Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Matusi Yanaongezeka
Watu wengi huko Amerika Kaskazini “si waungwana,” yasema makala katika gazeti The Toronto Star. Jambo hilo ni wazi kwani “matusi yanaongezeka.” Kulingana na P. M. Forni, msimamizi wa Mradi wa Uungwana katika Chuo Kikuu cha John Hopkins, limekuwa jambo la kawaida kutumia matusi hivi kwamba vijana hawaoni ubaya wake na watu wengi wazima hawatambui kuwa yanatumiwa au hata hawajali. Gazeti hilo lasema kwamba kulingana na Profesa Timothy Jay, “watoto huanza kutumia matusi wakiwa na umri wa mwaka 1, mara tu wanapoanza kuiga maneno wanayosikia kutoka kwa wazazi wao na katika televisheni.” Takwimu za uchunguzi mmoja zinaonyesha kwamba “asilimia 10 hivi ya maneno ambayo watu wazima hutumia kazini na asilimia 13 ya maneno wanayotumia wakati wa tafrija ni matusi.” Gazeti la Star lilitoa takwimu nyingine inayoonyesha kwamba nchini Marekani, “matusi katika televisheni yameongezeka zaidi ya mara tano kutoka 1989 hadi 1999.”
Mbayuwayu Hulalaje Wakiwa Angani?
Mbayuwayu huruka wakiwa wamelala usingizi na wakati huohuo wao hubaki katika eneo lao hewani bila kupeperushwa na upepo. Ili kujua jinsi wanavyofanya hivyo, wataalamu wa ndege Johan Bäckman na Thomas Alerstam wa Chuo Kikuu cha Lund, nchini Sweden, walitumia rada kuchunguza ndege hao wakiruka wakati wa usiku. Kulingana na ripoti ya gazeti la kisayansi la Ujerumani Bild der Wissenschaft, wataalamu hao waliona ndege hao wakiruka kwa njia fulani ambayo iliwasaidia kubaki katika eneo lao. Ndege hao hupaa juu sana, urefu wa meta 3,000, halafu wao huanza kuruka wakielekea upepo kwa mshazari, huku wakibadili upande wanaoruka kila baada ya dakika chache. Njia hiyo ya kuruka huwawezesha kusonga huku na huku katika eneo lao. Hata hivyo, wakati kulipokuwa na upepo mwanana, mbayuwayu walionekana wakizunguka-zunguka hewani wakiwa wamelala.
‘Ugonjwa Tunaoweza Kuepuka’
“Tunaweza kuepuka kuugua ugonjwa wa mifupa wa osteoporosis,” lasema gazeti The Sun-Herald la Australia. “Inawezekana sana kuzuia ugonjwa huo. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2020, thuluthi moja ya vitanda hospitalini vitakuwa na wanawake waliovunjika mifupa.” Kulingana na ripoti ya Shirika la Ugonjwa wa Mifupa la Australia, ugonjwa huo ambao hufanya mifupa iwe na mashimo na kuvunjika kwa urahisi, “huathiri watu wengi kuliko kolesteroli, mizio au mafua. Kutibu ugonjwa huo hugharimu pesa nyingi kuliko ugonjwa wa sukari au wa pumu. Isitoshe, idadi ya wanawake wanaokufa kwa kuvunjika nyonga ni kubwa kuliko idadi ya kansa zote za wanawake zikiwekwa pamoja.” Kulingana na Profesa Philip Sambrook, inakadiriwa kwamba nusu ya wanawake na thuluthi moja ya wanaume nchini Australia watavunjika mfupa katika maisha yao kutokana na ugonjwa huo. Kulingana na gazeti hilo “kinga nzuri zaidi ya ugonjwa huo, ni kujenga mifupa yenye nguvu katika miaka thelathini ya kwanza maishani kwa kufanya mazoezi na kula vyakula vyenye kalisi ya kutosha.” Hatari ya kupatwa na ugonjwa wa mifupa inaweza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa kujiepusha na uvutaji wa sigara na kunywa pombe au kafeini kupita kiasi. Hatari ya kupata ugonjwa huo inaweza kupunguzwa kwa kufanya mazoezi kwa ukawaida na kula vyakula vyenye kalisi nyingi na vitamini D.
“Mtakatifu” Anayefungua Mafundo
“Katika miaka ya majuzi, Mtakatifu Jude Thaddaeus, mtatuzi wa magumu; Mtakatifu Rita, mwokozi wa wasio na tumaini; Mtakatifu Hedwig, mlinzi wa wadeni, na Mtakatifu Expeditus, mharakishaji wa mambo, wamepata umaarufu,” lasema gazeti Veja. Sasa “mtakatifu” mwingine amepata umaarufu miongoni mwa Wakatoliki nchini Brazili naye anaitwa “Mama Yetu Anayefungua Mafundo.” Jina hilo la kipekee linatokana na picha iliyoko katika kanisa moja huko Augsburg, Ujerumani, inayoonyesha Bikira Maria akifungua mafundo ya utepe. Umaarufu wake umetokana na waandishi wa habari, na amepata wafuasi wengi wanaotafuta masuluhisho ya matatizo yao ya afya, ya ndoa, na ya kifedha. Hali hiyo imetokeza biashara ya kuuza nembo, rozari, sanamu, na vibandiko vya magari. Darci Nicioli, msimamizi wa kanisa kubwa zaidi la Katoliki nchini Brazili anasema: “Si vibaya kuwa mfuasi wa ‘Mama Anayefungua Mafundo,’ lakini msisimuko huo ni wa kitambo tu.”
Kuhubiri Injili Angani
Wanasayansi wanapoendelea kujadili kuhusu uwezekano wa kuwapo kwa uhai katika sayari nyingine, gazeti Berliner Morgenpost laripoti kuwa makasisi katika Kituo cha Angani cha Vatikani, wamefikia mkataa kwamba “kuna viumbe wengine wa Mungu ulimwenguni mbali na wanadamu walio duniani. Mungu aliumba watu wengine pia nje ya dunia.” Msimamizi wa kituo hicho, George Coyne, alieleza kuwa “ulimwengu ni mkubwa sana kuwa na watu wachache tu.” Makao fulani ya watawa yametuma ujumbe wa siri wa Agano Jipya huko angani ili kupeleka Injili kwa viumbe hao. Kulingana na gazeti hilo, Vatikani inataka pia kujua “kama Yesu Kristo amejidhihirisha katika sayari nyingine pia.” Coyne anaongeza kusema kwamba wanataka kujua “kama Yesu Kristo amewaokoa wakazi” wa sayari hizo pia.
Saa ya “Maangamizi” Yakaribia
Wasimamizi wa gazeti The Bulletin of the Atomic Scientists wamesogeza Saa maarufu ya Maangamizi “mbele kwa dakika mbili hadi saa sita kasoro dakika saba za usiku,” laripoti gazeti la kila siku la Paris International Herald Tribune. “Kukawizwa kwa jitihada za kupunguza silaha, usalama wa silaha za nyukilia zilizopo na ugaidi” ni mambo yaliyochangia badiliko hilo. Saa hiyo, ambayo huonyesha jinsi ulimwengu unavyokaribia maangamizi ya nyukilia, ilizinduliwa mnamo mwaka wa 1947, na tangu wakati huo imesogezwa mara 17. Wakati Muungano wa Sovieti ulipovunjika katika mwaka wa 1991, saa hiyo ilirudishwa nyuma hadi saa sita kasoro dakika 17, lakini tangu wakati huo imekuwa ikisogezwa karibu na saa sita za usiku. Saa hiyo ilibadilishwa kwa mara ya mwisho katika mwaka wa 1998, kutoka sasa sita kasoro dakika 14 hadi kasoro dakika 9. Tangu wakati huo ni silaha 3,000 tu za nyukilia zilizoharibiwa, huku zaidi ya silaha 31,000 zikibaki mikononi mwa mataifa yenye nguvu.
Uswisi Yaamua Kujiunga na Umoja wa Mataifa
‘Baada ya miaka mingi ya kujitenga, Uswisi isiyopendelea upande wowote imeamua kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jambo hilo liliamuliwa kwa kura chache kupitia kura ya maoni iliyofanywa kote nchini,’ laripoti gazeti The New York Times. Jambo linalobaki sasa ni kupeleka ombi rasmi kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuifanya iwe mwanachama wa 190 wa umoja huo. Wakati kura nyingine ya maoni ilipofanywa katika mwaka wa 1986, Waswisi wengi walikataa kujiunga na umoja huo, “wakihofia kwamba sera yao ya tangu zamani ya kutopendelea upande wowote ingevunjwa.” Basi kwa nini sasa wamebadili maoni yao? “Ingawa makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Ulaya yako katika nchi hiyo huko Geneva, na nchi hiyo hushiriki katika shughuli za baadhi ya mashirika ya Umoja huo, serikali ilihofia kwamba kuendelea kujitenga na Umoja huo kungeidhoofisha kisiasa na kiuchumi, na kuathiri jitihada zake za kutatua mizozo katika sehemu za mbali,” lasema gazeti Times. Pia huenda Uswisi iliona uhitaji wa kuboresha sifa yake baada ya madai ya hivi majuzi kwamba benki zake zilitwaa pesa za watu waliokumbwa na yale Maangamizi Makubwa ya Nazi na kwamba iliwazuia wakimbizi wengi kuingia nchini humo walipokuwa wakitoroka Ujerumani ya Nazi.
Dawa ya Steroidi Ni Hatari
Inakadiriwa kwamba nchini Poland “asilimia 60 hivi ya watu ambao hujenga misuli hutumia dawa ya steroidi,” laripoti gazeti la Poland la kila wiki Wprost. Vijana wenye umri wa kati ya miaka 17 na 18 huanza kutumia dawa hizo mapema katika mwaka “ili kufikia mwezi wa Juni wawe wamejenga misuli na kujionyesha wakati wanapoogelea katika vidimbwi visivyokuwa na paa.” Ingawa dawa za kuongeza nguvu “zinaweza kununuliwa karibu katika kila kituo cha kujenga misuli,” hizo ni hatari. “Dawa za kuongeza nguvu huharibu ini na misuli,” asema Profesa Janusz Nauman wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Warsaw. Dawa hizo husababisha magonjwa ya ngozi na nywele, kukosa utulivu, ujeuri, na matatizo ya hisia. Matatizo mengine ya kutumia dawa hizo huonekana miaka mingi baadaye. Kwa mfano, “wanariadha kutoka Ujerumani Mashariki [ya zamani], ambapo dawa zilitumiwa sana kuanzia miaka ya 1950, waliathiriwa kiafya katika miaka ya 1970 na 1980,” asema Nauman. Gazeti la Wprost, linaongeza kusema kwamba utumizi wa dawa za kuongeza nguvu “huongeza uwezekano wa kutumia heroini na dawa nyingine za kulevya.”