Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kupata Dhahabu Kutoka kwa Takataka

Kampuni moja ya kuchimba madini huko Japan imegundua njia rahisi na isiyo ghali ya kupata vito vya thamani. Badala ya kutumia wakati mwingi na pesa nyingi kutafuta mawe yenye madini, kampuni moja katika Jimbo la Akita huyeyusha simu za mkononi na kompyuta zilizotupwa ili kupata vito vya thamani, laripoti gazeti IHT Asahi Shimbun la Tokyo. Kulingana na msimamizi wa kampuni hiyo, “Tani 1 ya simu za mkononi zilizotupwa—zisizo na betri—inaweza kutoa dhahabu yenye uzito wa gramu mia kadhaa.” Kwa kutumia ‘uchimbaji huo wa kisasa,’ tani moja ya takataka hutokeza dhahabu mara kumi ya ile inayotokezwa kwa kuchimba madini ya dhahabu. Isitoshe, haikugharimu chochote kubadili vifaa vya kuyeyusha madini, kwani hakuna tofauti kubwa kati ya kupata dhahabu kutokana na simu za mkononi na kuitoa katika madini.

Wanyama aina ya Llama Walinda Kondoo

Wafugaji huko Amerika Kaskazini wanategemea wanyama aina ya llama ili kulinda kondoo wao. Kulingana na gazeti la Globe and Mail la Kanada, wanyama hao “hufanya urafiki wa karibu na wanyama wengine wanaoishi pamoja kwa muda.” Wao hulinda kondoo kijasiri kwa kutoa mlio wa onyo, kuwachunga, kufukuza na kuwapiga mateke au kuwashambulia wavamizi kwa kucha zao. Kwa kuwa hawagharimu sana, Wakulima fulani hupendelea llama kuliko mbwa wa kulinda. Isitoshe, gazeti hilo lasema, “kwa sababu llama hulisha na kulala pamoja na kondoo, hakuna gharama za ziada zinazohitajika kuwatunza, na pia wao huishi miaka mingi zaidi kuliko mbwa wa kawaida wa kulinda.” Mfugaji mmoja Mkanada ambaye ana wanyama hao alielezea faida zake akisema: “Hawagharimu chochote,” na “hawabweki.”

Kemikali ya Kiasili ya Kupasha Baridi

Kikundi cha watafiti huko Ujerumani kimegundua kemikali ya kiasili yenye nguvu ya kupasha baridi zaidi ya mara 35 ya ile ya mentholi, na ambayo haina ladha ya mnanaa. Kemikali hiyo, ambayo hupatikana kiasili katika mvinyo na wiski, iligunduliwa katika Kituo cha Ujerumani cha Utafiti wa Kemikali za Chakula huko Garching, Munich. Gazeti la New Scientist linamnukuu mkurugenzi wa kikundi hicho cha watafiti, Thomas Hofmann, akisema: “Kemikali hiyo itatia harufu baridi ya kipekee kwenye bidhaa nyingi, kutia ndani mvinyo, maji ya kunywa yaliyotiwa kwenye chupa, maji ya matunda, chokoleti na peremende.” Na kwa kuwa kemikali hiyo huwa baridi mara 250 kwenye ngozi kuliko mnanaa hata ikiwa kwenye michanganyiko mizito, inaweza kutumiwa katika vipodozi au mafuta ya ngozi.

Mbolea na Vijidudu Visivyoathiriwa na Dawa

“Mashamba huko Ulaya yana viuavijasumu vingi vinavyotokana na dawa ambazo hupewa wanyama wa kufugwa,” laripoti gazeti New Scientist. Kila mwaka, wanyama wa kufugwa katika Muungano wa Ulaya na Marekani hupewa zaidi ya tani 10,000 za viuavijasumu ili kuwasaidia wakue na kuwakinga na magonjwa. “Lakini utafiti uliofanywa hivi majuzi umeonyesha kwamba kuna uhusiano wa moja kwa moja wa ongezeko la utumizi wa dawa hizo na kutokea kwa vijidudu visivyoathiriwa na viuavijasumu, ambavyo huambukiza watu,” lasema gazeti hilo. “Huenda dawa hizo, ambazo huwa katika mbolea inayonyunyiziwa mashambani, zinaingia katika chakula chetu na maji. . . , [na hivyo] kudhuru mimea inayoliwa,” lasema gazeti New Scientist.

“Kuwatunza” Babu na Nyanya

Familia fulani huko Hispania zimepanga “kuwatunza” wazee 66 ambao hawana watu wao wa ukoo, laripoti gazeti la Hispania El País. “Kusudi la mpango huo . . . ni kuwapa wazee ambao hawawezi kuishi peke yao tena nafasi ya kuishi sehemu nyingine badala ya makao ya kuwatunzia wazee,” lasema gazeti hilo. Baadhi ya wale waliotaka kuwatunza watu wazee ni wenzi wa ndoa walio na miaka hamsini na kitu wanaotaka kuishi na mtu mzee. Familia nyingine zenye watoto wachanga zinasema kwamba zingependa kuwa na babu au nyanya nyumbani mwao. Ingawa familia zinazotaka kuwachukua na kuwatunza wazee hao zitapokea kiasi fulani cha pesa, “jambo linalowachochea hasa si pesa hizo,” aeleza mkurugenzi mkuu wa mpango huo, Marisa Muñoz-Caballero. “Iwapo wangetaka tu pesa, wangechoka haraka kwa sababu kuwatunza watu wazee ni kazi ngumu.”

Ulaya Yakumbwa na Jeuri ya Nyumbani

“Mwanamke mmoja kati ya watano huko Ulaya hutendewa jeuri na rafiki yake wa kiume wakati fulani maishani,” akasema Anna Diamantopoulou, mjumbe wa Ulaya anayehusika na uajiri na mambo ya kijamii. Katika Mkutano wa Mawaziri Kuhusu Kuzuia Jeuri Dhidi ya Wanawake, uliofanyika Hispania mapema mwaka huu, Diamantopoulou alisema: “Ulimwenguni pote, wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 44 wana uwezekano mkubwa wa kulemazwa au kufa kutokana na jeuri waliyotendewa na wanaume kuliko kutokana na ugonjwa wa kansa, malaria, misiba ya barabarani au vita zikijumlishwa.” Nchini Uingereza, “mwanamke mmoja hufa kila baada ya siku tatu kutokana na jeuri nyumbani,” huku “nusu ya wanawake wanaokufa nchini Ireland huwa wameuawa na rafiki zao wa kiume au waume zao.” Na nchini Austria, laripoti gazeti la Ufaransa la kila siku Le Monde, “nusu ya talaka zote hutokana na wanawake wanaolalamika kwamba wanatendewa jeuri na waume zao.”

Kuzuia Watoto Wasife maji

Katika mataifa 26 tajiri zaidi duniani, kufa maji ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya watoto wasiozidi umri wa miaka 14, laripoti gazeti BMJ (lililoitwa British Medical Journal hapo awali). Kulingana na gazeti hilo, “watoto wachanga wanaelekea kufa maji wakiwa nyumbani (hasa kwenye makarai makubwa ya kuogea); watoto wakubwa kidogo kwenye vidimbwi vya maji vilivyo karibu na nyumbani kama vile vya kuogelea au vya samaki; na wale wakubwa zaidi kwenye maziwa na mito.” Ili kuzuia misiba hiyo, wataalamu wanapendekeza mambo yafuatayo: Daima wachunge watoto wachanga sana wanapokuwa katika karai kubwa ya kuogea au karibu na dimbwi lolote; zungusha ua usioweza kuruhusu mtoto kupita katika dimbwi lililo shambani au la kuogelea; usiwaruhusu watoto waogelee peke yao au mahali palipojitenga; jifunze ufundi wa kumhuisha mtu.

Kubalehe Mapema

“Watoto wanabalehe mapema,” laripoti gazeti la Ujerumani Berliner Zeitung. Ni kawaida kuwaona watoto waliobalehe katika umri wa kati ya miaka 10 hadi 12 au hata mapema zaidi. Watafiti ulimwenguni pote wametambua jambo hilo lakini hawajui kisababishi. Kuboreshwa kwa chakula na kupunguka kwa magonjwa ya kuambukiza ni baadhi ya sababu zilizotajwa. Watu wengine wanalaumu uchafuzi wa mazingira, hasa kemikali ambazo hutenda kama homoni ya kike ya estrojeni. Hata sababu iwe nini, kubalehe mapema kunaweza kuwafanya vijana wajihusishe katika ngono mapema. “Mara nyingi, watoto wanakua haraka sana na kuwa watu waliobalehe na kujihusisha katika ngono,” lasema gazeti hilo.

Hasira Kali Inaweza Kukuua

“Watu wenye hasira kali wanakabili hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kiharusi,” lasema gazeti la Hispania Diario Médico. Kwa muda mrefu, madaktari wamesema kwamba watu wenye tabia za kijeuri wana hatari kubwa ya kuugua maradhi ya moyo. Utafiti wa hivi majuzi pia ulionyesha kwamba tabia hiyo huongeza pia hatari ya kupata ugonjwa wa kiharusi. Utafiti uliofanyiwa watu wazima 14,000, uligundua kwamba watu wenye umri wa chini ya miaka 60 wana hatari mara tatu zaidi ya kupata ugonjwa wa kiharusi. Kwa nini? Inaonekana hasira inaweza kusababisha shinikizo la damu “lipande sana,” kuziba kwa mishipa ya damu, na kuongezeka kwa kemikali za kugandisha damu, hali ambayo “inaweza kuathiri mzunguko wa damu katika ubongo baada ya muda fulani,” yasema ripoti hiyo.