Niliacha Vita Nikaanza Kutafuta Amani
Niliacha Vita Nikaanza Kutafuta Amani
SIMULIZI LA TOSHIAKI NIWA
Alikuwa rubani wa ndege za kivita za Japan aliyepata mafunzo ya kujilipua ya kamikaze kwenye meli za kivita za Marekani wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu na anasimulia jinsi alivyohisi alipokuwa akingojea safari yake ya kushambulia kwa kujilipia.
JITIHADA za Japan za kuteka eneo la Pasifiki zilikoma wakati iliposhindwa vibaya katika vita vilivyopiganwa karibu na visiwa vya Midway mnamo Juni 1942. Kuanzia wakati huo, Japan ilianza kushindwa kwenye pigano moja baada ya jingine na maeneo ambayo ilikuwa imeteka yakaanza kunyakuliwa na Marekani na washirika wake.
Mnamo Septemba 1943, serikali ya Japan ilitangaza kwamba wanafunzi wa vyuo vikuu ambao haikuwa lazima wawe jeshini sasa walipaswa kuandikishwa. Basi mwezi wa Desemba, nikiwa na umri wa miaka 20, nikaacha chuo kikuu nikajiunga na jeshi la wanamaji. Mwezi mmoja baadaye nilianza kupokea mafunzo ya kuwa rubani wa ndege ya kivita. Mnamo Desemba 1944, nilipata mafunzo ya kuendesha ndege za kivita zilizoitwa Zero.
Kikosi Maalumu cha Kamikaze
Japan ilielekea kushindwa vitani. Kufikia Februari 1945, Japan ilishambuliwa vikali na ndege za kijeshi aina ya B-29. Wakati huohuo, vikosi maalumu vya wanamaji vya Marekani vilikuwa vinakaribia Japan, jambo lililofanya iwe rahisi kushambuliwa na ndege zinazobebwa na meli.
Miezi michache mapema, viongozi wa kijeshi wa Japan waliamua kupigana vita ya mwisho kwa kutumia mbinu za kujiua. Ingawa kufikia wakati huo ilibainika wazi kwamba Japan haingeshinda vita hiyo, uamuzi huo uliongeza muda wa vita na idadi ya vifo na majeruhi.
Hivyo, Kikosi Maalumu cha Kamikaze kikaanzishwa. Jina hilo lilitokana na upepo wa kimungu ulioitwa kamikaze, ambao kulingana na mapokeo, ni kimbunga kilichopeperusha meli za Wamongolia waliowavamia katika miaka ya 1200. Shambulizi la kwanza la kamikaze lilifanywa kwa kutumia ndege tano aina ya Zero zilizokuwa na bomu lenye uzito wa kilogramu 250 kila moja na ndege hizo zingeendeshwa zijilipue kwenye meli za adui.
Amri ilitolewa ya kuunda kikosi maalumu cha wanajeshi wa kujiua kutokana na Kikosi cha Ndege cha Wanamaji cha Yatabe, na mimi nilikuwa katika kikosi hicho. Sote tulipokea fomu ya kujaza kuonyesha kama tulikuwa tayari kujitolea kuwa wanajeshi wa kujiua.
Niliona kwamba nilipaswa kudhabihu uhai wangu kwa ajili ya nchi yangu. Lakini hata kama ningejitolea kufa kwa kuendesha ndege ya kujiua, ndege yangu ingeangushwa kabla ya kushambulia, na hivyo ningepoteza uhai wangu bure. Je, mama yangu angefurahi iwapo ningekufa bila kutimiza wajibu wangu wa familia? Ilikuwa vigumu kuamua kama nilikuwa nikitumia maisha yangu vizuri kwa kujitolea kufa vitani. Bado niliamua kujitolea.
Mnamo Machi 1945, kikundi cha kwanza cha Kikosi Maalumu cha Yatabe kilianzishwa. Wenzangu 29 walichaguliwa, lakini niliachwa. Baada ya kupokea mafunzo ya pekee, walipangiwa kuondoka ili kufanya mashambulizi hayo hatari kutoka uwanja wa ndege wa Kanoya, huko Kagoshima katika mwezi wa Aprili. Kabla rafiki zangu hawajahamishwa hadi Kanoya, niliwatembelea baadhi yao ili nijue maoni yao kabla ya kufanya mashambulizi hayo ya kujiua.
“Bila shaka tutakufa,” mmoja alisema kwa utulivu, “lakini wewe usikimbilie kifo. Iwapo yeyote kati yetu ataokoka, anapaswa kuwaeleza wengine umuhimu wa amani na kujitahidi kuipata.”
Mnamo Aprili 14, 1945, wenzangu waliondoka. Baada ya saa nyingi kupita, sote tulisikiliza taarifa ya habari ili tujue matokeo. Mtangazaji alisema: “Kikundi cha kwanza cha Kikosi Maalumu cha Kamikaze cha Showa kilishambulia adui baharini, mashariki mwa Kikaiga-Shima. Wote walikufa kwenye mashambulizi hayo.”
Bomu la Kibinadamu la Ohka
Miezi miwili baadaye, nilihamishwa hadi Kikosi cha Ndege cha Wanamaji cha Konoike nikiwa mmoja wa Washambuliaji Maalumu wa Jinrai. Neno Jinrai lamaanisha “ngurumo ya kimungu.” Washambuliaji hao waliendesha ndege zilizosindikiza ndege za kupigana na za kurusha mabomu.
Ndege hiyo yenye injini mbili ilibeba Ohka, jina linalomaanisha “maua ya cheri.” Hiyo Ohka iliwakilisha marubani wachanga waliokuwa tayari kudhabihu uhai wao. Chombo cha Ohka kilikuwa na kiti kimoja na mabawa yenye upana wa meta 5 na uzito wa kilogramu 440. Kilikuwa na baruti zenye uzito wa tani moja mbele.
Ndege ilipokaribia shabaha, rubani aliingia ndani ya chombo cha Ohka nacho kilitenganishwa na ndege. Chombo hicho kiligonga shabaha baada ya kusafiri kwa msaada wa roketi tatu ambazo zilidumu kwa muda wa sekunde kumi kila moja. Chombo hicho kingeweza kusemwa kwa kufaa kuwa bomu la kibinadamu. Mara tu kilipoachiliwa, kwisha!
Wakati wa mazoezi, rubani wa Ohka aliruka kwa mwavuli kuelekea shabaha fulani kutoka kwenye ndege aina ya Zero iliyokuwa ikipaa kwa kimo cha meta 6,000 juu. Niliwaona marubani wengi wakifa katika mazoezi hayo.
Mapema, kabla ya kuhamishwa kwenye kikosi hicho, kikundi cha kwanza kilikuwa kimeondoka. Kilikuwa na ndege za kushambulia 18 zenye Ohka, na kilisindikizwa na ndege 19 za kivita. Ndege hizo zilikuwa nzito na hazikuwa na mwendo wa kasi. Hakuna hata moja iliyofikia shabaha yake. Zote ziliangushwa na ndege za Marekani.
Kikosi cha Jinrai kililazimika kwenda vitani bila kusindikizwa kwa sababu ndege zote ziliangushwa. Wote walioenda kwenye mashambulizi ya baadaye hawakurudi. Walikufa na kutoweka kwenye vita ya Okinawa.
Vita Yakaribia Mwisho
Mnamo Agosti 1945, nilihamishwa nikapelekwa kwenye Kikosi cha Ndege cha Wanamaji cha Otsu. Kituo nilichohamia kilikuwa chini ya Mlima Hieizan karibu na jiji la Kyoto. Kwa sababu vikosi vya Marekani vilitazamiwa kushambulia Japan, mipango ilifanywa ya kurusha vyombo vya Ohka kwenye meli za Marekani kutoka mlimani, vikiwa na wanajeshi wa kujiua. Reli zilizokusudiwa kutumiwa na Ohka zilitayarishwa mlimani.
Tulingoja amri ya kuondoka. Lakini amri hiyo haikutolewa. Mji wa Hiroshima na Nagasaki uliharibiwa kwa mabomu ya atomu Agosti 6 na 9. Kisha Agosti 15, Japan ilisalimu amri katika vita yake na Marekani na washiriki wake bila masharti yoyote. Hatimaye, vita ilimalizika. Niliponea chupuchupu.
Kufikia mwishoni mwa Agosti, nilirudi mjini kwetu huko Yokohama, lakini nyumba yangu ilikuwa majivu kutokana na mashambulizi ya mabomu ya ndege za B-29. Tayari familia yetu ilikuwa imekata tamaa. Dada yangu na mwanawe waliangamizwa na moto wa mabomu. Hata hivyo, tulifarijika ndugu yangu mdogo aliporudi nyumbani salama salimini.
Licha ya uharibifu mkubwa na ukosefu mwingi wa chakula, nilirejea kwenye chuo kikuu ili nikamilishe masomo yangu. Baada ya mwaka mmoja, nilifuzu na kupata kazi. Mnamo mwaka wa 1953, nilimwoa Michiko na baadaye nikawa baba ya wavulana wawili.
Jitihada Zangu za Kutafuta Amani
Mnamo mwaka wa 1974, Michiko alianza kujifunza Biblia na Shahidi wa Yehova. Punde si punde alianza kuhudhuria mikutano na kushiriki katika kazi ya kuhubiri. Sikupenda jinsi alivyokuwa akitoka mara nyingi. Alisema kwamba huduma ya Kikristo ilimfanya apate amani ya kweli na furaha. Nikafikiri kwamba iwapo hiyo ni kweli, basi sipaswi kumzuia. Inafaa nishirikiane naye.
Karibu na wakati huo, mlinzi fulani aliyefanya kazi katika kampuni yangu alistaafu. Kabla ya kupata mlinzi mwingine, niliwaajiri vijana wachache Mashahidi wafanye kazi ya kulinda usiku. Walipokuja, niliwauliza kuhusu dini yao na huduma yao. Nilishangaa kujua kwamba, tofauti na vijana wengine wa umri wao, walikuwa na mradi maishani na moyo wa kujitolea. Walijifunza sifa hizo katika Biblia. Walieleza kwamba Mashahidi duniani kote hawana ubaguzi wa rangi na wanatii amri ya Biblia ya kumpenda Mungu na majirani. (Mathayo 22:36-40) Wanawaona wenzao kuwa ndugu na dada, bila kujali mataifa waliyotoka.—Yohana 13:35; 1 Petro 2:17.
‘Hiyo haiwezekani,’ niliwaza. Kwa kuwa dini nyingi za Jumuiya ya Wakristo zilikuwa zinapigana, sikuamini kwamba Mashahidi wa Yehova ni tofauti.
Niliwaambia siamini. Wakitumia Yearbook of Jehovah’s Witnesses, vijana hao Mashahidi walinionyesha jinsi Mashahidi huko Ujerumani walivyofungwa, hata kuuawa, kwa sababu ya kukataa
kuunga mkono upande wowote wakati wa utawala wa Hitler. Nikasadiki kwamba Mashahidi wa Yehova ni Wakristo wa kweli.Mke wangu alionyesha wakfu wake kwa Mungu kwa ubatizo wa maji Desemba 1975. Wakati huo niliombwa nijifunze Biblia. Hata hivyo, nilipofikiri kuhusu majukumu yangu ya kifedha, kama ya kuwaelimisha wana wangu, kulipia nyumba yetu, sikupata ujasiri wa kukubali funzo hilo. Kutanikoni, wanaume waliokuwa wameoa walikuwa wakirekebisha kazi zao ili wapate nafasi zaidi kwa ajili ya mambo ya kiroho na kuwa na familia zao. Nilidhani kwamba ningehitajiwa kufanya hivyo pia. Lakini nilipoonyeshwa jinsi maisha ya Kikristo yanavyoweza kusawazishwa na kazi ya kimwili, hatimaye niliamua kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova.
Uamuzi wa Kumtumikia Mungu wa Amani
Baada ya kujifunza Biblia kwa miaka miwili, mwalimu wangu aliniuliza kama niliwahi kufikiria kuweka maisha yangu wakfu kwa Mungu. Hata hivyo, sikuweza kuchukua hatua hiyo, na jambo hilo lilinisumbua.
Siku moja muda mfupi baadaye, nilikuwa nikishuka orofani kwa haraka. Kwenye ile hekaheka nikajikwaa, nikaanguka, nikagongwa kisogo, nikapoteza fahamu. Niliporudiwa na fahamu, niliona nyuso nyingi zilizokuwa na wasiwasi. Nilikuwa na maumivu makali kichwani na nilipelekwa hospitali kwa ambulansi. Ingawa kisogo changu kilikuwa kimefura sana, sikuwa nimevunjika wala kuvuja damu kichwani.
Nilimshukuru Yehova sana kwa kuwa hai! Kuanzia wakati huo, niliazimia kutumia uhai wangu kufanya mapenzi ya Yehova, na nikajiweka wakfu kwake. Nilibatizwa Julai 1977, nikiwa na umri wa miaka 53. Mwanangu mkubwa, Yasuyuki, pia alijifunza Biblia na kubatizwa miaka miwili baadaye.
Miaka kumi baada ya kubatizwa, nilistaafu. Katika miaka yote hiyo, niliishi maisha ya Kikristo, nikiyasawazisha na kazi yangu ya kimwili. Sasa nina pendeleo la kutumikia nikiwa mzee katika kutaniko moja la Yokohama, nikitumia wakati mwingi katika huduma ya Kikristo. Mwanangu mkubwa anatumikia akiwa mzee na mtumishi wa wakati wote katika kutaniko jirani.
Nikiwa nimeokoka kikosi cha pekee cha kujiua, ninafurahi kuwa hai na ninahisi nimependelewa kushiriki kuhubiri “habari njema hii ya Ufalme.” (Mathayo 24:14) Ninasadiki kabisa kwamba njia bora zaidi ya kuishi ni kuwa miongoni mwa watu wa Mungu. (Zaburi 144:15) Kwenye ulimwengu mpya unaokaribia, wanadamu hawatapigana tena, kwa sababu “taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”—Isaya 2:4.
Ikiwa ni mapenzi ya Mungu, ningependa kukutana na watu niliowajua ambao walikufa vitani watakaofufuliwa. Itasisimua kama nini kuzungumza nao kuhusu taraja la kuishi kwa amani katika paradiso duniani chini ya utawala wenye uadilifu wa Ufalme wa mbinguni wa Mungu!—Mathayo 6:9, 10; Matendo 24:15; 1 Timotheo 6:19.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Nilipokuwa katika kikosi cha ndege cha wanamaji
[Picha katika ukurasa wa 18, 19]
Bomu la kibinadamu la “Ohka”
[Hisani]
© CORBIS
[Picha katika ukurasa wa 20]
Wanajeshi wenzangu kabla ya mashambulizi ya kujiua. Ni mimi tu ningali hai, wa pili kushoto
[Picha katika ukurasa wa 21]
Nikiwa na mke wangu Michiko, na mwana wetu mkubwa, Yasuyuki
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
U.S. National Archives photo