Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Matetemeko ya Ardhi Nilisoma mfululizo wa makala “Masimulizi ya Waokokaji wa Tetemeko la Ardhi.” (Machi 22, 2002) Kwenye makala hiyo mlinukuu chanzo kimoja kilichosema kwamba “matetemeko ya ardhi ya ukubwa wa 7.0 au zaidi kwenye kipimo cha Richter ‘hayakuongezeka sana’ katika karne yote ya 20.” Hata hivyo, kichapo cha World Almanac cha 1999 chasema kwamba kulikuwa na ongezeko kubwa la matetemeko ya ardhi katika miaka ya 1990.
F. A., Italia
“Amkeni!” linajibu: Bila kupendelea upande wowote, makala yetu ilionyesha jinsi baadhi ya wataalamu wa matetemeko ya ardhi wanavyosema kuhusu ukubwa wa matetemeko ya ardhi kwa ujumla katika karne ya 20. Makala hiyo ilisema kwamba ingawa wengine wanaamini kwamba idadi ya matetemeko ya ardhi ‘haikuongezeka sana,’ unabii wa Yesu katika Mathayo sura ya 24 unatimizwa wakati wetu. Yesu alisema kwamba kungekuwa na “matetemeko makubwa ya dunia.”—Luka 21:11.
Kuharibika kwa Mimba Nilipoona makala “Mimba Yangu Iliharibika” (Machi 22, 2002), machozi yalinitoka nilipokumbuka mtoto wetu aliyekufa kabla ya kuzaliwa. Papo hapo nilimshukuru Yehova kwa kuandaa habari hiyo muhimu sana na faraja. Inafariji kujua kwamba katika ulimwengu mpya wa Mungu, hakuna mtu atakayepatwa na tatizo hilo.
J. S., Marekani
Nilimzaa mtoto wangu akiwa amekufa katika juma la 30. Hilo lilikuwa tukio baya zaidi maishani mwangu. Makala hiyo ilikuwa msaada mkubwa na faraja kwangu, kwa kuwa ilizungumzia jambo ambalo mara nyingi huonwa kuwa mwiko, na pia ilitoa ushauri mzuri.
K. W., Ujerumani
Mtoto wangu pia alikufa kabla ya kuzaliwa. Nilijifanya kutohisi kitu. Lakini moyo wangu ulikuwa na maumivu makali na singeweza kufarijiwa na jambo lolote. Nililia nilipokuwa peke yangu. Huenda maumivu yangu hayatakwisha katika mfumo huu. Hata hivyo, makala hiyo ilinisaidia sana.
I. M., Japan
Mlisema kweli kabisa kwamba uhusiano wa mama na mtoto huanza mapema sana. Kuharibika kwa mimba huleta huzuni kubwa. Ingawa mimba yangu iliharibika miaka 19 iliyopita, bado mimi humlilia mtoto wetu ambaye hakuzaliwa.
C. C., Uingereza
Mimi huona vigumu kuzungumza na wale walio katika hali hiyo. Niliposikia kwamba mimba ya dada mmoja kutanikoni imeharibika, nilisoma makala hiyo tena. Kisha nikamwandikia barua dada huyo na wazazi wake, nikiwaeleza jinsi nilivyowasikitikia.
D. R., Ujerumani
Makala hiyo ilikuwa jibu la sala zangu. Asanteni kwa kufahamu huzuni na uchungu ambao mtu hupata mimba yake inapoharibika. Nilipokuwa nikisoma makala hiyo, nilihisi kana kwamba Yehova alikuwa akinikumbatia na kunifariji.
C. P., Marekani
Mama yangu alimpoteza mtoto aliyekuwa kati yangu na dada yangu mdogo, na jambo hilo lilimletea maumivu makali. Mara tu niliposoma sanduku lililosema “Jinsi Familia na Marafiki Wanavyoweza Kusaidia,” nilimwandikia barua.
M. Y., Japan
Kuna Mabara Mangapi? Kwenye ukurasa wa 25 wa toleo la Amkeni! la Februari 8, 2002, mliandika kwamba bara la Australia ndilo “dogo zaidi kati ya yale mabara matano ulimwenguni.” Sikuzote nimefikiri kwamba kuna mabara saba.
L. U., Kanada
“Amkeni!” linajibu: Kwa kweli kuna mabara saba—Asia, Afrika, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Antaktika, Ulaya, na Australia. Hata hivyo, wengine huona mabara ya Ulaya na Asia kuwa bara moja (Eurasia) na kusema kuna mabara sita. Wengine hawaoni Antaktika kuwa bara.