Michongo ya Alabasta Usanii wa Zamani wa Volterra
Michongo ya Alabasta Usanii wa Zamani wa Volterra
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
Hebu wazia bidhaa inayopatikana kiasili na inayoweza kutumiwa kutengeneza maumbo mbalimbali laini na yenye kupendeza—bidhaa yenye rangi mbalimbali maridadi, inayopitisha mwangaza, na inayoweza kutumiwa kutengeneza michongo bora sana ya aina mbalimbali. Hiyo ni bidhaa gani?
NI ALABASTA. Hatukujua mengi sana kuhusu jiwe hilo kabla ya kutembelea jiji la Volterra la Watuskan nchini Italia, ambapo lilichimbwa tangu zamani.
Jiji la Volterra linajulikana sana kwa michongo ya alabasta. Waetruria ambao walikuwa wenyeji wa kwanza wa jiji hilo walianzisha michongo hiyo. Baadhi ya vyombo vilivyotupendeza katika chumba cha vitu vya kale cha eneo hilo ni mamia ya masanduku yenye umbo la mstatili yaliyoundwa kwa alabasta ambamo majivu ya wafu yaliwekwa baada ya kuteketezwa na masanduku hayo kuzikwa. Masanduku hayo ni ya kutoka karne ya nne hadi ya kwanza K.W.K., na yamepambwa kwa michoro inayoonyesha ulimwengu ambao mfu anadhaniwa kuwa ameenda.
Bila shaka, sio Waetruria peke yao waliotumia alabasta katika nyakati za kale. Wamisri pia waliitumia sana. Hata hivyo, alabasta hiyo kutoka nchi za mashariki—ambayo pia imetajwa katika Biblia—inatofautiana na ile ya Volterra ambayo ni nyororo na ni kama chokaa.
Marumaru pia ilitumiwa sana katika usanii wa kale huko Ugiriki na Roma, lakini alabasta inayofanana na chokaa ilionwa kuwa duni sana ikilinganishwa na mawe hayo ya “hali ya juu.” Jiwe la alabasta ni jepesi, linaweza kupasuka haraka, kukwaruzwa kwa urahisi, hivyo vitu vya ujenzi na sanaa vilivyotengenezwa kwa jiwe hilo huonwa vikiwa vya hali ya chini vikilinganishwa na vile vilivyoundwa kwa marumaru. Vitu vilivyotengenezwa kwa alabasta huharibika vinapowekwa nje. Alabasta hutumiwa hasa katika sehemu za ndani za jengo. Lakini kwa sababu inaweza kufinyangwa kwa urahisi, alabasta hutumiwa kutengeneza mapambo madogo-madogo.
Usitawi wa Viwanda vya Alabasta
Hakuna uthibitisho wowote unaoonyesha kwamba alabasta ilitengenezwa huko Volterra karne nyingi baada ya Waetruria na Waroma. Hata hivyo, rekodi za kale zinaonyesha kwamba usanii huo ulikuwapo katikati ya karne ya 16. Wakati huo, mkuu wa Tuscany, Francesco de’ Medici, alinunua chombo maridadi cha kuwekea maua kilichotengenezwa kwa mashine kutoka kwa msanii wa Volterra na kumpa kiongozi wa Bavaria. Katika karne ya 17, wasanii walitengeneza vitu vingi vya sanaa na mapambo madogo ya aina mbalimbali. Kazi hiyo ya sanaa ilisitawi sana katika karne ya 18, wakati michongo ya vitu vya kale vya Wagiriki na Waroma ilipotengenezwa. Kufikia wakati huo, michongo ya alabasta
ya Volterra ilikuwa inajulikana sana kotekote Ulaya na kwingineko.Katika kipindi hicho, Marcello Inghirami Fei, aliyejulikana kwa kipawa chake cha kutengeneza vitu vya sanaa na uhodari wake katika biashara, alisaidia kusitawisha biashara ya vyombo vya alabasta. Alianza kuchimba alabasta katika maeneo mapya yaliyokuwa yamegunduliwa, na mnamo mwaka wa 1791 akaanzisha shule ya kufundisha sanaa hiyo. Zaidi ya wanafunzi 100 walifunzwa na wasanii stadi kutoka maeneo ya Italia na nchi nyinginezo. Hivyo biashara hiyo ikasitawi sana.
Vile viwanda vinane au tisa hivi vya alabasta vilivyokuwapo katika mwaka wa 1786 viliongezeka hadi 60 kufikia mwaka wa 1830. Katika miaka hiyo, karibu wafanya-biashara 50 kutoka Volterra, walitembelea masoko ya kimataifa huko Ulaya, Amerika, India, na nchi nyingine za Asia wakiuza bidhaa za hali ya juu za alabasta. Wengi walipata pesa nyingi. Ufanisi huo uliendelea hadi mwaka wa 1870, lakini tangu wakati huo biashara hiyo imekuwa ikipanda na kushuka. Hata hivyo, utengenezaji wa vyombo vya alabasta umekuwa mojawapo ya nguzo za uchumi wa Volterra.
Kutalii Volterra Wakati wa Alasiri
Volterra ina mazingira ya kipekee kwani ina barabara na nyumba za mawe, kona zenye picha maridadi, bustani nyangavu, na imezungukwa na veranda zenye kupendeza. Ni kana kwamba tumerudi katika Zama za Kati. Alasiri moja wakati wa kiangazi tunatembea pamoja na marafiki kupitia lango lililopindwa na lenye kupendeza la Porta all’Arco lililotengenezwa na Waetruria katika karne ya nne K.W.K., ambalo ni sehemu ya kuta za jiji zilizojengwa katika zama za kati.
Tunafurahia kutembea kando ya maduka tukitazama kwa mshangao michongo ya makundi ya ndege wanaoruka, farasi wanaokwenda kwa mwendo taratibu, na watu waliochongwa vizuri. Michongo hiyo ilitengenezwa kwa alabasta lakini ni miangavu kwa sababu ya kioo ambacho kimefunika madirisha hayo. Vyumba vyenye dari zilizopindwa vinatumiwa kuonyesha vyombo maridadi sana vya kuwekea majivu ambavyo vimepambwa kwa mizabibu yenye matunda na sanamu za mandhari ya kale ya Ugiriki na Roma, vyombo vya kuwekea maua vilivyopambwa sana, mishumaa, vifaa vya kuchezea chesi, vyombo vya kuweka vito, na mapambo mengine mengi.
Wanapoona upendezi wetu, marafiki zetu wanatupeleka kwenye viwanda vya alabasta vilivyojaa vumbi ili tujionee jinsi wasanii wanavyounda vyombo hivyo vyenye kupendeza. Tunaambiwa kwamba miamba yenye umbo la yai, ya uzani wa kilogramu 2 hadi 1,000, inapatikana kotekote chini ya ardhi yenye chokaa ya Volterra. Mawe ya alabasta huchimbuliwa kutoka kwa mashimo yaliyo wazi yenye kina cha meta 280. Alabasta hiyo ina rangi tofauti-tofauti kama vile rangi nyeupe-nyangavu, rangi ya pembe ya ndovu, rangi ya manjano, rangi nyekundu, kahawia-nyeusi, rangi ya kijivu-kijani na rangi nyeusi. Nyingi kati ya rangi hizo zina mpangilio mbalimbali na hali mbalimbali za kutopenyeza mwanga.
Katika viwanda mbalimbali vya alabasta ambavyo tunatembelea, wasanii wanatumia mbinu mbalimbali. Tunakutana na Gloria ambaye anatia mapambo mbalimbali kwenye sahani ya alabasta, na Franco, anayetia mapambo kwa kutumia mashine. Mbinu hiyo hutumiwa kutengeneza vitu vingi vya mviringo, kama sahani, mabakuli, na vifuniko vya taa—ambavyo vinafaa kutengenezwa kwa alabasta kwa sababu inapitisha mwanga. Vifaa vya kufanya kazi hiyo vimewekwa kiholela-holela—tupa za aina mbalimbali, nyundo za mawe na patasi, vifaa vya kukata na kutengeneza maumbo, misasa, na sanamu za binadamu ambazo hazijakamilika. Tunaambiwa kwamba sanamu za binadamu na wanyama ambazo zimetapakaa kila mahali hutumiwa kama vigezo vya kutengeneza michongo ya aina yake.
Ungaunga mweupe wa alabasta umetapakaa kila mahali. Lakini ungaunga huo una matumizi yake. Visanamu vingi vidogo-vidogo hutengenezwa kwa kuweka mchanganyiko wa ungaunga wa alabasta na utomvu wa plastiki kwenye kalibu—lakini wasanii hao wanasema kwamba visanamu hivyo si sawa na michongo halisi inayofanywa kwa mikono.
Mjadala Unaopendwa
Inasemekana kwamba wenyeji wa Volterra wanapenda sana alabasta, na tunapoanza kuzungumza na wasanii wachangamfu inathibitika wazi kwamba kuna mjadala fulani wanaoupenda kuhusu sanaa yao ya tangu zamani. Wengine wanasisitiza kwamba bidhaa duni za bei nafuu zinaharibu sifa njema ya bidhaa zao zilizokuwa maarufu hapo zamani. Wanasema kwamba bidhaa duni zinaharibu soko, lakini kuna wale wanaosema bado kuna wateja wengi wanaotaka kununua bidhaa za hali ya juu za sanaa na mapambo. Mjadala huo si mpya, na bado unaendelea. Bila shaka kuna mashindano makali katika biashara na shughuli nyingi za wanadamu, na yaonekana hali hiyo itaendelea kuwapo.
Hata hivyo, jambo moja ni hakika. Ustadi wa usanii ambao wanadamu walipewa na Muumba wao utadumu milele. Usanii tuliojionea tulipotembelea Volterra ni mojawapo ya stadi ambazo watu wote walio hai wataweza kuziboresha kikamili watakapoona utimizo wa unabii huu wa Yehova Mungu: “Wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.”—Isaya 65:22.
[Picha katika ukurasa wa 26]
1. Mawe ya alabasta yanachimbuliwa kutoka kwa mashimo yenye kina cha meta 280. 2. Msanii akipamba chombo cha kuwekea maua cha alabasta kwa kutumia mashine. 3. Chombo maridadi cha alabasta cha kuwekea majivu. 4. Mchongo wa kisasa wa alabasta