Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Macho ya Tai

Macho ya Tai

Macho ya Tai

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI HISPANIA

WAHISPANIA husema kwamba mtu anayeona vizuri sana ana macho kama ya tai (vista de águila). Wajerumani pia wana msemo kama huo (Adlerauge). Kwa sababu nzuri, uwezo wa tai wa kuona vizuri umejulikana tangu zamani sana. Kitabu cha Ayubu, kilichoandikwa zaidi ya miaka elfu tatu iliyopita, chasema hivi kumhusu tai: ‘Macho yake huangalia toka mbali.’—Ayubu 39:27, 29.

Je, tai anaweza kuona umbali gani? “Katika hali za kawaida tai (Aquila chrysaetos) anaweza kumwona sungura anaposogea kidogo tu akiwa umbali wa zaidi ya kilometa 2,” chasema kichapo The Guinness Book of Animal Records. Wengine wamekadiria kwamba tai anaweza kuona mbali hata zaidi!

Ni nini ambacho humwezesha tai kuona mbali sana hivyo? Kwanza kabisa, tai ana macho mawili makubwa ambayo huchukua nafasi kubwa ya kichwa. Kitabu Book of British Birds chasema kwamba macho ya tai “ni makubwa sana lakini si mazito sana kumfanya ashindwe kuruka.”

Isitoshe, idadi ya chembe zinazotambua mwangaza za jicho la tai ni mara tano zaidi kuliko idadi ya chembe zetu—tai wengine wana chembe 1,000,000 kwa kila milimeta moja ya mraba zinazochochewa na mwangaza lakini sisi tuna chembe 200,000. Karibu kila chembe ya kutambua mwangaza imeunganishwa na chembe ya neva. Hivyo, kila chembe ya neva inayochukua habari kutoka kwenye jicho la tai hadi kwenye ubongo ina miunganisho mara mbili zaidi ya ile ya wanadamu. Basi si ajabu kwamba viumbe hao huona rangi vizuri! Hatimaye, ndege wawindaji, kama ndege fulani, wana lenzi zenye nguvu ambazo zinaweza kubadilika upesi kutoka kutazama vitu vilivyo karibu sana hadi kuona vitu vilivyo mbali sana. Macho ya ndege hao yanashinda yetu katika jambo hilo pia.

Tai huona vizuri mchana, lakini bundi huona vizuri usiku. Bundi huwinda usiku na macho yake yana chembe nyingi za kutambua mwangaza na lenzi pana. Hivyo, bundi huona mara 100 vizuri zaidi kuliko sisi usiku. Hata hivyo, mara moja-moja kunapokuwa na giza totoro, bundi hutumia uwezo wake bora wa kusikia kutambua windo lake.

Ni nani aliyewapa ndege hao uwezo huo? Mungu alimuuliza hivi Ayubu: “Je, tai hupaa juu kwa amri yako?” Bila shaka, hakuna mtu awezaye kujivunia maajabu hayo ya uumbaji. Ayubu mwenyewe alitambua jambo hilo aliposema: “Najua ya kuwa [Yehova] waweza kufanya mambo yote.” (Ayubu 39:27; 42:1, 2) Macho ya tai ni uthibitisho mwingine wa hekima ya Muumba wetu.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Tai

[Picha katika ukurasa wa 24]

Bundi wa theluji