Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

UKIMWI Waenea Katika Afrika

UKIMWI Waenea Katika Afrika

UKIMWI Waenea Katika Afrika

“Tunakabiliana na msiba mkubwa sana.”

MANENO hayo ya Stephen Lewis, mwakilishi wa UM wa masuala ya UKIMWI katika Afrika, yanaonyesha jinsi watu wengi wanavyohangaikia janga la UKIMWI katika eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara.

Mambo kadhaa yanachangia kuenea kwa virusi vya UKIMWI. Na UKIMWI umeongeza matatizo mengine. Mara nyingi, hali zilizo katika nchi fulani za Afrika na katika sehemu nyingine za ulimwengu ambako UKIMWI unaenea sana huhusiana na mambo yafuatayo.

Maadili. Kwa kuwa virusi vya UKIMWI huenezwa hasa kupitia ngono, ni wazi kwamba ukosefu wa maadili unachangia sana kuenea kwa ugonjwa huo. Hata hivyo, wengi wanaonelea kwamba haiwezekani kuwazuia watu ambao hawajafunga ndoa kufanya ngono. Francois Dufour anaandika hivi katika gazeti la The Star la Johannesburg, Afrika Kusini: “Kuwaonya vijana wasifanye ngono hakuwezi kufua dafu. Kila siku kuna sinema zinazoonyesha mambo ya ngono na jinsi wanavyopaswa kuwa na jinsi wanavyopaswa kutenda.”

Mwenendo wa vijana unaonyesha wazi jambo hilo. Kwa mfano, uchunguzi uliofanywa katika nchi moja ulionyesha kwamba theluthi moja hivi ya vijana wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wamewahi kufanya ngono.

Ubakaji umetajwa kuwa tatizo kubwa nchini Afrika Kusini. Ripoti moja katika gazeti la Citizen la Johannesburg ilisema kwamba ubakaji “umeongezeka sana na kuwa kisababishi kikuu cha madhara ya afya kwa wanawake wa nchi hii na zaidi kwa watoto.” Makala hiyohiyo ilisema hivi: “Visa vya ubakaji wa watoto vimeongezeka maradufu hivi karibuni . . . Matendo hayo yanafanywa eti kwa sababu inaaminika kwamba mtu mwenye virusi vya UKIMWI hupona anapombaka bikira.”

Magonjwa yanayoambukizwa kingono. Watu wengi wameambukizwa magonjwa hayo katika eneo hilo. Jarida la South African Medical Journal lilisema hivi: “Hatari ya kuambukizwa virusi vya UKIMWI vinavyoitwa HIV-1 huongezeka mara 2 au hata mara 5 kwa mtu aliye na ugonjwa unaoambukizwa kingono.”

Umaskini. Nchi nyingi za Afrika zinakumbwa na umaskini, na hilo huchangia sana kuenea kwa UKIMWI. Vitu vinavyoonwa kuwa vya msingi katika nchi zilizoendelea havipatikani katika nchi nyingi zinazoendelea. Jamii nyingi kubwa hazina umeme wala maji safi. Barabara ni chache sana katika maeneo ya mashambani na sehemu nyingine hazina barabara. Wakazi wengi hawana chakula cha kutosha, na hospitali ni chache sana.

UKIMWI huathiri sana biashara na viwanda. Mapato ya makampuni ya kuchimba migodi yanapungua kadiri wafanyakazi wengi wanavyoambukizwa virusi vya UKIMWI. Makampuni kadhaa yanafikiria njia za kuendesha shughuli fulani kwa mashine ili kulipia hasara hiyo. Katika kampuni moja ya kuchimbua platinamu, ilikadiriwa kwamba idadi ya wafanyakazi wenye ugonjwa wa UKIMWI iliongezeka karibu maradufu mnamo mwaka wa 2000, na asilimia 26 hivi ya wafanyakazi waliambukizwa virusi vya UKIMWI.

Jambo moja la kusikitisha kuhusu UKIMWI ni kwamba watoto wengi sana huwa mayatima wazazi wao wanapokufa kutokana na ugonjwa huo. Mbali na kupoteza wazazi wao ambao wanawatunza, watoto hao hulazimika kukabiliana na aibu inayohusianishwa na UKIMWI. Mara nyingi watu wa ukoo au watu wa jumuiya huwa maskini sana hivi kwamba hawawezi kusaidia au hawataki kufanya hivyo. Mayatima wengi huacha shule. Wengine huanza ukahaba na hivyo kuchangia kuenea kwa UKIMWI. Nchi kadhaa zimeanzisha miradi ya serikali au ya kibinafsi kuwasaidia mayatima hao.

Kutojua. Watu wengi hawajui kuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Wengi hawataki kupimwa kwa sababu wanahofu kuaibika na kutengwa wanapojulikana kuwa wana ugonjwa huo. Taarifa moja kwa waandishi wa habari iliyotolewa na Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) ilisema hivi: “Watu walio na virusi vya UKIMWI, au wale wanaoshukiwa kuwa navyo wanaweza kukataliwa hospitalini, kutoruhusiwa kukodisha nyumba, kutoajiriwa kazi, kuhepwa na marafiki na wafanyakazi wenzao, kutoruhusiwa kukata bima au kutokubaliwa katika nchi nyingine.” Wengine hata wameuawa ilipogunduliwa kuwa wana virusi vya UKIMWI.

Utamaduni. Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, mara nyingi wanawake hawaruhusiwi kuwauliza wenzi wao kuhusu mahusiano haramu ya ngono, kukataa ngono, au kuwaomba watumie vifaa vya kujikinga na magonjwa yanayoambukizwa kingono. Tamaduni nyingi hupinga kuwapo kwa UKIMWI. Kwa mfano, nyakati nyingine inadaiwa kwamba ugonjwa huo husababishwa na uchawi, na kwamba wachawi wanaweza kuutibu.

Ukosefu wa hospitali za kutosha. Katika maeneo yenye hospitali chache, tayari hospitali zimejaa kupita kiasi kwa sababu ya UKIMWI. Hospitali mbili kubwa zinaripoti kwamba zaidi ya nusu ya wagonjwa waliolazwa humo wana virusi vya UKIMWI. Afisa mkuu wa tiba katika hospitali moja huko KwaZulu-Natal alisema kwamba idadi ya wagonjwa waliolazwa kwenye vyumba vya wagonjwa inazidi kwa asilimia 40 idadi inayotakikana. Nyakati nyingine, wagonjwa wawili hulazimika kulala kwenye kitanda kimoja, na mgonjwa mwingine hulala sakafuni chini ya kitanda!—South African Medical Journal.

Tayari hali ni mbaya sana katika Afrika, na inaonekana itakuwa mbaya hata zaidi. Peter Piot wa UNAIDS alisema hivi: “Tungali katika hatua za mwanzo-mwanzo za ugonjwa huo.”

Ni wazi kwamba katika nchi kadhaa jitihada zinafanywa ili kupambana na ugonjwa huo. Na kwa mara ya kwanza, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifanya kongamano maalum la kuzungumzia ugonjwa wa UKIMWI mnamo Juni 2001. Je, jitihada za wanadamu zitafanikiwa? Ugonjwa hatari wa UKIMWI utakomeshwa lini?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

DAWA YA UKIMWI YA NEVIRAPINE NA TATIZO LINALOKUMBA AFRIKA KUSINI

Dawa ya Nevirapine ni nini? Kulingana na Nicole Itano, ambaye ni mwandishi wa habari, hiyo ni “dawa ya kuzuia utendaji wa virusi ambayo imejaribiwa na ikaonekana kwamba inaweza kupunguza kwa asilimia 50 uwezekano wa mama kumwambukiza mtoto wake UKIMWI.” Kampuni moja ya kutengeneza dawa huko Ujerumani ilijitolea kuipatia nchi ya Afrika Kusini dawa hiyo bila malipo kwa miaka mitano ijayo. Hata hivyo, kufikia Agosti 2001, serikali haikuwa imekubali msaada huo. Tatizo ni nini?

Watu milioni 4.7 wana virusi vya UKIMWI nchini Afrika Kusini. Hiyo ndiyo idadi kubwa zaidi ulimwenguni pote. Mnamo Februari 2002, gazeti la The Economist la London liliripoti kwamba Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini “anashuku yale maoni ya kawaida kwamba virusi vya HIV husababisha UKIMWI” na pia “ana shaka kuhusu gharama za dawa zinazozuia utendaji wa virusi vya UKIMWI, athari zake, na ikiwa zinafanya kazi. Hajazipiga marufuku, lakini madaktari wa Afrika Kusini wanavunjwa moyo wasizitumie.” Kwa nini jambo hilo linasababisha hangaiko kubwa? Kwa sababu kila mwaka maelfu ya watoto huzaliwa na virusi vya UKIMWI huko Afrika Kusini na asilimia 25 ya wanawake wajawazito wana virusi hivyo.

Kwa sababu ya maoni hayo yanayotofautiana, kesi iliwasilishwa mahakamani ili kuilazimisha serikali igawe dawa ya nevirapine. Mahakama ya Sheria ya Afrika Kusini ilitoa uamuzi wake mnamo Aprili 2002. Kulingana na taarifa ambayo Ravi Nessman aliandika katika gazeti la The Washington Post, mahakama hiyo iliamua kwamba “serikali inapaswa kuruhusu dawa hiyo katika taasisi za matibabu ambazo zinaweza kuigawa kwa njia inayofaa.” Ijapokuwa serikali ya Afrika Kusini ilikuwa ikigawanya dawa hiyo katika vituo 18 vya majaribio nchini humo, inasemekana kwamba uamuzi huo umewapa tumaini wanawake wote wajawazito wenye virusi vya UKIMWI katika nchi hiyo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

VIRUSI INAYOVAMIA CHEMBE KWA UJANJA

Hebu fikiria kidogo juu ya virusi ya UKIMWI (HIV) ambayo ni ndogo sana. Mwanasayansi mmoja alisema hivi: “Baada ya kuchunguza kwa miaka mingi chembechembe za virusi kwa hadubini, bado ninastaajabishwa na muundo tata na wenye usahihi kabisa wa kitu hicho kidogo sana.”

Virusi ni ndogo kuliko bakteria, na bakteria ni ndogo sana kuliko chembe ya mwili wa mwanadamu. Kulingana na kitabu kimoja, virusi ya UKIMWI ni ndogo sana hivi kwamba “chembechembe milioni 230 [za virusi mbalimbali vya UKIMWI] zinaweza kutoshea kwenye alama ya kituo inayomalizia sentensi hii.” Virusi haiwezi kuongezeka bila kuingia katika chembe na kudhibiti utendaji humo.

Virusi ya UKIMWI inapoingia katika mwili wa mwanadamu, inalazimika kupambana na silaha kali za mfumo wa kinga. * Kinga zinazotia ndani chembe nyeupe za damu hufanyizwa katika uboho wa mfupa. Chembe nyeupe za damu hutia ndani aina mbili kuu za chembe za limfu, zinazoitwa chembe za T na chembe za B. Chembe nyingine nyeupe huitwa fagositi, au “walaji wa chembe.”

Aina tofauti-tofauti za chembe za T hufanya kazi mbalimbali. Chembe fulani za T (helper T cells) hutimiza daraka muhimu katika pambano hilo kwa kutambua virusi na kutoa habari ili chembe za kushambulia na kuangamiza virusi zifanyizwe. Virusi ya UKIMWI hulenga hasa chembe hizo za T. Chembe nyingine za T (killer T cells) husisimuliwa ili ziharibu chembe za mwili ambazo zimekwisha kushambuliwa. Chembe za B hufanyiza kinga za mwili ambazo hupambana na maambukizo.

Shambulizi la Ujanja

Virusi ya UKIMWI imefanyizwa kwa molekuli za RNA (ribonucleic acid) wala si za DNA (deoxyribonucleic acid). Virusi ya UKIMWI ni mojawapo ya virusi vinavyoweza kukaa kwa muda mrefu bila kutenda kabla ya dalili za ugonjwa kuonekana.

Virusi ya UKIMWI ikiisha kuingia katika chembe ya kiumbe, inaweza kutumia chembe hiyo kutimiza lengo lake. Virusi hiyo “hubadili” DNA ya chembe ili kuzaa virusi vingi vya UKIMWI. Lakini kabla ya kufanya hivyo, ni lazima virusi hiyo itumie mbinu nyingine. Ni lazima ibadili RNA yake kuwa DNA ili iweze kukubaliwa na kueleweka na chembe hiyo. Ili kutimiza hilo, virusi ya UKIMWI hutumia kimeng’enya kinachoitwa reverse transcriptase. Muda si muda, chembe iliyovamiwa hufa, baada ya kufanyiza maelfu ya virusi vya UKIMWI. Virusi hivyo huambukiza chembe nyingine.

Zile chembe za T zinazotambua virusi zikiisha pungua sana, viini vingine vinaweza kushambulia mwili bila kizuizi chochote. Mwili hushambuliwa na magonjwa na maambukizo ya kila aina. Kufikia hapo, mtu aliyeambukizwa huwa anadhoofishwa kabisa na UKIMWI. Virusi vya UKIMWI vimefaulu kuangamiza mfumo wote wa kinga.

Hayo ni maelezo sahili. Tunapaswa kukumbuka kwamba bado watafiti hawafahamu mambo mengi kuhusu mfumo wa kinga na utendaji wa virusi vya UKIMWI.

Kwa miaka 20 hivi, wataalamu hodari wa tiba ulimwenguni pote wametumia ujuzi wao na pesa nyingi kuchunguza virusi hiyo ndogo. Hivyo, wamejifunza mengi kuhusu virusi ya UKIMWI. Dakt. Sherwin B. Nuland, ambaye ni daktari-mpasuaji, alisema hivi miaka kadhaa iliyopita: “Habari ambazo . . . zimekusanywa kuhusu virusi ya UKIMWI na maendeleo yaliyofanywa kukinga mashambulizi yake yanastaajabisha sana.”

Hata hivyo, ugonjwa hatari wa UKIMWI unazidi kuenea haraka sana.

[Maelezo ya Chini]

[Picha]

Virusi ya UKIMWI hushambulia chembe za limfu za mfumo wa kinga na kuzibadili ili zifanyize virusi vingi zaidi

[Hisani]

CDC, Atlanta, Ga.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Maelfu ya vijana hutii viwango vya Biblia