Je, Bado Ni Salama Kusafiri kwa Ndege?
Je, Bado Ni Salama Kusafiri kwa Ndege?
NDEGE nne kubwa za abiria zatekwa nyara. Ndege hizo nne zakumbwa na msiba. Majengo maarufu yaharibiwa. Ndege aina ya 767 yagonga mojawapo ya yale majengo ya Twin Towers, na tukio hilo laonyeshwa tena na tena kwenye televisheni.
Magaidi walitumia mbinu mpya zenye kuogopesha katika mashambulizi ya Septemba 11, 2001. Mashirika ya ndege yalitumiwa kutimiza lengo hatari, na ndege zikatumiwa kama mabomu.
Kutokana na hilo, baadhi ya wasafiri wa ndege wameanza kuogopa jambo fulani: Ijapokuwa hapo awali walihisi salama kusafiri kwa ndege, sasa wanaogopa mashambulizi ya magaidi. Isitoshe, baada ya Septemba 11 kumekuwa na misiba ya ndege ambayo haikusababishwa na magaidi, nayo imewafanya wengi waogope kusafiri kwa ndege hata zaidi.
Ni kweli kwamba usafiri wa ndege ni wa bei ghali na mamilioni ya watu ulimwenguni hawawezi kuugharimia. Hata hivyo, wengine hulazimika kusafiri kwa ndege mara nyingi. Wale walio na kazi zinazowalazimu kusafiri sana, hawana budi kupanda ndege. Mara nyingi mishonari na wahudumu Wakristo huhitaji kusafiri mbali kwa ndege ili wafike au watoke mahali walikotumwa. Nyakati nyingine, hata watu maskini hulazimika kusafiri kwa ndege wanapohitaji matibabu ya dharura. Na maelfu ya marubani na wafanyakazi wa ndege hujiruzuku kupitia usafiri wa ndege.
Wengi kati ya watu hao wanaosafiri kwa ndege wanalazimika kuwatuliza wenzi wao wa ndoa na watoto wao wenye wasiwasi kabla ya kufunga safari zao, japo huenda ikawa wao wenyewe wana wasiwasi. Kwa kuwa safari hizo sasa zimekuwa zenye kuogopesha tofauti na ilivyokuwa hapo zamani, wasafiri wanajiuliza iwapo kusafiri kwa ndege kungali salama.
Ili kuzungumzia mahangaiko hayo, gazeti la Amkeni! liliwahoji wataalamu wa usalama, wafanyakazi kwenye viwanja vya ndege, maafisa wa mashirika ya ndege, na mafundi wa ndege. Yaonekana wote wanakubaliana juu ya jambo hili: Ijapokuwa usafiri wa ndege ungali mojawapo ya njia salama zaidi za usafiri, hatari zilizotokea hivi karibuni zinaonyesha kwamba hatua mpya zinapasa kuchukuliwa kuimarisha usalama wa wasafiri.
Makala zinazofuata zitazungumzia matatizo yanayohusika na mambo unayoweza kufanya ili uwe salama na ustarehe zaidi unaposafiri kwa ndege.