“Ugonjwa Hatari Ambao Umeenea Zaidi Katika Historia Yote”
“Ugonjwa Hatari Ambao Umeenea Zaidi Katika Historia Yote”
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
“Ugonjwa hatari wa UKIMWI unaangamiza watu wengi zaidi kuliko vita yoyote ulimwenguni.” —COLIN POWELL, WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA MAREKANI.
RIPOTI rasmi ya kwanza kuhusu UKIMWI (ukosefu wa kinga mwilini) ilitolewa mnamo Juni 1981. Peter Piot, mkurugenzi-mkuu wa Mradi wa Umoja wa Mataifa Kuhusu UKIMWI (UNAIDS) anasema hivi: “Sisi tulioshughulika na ugonjwa wa Ukimwi wakati ulipozuka hatungewazia kwamba ungeenea kwa kiwango kikubwa hivyo.” Katika kipindi cha miaka 20, UKIMWI umekuwa ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza kuwahi kutokea, na inaonekana kwamba utaendelea kuenea.
Inakadiriwa kwamba zaidi ya watu milioni 36 wana virusi vya UKIMWI (HIV), na watu milioni 22 tayari wamekufa kutokana na ugonjwa huo. * Mnamo mwaka wa 2000, watu milioni tatu ulimwenguni pote walikufa kutokana na UKIMWI. Hiyo ndiyo idadi kubwa ya vifo kuwahi kutokea katika mwaka mmoja tangu ugonjwa huo ulipozuka. Vifo hivyo vilitukia licha ya kwamba kuna dawa za kuzuia utendaji wa virusi vya UKIMWI, hasa katika nchi tajiri.
UKIMWI Waenea Afrika
Eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara, ndilo limeathiriwa sana na ugonjwa huo. Inakadiriwa kwamba wakazi milioni 25.3 wa eneo hilo wameambukizwa. Katika eneo hilo peke yake, watu milioni 2.4 walikufa kutokana na UKIMWI katika mwaka wa 2000. Hiyo ni asilimia 80 ya idadi ya wale waliokufa ulimwenguni pote. Ugonjwa wa UKIMWI ndio kisababishi kikuu cha vifo katika eneo hilo. *
Kati ya nchi zote ulimwenguni, nchi ya Afrika Kusini ndiyo ina idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa. Inakadiriwa
kwamba watu milioni 4.7 wameambukizwa. Katika nchi hiyo, watoto 5,000 huzaliwa na virusi vya UKIMWI kila mwezi. Alipokuwa akihutubia Kongamano la 13 la Kimataifa Kuhusu UKIMWI lililofanywa huko Durban mwezi wa Julai 2000, Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini alisema hivi: “Tulishtuka kugundua kwamba nusu ya vijana wa Afrika Kusini watakufa kutokana na UKIMWI. Jambo lenye kutia hofu hata zaidi ni kwamba maambukizo yote hayo, na mateso yanayosababishwa nayo . . . yangeweza na yanaweza kuzuiwa.”UKIMWI Waenea Haraka Katika Nchi Nyingine
Idadi ya watu wanaoambukizwa inaongezeka haraka katika Ulaya Mashariki, Asia, na Karibea. Mwishoni mwa mwaka wa 1999, watu 420,000 walikuwa wameambukizwa katika Ulaya Mashariki. Mwishoni mwa mwaka wa 2000, ilikadiriwa kwamba idadi hiyo ilikuwa imefikia 700,000.
Uchunguzi uliofanywa katika majiji makubwa sita ya Marekani ulifunua kwamba asilimia 12.3 ya wanaume vijana wanaofanya ngono na wanaume wenzao wameambukizwa virusi vya UKIMWI. Isitoshe, ni asilimia 29 tu waliojua kwamba wana virusi hivyo. Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza aliyesimamia uchunguzi huo alisema hivi: “Tulisikitika sana kugundua kuwa ni wanaume wachache sana wenye virusi vya UKIMWI ambao walijua kwamba wameambukizwa. Hiyo inamaanisha kwamba watu walioambukizwa hivi majuzi wanaeneza virusi hivyo bila kujua.”
Kwenye mkutano wa wataalamu wa UKIMWI uliofanywa Mei 2001 huko Switzerland, ugonjwa huo ulitajwa kuwa “ugonjwa hatari zaidi wa kuambukiza kuwahi kutokea.” Kama ilivyotajwa, UKIMWI umeenea zaidi katika eneo la Afrika lililoko kusini mwa jangwa la Sahara. Makala inayofuata inaonyesha sababu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Takwimu zilizoonyeshwa ni makadirio yaliyochapishwa na UNAIDS.
^ fu. 7 Ona gazeti la Amkeni! la Februari 22, 2001, ukurasa wa 14-15.
[Blabu katika ukurasa wa 3]
“Jambo lenye kutia hofu hata zaidi ni kwamba maambukizo yote hayo, na mateso . . . yangeweza na yanaweza kuzuiwa.”—NELSON MANDELA
[Picha katika ukurasa wa 3]
Watu wengi wenye virusi vya UKIMWI hawajui kwamba wameambukizwa
[Picha katika ukurasa wa 3]
UN/DPI Photo 198594C/Greg Kinch