Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, UKIMWI Utakomeshwa? Ikiwa Ndivyo, Jinsi Gani?

Je, UKIMWI Utakomeshwa? Ikiwa Ndivyo, Jinsi Gani?

Je, UKIMWI Utakomeshwa? Ikiwa Ndivyo, Jinsi Gani?

KWA miaka kadhaa watu katika nchi nyingi za Afrika wamepinga kuwepo kwa ugonjwa wa UKIMWI. Watu fulani hata hawataki kuzungumza juu yake. Hata hivyo, katika miaka ya hivi majuzi, jitihada zimefanywa kuwatia watu moyo kuzungumza waziwazi kuhusu ugonjwa huo na kuwaelimisha vijana hasa. Jitihada hizo hazijafaulu sana. Watu wamejikita katika maisha na desturi zao, na ni vigumu kuleta mabadiliko.

Maendeleo ya Tiba

Kwa habari ya tiba, wanasayansi wamejifunza mengi kuhusu virusi vya UKIMWI na kuvumbua dawa ambazo zimerefusha maisha ya watu wengi. Dawa tatu za kuzuia utendaji wa virusi zimetumiwa pamoja kwa mafanikio.

Ijapokuwa dawa hizo haziponyi UKIMWI, zimepunguza idadi ya vifo vya watu wenye virusi vya UKIMWI, hasa katika nchi zilizoendelea. Watu wengi wanasisitiza kwamba ni muhimu dawa hizo zipelekwe katika nchi zinazoendelea. Hata hivyo, dawa hizo ni ghali, na watu wengi katika nchi hizo hawawezi kuzigharimia.

Jambo hilo limezusha suala hili: Je, faida za kifedha ni muhimu kuliko uhai wa wanadamu? Dakt. Paulo Teixeira, mkurugenzi wa mradi wa Brazili wa kupambana na UKIMWI, aliunga mkono wazo hilo aliposema hivi: “Hatuwezi kuacha maelfu ya watu waumie kutokana na kukosa dawa eti kwa sababu ya faida za kifedha ambazo zinazidi zile zinazopatikana kwa ukawaida.” Aliongeza hivi: “Ninasisitiza sana kwamba faida za kifedha hazipasi kuonwa kuwa muhimu kuliko maadili na wanadamu.”

Nchi kadhaa zimeamua kutengeneza dawa zisizokuwa na jina rasmi na kuziuza kwa bei ya chini katika nchi nyingine, hivyo zikipuuza sheria za kuzuia uigaji wa dawa zinazotengenezwa na makampuni fulani makubwa. * Uchunguzi mmoja ulioripotiwa katika jarida la South African Medical Journal unaonyesha kwamba “bei za chini kabisa [za dawa hizo zisizokuwa na jina rasmi] zilikuwa asilimia 82 chini ya bei za kawaida za Marekani.”

Matatizo ya Matibabu

Baada ya muda, yale makampuni makubwa yenye kibali cha kutengeneza dawa yalianza kuuzia nchi zinazoendelea dawa za UKIMWI kwa bei ya chini zaidi. Kwa kufanya hivyo, ilitumainiwa kwamba watu wengi zaidi wangefaidika kutokana na dawa hizo. Hata hivyo, kuna matatizo mengi makubwa yanayopasa kusuluhishwa ili dawa hizo zipatikane kwa urahisi katika nchi zinazoendelea. Tatizo moja ni gharama. Hata baada ya bei ya dawa hizo kupunguzwa sana, bado watu wengi wanaozihitaji hawawezi kuzigharimia.

Tatizo jingine ni kwamba si rahisi kutoa dawa hizo kwa kiwango kinachofaa. Tembe nyingi zinapasa kumezwa kila siku kwa wakati maalum. Dawa hizo zisipotumiwa ipasavyo au zikiacha kutumiwa, hilo linaweza kufanyiza virusi sugu vya UKIMWI ambavyo hukinza dawa. Katika mazingira ya Afrika, ni vigumu kuhakikisha kwamba wagonjwa wanatumia kiwango kinachofaa cha dawa mahali ambako hakuna chakula cha kutosha, maji safi, na hospitali za kutosha.

Isitoshe, wale wanaotumia dawa hizo wanapaswa kupewa uangalifu. Dawa hizo zapasa kubadilishwa zinapoacha kufanya kazi mwilini. Ili kufanya hivyo, wafanyakazi stadi wa huduma za afya wanahitajiwa, na kupimwa kunagharimu pesa nyingi sana. Vilevile, dawa hizo zina athari zake, na virusi fulani sugu vya UKIMWI vimeanza kukinza dawa.

Kwenye kongamano maalum kuhusu UKIMWI lililofanywa Juni 2001 na Baraza Kuu la UM, ilipendekezwa kwamba kuwe na Hazina ya Afya ya Ulimwenguni Pote ya kusaidia nchi zinazoendelea. Ilikadiriwa kwamba kati ya dola bilioni 7 na bilioni 10 za Marekani zinahitajika. Kufikia sasa, jumla ya fedha ambazo wameazimia kuchanga hazijafikia kiasi kinachotakikana.

Wanasayansi wana matumaini makubwa ya kupata chanjo, na chanjo tofauti-tofauti zinajaribiwa katika nchi mbalimbali. Hata jitihada hizo zikifua dafu, miaka kadhaa itapita kabla ya chanjo kupatikana, kujaribiwa, na kuthibitishwa kuwa salama kwa ajili ya matumizi ya umma.

Nchi fulani kama vile Brazili, Thailand, na Uganda, zimefanikiwa sana katika miradi ya matibabu. Dawa zinazotengenezwa huko Brazili zimetumiwa nchini humo kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na UKIMWI kwa asilimia 50. Botswana, ambayo ni nchi ndogo yenye uwezo wa kifedha, inajitahidi kutoa dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI kwa wote wanaozihitaji na vilevile kuandaa huduma za afya.

Kukomeshwa kwa UKIMWI

UKIMWI unatofautiana na magonjwa mengine ya kuambukiza katika jambo hili muhimu: Unaweza kuzuiwa. Iwapo watu wako tayari kufuata kanuni za Biblia za msingi, wengi wao, au hata wote, wanaweza kuepuka kuambukizwa.

Kanuni za Biblia kuhusu maadili ziko wazi. Wale ambao hawajafunga ndoa hawapaswi kufanya ngono. (1 Wakorintho 6:18) Wenzi wa ndoa wanapaswa kuwa waaminifu kwa wenzi wao na hawapaswi kufanya uzinzi. (Waebrania 13:4) Pia, kutii shauri la Biblia kuhusu kujiepusha na damu ni ulinzi.—Matendo 15:28, 29.

Kwa kujifunza kuhusu ulimwengu usio na magonjwa ambao Mungu anaahidi utakuwepo hivi punde na kwa kutimiza matakwa ya Mungu, wale ambao wamekwisha kuambukizwa wanaweza kupata shangwe nyingi na faraja.

Biblia inatuhakikishia kwamba hatimaye dhiki zote za wanadamu, kutia ndani magonjwa, zitakwisha. Ahadi hiyo inapatikana katika kitabu cha Ufunuo: “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha ufalme ikisema: ‘Tazama! Hema la Mungu liko pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao, nao watakuwa vikundi vya watu wake. Na Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala ombolezo wala kupaaza kilio wala umivu halitakuwapo tena kamwe. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.’”—Ufunuo 21:3, 4.

Ahadi hiyo hakika si kwa wale tu wanaoweza kugharimia matibabu ya pesa nyingi. Uhakika wa ahadi hiyo ya kiunabii ya Ufunuo sura ya 21 unaimarishwa na andiko la Isaya 33:24: “Hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” Kisha, wote wanaoishi duniani watafuata sheria za Mungu na kufurahia afya kamilifu. Hivyo, ugonjwa hatari wa UKIMWI na magonjwa mengine yote yatakomeshwa kabisa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Dawa hizo hutengenezwa kwa kuiga zile zinazotengenezwa na makampuni yaliyo na kibali cha kuzitengeneza. Katika hali za dharura, nchi ambazo ni sehemu ya Shirika la Biashara Ulimwenguni zinaweza kupuuza sheria hizo kuhusu utengenezaji wa dawa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9, 10]

HIYO NDIYO DAWA NILIYOKUWA NIKITAFUTA

Ninaishi kusini mwa Afrika, na nina umri wa miaka 23. Ninakumbuka siku niliyogundua kwamba nina virusi vya UKIMWI.

Nilikuwa pamoja na mamangu katika chumba cha daktari wakati daktari alipotueleza habari hiyo. Sijawahi kamwe kupata habari mbaya kama hiyo. Nilivurugika. Sikuamini jambo hilo. Nilidhani kwamba huenda matokeo ya maabara yalikuwa na kasoro. Nilipumbaa. Nilitaka kulia, lakini machozi hayakutoka. Daktari alianza kumweleza mamangu kuhusu dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI na mambo mengine, lakini nilikuwa nimeduwaa sana kiasi cha kwamba sikuelewa jambo lolote.

Nilitambua kuwa labda niliambukizwa na mtu fulani katika chuo kikuu. Nilitaka sana kuongea na mtu yeyote ambaye angeelewa hali yangu, lakini sikujua nizungumze na nani. Nilihisi kuwa sifai na kwamba maisha yangu yameharibika. Ingawa nilitegemezwa na familia yetu, nilikata tamaa na kuogopa sana. Kama ilivyo na vijana wote, nilikuwa na matumaini mengi mno maishani. Ningehitimu kwa digrii ya sayansi baada ya miaka miwili tu, lakini matumaini hayo yalididimia.

Nilianza kutumia dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI na kwenda kupata ushauri kuhusu ugonjwa huo, lakini bado nilishuka moyo. Nilimwomba Mungu anionyeshe Ukristo wa kweli kabla sijafa. Nilikuwa mshiriki wa kanisa moja la Pentekoste, lakini hakuna hata mshiriki mmoja aliyenitembelea. Nilitaka kujua ukweli kuhusu mahali ambapo ningeenda baada ya kifo.

Asubuhi moja mwanzoni mwa Agosti 1999, Mashahidi wa Yehova wawili walibisha mlango wangu. Nilikuwa mgonjwa sana siku hiyo, lakini niliweza kuketi sebuleni. Wanawake hao wawili waliniambia majina yao na kusema kwamba wanawasaidia watu kujifunza Biblia. Nilifarijiwa sana kuona sala zangu zikijibiwa hatimaye. Lakini kufikia wakati huo nilikuwa mnyonge sana hivi kwamba singeweza kusoma wala kukaza fikira kwa muda mrefu.

Hata hivyo, niliwaeleza kwamba ningependa kujifunza Biblia, na wakaahidi kurudi. Lakini kwa kusikitisha, kabla ya wakati huo, nilipelekwa kwenye hospitali ya magonjwa ya akili kwa sababu ya kushuka moyo. Majuma matatu baadaye, niliondoka hospitalini na nilifarijiwa sana kuona kwamba bado Mashahidi hao walinikumbuka. Nakumbuka kwamba mmoja wao aliendelea kunijulia hali. Nilipata nafuu kwa kadiri fulani, na nikaanza kujifunza Biblia mwishoni-mwishoni mwa mwaka huo. Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi kwani nilikuwa mgonjwa mara kwa mara. Lakini yule aliyejifunza nami alielewa na alikuwa mwenye subira.

Nilisisimuka sana nilipojifunza kuhusu Yehova na sifa zake katika Biblia, na pia maana ya kumjua na kutarajia uhai wa milele. Kwa mara ya kwanza, nilielewa pia kwa nini wanadamu huteseka. Nilipata shangwe nyingi nilipojifunza kuhusu Ufalme wa Mungu, ambao hivi punde utachukua mahali pa serikali zote za wanadamu. Hilo lilinichochea kubadili maisha yangu kabisa.

Hiyo ndiyo dawa niliyokuwa nikitafuta. Nilifarijika sana kujua kwamba Yehova bado ananipenda na kunijali! Hapo awali, nilifikiri kwamba Mungu ananichukia na ndiyo sababu niliambukizwa ugonjwa huo. Lakini nilijifunza kwamba Yehova alifanya mpango kwa upendo ili tusamehewe dhambi kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu Kristo. Nikajua kwamba Mungu kweli anajali, kama vile 1 Petro 5:7 inavyosema: ‘Tupeni hangaiko lenu lote juu yake, kwa sababu yeye huwajali nyinyi.’

Kwa kujifunza Biblia kila siku na kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme, ninajitahidi niwezavyo kumkaribia Yehova zaidi. Ijapokuwa si rahisi sikuzote, mimi humtupia Yehova mahangaiko yangu kupitia sala na kumwomba nguvu na faraja. Washiriki wa kutaniko hunitegemeza pia, kwa hiyo nina furaha.

Mimi huhubiri kwa ukawaida pamoja na kutaniko letu. Ninataka kuwasaidia wengine kiroho, hasa wale wanaokabili hali sawa na yangu. Nilibatizwa mnamo Desemba 2001.

[Picha]

Nilipata shangwe nyingi nilipojifunza kuhusu Ufalme wa Mungu

[Picha katika ukurasa wa 8]

Kikundi cha watu wanaotoa mashauri kuhusu UKIMWI huko Botswana

[Picha katika ukurasa wa 10]

Katika dunia Paradiso, watu wote watafurahia afya kamilifu