kwa kuwa simu hupokewa moja kwa moja na mtu anayehusika, wala haipokewi nyumbani, kuna hatari ya wazazi kutojua watoto wao wanazungumza na nani au kama wanapiga simu au la.” Kwa hiyo vijana wengine hutumia simu kutafuta kisiri marafiki wa jinsia tofauti. Wengine wamekosa tahadhari, na kupuuza kanuni wanazopaswa kufuata wakati wanapowasiliana. Jinsi gani?

“[Vijana] wanapoandikiana ujumbe, hakuna awezaye kujua mambo ambayo yanaendelea,” lasema gazeti The Daily Telegraph la London. Mtu anaweza kuathiriwa kwa kuwa hamwoni wala kumsikia yule anayewasiliana naye. “Wengine huona kuandika ujumbe kuwa njia isiyo ya moja kwa moja ya kuwasiliana,” asema Timo. “Watu fulani wanaweza kuandika mambo ambayo hawawezi kumwambia mtu huyo moja kwa moja.”

Keiko, msichana Mkristo mwenye umri wa miaka 17, alipoanza kutumia simu ya mkononi, aliwapatia wengi wa marafiki zake namba yake. Muda si muda alianza kuwasiliana kila siku na mvulana mmoja wa kutaniko lao. Keiko asema: “Mwanzoni tulizungumza kuhusu mambo ya kawaida tu, lakini baadaye tulianza kuambiana matatizo yetu. Tulisitawisha uhusiano wa pekee kwa kutumia simu.”

Jambo zuri ni kwamba alipata msaada kutoka kwa wazazi wake na wazee Wakristo kabla ya kuingia katika matatizo makubwa. Sasa anasema: “Ingawa wazazi wangu walinionya kuhusu kuwasiliana na watu wa jinsia tofauti kabla ya kunipa simu ya mkononi, nilimtumia mvulana huyo ujumbe kila siku. Hiyo haikuwa njia nzuri ya kutumia simu.” *

Biblia hutuhimiza ‘tuwe na dhamiri njema.’ (1 Petro 3:16) Kama Koichi anavyosema, kufanya hivyo kunamaanisha kwamba unapotumia simu ya mkononi, hupaswi “kuwa na lolote la kuaibikia,” hata mtu mwingine akisoma ujumbe wako au kusikia mazungumzo yako. Sikuzote kumbuka kwamba huwezi kumficha Baba yetu wa mbinguni jambo lolote. Biblia hueleza: “Hakuna kiumbe kisichokuwa dhahiri machoni pa [Mungu], bali vitu vyote viko uchi na vikiwa vimefunuliwa wazi machoni pake ambaye kwake sisi tuna kutoa hesabu.” (Waebrania 4:13) Kwa nini basi tuwe na marafiki wa siri?

Jiwekee Mipaka

Iwapo umepanga kununua simu ya mkononi, chunguza hali zako kwa makini uone ikiwa kweli unaihitaji. Zungumzia jambo hilo pamoja na wazazi wako. Wengine wana maoni kama ya Jenna, anayesema: “Kuwa na simu ya mkononi ni daraka zito sana kwa vijana wengi.”

Hata ukiamua kuwa na simu ya mkononi, ni vizuri kudhibiti jinsi unavyoitumia. Jinsi gani? Kwa kujiwekea mipaka inayofaa. Kwa mfano, dhibiti idadi ya huduma unazotumia au muda na kiasi cha pesa unachotumia kupiga simu. Kwa sababu kampuni nyingi za simu hutoa orodha ya matumizi ya simu, chunguza orodha hiyo pamoja na wazazi wako mara kwa mara. Wengine hutumia njia za kulipa gharama mapema ili kudhibiti utumizi wao.

Pia, fikiria kwa makini wakati unaotumia na mambo unayosema na kuandika unapotumia simu. Jiwekee sheria zako mwenyewe zenye usawaziko. Shinji anaeleza: “Mimi husoma mara moja tu kwa siku ujumbe ambao nimepokea, na kujibu ule tu ambao ni muhimu. Kwa sababu hiyo marafiki wangu hunitumia ujumbe ambao ni muhimu peke yake. Isitoshe, iwapo kuna jambo la dharura, watanipigia simu.” Jambo muhimu hata zaidi ni kuteua watu ambao unawasiliana nao. Uwe mwangalifu kuhusu watu unaopatia namba yako ya simu. Tumia kanuni zilezile unazotumia kuchagua marafiki bora.—1 Wakorintho 15:33.

Biblia inasema: “Kwa kila jambo kuna majira yake, . . . wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena.” (Mhubiri 3:1, 7) Bila shaka, kuna wakati ambapo simu za mkononi zinapaswa pia “kunyamaza.” Wakati wa mikutano na huduma ya Kikristo ni “majira” ya kuabudu Mungu, si ya kuzungumza kwa simu. Wasimamizi wa mikahawa na majumba ya sinema huwaomba wateja wao wasitumie simu za mkononi na sisi hufuata maagizo yao. Bila shaka, Mwenye Enzi Kuu ya ulimwengu wote anastahili kuheshimiwa hata zaidi!

Watu wengine huzima simu wakati hawatarajii ujumbe muhimu, au hupunguza sauti wakati wanapofanya kazi muhimu. Wengine hata huiacha nyumbani. Je, si kweli kwamba ujumbe fulani unaweza kusomwa baadaye?

Iwapo umeamua kununua simu ya mkononi, azimia kudhibiti matumizi yako badala ya kuiruhusu ikudhibiti. Bila shaka, unahitaji kuwa macho na kutanguliza mambo ya maana zaidi. Biblia hutuhimiza: “Hali yenu ya kukubali sababu na ijulikane kwa watu wote.” (Wafilipi 4:5) Ukiamua kuwa na simu ya mkononi, jitahidi kuitumia kwa busara.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Baadhi ya majina yamebadilishwa.

^ fu. 7 Ili kupata habari zaidi kuhusu kazi za baada ya shule, tafadhali ona makala “Vijana Huuliza—Kuna Ubaya Gani Kuchuma Pesa?” katika gazeti la Amkeni! la Septemba 22, 1997.

^ fu. 18 Kuzungumza kwa ukawaida na mtu wa jinsia tofauti kwa simu au kutumiana ujumbe ni namna ya kutafuta uchumba. Tafadhali ona makala “Vijana Huuliza—Kuna Hatari Gani Mvulana na Msichana Wanapokutana Kirafiki?” katika gazeti la Amkeni! la Desemba 22, 2001.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Vijana wengine huendeleza urafiki wa siri kwa kutumia simu za mkononi