Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Akina Mama Asanteni kwa mfululizo wa makala “Je, Mama Wana Kazi Nyingi Mno?” (Aprili 8, 2002) Watu wengi leo hufikiri kwamba akina mama wa nyumbani hawana kazi nyingi kama wale ambao hufanya kazi ya kuajiriwa. Makala yenu iliwasaidia wasomaji watambue kwamba akina mama wote ni wafanyakazi!
T. M., Marekani
Jambo la kwanza lililonivutia ni ule mchoro wa mwanamke wa mfano katika ukurasa wa 2. Mchoro huo ulinifanya nitamani kusoma makala hiyo wakati uo huo. Mimi nina watoto wawili wachanga, na ninakubali kwamba makala hizo zilieleza kwa usahihi kazi ambazo akina mama hufanya kila siku.
C. L., Ujerumani
Mimi ni msichana wa miaka 12. Nilipolipokea gazeti hilo nililisoma wakati uo huo. Sasa ninatambua mambo ambayo mama yangu hutufanyia tukiwa na baba yangu. Sasa ninamthamini zaidi na ninamsaidia kufanya kazi nyingi zaidi!
A. L., Marekani
Miaka miwili iliyopita, nilijifungua mtoto wa kiume. Kufikia wakati huo, nilikuwa mhubiri wa wakati wote na pia nilikuwa na kazi ya muda. Kwa sababu nilitamani kuendelea kuishi kama hapo awali, nilihisi ni kama sikutimiza daraka la mama jinsi inavyostahili. Makala hizo zilinipatia ujasiri niliohitaji.
S. T., Italia
Nimeanza kuona faida za kutumia ushauri mliotoa kuhusu kutenga wakati wa kupumzika. Tayari nilikuwa nimeanza kufanya hivyo kabla ya kusoma makala hizo, lakini nilihisi nikiwa na hatia kwa kufanya hivyo. Asanteni kwa kunisaidia nitambue kwamba sipaswi kuhisi hatia maadamu ninafanya jambo hilo kwa usawaziko.
C. C., Marekani
Akina mama wengine ambao hufanya kazi kwa bidii huhisi kwamba kazi yao haithaminiwi inavyostahili. Makala hizo ziliwapa uthamini waliohitaji. Mimi ni mama ya watoto wanne, na ninafahamu ugumu wa kusawazisha kazi za nyumbani na ya kuajiriwa. Nilipotambua kwamba Yehova alimpulizia Solomoni aandike mawazo yanayohusu akina mama ambao hufanya kazi kwa bidii, nilifarijiwa na kutiwa moyo nifanye yote ninayoweza.
E. S., Ujerumani
Nina mtoto wa miaka mitatu, nami huhisi nikiwa na hatia kwa sababu huwa nimechoka nyakati zote. Makala hizi zilinisaidia kutambua kwamba sio mimi pekee ninayehisi hivyo, na zilinipatia madokezo mazuri sana ya kunisaidia niboreshe hali yangu.
K. J., Marekani
Jalada la gazeti hilo linaonyesha picha ya mama ambaye amembeba mtoto wake mchanga. Yaonekana mtoto huyo anakula soseji. Mke wangu na mimi tumemaliza kuhudhuria mtaala kuhusu kumsaidia mtoto anayeshindwa kupumua vizuri. Mwalimu wetu alisema kwamba soseji hasa ndizo huwanyonga watoto wachanga na wakubwa. Alisisitiza kwamba watoto wachanga wasipewe soseji.
G. E., Marekani
“Amkeni!” lajibu: Bila shaka kula soseji kunaweza kuwanyonga vitoto na watoto. Kwa kweli, mtoto aliyeonyeshwa kwenye jalada letu ananyonya karoti huku akiwa amebebwa na mama yake.
Mawasiliano ya Wanyama Asanteni sana kwa makala “Lugha ya Mbugani—Siri za Mawasiliano ya Wanyama.” (Aprili 8, 2002) Niliangua kicheko niliposoma kuhusu njia ya ajabu ambayo nyumbu hutumia kumkengeusha adui. Kwa upande mwingine, nililia niliposoma maelezo ya Joyce Poole kuhusu “majonzi” ya tembo wa kike ambaye alifiwa na mtoto wake alipokuwa tumboni. Makala hizo nzuri, zenye kuvutia, hutusaidia kufikiri na kutambua jinsi ‘lugha hiyo ya wanyama’ ‘humtukuza yule aliyeianzisha, Yehova Mungu.’ Endeleeni kuandika makala kama hizo!
A. G., Poland