Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Cheka Uwe na Afya Bora!
Kicheko cha kutoka moyoni hutimiza mambo mengi zaidi ya kuleta furaha. Kulingana na madaktari kadhaa huko Japan, kicheko husawazisha mifumo ya tezi, ya neva, na ya kinga, huimarisha mpigo wa moyo na kupumua, na unaweza kuwatuliza kwa muda wale wanaougua baridi-yabisi. Kicheko huimarisha mzunguko wa damu kwenye misuli na kuongeza utendaji wa ubongo. Sisi huzoeza misuli yetu tunapoangua kicheko. Uchunguzi uliotajwa katika gazeti la IHT Asahi Shimbun, ulisema kwamba misuli katika tumbo la mcheshi fulani “ilipata mazoezi sawa na ya mtu aliyefanya mazoezi ya kulala chali na kuketi.” Daktari mmoja wa akili huko Osaka, Michio Tanaka, alisifu matokeo mazuri ya ucheshi. Tanaka alisema kwamba kicheko “ni kama dawa nzuri isiyo na madhara yoyote.”
Wanyama “Madaktari”
“Idadi inayoongezeka ya wataalamu wa tabia za wanyama sasa wanafikiri kwamba wanyama wa mwitu wanaweza na hushughulikia mahitaji yao ya kitiba,” laripoti gazeti The Economist la London. Sokwe huko Tanzania huondoa minyoo tumboni kwa kula sehemu ya mmea wenye kemikali ambazo huua minyoo hao. Na sokwe kotekote Afrika hula majani yenye miiba midogo sana ambayo huondoa minyoo tumboni. Aina fulani za kasuku wanaokula mbegu zenye sumu pia hula udongo wa mfinyanzi, ambao huondoa sumu katika mlo huo hatari. Dubu wa kahawia wa Alaska, bata bukini wa theluji wa Kanada, na mbwa-mwitu hula mimea ili kuondoa wadudu tumboni. Uchunguzi wa damu ya baadhi ya wanyama wa mwitu unaonyesha kwamba wengi wao wameepuka kupata maambukizo hatari ya virusi na bakteria katika makao yao ya kiasili ambayo mara nyingi huua wanyama waliofungiwa. “Matokeo ya uchunguzi huo yanadokeza kwamba wanyama wa mwitu wanaweza kufanya mambo fulani kudumisha afya yao ambayo wanyama waliofungiwa hawawezi,” lasema gazeti The Economist.
Kisababishi Kikuu cha Kifo
“UKIMWI unatazamiwa kuenea zaidi hata kuliko ile tauni iliyotokea Asia na Ulaya katika karne ya 14,” lasema gazeti New Scientist. “Tauni hiyo ya karne ya 14 ilisababisha vifo vya watu milioni 40 hivi huko Ulaya na Asia. Sasa, miaka 700 hivi baadaye, jambo kama hilo linatokea tena.” Kulingana na ripoti ya jarida British Medical Journal karibu watu milioni 65 watakufa kufikia mwaka wa 2010 kutokana na virusi vya HIV. Ingawa watu wengi wanaathiriwa na maradhi ya kifua kikuu na malaria, magonjwa hayo hayaathiri uchumi na jamii sana kama ugonjwa wa UKIMWI.
Wazazi na Vijana
Kulingana na ripoti katika gazeti la The Times la London, wazazi huathiriwa zaidi kihisia na kiakili na migogoro katika jamaa kuliko vijana wao. Ripoti hiyo inadokeza kwamba wazazi hawapaswi “kusumbuka kupita kiasi huku wakiogopa kuumiza hisia nyepesi za vijana hao.” Kinyume chake, ‘wazazi wanapaswa kuwa thabiti ili kuepuka kujiumiza.’ Profesa Laurence Steinberg, mtafiti wa masuala ya vijana waliobalehe katika Chuo Kikuu cha Temple, Philadelphia, Pennsylvania, Marekani, anasema kwamba watoto wana uwezo mkubwa zaidi wa kurudia hali yao ya kawaida baada ya mgogoro kuliko jinsi ambavyo watu hufikiri. Baada ya kuchunguza maelfu ya wazazi kwa zaidi ya miaka kumi, Profesa Steinberg asema: “Mzazi aliye na mamlaka zaidi ni mchangamfu na mwenye kujali, lakini thabiti na asiye na kigeugeu kwa kuweka na kushikilia miongozo, viwango na kanuni.” Ripoti hiyo inasema kwamba vijana wanaobalehe waliolelewa katika jamaa kama hizo hufanikiwa sana, huwa wenye furaha zaidi, na hivyo hawaelekei kujihusisha na tabia mbaya na uhalifu.
Uhitaji wa Kuguswa
“Tunahitaji kuguswa kama vile tunavyohitaji mwangaza wa jua, maji, na chakula,” lasema gazeti la Poland la kila juma Polityka. Ngozi yetu ina chembe nyingi zinazotambua mguso. Tunapoguswa na mtu, “ubongo wetu hutambua jambo hilo, hulielewa, na kutokeza tabasamu, furaha, au hisia nyingine ya kirafiki.” Watoto wanahitaji kuguswa, hasa wanapokuwa wachanga. Kwa kusikitisha, wazazi wengi huwashika watoto wao wakati tu wanapowavisha, wanapowaosha, wanapowalisha, au kuwaadhibu. Lakini uchunguzi umeonyesha kwamba watoto wanaoshikwa, kukumbatiwa, kupigwa busu, na kupapaswa huwa na afya bora na hukua na kuwa wenye akili kuliko wale “wasioshikwa,” lasema gazeti Polityka.
Maziwa ya Ulimwenguni Yamo Taabani
“Hakuna ziwa lolote duniani ambalo halijaathiriwa na utendaji wa wanadamu,” asema William Cosgrove, naibu-msimamizi wa Baraza la Maji Duniani. “Tunaharibu maziwa yetu, na hilo laweza kuwaathiri sana watu wanaotegemea maziwa hayo.” Cosgrove alisema kwamba maziwa hayo huchafuliwa na viwanda, mashamba, na maji machafu; na ziwa linaweza kuonekana likiwa safi hata ingawa limeharibiwa. Halafu akaongezea hivi: “Kisha jambo fulani linaweza kutokea—kama badiliko katika joto la maji—na kulibadili ziwa kabisa. Badiliko hilo lianzapo, ni vigumu kulikomesha.” Mfano mmoja ni wa Ziwa Viktoria, ziwa kubwa zaidi Afrika. Kwa muda wa miaka ishirini iliyopita, aina kadhaa za samaki zimetoweka kwa sababu ya uchafuzi uliotia ndani maji machafu yaliyoingizwa humo bila kutiwa dawa. Ziwa jingine lililo taabani ni Ziwa Tai Hu nchini China. “Wataalamu husema kwamba mtu anaweza kujaribu kutembea juu ya maji ya ziwa hilo kwa sababu limechafuliwa sana,” ilisema taarifa ya Baraza la Maji Duniani. Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Reuters, karibu asilimia 90 ya maji safi ambayo watu hutumia hutoka kwenye maziwa.
‘Moyo Umefurika Lakini Ubongo Hauna Chochote’
Barua za mapenzi zilizoandikwa na wataalamu wa kuandika barua zinapendwa na watu wengi, kulingana na gazeti la Ujerumani la kila juma Die Woche. Watu ambao hawawezi kuelezea hisia zao katika maandishi wanaweza kulipia huduma za uandishi zinazopatikana. Ikitegemea ombi la mteja, huenda barua hizo zikawa za kueleza hisia au za kibiashara. Pia, kuna mashairi ambayo mtu anaweza kulipia kiasi ambacho wamekubaliana na mwandishi. Kuna njia nyingi za kutunga hisia hizo bandia za kimapenzi. Waandishi wengine ni waandishi mashuhuri au waandishi wa habari, lakini wengine huandika ili tu kujifurahisha. Kwa kutumia kompyuta, wengine hutuma maswali kwa wateja na kompyuta huandika barua kulingana na habari zilizotolewa. Vyovyote vile, hakuna uhakika wa kufanikiwa. Baada ya kutuma “barua zenye hisia tele na ahadi nyingi” zilizotungwa na mwandishi fulani kwa muda wa miaka mitatu, bado mteja fulani mwaminifu hakufanikiwa kumsadikisha rafiki yake msichana akubali kuolewa naye.
Mazoezi na Kutokwenda Kazini
Kufanya mazoezi hupunguza tatizo la kutokwenda kazini kwa sababu ya ugonjwa, kulingana na uchunguzi uliofanywa na Chama cha Mazoezi ya Kimwili cha Finland. Waajiri wengi nchini Finland wametambua umuhimu wa jambo hilo katika kuwasaidia wafanyakazi wasikose kufika kazini. “Nusu ya wafanyakazi nchini Finland hufanya kazi katika makampuni yenye programu za kufanya mazoezi,” charipoti kichapo Finnfacts, cha Muungano wa Wenye Viwanda na Waajiri wa Finland. “Kampuni zina programu za kuwasaidia watu waache kuvuta sigara na aina mbalimbali za mazoezi.” Kampuni nchini Finland hutumia zaidi ya dola 67,000,000 za Marekani kila mwaka katika programu hizo, kwani wafanyakazi wakipunguza siku za kutokwenda kazini, faida zitaongezeka mara nyingi zaidi.
Tunza Mgongo Wako!
“Kuketi vibaya, kuwa mnene kupita kiasi, na kutofanya mazoezi ya kutosha ya kimwili hudhoofisha uti wa mgongo pole kwa pole,” lasema gazeti la Hispania El País Semanal. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya watu katika nchi zilizoendelea hupata matatizo ya mgongo maishani mwao. Kliniki ya Kovacs ya Hispania, ambayo hushughulikia matatizo ya uti wa mgongo hupendekeza kwamba tujifunze kurekebisha jinsi tunavyoketi ili tuzuie na kupunguza maumivu ya mgongo. Mapendekezo rahisi ni: Lala kwa upande, huku uti wa mgongo ukiwa umenyooka. Unapoketi, pumzisha mgongo wako kitini. Unapotumia kompyuta, acha mabega yako yastarehe. Ikiwa ni lazima uiname, kunja magoti yako badala ya mgongo. Ukihitaji kusimama kwa muda mrefu, simama kwa mguu mmoja na upumzishe ule mwingine kwenye stuli au katika hatua ya ngazi.