Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Abrolhos—Inavutia Macho

Abrolhos—Inavutia Macho

Abrolhos—Inavutia Macho

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

KATIKA karne ya 16, mabaharia waliokuwa karibu na pwani ya jimbo la Bahia huko Brazili, waliwatahadharisha mabaharia wenzao kuhusu miamba ya matumbawe iliyokuwa karibu kwa kusema: “Abra os olhos!” (Kaeni Macho!) Kulingana na masimulizi, visiwa vitano vidogo katika eneo hilo viliitwa Abrolhos kutokana na tahadhari hiyo iliyorudiwa mara nyingi.

Visiwa vya Abrolhos viko Kusini mwa Bahari ya Atlantiki, kilometa 80 tu kutoka kwenye miji ya pwani ya Caravelas na Alcobaça. Hata hivyo, eneo hilo limezungukwa na kutenganishwa na miamba ya matumbawe. Kama yule nyangumi mwenye nundu hangepatikana huko, mabaharia wengi hawangethubutu kufika kwenye eneo hilo ambalo lina miamba ya matumbawe iliyofichika na ambalo hukumbwa na dhoruba kali. Nyangumi huyo ana faida kubwa kiuchumi.

Kuwawinda na Kuwatazama Nyangumi

Katika miaka ya 1800, wakazi wengi wa miji ya pwani walijiruzuku hasa kutokana na nyangumi wa Abrolhos. Kabla ya kusafiri kwa mashua zenye tanga au za makasia hadi kwenye visiwa hivyo, wavuvi walihudhuria ibada maalumu ya Misa ambapo padri alibariki mashua zao. Wavuvi hao waliwezaje kumwua kiumbe mkubwa hivyo? Walimtega kwa upendo wake wa kisilika kwa watoto wake. Wavuvi hao walimdunga nyangumi mchanga kwa mkuki kisha wakajaribu kumvutia mamake kwa chambo hicho. Nyangumi waliouawa walivutwa hadi ufuoni kisha wakapelekwa kwenye mojawapo ya vile viwanda sita vya Caravelas ili mafuta yao yenye thamani yakamuliwe.

Hata hivyo, katikati ya miaka ya 1800, wateja wa mafuta ya nyangumi walipungua na biashara hiyo ilididimia. Kwa kuwa walikuwa wamevuliwa kwa makumi ya miaka, kufikia karne ya 20 karibu nyangumi wote wenye nundu walikuwa wameacha kuzaana katika eneo la Abrolhos. Hivyo, wavuvi waliacha kuvua nyangumi karibu na visiwa hivyo. Nyangumi wa mwisho alivuliwa katika eneo hilo mwaka 1929.

Mabadiliko yalitokea huko Abrolhos mnamo mwaka 1983 wakati vile visiwa vitano na miamba ya matumbawe ya Abrolhos—eneo lenye ukubwa wa kilometa 910 za mraba—vilipotangazwa na serikali kuwa hifadhi ya viumbe wa baharini. Kwa muda wa miaka 50 nyangumi hawakuwa wameonekana huko, lakini mnamo 1987, watafiti waliripoti kwamba nyangumi wameonekana katika hifadhi hiyo na wakaamua kufanya uchunguzi. Walistaajabu walipogundua kwamba nyangumi wenye nundu walikuwa wakizaana tena karibu na visiwa hivyo.

Habari kuhusu kuonekana kwa nyangumi na kuhusu mandhari zenye kupendeza za Abrolhos ziliwavutia wageni wachache kwenye eneo hilo. Asubuhi moja wakati wa kiangazi, familia moja ilisafiri kwa mashua ndogo toka Caravelas hadi Abrolhos. Safari hiyo inachukua saa sita. Hivi ndivyo mmoja wao alivyosimulia safari hiyo.

Miamba ya Matumbawe Yaliyo Kama Kuta na Kofia

“Nahodha wetu Manoel alipokuwa akiiongoza mashua kati ya miamba ya matumbawe inayoitwa Kuta za Miamba ya Matumbawe, nilielewa kile kilichowafanya mabaharia Wareno waogope eneo hilo. Nguzo za matumbawe yenye rangi mbalimbali zilitokeza juu ya maji. Nguzo hizo zina urefu wa meta 20 na upana wa meta 50 karibu na uso wa maji. Kwa kuwa miamba hiyo ya matumbawe ina umbo la uyoga, wenyeji wa eneo hilo wameiita kofia kubwa. Nguzo nyingi chini ya maji zimeshikamana na kuwa matao makubwa na vijia na hata kuta zenye urefu wa kilometa 20 ambazo zinatokeza juu ya maji kama majukwaa ya miamba. Hizo ndizo zinazoitwa Kuta za Miamba ya Matumbawe.

“Baada ya kuondoka kwenye miamba hiyo ya matumbawe, tuliona visiwa vya Abrolhos. Kwa mbali, visiwa hivyo vitano vinaonekana kama kabari kubwa sana zinazoelea juu ya bahari. Wanajiolojia wamedokeza kwamba hapo kale lava iliyokuwa ikipanda juu kutoka sakafu ya bahari iliinua miamba hiyo mikubwa na kuifanya itokeze. Ndiyo sababu visiwa hivyo vina maumbo sawa. Upande wa kusini-mashariki wa visiwa hivyo una jabali lenye mwinuko mkali ambalo limetokeza juu ya maji, na upande wa kusini-magharibi una mteremko usio mkali ambao unaishia kuwa ufuo mwembamba.

“Kisha tukaona mnara wa taa na nyumba zenye orofa mbili kwenye kisiwa kikubwa zaidi cha Abrolhos kinachoitwa Santa Bárbara. Wafanyakazi wa Taasisi ya Mazingira na Mali za Asili ya Brazili (IBAMA) na vilevile wanajeshi wa majini wa Brazili wanaoishi kwenye kisiwa hicho hutegemea bidhaa zinazoletwa kwa meli baada ya kila majuma mawili. Yaonekana hata mbuzi wa kisiwa hicho hutarajia meli hiyo kwa hamu, kwani isipofika wao ndio watakaokuwa kitoweo. Nyumba za wageni, mahoteli, mabaa, au mikahawa hairuhusiwi. Watalii wanaotaka kulala huko hulazimika kulala kwenye mashua zilizotiwa nanga karibu na visiwa hivyo.

“Manoel alipotia nanga kwa utaratibu, huku akiwa macho ili asigonge miamba ya matumbawe, wafanyakazi wawili wa taasisi ya IBAMA waliingia katika mashua yetu na kutueleza baadhi ya sheria za hifadhi hiyo. Watalii hutembelea visiwa viwili tu, Siriba na Redonda, nao hufuata vijia vyenye alama, na kuandamana sikuzote na mfanyakazi mmoja wa hifadhi hiyo. Hawapaswi kuvua samaki wala kuchukua kitu chochote—hata kijiwe kilicho ufuoni. Pia, kuna masharti ya kuwatazama nyangumi. Mashua tatu peke yake ndizo zinazoruhusiwa kuwakaribia nyangumi, na zinapaswa kuwa umbali wa meta 100 au zaidi. Nyangumi akikaribia mashua, injini inapasa kuzimwa na kuwashwa tu wakati nyangumi anapoibuka tena. Mashua zinapaswa kuondoka kwenye eneo hilo wakati nyangumi wanapoonekana kuwa wamesumbuka.”

Ndege Wanaovutia Macho

“Kuna ndege wengi huku. Kuna makundi ya ndege wa tropiki, polisi bawajeusi, polisi kahawia, ndege wa kustaajabisha anayeitwa frigate, na buabua mweusi.

“Tulipokuwa tukipanda kwenye ufuo wa Siriba wenye miamba-miamba siku ya kwanza ya safari yetu, Jordan, mtafiti wa taasisi ya IBAMA, alituonyesha viota vya ndege wanaoitwa polisi na vile vya ndege wa tropiki wenye mdomo mwekundu. Polisi hujenga kiota ardhini, lakini ndege huyo wa kitropiki hujenga kiota kwenye nyufa miambani ambako anajilinda na pepo kali zinazoweza kupeperusha kiota chake kwa urahisi.

“Ndege mwenye kustaajabisha zaidi kati ya ndege wote ni ndege anayeitwa frigate, ambaye ni mkubwa kama kuku. Katika kipindi cha kujamiiana, kifuko cha ndege wa kiume kilicho kwenye koo huwa na rangi nyekundu nyangavu na hufura kama mpira wa kandanda. Kwa kushangaza, ndege huyo hupata chakula baharini lakini anaogopa maji. Hana mafuta mengi ya kupaka kwenye manyoya yake, kwa hiyo hawezi kupiga mbizi ili kuwakamata samaki kwani atalowa.

“Kwa kuwa hawezi kupiga mbizi, ndege huyo hutumia uwezo wake wa kuruka. Ndege huyo ana mabawa yenye urefu wa meta mbili toka ncha moja hadi ncha nyingine, naye huelea hewani bila kusonga sana kwa kutumia mikondo ya hewa yenye joto. Yeye huwa macho kumnyemelea ndege anayeitwa polisi wakati anapokamata samaki. Polisi anapokamata samaki, ndege wa frigate humvamia kwa kasi na kumshambulia kwa mdomo wake mrefu uliojipinda. Nyakati nyingine yeye humnyang’anya samaki toka mdomoni. Polisi akimwangusha samaki, ndege wa frigate hushuka chini na kumkamata samaki huyo kabla hajatumbukia majini. Vipi polisi akimeza samaki kwanza? Inasemekana kwamba ndege wa frigate anaweza kumfuata polisi na kumlazimisha atapike chakula chake!”

Kutazama Ndani ya Bahari

“Siku ya pili ya safari yetu, tulipiga mbizi ndani ya bahari. Kwa kawaida halijoto ya maji kwenye eneo hilo haiwi chini ya nyuzi 24 Selsiasi, na unaweza kuona hadi kina cha meta 15. Huhitaji kuwa na vifaa vya bei ghali ili upige mbizi ndani ya maji matulivu yenye kina kifupi karibu na visiwa hivyo. Unahitaji tu kifaa cha kuingiza hewa, kinyago, na viatu vya mpira vya kupiga mbizi. Jua lilipoangaza, miale yake ilimulika makundi ya samaki, matumbawe ya kijani, ya zambarau, na ya manjano, na vilevile sifongo na mwani mwekundu. Tuliona mwangaza wenye rangi mbalimbali. Ijapokuwa hakuna aina nyingi za matumbawe katika eneo hili kwa kulinganishwa na maeneo mengine yenye miamba ya kitropiki, aina fulani za matumbawe zinapatikana katika eneo hili tu.

“Zaidi ya aina 160 za samaki huishi ndani ya maji ya bluu yenye kuvutia yanayozunguka kisiwa hicho. Kuna viumbe wenye maumbo na ukubwa mbalimbali kama vile aina fulani ya kasa, ruguu, kangaja, mkule, pono, mkandaa, na mkunga. Samaki hao ni wapole sana hivi kwamba unaweza kuwalisha, na chakula kinapokwisha, wao huuma-uma vidole vyako polepole wakitafuta chakula kingine.”

Nyangumi Wenye Nundu Warudi

“Siku ya tatu ya safari yetu kwenye visiwa hivyo, tulianza kurudi Caravelas wakati wa alasiri huku tukiwa na furaha na huzuni. Nilifurahia eneo la Abrolhos lakini nilisikitika kwa sababu hatukuwa tumemwona hata nyangumi mmoja. Hata hivyo, baada ya kusafiri kwa dakika 30 hivi, Manoel alipiga kelele kwa ghafula: ‘Nyangumi! Nyangumi!’ Nyangumi watatu wenye nundu—nyangumi wawili waliokomaa na nyangumi mchanga—walitokezea meta 200 hivi kutoka mahali tulipokuwa. Tuliona vizuri sana sehemu nyeupe chini ya vikono vyao vikubwa. Nyangumi mmoja alitukaribia na kuogelea karibu nasi kwa dakika chache. Sikuamini nilipoona nyangumi huyo akiruka juu ya maji. Alitokeza nusu ya mwili wake mkubwa nje ya maji na kujibwaga tena kwa mgongo wake. Hilo lilifanyiza mkato mkubwa ndani ya maji! Tuliposonga mbali na visiwa hivyo, bado tuliweza kuona mapezi kwenye mikia ya nyangumi hao na vilevile maji yakirushwa juu. Tulifurahi kuona kwamba nyangumi hao wamerudi tena kwenye eneo hilo.”

Wakati Ujao Usiojulikana

Huenda wavuvi wa nyangumi wametokomea, lakini bado kuna hatari nyingine. Visiwa hivyo pia hukumbwa na matatizo ya mazingira. Mtaalamu mmoja wa mambo ya bahari alisema hivi: ‘Haitoshi kuhifadhi visiwa na kuwazuia watu wasivitembelee sana huku vitu vingine vyote katika mazingira vikiharibiwa.’

Wanasayansi wengi wanaamini kwamba kuongezeka kwa halijoto duniani kumesababisha rangi ya Kuta za Miamba ya Matumbawe kufifia, na hilo linaonyesha kwamba mwani ulio kwenye eneo hilo unatoweka. Yaonekana kwamba matumbawe ya visiwa hivyo yataathiriwa na ukataji wa misitu na mmomonyoko wa udongo, ambao unasababisha mchanga mwingi zaidi upelekwe na mito hadi baharini. Na kwa kuwa idadi ya watalii inaongezeka kila mwaka, wanamazingira hawana budi kuwa macho ili kuzuia uharibifu wa eneo maridadi la Abrolhos.

Hata hivyo, kufikia sasa, matatizo hayo hayajaharibu uzuri wa eneo maridadi la Abrolhos lenye nyangumi wanaorukaruka, ndege wenye kustaajabisha, na matumbawe ya kipekee. Miaka 500 hivi imepita tangu eneo la Abrolhos livumbuliwe, na bado linavutia macho. Mtu anapotembelea eneo hilo hawezi kusahau kamwe mambo mazuri aliyoona.

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BRAZILI

ABROLHOS

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

VISIWA VYA ABROLHOS

Siriba

Redonda

Santa Bárbara

Guarita

Sueste

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mnara wa taa wa Abrolhos, uliojengwa mwaka 1861

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ndege wa “frigate”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Tumbawe

[Hisani]

Enrico Marcovaldi/Abrolhos Turismo

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ruguu

[Picha katika ukurasa wa 16]

Polisi bawajeusi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Redonda

[Hisani]

Foto da ilha: Maristela Colucci

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mkunga

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kangaja

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndege wa kitropiki mwenye mdomo mwekundu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyangumi mwenye nundu na mtoto wake