Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hatua ya Kwanza Mjadala Katika Mahakama ya Juu

Hatua ya Kwanza Mjadala Katika Mahakama ya Juu

Hatua ya Kwanza Mjadala Katika Mahakama ya Juu

FEBRUARI 26, 2002, ndiyo siku ambayo mjadala wa kesi ulifanywa mbele ya Jaji Mkuu William Rehnquist na majaji wanane wengine wa Mahakama ya Juu. Mashahidi wa Yehova waliwakilishwa na mawakili wanne.

Wakili aliyeongoza upande wa Mashahidi alianza hoja zake kwa utangulizi wenye kuvuta fikira: “Tuseme hii ni siku ya Jumamosi mwendo wa saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Stratton. [Kisha akagonga kinara cha msemaji mara tatu.] ‘Habari za asubuhi. Kutokana na matukio ya hivi majuzi, nimekuja kwako kuzungumza nawe kuhusu jambo zuri ambalo Nabii Isaya alilitaja. Hiyo ni habari njema ambayo Kristo Yesu alizungumzia, habari njema ya Ufalme wa Mungu.’”

Aliendelea kusema: “Katika Kijiji cha Stratton, ni hatia kwenda nyumba hadi nyumba kuwaeleza watu ujumbe huo isipokuwa kwanza uwe umepata kibali cha wenye mamlaka wa kijiji hicho.”

‘Nyinyi Hamwombi Pesa?’

Jaji Stephen G. Breyer aliwauliza Mashahidi maswali hususa. Aliuliza hivi: “Je, ni kweli kwamba Mashahidi hawaombi pesa zozote, hata peni moja, na [kwamba] hawauzi Biblia, wala kitu chochote, kwamba wanataka tu kuzungumza na watu kuhusu dini?”

Wakili wa Mashahidi akajibu: “Mheshimiwa, mambo ya hakika yanaonyesha wazi kwamba Mashahidi wa Yehova hawakuomba pesa katika Kijiji cha Stratton. Katika maeneo mengine, mambo ya hakika pia yanaonyesha kwamba nyakati nyingine wao hutaja mchango wa hiari. . . . Sisi hatuombi-ombi pesa. Tunataka tu kuzungumza na watu kuhusu Biblia.”

Je, Kibali cha Serikali Kinahitajiwa?

Jaji Antonin Scalia aliuliza hivi kwa busara: “Je, nyinyi mnaona kwamba hamhitaji kwenda kwa meya kumwomba ruhusa ya kuzungumza na majirani kuhusu habari ya kupendeza?” Wakili wa Mashahidi akajibu: “Hatufikiri kwamba Mahakama hii inapaswa kuruhusu amri ya Serikali ambayo inadai kwamba ni lazima raia apate leseni ili azungumze na raia mwenzake nyumbani mwake.”

Mjadala Wapamba Moto

Sasa ilikuwa zamu ya Kijiji cha Stratton kutoa malalamiko yake. Wakili aliyeongoza upande wa kijiji hicho alieleza amri ya Stratton kwa kusema hivi: “Stratton inatumia mamlaka yake ili kulinda faragha ya wakazi wake, na kuzuia uhalifu. Amri inayopinga kwenda kwenye makao ya watu ili kuombaomba inataka tu watu wasajiliwe kwanza na kubeba kibali wakati wanapoenda nyumba hadi nyumba.”

Jaji Scalia aliingia kwenye kiini cha kesi yenyewe alipouliza hivi: “Je, mnajua kesi nyingine [ya Mahakama ya Juu] iliyohusiana na amri ya aina hii, amri inayohusu kuombaomba, wala si kuomba pesa wala kuuza bidhaa, bali, kuwaeleza watu kuhusu Yesu Kristo, au kuongea juu ya kulinda mazingira? Je, tumewahi kushughulikia kesi ya aina hiyo?”

Jaji Scalia aliendelea kusema: “Sijawahi kusikia kesi ya aina hii kwa zaidi ya miaka 200.” Kisha Jaji Mkuu Rehnquist akamfanyia utani kwa kusema: “Hujaishi muda mrefu hivyo.” Maneno hayo yalisababisha kicheko mahakamani. Jaji Scalia akaendelea na hoja yake: “Sijawahi kamwe kusikia jambo la aina hii.”

Je, Unafikiri Hilo Ni Wazo Mwafaka?

Jaji Anthony M. Kennedy aliuliza swali hili hususa: “Je, unafikiri ni wazo mwafaka kwamba ni lazima niiombe Serikali ruhusa kabla ya kwenda mtaani, ambako sijui watu wote, ili niwaambie kwamba ningependa kuzungumza nao kwa sababu ninahangaikia ukusanyaji wa takataka, au juu ya Mbunge wetu, na kadhalika? Je, lazima niombe Serikali ruhusa kabla ya kufanya hivyo?” Kisha akaongeza hivi: “Hilo ni wazo la kiajabu.”

Kisha Jaji Sandra Day O’Connor akajiunga na mjadala huo, kwa kuuliza: “Vipi juu ya wale watoto ambao huenda nyumba hadi nyumba wakiomba peremende wakati wa sikukuu ya Halloween? Je, wanapaswa kupata kibali?” Jaji O’Connor na Jaji Scalia waliendelea kujadili wazo hilo. Jaji O’Connor alianzisha hoja nyingine: “Vipi juu ya kumwomba jirani yako sukari? Je, ninahitaji kwanza kupata kibali ili nimwombe jirani yangu sukari?”

Je, Mashahidi Ni Waombaji?

Jaji David H. Souter aliuliza: “Kwa nini amri hii inawahusu Mashahidi wa Yehova? Je, wao ni waombaji, wachuuzi, wafanyabiashara wanaozunguka mitaani wakiuza bidhaa au huduma? Wao si watu wa aina hiyo, sivyo?” Wakili wa Kijiji hicho alinukuu amri iliyotolewa na wenye mamlaka wa Stratton na akasema kwamba mahakama ya wilaya ilikuwa imewafafanua Mashahidi wa Yehova kuwa waombaji. Kisha Jaji Souter akaongeza: “Ikiwa mnawaona Mashahidi wa Yehova kuwa waombaji, basi mnaelewa neno waombaji kwa njia pana sana.”

Kisha Jaji Breyer akasoma ufafanuzi wa neno hilo katika kamusi ili kuonyesha kwamba haliwahusu Mashahidi. Halafu akaongeza: “Sijasoma hata jambo moja katika hati yenu ya malalamishi linaloonyesha kusudi la kuwataka watu hawa [Mashahidi wa Yehova] ambao hawaombi pesa, wala kuuza bidhaa, wala kuomba kura, waende kwenye ofisi ya baraza la jiji ili kusajiliwa. Kwani jiji lenu linataka nini?”

“Pendeleo” la Kuzungumza na Watu

Kisha wakili wa Kijiji hicho akasema kwamba “jiji linataka kuzuia wenye nyumba wasisumbuliwe.” Aliendelea kusema kwamba kusudi lilikuwa kuwalinda wakazi dhidi ya ulaghai na wahalifu. Jaji Scalia alinukuu amri iliyotolewa na wenye mamlaka wa kijiji kuonyesha kwamba meya anaweza kuomba habari zaidi kuhusu mtu anayetaka kusajiliwa na kuhusu kusudi lake ili “kubainisha kwa usahihi pendeleo analotaka.” Halafu akatoa kauli hii: “Eti ni pendeleo kwenda kuzungumza na raia wenzako kuhusu mambo mawili matatu—ni ajabu.”

Jaji Scalia alizidi kukazia hoja yake: “Kwa hiyo, je, kila mtu anayetumia kengele mlangoni anapaswa kwenda kwenye ofisi ya baraza la jiji ili alama zake za vidole zichukuliwe kabla hajabonyeza kengele mlangoni? Je, inafaa kuwalazimisha watu wote wanaotaka kubonyeza kengele mlangoni waende kwenye baraza la jiji ili wasajiliwe eti kwa sababu ya uwezekano mdogo wa kutokea kwa uhalifu? La hasha.”

Je, Amri Hiyo Iliwalinda Wakazi?

Baada ya dakika zake 20 kumalizika, wakili wa upande wa Kijiji cha Stratton aliacha mwanasheria mkuu wa jimbo la Ohio aendeleze mjadala huo. Mwanasheria huyo alibisha kwamba amri hiyo inayozuia kuombaomba iliwalinda wakazi wasitembelewe na mtu wasiyemjua, “mtu asiyealikwa, [ambaye] amekuja nyumbani.” Kisha akasema: “Ninafikiri kuwa wanakijiji wana haki ya kusema kwamba wana wasiwasi kuhusu shughuli ya aina hiyo.”

Jaji Scalia akasema: “Eti wanakijiji wanasema kwamba watu hawa [Mashahidi wa Yehova] bado wanahitaji kwenda kusajiliwa na meya ili wapate pendeleo la kuwatembelea watu nyumbani mwao, hata ingawa watu hao ambao wanawakaribisha Mashahidi wa Yehova wanahisi upweke na wangependa kuzungumza na mtu kuhusu jambo lolote.”

“Amri Isiyodai Mambo Mengi”

Wakati wa kuuliza maswali ya kuthibitisha ushahidi ulipofika, Jaji Scalia alitoa hoja nzito aliposema hivi: “Sote twaweza kukubali kwamba jamii salama zaidi ulimwenguni ni zile za udikteta. Hakuna uhalifu mwingi katika jamii hizo. Huu ndio ukweli wa mambo. Hasara moja inayosababishwa na uhuru katika jamii ni uhalifu mwingi. Basi suala ni hili, je, amri hii inaweza kuzuia uhalifu vya kutosha hivi kwamba inafaa kuwashurutisha watu kuomba ruhusa ili kutembelea nyumba za watu?” Kisha mwanasheria mkuu akajibu kwa kusema kwamba hiyo ni “amri isiyodai mambo mengi.” Naye Jaji Scalia akajibu kwamba ikiwa amri hiyo haidai mengi mno mbona “hakuna hata manispaa moja ambayo imewahi kutoa amri kama hiyo. Kwa maoni yangu, huko ni kudai mengi mno.”

Hatimaye, baada ya kushinikizwa na jaji mmoja, mwanasheria mkuu alilazimika kukubali hivi: “Siwezi kusema kwa uhakika kwamba unaweza kuwazuia watu kabisa wasibonyeze kengele mlangoni au kubisha hodi.” Na hoja yake ikakomea hapo.

Wakati wa kukanusha hoja ulipofika, wakili wa Mashahidi alisema kwamba amri hiyo haina njia ya kuhakikisha ikiwa mtu anasema kweli au uwongo. “Ninaweza kwenda kwenye ofisi za usimamizi wa kijiji hicho na niseme, ‘Mimi ni [Fulani wa Fulani],’ kisha nipate kibali cha kwenda nyumba hadi nyumba.” Pia alitaja kwamba meya ana mamlaka ya kutompa kibali mtu anayesema kwamba yeye si mshiriki wa shirika lolote. Wakili huyo alisema: “Tunaamini kwamba kufanya hivyo ni kutumia mamlaka kuwaamulia wengine mambo.” Kisha akaongeza hivi: “Ninasema kwa heshima kwamba shughuli yetu [Mashahidi wa Yehova] inahusiana kabisa na kiini cha Marekebisho ya Kwanza.”

Muda mfupi baadaye, Jaji Mkuu Rehnquist alifunga mjadala huo kwa kusema: “Kesi hii imewasilishwa [kwa Mahakama ya Juu].” Mjadala huo ulichukua zaidi ya saa moja tu. Umuhimu wa saa hiyo umeonyeshwa katika hati yenye uamuzi ambayo ilitangazwa mwezi Juni.

[Picha katika ukurasa wa 6]

Jaji Mkuu Rehnquist

Jaji Breyer

Jaji Scalia

[Credit lines]

Rehnquist: Collection, The Supreme Court Historical Society/Dane Penland; Breyer: Collection, The Supreme Court Historical Society/Richard Strauss; Scalia: Collection, The Supreme Court Historical Society/Joseph Lavenburg

[Picha katika ukurasa wa 7]

Jaji Souter

Jaji Kennedy

Jaji O’Connor

[Hisani]

Kennedy: Collection, The Supreme Court Historical Society/Robin Reid; O’Connor: Collection, The Supreme Court Historical Society/Richard Strauss; Souter: Collection, The Supreme Court Historical Society/Joseph Bailey

[Picha katika ukurasa wa 8]

Ndani ya mahakama

[Hisani]

Photograph by Franz Jantzen, Collection of the Supreme Court of the United States