Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Unajua Tofauti?

Je, Unajua Tofauti?

Je, Unajua Tofauti?

“Chombo hicho ni piano!” “La, nafikiri ni synthesizer.” “Bila shaka ni kinanda!” “La, nyote mmekosea, ni kinubiuzi.” Basi chombo hicho ni kipi?

BILA shaka, kibodi za vyombo vyote hivyo vya muziki zinafanana sana. Lakini sauti za vyombo hivyo na namna vinavyochezwa ni tofauti kabisa. Basi kibodi ilianzaje kutumiwa? Hebu tuchunguze historia yake ya miaka mingi.

Hydraulus Ilikuwa Nini?

Yaaminika kibodi ya kwanza kutumiwa ilikuwa ya chombo kilichoitwa hydraulus, yaani, “kinanda cha maji.” Inadhaniwa kuwa chombo hicho kilitengenezwa na mhandisi wa Alexandria, kwa jina Ktesibios, katika nusu ya kwanza ya miaka ya 200 K.W.K. Kulingana na kitabu Musical Instruments of the West, “hewa ilipulizwa . . . katika chombo chenye mashimo (pnigeus) kilichowekwa ndani ya mtungi wa maji. Hewa hiyo iliingia katika sehemu ya kuhifadhi hewa iliyokuwa chini ya filimbi [nyingi], na maji yalisukuma hewa hiyo daima.” Vibonyezo vikubwa vilitumiwa ili kutokeza sauti kwenye filimbi. Kwa kuwa kilitoa sauti kubwa na nzito, chombo hicho kilifaa kutumiwa katika maonyesho ya sarakasi na burudani, na katika sherehe kubwa za muziki zilizofanyiwa nje. Kilikuwa maarufu sana wakati wa utawala wa Milki ya Roma, na inasemekana Maliki Nero mwenyewe alicheza chombo hicho cha muziki kwa ustadi.

Mbona Kinanda cha Kupuliza Kilipendwa?

Badala ya chombo cha maji, chombo cha kupuliza kilianza kutumiwa, na huo ukawa mwanzo wa enzi ya kinanda cha kupuliza. Kwa kutumia chombo cha kupuliza mchezaji angeweza kuketi juu yake na kufungulia hewa kwa miguu au mikono. Mabaki ya vyombo vya kupuliza ambayo yamepatikana ardhini yameonyesha kwamba vilitumiwa katika miaka ya 200 W.K., na viliendelea kutumiwa sana kwa mamia ya miaka baadaye. Kibodi hizo zilikuwa duni sana na sauti zake zilikuwa za mwendo wa polepole. Hiyo ilikuwa kwa sababu ukubwa wa vibonyezo ulipasa kupatana na ukubwa wa filimbi. Ili kutoa noti ya chini, ilimbidi mchezaji atumie mkono mzima au hata ngumi ili kufinya kibonyezo hicho kipana.

Kufikia miaka ya 1300, kinanda kilitumiwa “hasa makanisani huko Ulaya magharibi.” (The Encyclopedia of Music) Ufundi wa rola ulibadili muundo na utumizi wa kibodi ya kinanda. Rola iliwezesha filimbi kuundwa zikiwa mbali na kibodi na vibonyezo vyembamba vilitumiwa. Hatimaye, kwa kutumia kidole kimoja kwa kila kibonyezo, mchezaji angecheza muziki vizuri na kwa haraka. Mozart alipenda kinanda sana hivi kwamba alikiita mfalme wa vyombo vya muziki.

Kibodi za Mapema za Nyuzi

Biblia inataja vyombo vya nyuzi kwa mara ya kwanza katika Mwanzo 4:21, na pia kuhusiana na taifa la Israeli. Lakini ni katika miaka ya 1400 W.K. ambapo vyombo vya nyuzi (vilivyochezwa kwa kutumia vidole au chombo kingine) vilipounganishwa na kibodi. Kibodi ya leo ilitumiwa kwanza katika aina fulani ya marimba. Ilikuwa sahili yenye muundo wa sanduku lenye nyuzi zilizofungwa kutoka kushoto hadi kulia. Mchezaji alipofinya kibonyezo, kipande cha shaba nyeupe kiligonga uzi uliokuwa juu yake.

Halafu kukatokea kinubiuzi, ganuni, na virginal. * Vyombo hivyo, hasa kinubiuzi, vilikuwa maarufu kati ya vyombo vya kibodi katika miaka ya 1500 na 1600. Mbinu hiyo mpya ya kinubiuzi ilileta mabadiliko makubwa. Kitabu The History of Musical Instruments chaeleza: “Tofauti na marimba ambayo ilikuwa na kipande cha chuma kilichopiga nyuzi, ilichezwa kwa kipande cha chuma, au unyoya ndiyo uliotumiwa kuzigonga. Upande wa nyuma wa kila kibonyezo ulikuwa na kipande kidogo cha mbao kilichokuwa wima, ambapo palikuwa na unyoya mdogo au kipande chembamba cha ngozi. . . . Kibonyezo kilipofinywa, kipande cha mbao kiliruka na unyoya ukagonga uzi, halafu kilirudi mahali pake bila kuugonga tena.”

Kinubiuzi kilichotengenezwa kwa kutumia mbinu hiyo mpya kilitoa sauti ya kipekee. Mmoja aliyecheza piano katika sherehe alieleza tofauti iliyokuwapo kati ya sauti ya kinubiuzi na ile ya piano ya kisasa aliposema hivi: “Kina sauti nyembamba na nzito, na noti zake ni fupi.”

Muundo wa kinubiuzi ulibadilika sana kadiri miaka ilivyopita. Vinubi vya mapema vilikuwa na kibodi moja na kila kibonyezo kiliunganishwa na uzi mmoja tu. Baadaye, vinubi vingine vya hali ya juu vilikuwa na kibodi mbili, nyuzi kadhaa kwa kila kibonyezo, na vifaa vingine vya kuboresha sauti. Watungaji wa muziki mashuhuri wa wakati huo kama Johann Sebastian Bach (1685-1750) na Domenico Scarlatti (1685-1757), walitumia vinubi hivyo vyenye sauti bora na vya hali ya juu kucheza muziki mtamu sana, na mwingine hutumiwa hadi leo.

Kodiani zilibuniwa katika miaka ya 1800, na kodiani ya piano ilitumiwa hasa katika miaka ya 1900. Kodiani hiyo ina kibodi na vyombo vya kupuliza pia. Kodiani ya kisasa ina sauti nzito 140 ambazo hutokana na vibonyezo vilivyopangwa katika mistari saba na kibodi yenye vikundi viwili hadi vinne vya noti nane.

Enzi ya Vyombo vya Elektroni

Kibodi za elektroni zilibuniwa katika miaka ya 1900. Katika mwaka wa 1906, Thaddeus Cahill alibuni chombo cha elektroniki kilichoitwa telharmonium. Vinanda vinavyotumia umeme vilianza kutumiwa katika miaka ya 1930 na vilifuatwa muda mfupi baadaye na vinubi na piano za umeme. Tofauti kabisa na chombo cha hydraulus, kibonyezo cha kinanda cha umeme hutoa noti kwa kutumia umeme na sauti hiyo huboreshwa na kuongezwa.

Chombo kimoja cha muziki kinachotumiwa sana leo ni synthesizer. Kilianza kubuniwa katika miaka ya 1940 na bendi nyingi za kisasa na vikundi vya muziki hukitumia sana. Chombo hicho hutoa aina nyingi za sauti—kutia ndani sauti ya mbwa anayebweka na sauti aina tofauti-tofauti za okestra.

Si ajabu kwamba kompyuta hutumiwa kucheza muziki wa kisasa. Mara nyingi synthesizer za kisasa hutumia kompyuta, au kompyuta inaweza kutumiwa kutoa sauti, na hivyo kompyuta hutumiwa kama chombo cha muziki. Ingawa mara nyingi kibodi ya muziki hutumiwa kuendesha kompyuta, wanamuziki wa leo wanaweza pia kutumia usukani wa kompyuta (mouse) au kibodi ya kompyuta kutunga muziki kwenye kompyuta. “Leo karibu studio zote za kurekodi muziki zina vifaa vingi vya kompyuta. Muziki huhifadhiwa katika kompyuta, kisha sauti huchanganywa kwa kutumia programu za hali ya juu za kompyuta, kabla ya kurekodiwa katika ukanda wa kompyuta.”—The Encyclopedia of Music.

Je, maendeleo yote hayo yatafanya kibodi ya muziki iache kutumiwa? Haielekei kuwa hivyo ukizingatia jinsi ambavyo wanamuziki kama Beethoven huelezea hisia zao kwa urahisi katika muziki kama ule unaoitwa “Moonlight Sonata” na “Für Elise,” ama mwanamuziki Debussy katika “Clair de Lune.” Lakini ukifikiri kuhusu mamia ya miaka ambayo muziki wa kibodi umetumiwa na jinsi umeathiri mamilioni ya watu, hatuna budi kukubali kwamba umetoa mchango mkubwa katika ulimwengu wa muziki na umewatumbuiza watu kwa karne nyingi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Chombo cha virginal kilitumiwa kuanzia miaka ya 1400 na kilikuwa na nyaya 32. Kilifanana na marimba lakini kilitoa sauti kama ya kinubiuzi. Ganuni ilikuwa aina ndogo ya kinubiuzi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 20, 21]

Jinsi Piano Ilivyobuniwa

Kati ya mwaka wa 1775 na 1800, kinubi kiliacha kutumiwa pole kwa pole na badala yake kibodi iliyopendwa zaidi ilianza kutumiwa, yaani pianoforte, au kama inavyojulikana sana, piano. Jina hilo lilitoka wapi? Bado haijulikani ni nani aliyebuni chombo hicho na wakati kilipobuniwa, lakini Mwitaliano Bartolomeo Cristofori alikifanyia majaribio mapema katika miaka ya 1700. Jina ambalo Cristofori alikipatia, gravicembalo col piano e forte (kinubi kinachotoa sauti ya chini na ya juu), lilikazia faida moja ambayo ilikifanya kiwe bora kuliko kinubi, yaani jinsi mchezaji alivyoweza kucheza muziki wa sauti tofauti-tofauti. Mtu alipofinya kibonyezo cha pianoforte, kigongeo kiligonga uzi mara moja kutoka chini. Mchezaji angeweza kubadili sauti ya noti kwa kutumia kibonyezo. Kwa hiyo, angeweza kuwasilisha hisia zake katika muziki kwa urahisi na pia angecheza muziki wenye sauti ya chini (piano) au ya juu (forte).

Pia, aina tatu za noti zingeweza kuchezwa kwa kukawiza kidole kwenye vibonyezo. Kwa hiyo, sauti zingechezwa kwa kuendelea, sauti nyingi zingechezwa kwa wakati mmoja, na hata kupunguzwa.

Piano iliendelea kuimarishwa na kuboreshwa katika miaka ya 1700 huko Ulaya. Mapema katika miaka ya 1740, piano ya miraba minne iliyokuwa ndogo na rahisi kutumia ilibuniwa. Piano kubwa huchukua nafasi kubwa kwa sababu ina nyuzi fupi na ndefu zilizolala. Mwanzoni mwa miaka ya 1800, piano iliyo wima ilibuniwa, na inaendelea kutumiwa hata leo.

Amkeni! lilimwuliza mchezaji mmoja wa piano tofauti iliyopo kati ya piano kubwa na piano iliyo wima. Alisema: “Sauti yake ni safi, wazi, na bora. Piano kubwa hutoa sauti nyingi za kila aina. Hiyo hutoa sauti iliyo wazi na yenye nguvu. Piano iliyo wima hutoa sauti laini ikilinganishwa na ile nyingine. Hiyo ni kwa sababu mara nyingi piano iliyo wima huegemezwa ukutani, na hivyo kiasi cha sauti hupungua.”

[Picha]

Piano kubwa yenye urefu wa meta 2.7

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kutumia “virginal” bustanini, 1666, Uingereza

Kinubiuzi kilichotengenezwa kwa koa la kobe (picha ndogo), 1760, Ujerumani

Marimba, 1906, Marekani

Kodiani ya piano, 1960, Italia

“Synthesizer” ya kisasa na kompyuta

[Hisani]

Picha nne zilizo juu: Courtesy of the Yale University Collection of Musical Instruments

[Picha katika ukurasa wa 19]

“Hydraulus”

[Hisani]

Courtesy Macedonian Heritage

[Picha katika ukurasa wa 19]

Kinanda cha kupuliza, Nyumba ya Opera ya Sydney, Australia

[Hisani]

By courtesy of Australian Archives, Canberra, A.C.T.