Kuhangaikia Usalama
Kuhangaikia Usalama
KUSAFIRI kwa ndege kilometa 11 juu ya dunia kwaweza kuwaogopesha watu fulani. Huenda likaonekana kuwa jambo lisilopatana na sheria za asili. Kwa kuwa sasa usalama umeimarishwa na usafiri wa ndege unategemeka zaidi, hatari zinazoweza kutokea kwa kusafiri haraka ndani ya ndege zimepungua. Hata hivyo, misiba ya ndege hutukia mara mojamoja.
Kukabiliana na Woga
Ingawa msiba unaweza kutokea, tangu zama za kale, mwanadamu ameonyesha tamaa yake ya kusafiri hewani. Miaka elfu moja kabla ya Kristo, Mfalme Daudi aliandika hivi: “Laiti ningekuwa na mabawa kama njiwa! Ningeruka mbali.” (Zaburi 55:6, Biblia Habari Njema) Kama ilivyotajwa tayari, tekinolojia ya kisasa imefanya usafiri wa ndege uwe mojawapo ya njia salama zaidi za kusafiri. Lakini usafiri huo haukosi dosari. Hakuna kitu ulimwenguni kilicho salama kabisa wala kinachoweza kujulikana kimbele kwa ukamili.
Ni muhimu kukumbuka jambo hilo iwapo tunakuwa na wasiwasi wakati
mtu mwingine anapoendesha mambo. Watu wengine wanaweza kufikiri hivi, ‘Mimi mwenyewe nikiendesha shughuli fulani, wasiwasi wangu hupungua.’ Watu kama hao wanaweza kusumbuka sana wanapojipata mahali ambapo hawawezi kufanya lolote au hawana uhuru wa kudhibiti mambo. Usafiri wa ndege ni mojawapo ya hali hizo.Licha ya jitihada za kuimarisha usalama katika usafiri wa ndege, mtu yeyote hapaswi kuchukua mambo kimchezo. Wote wanaohusika katika usafiri wa ndege wanaweza kushirikiana kupunguza visababishi vya hatari. Na bado wenye mamlaka hutoa maonyo kuhusu hatari zilizopo. Mithali moja yenye hekima katika Biblia inasema: “Mtu mwenye busara huona hatari iliyo mbele mapema na kutahadhari.” (Mithali 22:3, New Living Translation) Ni jambo la hekima kutambua kwamba hatari fulani yaweza kutokea katika shughuli yoyote ile. Kumbuka kwamba mtu anaposafiri kwa ndege anapaswa kuchukua tahadhari zilezile za kujilinda ambazo zinahitajika katika hali nyinginezo.
Watu ambao husafiri kwa ndege mara nyingi wanaweza kujua vizuri zaidi jinsi ya kushughulika na hali hizo ngumu. Hiyo ni kwa sababu wamezoea ndege na viwanja vya ndege kuliko abiria wengine. Wewe pia unaweza kuzoea hali hizo na kustarehe kama wao kwa kufuata hatua sahili zinazoonyeshwa kwenye masanduku yaliyo katika makala hii.
Kusafiri Bila Wasiwasi
Japo vituo vya ukaguzi ni muhimu, wasafiri fulani—hasa wale wenye haraka—huudhiwa navyo. Kwa kuwa usalama umeimarishwa katika viwanja vingi vya ndege, huenda ungependa kutumia madokezo yanayofuata ili usisumbuke kwenye vituo vya ukaguzi.
▪ Fika mapema. Kwa kupanga kufika mapema kwenye uwanja wa ndege, unaweza kufanya mambo bila haraka, kutulia, na kuepuka mfadhaiko unaoweza kutokana na hali zisizotarajiwa au hali nyingine zenye kutatiza.
▪ Unapochagua shirika la ndege, chagua shirika linalotumiwa hasa na wafanyabiashara. Wao wamezoea kusafiri, hawabebi mizigo mingi, na hutaka kusafiri haraka.
▪ Kabla ya kupita kwenye mlango wenye kifaa cha kutambua vitu vya chuma, ondoa vitu ambavyo unafikiri vitasababisha king’ora kilie. Vitu hivyo vinatia ndani funguo, sarafu, vito, na simu za mkononi. Mkabidhi mhudumu vitu hivyo unapojitayarisha kupita kwenye mlango huo.
▪ Laza kabisa mifuko na mizigo mingine kwenye mkanda unaochukua mizigo; mhudumu anayetazama picha za eksirei anapoona kitu kilicho shaghalabaghala, anaweza kukuambia ufungue mfuko wako au uuweke tena kwenye mkanda huo.
▪ Mweleze mhudumu kuhusu vitu vyovyote vya kiajabu ambavyo unadhani vitavuta fikira zake. Yaelekea hatataka kufungua mfuko wako unapomweleza vizuri kitu ulichotia mfukoni ambacho kinaonekana kikiwa na umbo la ajabu kwenye picha ya eksirei. Iwapo una haraka sana, ondoa kitu hicho mfukoni mapema na uombe kikaguliwe kwa mkono.
▪ King’ora kikilia, shirikiana na mhudumu na utoe maelezo bila kukawia. Iwapo mhudumu anajua kwamba kitu kimoja tu ndicho kimesababisha king’ora kilie na kuna mhudumu mwingine mwenye kifaa cha kutambua chuma ambacho hushikwa kwa mkono, atakuelekeza kwake.
▪ Ama kwa hakika, ukifanya mzaha kuhusu utekaji nyara au bomu, safari yako itaishia hapo.
Zaidi ya kukaguliwa kabisa na maafisa wa usalama kwenye uwanja wa ndege, huenda pia ukashtakiwa.Safiri Salama!
Je, inawezekana kuchagua ndege salama? Ndiyo. Hata ukichagua kusafiri kwa ndege yoyote ile, kuna uwezekano mkubwa sana wa kuwasili salama salimini. Ukiwa na shaka, chunguza rekodi za usalama za shirika la ndege unalotaka kutumia. Kumbuka kwamba ijapokuwa misiba ya ndege hutokea, usafiri wa ndege ungali mojawapo ya njia salama zaidi za kusafiri.
Kwa sasa, sote tunaweza kutarajia wakati ambapo kutakuwa na usalama na hali ya kuaminiana chini ya utawala wa Mungu juu ya dunia. Katika jamii ya wanadamu yenye amani na inayomhofu Mungu, watu wanaohatarisha uhai wa wanadamu hawatakuwapo. Watu “watakuwa salama salimini bila hofu ya msiba.”—Mithali 1:33, Holy Bible—Contemporary English Version. *
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 19 Ili upate habari nyingine zinazohusiana na hizi ona makala “Kufanya Usafiri wa Ndege Uwe Salama Zaidi,” Amkeni!, Septemba 22, 2000; “Safiri Salama!” Amkeni!, Septemba 8, 2000; “Ni Nini Kinachohusika ili Ziendelee Kusafiri Angani?” Amkeni!, Septemba 8, 1999; “Ndege Ni Salama Kadiri Gani?” Amkeni!, Machi 8, 1999.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10, 11]
MADOKEZO FULANI KUHUSU USALAMA
Safiri kwa ndege inayoenda moja kwa moja bila kutua kwenye viwanja mbalimbali. Misiba mingi hutokea wakati ndege inapoanza safari, inapopaa, inaposhuka, au kutua. Kusafiri kwa ndege inayoenda moja kwa moja bila kutua kwenye viwanja mbalimbali kutapunguza hatari hizo.
Chagua ndege kubwa. Kwa kawaida ndege inayoweza kubeba zaidi ya abiria 30 huundwa na kukaguliwa kulingana na viwango vya juu kuliko ndege ndogo. Pia, ijapokuwa uwezekano wa kupata msiba mkubwa ni mdogo sana, ni rahisi zaidi kwa abiria wa ndege kubwa kuokoka.
Sikiliza kwa makini madokezo yanapotolewa kabla ya safari kuanza. Ijapokuwa huenda ikawa umesikia madokezo hayo mara nyingi, milango ya dharura iliyo karibu nawe inaweza kuwa mahali tofauti kabisa ikitegemea ndege unayotumia au mahali kiti chako kilipo.
Usiweke vitu vizito kwenye sehemu ya mizigo iliyo juu yako. Huenda sehemu za kuwekea mizigo zilizo juu yako zisiweze kuhimili vitu vizito sana kunapotokea msukosuko angani, kwa hiyo iwapo unabeba kitu kizito, acha kiwekwe pamoja na ile mizigo mingine mapema.
Funga mkanda wa usalama unapoketi. Kufunga mkanda wa usalama unapoketi kutakukinga endapo ndege itakumbwa na msukosuko wa ghafula angani.
Wasikilize wahudumu wa ndege. Wahudumu wa ndege huwa ndani ya ndege hasa kwa sababu ya usalama, kwa hiyo mmoja wao akikuambia ufanye jambo fulani, tii mara moja, ukiwa na maswali muulize baadaye.
Usibebe kitu chochote hatari. Kuna vitu vingi hatari ambavyo haviruhusiwi, lakini hata wewe mwenyewe unajua kwamba haifai kubeba petroli, kemikali au asidi kali, gesi zenye sumu, na vifaa vingine kama hivyo katika ndege isipokuwa uwe umepewa ruhusa na shirika la ndege na viwe vimepakiwa katika kontena inayofaa.
Usinywe kileo kupita kiasi. Kileo huathiri mtu zaidi anapokuwa ndani ya ndege kuliko anapokuwa ardhini. Kuwa na kiasi ni muhimu kila mahali.
Uwe chonjo. Japo si rahisi kutokee hali ya dharura, hali kama hiyo ikitokea, kama vile abiria wakihitaji kuhamishwa haraka ili kuepuka hatari, fuata maagizo ya wahudumu wa ndege na wafanyakazi wengine na uondoke katika ndege haraka iwezekanavyo.
[Hisani]
Chanzo: AirSafe.com
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]
KUWATULIZA WATU WA FAMILIA YAKO
Madokezo yafuatayo yanaonyesha jinsi unavyoweza kuwasaidia watu wa familia yako wasiwe na wasiwasi unaposafiri. Yametolewa kwenye kituo cha Internet cha United Behavioral Health
Zungumza na watu wa familia yako. Kabla ya kwenda safarini, tumia muda fulani pamoja na wapendwa wako ili mzungumzie usalama wako na vilevile usalama wao. Eleza hatua mpya ambazo zimechukuliwa kuimarisha usalama na jinsi zinavyochangia usalama wako unaposafiri.
Acha waeleze mahangaiko yao. Acha watu wa familia yako waeleze wasiwasi wao. Wanakupenda na wanataka tu uwe salama. Sikiliza kwa makini bila kuwachambua, na uchukue mahangaiko yao kwa uzito.
Wape uhakikisho wa kweli. Zungumzia jinsi ambavyo mashirika mbalimbali yanajaribu kuzuia mashambulizi mengine ya magaidi. Hiyo inatia ndani hatua zaidi za kuimarisha usalama kwenye viwanja vya ndege na ndani ya ndege. Uwezekano wa msiba kutokea unaposafiri kwa ndege ni mdogo sana.
Endelea kuwasiliana nao. Waahidi kuwa utawapigia simu utakapofika. Endelea kupiga simu nyumbani kwa ukawaida kwa muda ambao utakuwa safarini. Pia, ni muhimu familia yako ijue namna ya kuwasiliana nawe endapo hali za dharura zitatokea.
[Hisani]
Taken from the United Behavioral Health Web site
[Picha katika ukurasa wa 10]
Uwe tayari kushirikiana na wahudumu kwenye vituo vya ukaguzi