Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Michezo Mipya ya Kompyuta

Michezo Mipya ya Kompyuta

Michezo Mipya ya Kompyuta

Kulingana na gazeti la “Newsweek,” mchezo wa “Grand Theft Auto 3” ndio “mchezo wa video ulionunuliwa sana mwaka jana.” Katika mchezo huo, wachezaji hupata cheo katika shirika la wahalifu kwa kushiriki matendo mbalimbali ya uhalifu, kama vile ukahaba na kuua. Gazeti la “Newsweek” linasema kwamba “mambo yote unayofanya katika mchezo huo yana matokeo fulani.” Ukiiba gari kisha uwagonge na kuwaua watu wanaotembea kwa miguu, polisi watakuandama. Ukimpiga risasi polisi mmoja, majasusi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wataanza kazi. Ukimuua jasusi wa FBI, wanajeshi watajitahidi juu chini kukuangamiza. Ijapokuwa mchezo huo ulikusudiwa watu wenye umri wa miaka 17 na zaidi, watoto wadogo wameuziwa mchezo huo. Inasemekana kwamba, hata watoto wenye umri wa miaka 12 wanataka kuucheza.

MCHEZO wa kwanza wa kompyuta, unaoitwa Spacewar, ulibuniwa mwaka 1962. Mchezaji alipaswa kuepuka sayari ndogo na vyombo vya anga vya maadui. Baadaye, michezo mingi kama hiyo ilibuniwa. Kompyuta zenye uwezo mkubwa zaidi wa kuhifadhi habari zilipoanza kutumiwa sana katika miaka ya 1970 na 1980, michezo ya kompyuta pia ilienea. Kulikuwa na michezo yenye vituko, michezo ya kuchemsha bongo, michezo ya kupanga mikakati, na michezo ya kivita. Kwa mfano, katika mchezo mmoja wa kupanga mikakati, mchezaji huhitajika kupanga na kudhibiti ongezeko la watu katika majiji au tamaduni mbalimbali. Kuna michezo mingi ya kompyuta inayoigiza michezo ya kawaida kama vile hoki inayochezwa kwenye barafu na gofu.

Michezo mingine husifiwa kwa sababu inaelimisha na kufurahisha. Katika michezo fulani, unaweza kujaribu kuendesha ndege kubwa, gari linaloenda kasi, au hata gari-moshi. Unaweza pia kuteleza kwenye theluji kwa kutumia ubao au kutembelea sehemu mbalimbali za ulimwengu. Hata hivyo, michezo fulani ya kivita, kama ile inayohusisha sana kufyatua risasi, hushutumiwa kwa sababu ina jeuri nyingi. Katika michezo hiyo, mchezaji huchagua silaha kisha kuwapiga risasi na kuwaua wanadamu walio maadui au maadui wengine ambao si wanadamu.

Michezo ya Internet Imepamba Moto

Nchi ya Britannia ina wakazi 230,000. Wakazi hao ni watu wa aina zote—wanajeshi, washonaji wa nguo, wafua-vyuma, na wanamuziki. Wao hupigana vita, hujenga majiji, hufanya biashara, huoa na kuolewa, na kufa. Lakini nchi hiyo ya Britannia ni ya kuwaziwa tu. Wachezaji huona nchi hiyo ya zama za kati katika mchezo fulani wa Internet wanaposhindana na wachezaji wengine kwa wakati uleule. Mchezo huo umependwa na wengi na unatarajiwa “kupamba moto” hata zaidi katika biashara ya michezo ya kompyuta. Mchezo unaoitwa Ultima Online—ambao unatia ndani nchi hiyo ya kuwaziwa ya Britannia—ulianzishwa mwaka wa 1997 na ndio mchezo wa kwanza wa Internet. Tangu wakati huo, michezo mingineyo ya Internet imetokea, na mingine ingali inatayarishwa.

Michezo ya Internet inatofautianaje na michezo mingine ya kompyuta? Wahusika mbalimbali katika michezo hiyo hawaendeshwi kwa kompyuta, bali wanaendeshwa na wachezaji wengine ambao wanacheza wakati huohuo kupitia Internet. Maelfu ya watu wanaweza kucheza pamoja wakati uleule. Kwa mfano, inasemekana kwamba wakati fulani mchezo wa Ultima Online ulichezwa na watu kutoka nchi 114 wakati uleule. Huenda michezo hiyo inapendwa kwa sababu watu hupata nafasi ya kushirikiana. Wachezaji wanaweza kuwasiliana, na hilo linawafanya wahisi kwamba wao ni watu wa jamii moja.

Biashara Kubwa

Inatazamiwa kwamba biashara ya michezo ya kompyuta itapata ufanisi mkubwa. Kufikia mwaka wa 1997 mapato ya kila mwaka kutokana na biashara ya michezo ya kompyuta na ya video huko Marekani ilikuwa dola bilioni 5.3 za Marekani, na mapato ulimwenguni pote yalikuwa angalau dola bilioni 10 za Marekani. Na yaonekana kwamba biashara hiyo itazidi kutia fora. Biashara hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 50 hadi 75 katika miaka mitano ijayo.

Kulingana na shirika la Forrester Research, kila siku zaidi ya watu milioni moja huanza kucheza michezo mbalimbali ya Internet na yasemekana kwamba faida inayotokana na michezo hiyo itaongezeka wakati mbinu mpya ya kuwaunganisha watu haraka kwenye Internet itakapotumiwa katika sehemu nyingi. Watoto ambao wamecheza michezo ya kompyuta tangu utotoni huendelea kucheza hata wanapokuwa wakubwa. Mtu mmoja ambaye amecheza michezo hiyo kwa muda mrefu anasema: “Kucheza michezo ya kompyuta ni njia ya kushirikiana na marafiki kutoka sehemu zote za ulimwengu.”

Je, michezo yote ya kompyuta ni burudani tu, au kuna hatari fulani zinazohusika? Na tuone.