Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wimbi Jipya la Jeuri Kwenye Michezo ya Watoto

Wimbi Jipya la Jeuri Kwenye Michezo ya Watoto

Wimbi Jipya la Jeuri Kwenye Michezo ya Watoto

▪ Kikundi cha wanafunzi wa shule ya sekondari chakutana ili kucheza mpira. Baada ya mechi kwisha ghasia zinatokea, wazazi, makocha, na wachezaji zaidi ya 100 wanapiga makelele na kurushiana ngumi timu moja inaposhinda katika muda wa ziada.

▪ Kikundi cha vijana wenye umri wa kati ya miaka 9 hadi 12 wanacheza mpira wa wasichana na wavulana. Mchezaji mwenye umri wa miaka kumi anarushiwa mpira, lakini unapoanguka kocha anamwangusha chini na kumvunja mikono yote miwili.

▪ Kocha wa ligi ndogo ya besiboli amwondoa mchezaji wake mmoja. Baba ya kijana huyo atisha kumuua kocha na anafungwa jela kwa siku 45.

▪ Wakati wa mazoezi ya mpira wa magongo unaochezwa juu ya barafu, baba wawili wanabishana kuhusu sheria za mchezo huo. Baba mmoja ampiga mwingine na kumuua huku watoto wake watatu wakitazama.

RIPOTI zenye kuogofya kama hizo zimeongezeka sana. Kwenye viwanja mbalimbali na njia za kutelezea juu ya barafu, wimbi jipya la jeuri linazidi kuenea. Jeuri hiyo inasababishwa na wazazi na makocha ambao wanaona ni afadhali kupigana kuliko kukubali kushindwa. Msimamizi wa Shirika la Riadha la Jupiter-Tequesta (Florida) Jeffrey Leslie anasema: “Nimewaona wazazi wakiwafokea watoto wao, wakiwashurutisha wakazane zaidi; wakiwachochea watoto wao wapigane wakati wa michezo; wakiwaaibisha watoto wao na kuwafanya walie.” Anaongeza kusema: “Hakuna jambo jingine ambalo huwafanya wazazi watende vibaya kama michezo ya vijana.” Ili kulinda watoto dhidi ya jeuri, jamii nyingine zimewazuia wazazi fulani kuwepo wakati watoto wao wanapocheza.

Wimbi hilo la jeuri limekuwa na matokeo gani? “Mwenendo huo wenye aibu wa idadi inayoongezeka ya watu wazima,” asema Fred Engh, mwanzilishi na msimamizi wa Muungano wa Kitaifa wa Michezo ya Vijana huko Florida, “unaharibu michezo ya vijana, hauleti furaha, na unawawekea mamilioni ya watoto mfano mbaya.”

Kupata Ushindi kwa Vyovyote

Inaonekana tatizo hilo linasababishwa na wazazi wanaotaka watoto wao washinde kwa vyovyote. Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia Watoto Wasitendewe Vibaya, nchini Kanada asema: “Ikiwa kushinda ndilo jambo muhimu zaidi, ikiwa lengo kuu ni kuwa bingwa, basi wale walio dhaifu huumia. Kwenye michezo hiyo, watoto ndio ambao huumia.” Afisa wa Shirika la Mafunzo ya Kujenga Mwili na Afya la Ontario (Kanada) asema kwamba watoto wanaoshurutishwa kushinda “wanaweza kupata matatizo ya akili wakiwa bado ni wachanga. Wanapokuwa wakubwa, [huenda] ikawa vigumu kwao kukubali kushindwa.”

Si ajabu kwamba mara nyingi wanariadha wachanga huathiriwa na tabia ya wazazi wenye hasira na makocha wenye bidii ya kupita kiasi. Katika mechi ya voliboli ya wasichana, marefa walishambuliwa mara saba na wachezaji. Msichana mmoja aliharibu gari la afisa alipotolewa katika mchezo wa tenisi. Refa alipopuliza filimbi ya kuonyesha kwamba mpiganaji wa mieleka wa shule ya sekondari alicheza vibaya, mchezaji huyo alimgonga refa kichwani kwa kichwa chake mpaka refa akazirai. “Michezo ya vijana [ilijulikana] kuwa yenye utulivu,” asema Darrell Burnett, mwanasaikolojia wa watoto na michezo ya vijana. “Lakini sasa hali zimebadilika. Hiyo si michezo tena.”

Jambo Ambalo Wazazi Wanaweza Kufanya

Inafaa wazazi wakumbuke kwamba watoto hupendezwa na michezo kwa sababu ya kupata furaha na kufanya mazoezi kwenye michezo hiyo. Wazazi wanapoigeuza michezo ya watoto iwe kazi yenye kuleta mkazo mwingi na mahali pa kuwafokea watoto, hawawezi kupata matokeo yaliyokusudiwa na hilo si tendo la upendo. Biblia inasema: “Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu.”—Waefeso 6:4, Biblia Habari Njema.

Mzazi awezaje kudumisha usawaziko katika jambo hilo? Kwanza kabisa, huenda ikafaa kukumbuka hali yako ulipokuwa kijana. Je, ulicheza kama bingwa? Je, inafaa kumtazamia mwanao acheze kama bingwa? Ukweli ni kwamba “watoto ni dhaifu.” (Mwanzo 33:13, Zaire Swahili Bible) Pia, jaribu kuwa na maoni yanayofaa kuhusu kushinda na kushindwa. Biblia husema kwamba roho ya ushindani isiyodhibitiwa ni “ubatili na kujilisha upepo.”—Mhubiri 4:4.

Kwa kupendeza, aliyekuwa mchezaji wa ligi kuu ya besiboli huwahimiza wazazi wadumishe maoni yanayofaa kuhusu kushinda na kushindwa, wasikasirike watoto wao wasiposhinda wala kusisimuka kupita kiasi wanaposhinda. Badala ya kuona ushindi ukiwa jambo la maana zaidi, wazazi wanapaswa kuzingatia furaha ya watoto na afya yao njema.

Hivyo, wazazi wengine wameona kwamba michezo mingi ya watoto huchochea roho isiyofaa ya ushindani. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba watoto wao hawawezi kucheza pamoja na wengine. Kwa mfano, wazazi wengi Wakristo wametambua kwamba watoto wao hufurahi wanapocheza pamoja na waamini wenzao katika ua wa nyumbani au bustanini. Hapo wazazi wanaweza kudhibiti mashirika ya watoto wao. Pia, watoto wanaweza kucheza wakati wa matembezi ya familia. Ni kweli, kucheza kwenye ua wa nyumbani huenda kusitokeze msisimuko mwingi kama kushiriki katika mashindano. Hata hivyo, usisahau kwamba “mazoezi ya kimwili ni yenye manufaa kidogo (tu); lakini ujitoaji-kimungu ni wenye manufaa kwa mambo yote.” (1 Timotheo 4:8) Kwa kudumisha mtazamo huo wenye usawaziko kuhusiana na michezo, unaweza kumwepusha mtoto wako kutokana na madhara yanayoletwa na wimbi jipya la jeuri.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Michezo yapasa ifurahishe, si kuzusha mapigano