Unaweza Kuona Ubuni Katika Uumbaji
Unaweza Kuona Ubuni Katika Uumbaji
WATU wengi hutambua uzuri wa uumbaji wanapotembea mashambani. Wanaweza kuuona katika maua, ndege maridadi, miti mikubwa sana, au mandhari ya kuvutia. Watu wengi wanatambua kwamba ni Muumba au Mbuni Stadi aliyetokeza vitu hivyo.
Labda unadhani kwamba ni wanasayansi pekee ambao wanaweza kutambua uzuri wa uumbaji. Hata hivyo, huhitaji vifaa vya hali ya juu vya kisayansi ili utambue umaridadi wa uumbaji. Unahitaji tu kutazama vizuri, kufikiri kidogo, na kutambua uzuri na namna mbalimbali ya uumbaji. Labda unahitaji kutazama kwa makini zaidi vitu vya kawaida ambavyo pengine hujawahi kuvifikiria sana.
Umbo mojawapo sahili zaidi ni la zongomo. Umbo hilo laweza kupatikana katika vitu vya kawaida vilivyotengenezwa na wanadamu kama kamba au kifaa cha kuchomoa vifuniko. Hata hivyo, koa za baharini au mbegu za misonobari zina zongomo bora zaidi. Pia, ukiangalia kwa makini katikati ya ua la alizeti, unaweza kuona umbo la zongomo. Zongomo pia huonekana katikati ya waridi na utando wa buibui, ingawa si dhahiri sana.
Tazama kwa makini utando wa buibui. Kwanza, buibui huweka nguzo za utando kama nyaya za gurudumu. Baadaye yeye huanza kuunganisha nguzo hizo pamoja kwa uzi wa hariri wenye kunata kuanzia katikati ya utando. Buibui huendelea kuzungusha uzi huo hatua kwa hatua mpaka utando ukamilike. Umbo hilo la zongomo hutokana na uzi huo ambao huzidi kupanuka.
Umbo jingine la kupendeza linalopatikana kiasili ni mfano wa jicho. Umbo hilo hupatikana mahali pasipotarajiwa kabisa—kwenye manyoya ya ndege, katika mabawa ya kipepeo, au hata kwenye magamba ya samaki. Wanasayansi husema kwamba mfano huo wa jicho unaweza kusaidia kuanzisha kujamiiana, kukengeusha washambuliaji, au kuepusha wanyama wengine. Labda tausi ndiye mfano bora zaidi wa ndege mwenye mfano wa jicho, na dansi yake wakati wa kujamiiana ni mojawapo ya maajabu ya uumbaji. Aleksanda Mkuu alivutiwa sana na urembo wa tausi hivi kwamba akapendekeza ndege hao walindwe kotekote katika milki yake.
Maumbo mengine ya kawaida ni mviringo na duara. Sisi huvutiwa daima na umbo la duara la jua lenye rangi ya dhahabu wakati wa machweo au la mwezi mpevu wenye rangi ya fedha. Maua aina nyingi ya kibibi yana umbo la jua, nayo hutoa maua yenye rangi mbalimbali, na kitovu chenye rangi ya manjano. “Jicho” la maua hayo ambayo hupatikana katika maeneo mbalimbali, lina kinywaji kinachowavutia vipepeo, jinsi ufuo wenye kupendeza huwavutia watalii.
Kwa kuwa umbo la duara ndilo umbo linalofaa zaidi, matunda na beri huwa katika umbo hilo. Rangi zake zenye kupendeza huwavutia ndege, ambao hutawanya mbegu za matunda hayo kwa kubadilishana na mlo mtamu.
Bila shaka zongomo, mfano wa jicho, mviringo na duara ni mifano michache tu ya maumbo mengi ya asili. Ingawa mengine huenda yakawa na kazi hususa, mengine ni mapambo au ya kupumbaza tu. Vyovyote vile, yaangalie na uyafurahie.
[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 26]