Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kufanya Mimba Yako Iwe Salama Zaidi

Kufanya Mimba Yako Iwe Salama Zaidi

Kufanya Mimba Yako Iwe Salama Zaidi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

KULINGANA na Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Idadi ya Watu, zaidi ya wanawake nusu milioni hufa kila mwaka kutokana na matatizo yanayohusiana na mimba. Isitoshe, Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Watoto linasema kwamba kila mwaka zaidi ya wanawake milioni 60 huugua vibaya wakiwa wajawazito hivi kwamba karibu thuluthi moja kati yao hupata majeraha au maambukizo yanayodumu maisha yote. Katika nchi zinazoendelea, wanawake wengi hupata mimba moja baada ya nyingine, hujifungua, na kujiachilia, jambo ambalo huwafanya wawe wachovu na wagonjwa. Naam, mimba inaweza kuleta madhara—hata kuhatarisha uhai. Je, mwanamke anaweza kufanya nini ili mimba yake iwe salama zaidi?

Utunzaji wa Kiafya Kabla ya Kuwa Mjamzito

Kupanga. Huenda waume na wake wakahitaji kuzungumza kuhusu idadi ya watoto ambao watapata. Katika nchi zinazoendelea, ni kawaida kuwaona wanawake wenye watoto wanaonyonya wakiwa wajawazito. Kwa kupanga vizuri na kutumia ufikirio unaweza kuruhusu wakati upite kabla ya mtoto mwingine kuzaliwa, hivyo kumpa mama nafasi ya kurudia hali yake ya kawaida. Jambo hilo pia litamruhusu apate nafuu baada ya kujifungua.

Ulaji. Kulingana na Muungano wa Matokeo Bora ya Uzazi, mwanamke anahitaji angalau miezi minne kabla ya kuwa na mimba baada ya kufanya kazi karibu na bidhaa zinazodhuru, ili pia apate kuwa na afya bora. Kwa mfano, hatari ya kupinda uti wa mgongo inayoletwa na kutoziba kwa mrija wa neva wa kitoto kilicho tumboni, inaweza kuzuiwa iwapo mama mjamzito ana kiasi cha kutosha cha aina fulani ya vitamini ya C. Kwa kuwa mrija huo huziba siku ya 24 hadi ya 28 baada ya mimba kutungwa—muda mrefu kabla ya wanawake wengi kugundua wana mimba—baadhi ya wanawake wanaopanga kupata mimba hula vyakula vyenye vitamini hiyo.

Chuma ni madini muhimu pia. Kwa hakika, mwanamke huhitaji madini mengi zaidi ya chuma anapokuwa mjamzito. Asipokuwa na kiasi cha kutosha—hali ambayo huwapata wanawake wengi katika nchi zinazoendelea—damu yake inaweza kuwa na upungufu wa madini hayo. Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi mwanamke apatapo mimba moja baada ya nyingine, kwa kuwa hana nafasi ya kurudisha kiasi kinachohitajika cha madini ya chuma. *

Umri. Wasichana wenye umri wa chini ya miaka 16 ambao ni wajawazito wanakabili hatari ya kufa ya asilimia 60 zaidi kuliko wale walio na umri wa miaka 20 na kitu. Kwa upande mwingine, wanawake wenye umri unaozidi miaka 35 wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuzaa watoto wenye kasoro, kama vile ugonjwa wa Down. Akina mama wachanga sana au wenye umri mkubwa wanaweza kuugua ugonjwa wa preeclampsia. Ugonjwa huo, ambao dalili zake zinatia ndani shinikizo la juu la damu baada ya juma la 20 la mimba pamoja na kuwa na umajimaji usio wa kawaida kwenye viungo na ongezeko la protini kwenye mkojo, huongeza hatari ya mtoto na mama kufa.

Maambukizo. Maambukizo ya mfumo wa mkojo, mlango wa kizazi na sehemu ya siri, na mfumo wa chakula yanaweza kuzidi wakati wa mimba na kuongeza uwezekano wa kuugua ugonjwa wa preeclampsia na mtoto kuzaliwa kabla ya wakati. Inafaa maambukizo yoyote yatibiwe kabla ya mwanamke kuwa mjamzito.

Utunzaji wa Kiafya Akiwa Mjamzito

Utunzaji kabla ya kujifungua. Mwanamke anaweza kupunguza hatari ya kufa akiendelea kumwona daktari mara kwa mara anapokuwa mjamzito. Hata katika nchi ambako haiwezekani kutembelea kliniki na hospitali kwa ukawaida, wakunga waliozoezwa vizuri wanaweza kupatikana.

Utunzaji wa kabla ya kujifungua unaweza kuwasaidia wataalamu kuona hali ambazo huenda zikahitaji utunzaji wa pekee. Hali hizo zinatia ndani kuwepo kwa watoto zaidi ya mmoja tumboni, shinikizo la juu la damu, matatizo ya moyo na figo, na ugonjwa wa sukari. Katika nchi fulani, mwanamke mjamzito anaweza kupewa chanjo ya pepo-punda ili kumkinga na ugonjwa huo wakati wa kujifungua. Anaweza pia kupimwa kama ana bakteria za kundi la B streptococcus kwenye juma la 26 hadi la 28 la mimba. Bakteria hizo zinaweza kuambukiza mtoto wakati wa kuzaliwa, zikiwa kwenye utumbo mkubwa.

Mwanamke anapaswa kuwapatia wataalamu wa afya habari nyingi iwezekanavyo, kutia ndani rekodi yake ya tiba. Pia, anapaswa kuuliza maswali kwa uhuru. Anapaswa kuomba msaada wa kitiba mara moja ikiwa damu inatoka kupitia sehemu ya siri, uso wake unafura ghafula, ana maumivu makali yenye kuendelea kichwani au uchungu kwenye vidole, apoteza uwezo wake wa kuona ghafula au haoni vizuri, anaumwa na tumbo sana, anatapika sana, anaugua homa, mtoto aliye tumboni anaruka isivyo kawaida, umajimaji unatoka kupitia sehemu ya siri, anasikia maumivu anapokojoa, au hapati mkojo kama kawaida.

Pombe na dawa za kulevya. Mama anayekunywa pombe na kutumia dawa za kulevya (kutia ndani tumbaku) huzidisha hatari ya kumzaa mtoto aliye na akili punguani, mlemavu, na hata aliye na tabia yenye kasoro. Inajulikana kuwa watoto waliozaliwa na wazazi ambao wamezoea kutumia dawa za kulevya huwa na matatizo kama ya watu ambao walitumia dawa za kulevya zamani. Ingawa wengine hudai eti kunywa pombe kidogo hakuwezi kudhuru, mara nyingi wataalamu hupendekeza akina mama wajawazito wasiinywe hata kidogo. Wanapaswa pia kuepuka moshi wa sigara.

Dawa. Hakuna dawa zinazopaswa kutumiwa ila tu zile zilizopendekezwa na daktari anayejua kuhusu mimba hiyo na ambaye amechunguza athari zake. Vitamini fulani pia zinaweza kudhuru. Kwa mfano, kiasi kikubwa sana cha vitamini ya A chaweza kumlemaza mtoto aliye tumboni.

Kuongeza uzito. Mwanamke mjamzito anapaswa kuepuka kupita kiasi katika ulaji. Kulingana na kichapo Krause’s Food, Nutrition and Diet Therapy, mtoto anayezaliwa akiwa na uzito wa chini sana anakabili hatari ya kufa mara 40 zaidi kuliko yule aliyezaliwa akiwa na uzito wa kawaida. Kwa upande mwingine, kula chakula cha watu wawili hunenepesha tu. Ongezeko linalofaa la uzito—ambalo huanza kuonekana katika mwezi wa nne wa mimba na kuendelea—huonyesha kwamba mama anakula chakula cha kutosheleza mahitaji yake yanayoongezeka. *

Usafi na mambo mengine. Kuoga kwenye karai na kutumia maji ya bomba kunaweza kufanywa kama kawaida, lakini haifai kuingiza maji kwa nguvu kupitia sehemu ya siri. Mwanamke mjamzito anapaswa kuepuka kumkaribia yeyote mwenye ugonjwa wa virusi, kama surua ya rubella. Zaidi ya hayo, ili kuzuia ugonjwa unaoambukiza ubongo na uti wa mgongo hasa katika mtoto mchanga, ni lazima awe mwangalifu asile nyama ambayo haijaiva vizuri wala kugusa kinyesi cha paka. Ni muhimu kudumisha usafi wa kawaida kama kunawa mikono na kuosha vyakula kabla havijapikwa. Mara nyingi kufanya ngono hakuleti tatizo lolote, ila tu katika majuma ya mwisho-mwisho ya mimba au kukiwa na mtiririko wa damu, maumivu tumboni, au ikiwa mimba ya awali ilitoka.

Kujifungua kwa Mafanikio

Yaelekea mwanamke mjamzito anayejitunza hatapata matatizo wakati wa kujifungua. Kwa kawaida, yeye atapanga kama atapenda kujifungulia nyumbani au hospitalini. Atafahamu vizuri zaidi mambo yatakayotukia na jinsi ya kushirikiana na mkunga au daktari. Huyo naye atafahamu mapendezi ya mwanamke huyo yanayotegemea ujuzi aliopata—mahali ambapo anaweza kuchagua—jinsi atakavyokaa anapojifungua, kupasua ili kumtoa mtoto, na utumizi wa vifaa vya kumvuta mtoto, dawa za kupunguza maumivu, na kuchunguza mtoto kwa kutumia mbinu za elektroni. Pia ni lazima wakubaliane kuhusu mambo mengine: je, ni hospitali au kliniki gani atakayopelekwa iwapo hataweza kujifungulia nyumbani? Ni hatua gani itakayochukuliwa iwapo atapoteza damu nyingi? Kwa kuwa wanawake wengi hufa wanapojifungua kwa sababu ya kupoteza damu nyingi, ni lazima kuwe na vitu ambavyo huongeza kiasi cha damu kwa wale ambao hawakubali kutiwa damu mishipani. Pia, ni lazima wafikirie kimbele kuhusu upasuaji wa kutoa mtoto iwapo utahitajika.

Biblia husema kwamba watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, “urithi.” (Zaburi 127:3) Kadiri mwanamke anavyofahamu mambo mengi zaidi kuhusu mimba yake, ndivyo alivyo na nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa kujifungua kwa usalama. Kwa kujitunza kabla na wakati wa kujifungua na kufikiria kimbele mambo mbalimbali yanayohusiana na kujifungua, mwanamke atakuwa amefanya yote awezayo kuhakikisha mimba yake ni salama.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Aina hiyo ya vitamini ya C na madini ya chuma yaweza kupatikana katika maini, maharagwe, mboga zenye majani mabichi, njugu, na nafaka zilizoongezwa vitamini na madini mbalimbali. Kuchanganya chakula chenye vitamini ya C, kama matunda yaliyotoka shambani karibuni, pamoja na chakula chenye madini ya chuma huongeza madini hayo mwilini.

^ fu. 16 Ongezeko linalopendekezwa kwa mwanamke mwenye uzito unaofaa anapokuwa na mimba ni kilogramu 9 hadi 12 kufikia wakati wa kujifungua. Hata hivyo, wasichana au wanawake ambao hawakuwa wakila chakula cha kutosha wanapaswa kuongeza kati ya kilogramu 12 hadi 15, na wale wanene wanapaswa kuongeza kilogramu 7 hadi 9 tu.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

MADOKEZO YA KUWASAIDIA WANAWAKE WAJAWAZITO

● Kila siku mwanamke mjamzito anahitaji kula matunda, mboga (hasa zilizo na majani ya rangi nzito ya kijani, na zenye rangi ya machungwa, au nyekundu), maharagwe mbalimbali (kutia ndani soya, dengu, na njegere), nafaka (kutia ndani ngano, mahindi na shayiri—hasa zile ambazo hazijatolewa maganda au zilizotiwa vitu vingine), chakula kinachotokana na wanyama (samaki, nyama ya kuku, nyama ya ng’ombe, mayai, jibini, na maziwa, hasa yale ambayo yametolewa mafuta). Mafuta, sukari na chumvi vinapaswa kutumiwa kwa kiasi. Kunywa maji mengi. Epuka vinywaji vyenye kafeini, na vyakula vilivyotiwa dawa za kuhifadhi na kemikali nyinginezo (kama za kutia rangi na ladha). Wanga, udongo wa mfinyanzi, na vitu vingine visivyoliwa vyaweza kusababisha utapiamlo na kumtia sumu.

● Jihadhari na hatari ya mambo yanayochafua mazingira, kama minururisho ya eksirei na kemikali hatari. Punguza utumizi wa dawa za kupulizia na dawa nyingine za nyumbani. Usijipashe joto kupita kiasi kwa kukaa mahali penye joto sana au kwa kufanya mazoezi sana. Epuka kusimama kwa muda mrefu na kujikaza kupita kiasi. Funga mkanda wa usalama vizuri.