Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukutana Uso kwa Uso na Panyabuku

Kukutana Uso kwa Uso na Panyabuku

Kukutana Uso kwa Uso na Panyabuku

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

JE, UNGEPENDA kujifunza juu ya kiumbe mdogo mwenye haya ambaye anapendeza na kufurahisha? Acha nikueleze jinsi mimi na mke wangu tulivyokutana uso kwa uso na kundi la wanyama wadogo wenye manyoya mengi wanaoitwa panyabuku.

Tupo penye safu ya milima ya Dolomites iliyo kaskazini mwa Italia. Twaweza kuona vilele virefu vya milima miwili—Latemar na Catinaccio. Tumechagua kupita kwenye kijia chenye mwinuko mkali kinachoelekea kwenye Mlima Catinaccio. Maua ya aina mbalimbali yanakua katika eneo lililo wazi. Tunatua kidogo kutazama aina fulani ya ua la yungiyungi linalovutia. Pia tunavutiwa na ua dogo jeusi la jamii ya okidi ambalo lina harufu ya vanila. Baadaye asubuhi jua lilikuwa limeangaza juu ya misonobari ya aina mbalimbali na kufanya harufu kali ya marhamu ienee hewani.

Baadaye tunafika kwenye bonde ambalo halina miti. Kwenye upande wa kulia kuna mwinuko mkali wenye nyasi. Kwenye upande wa kushoto kuna majabali makubwa. Kwa ghafula, tunaona kitu kikisonga haraka. Ninageuka mara moja, lakini sioni chochote. Ninapotazama kwa makini, ninaona panyabuku akiwa juu ya ncha ya mwamba. Yaonekana kwamba kundi la panyabuku linaishi katikati ya majabali hayo.

Panyabuku ndiye mnyama mkubwa zaidi kati ya wanyama wote wa jamii ya kuchakuro. Mnyama anayeitwa woodchuck ndiye anayejulikana sana kati ya wanyama wa jamii hiyo, naye anapatikana katika Amerika Kaskazini. Panyabuku wanaopatikana huku kwetu huitwa panyabuku wa Milima ya Alps. Wao hupenda kuchangamana na kuishi pamoja katika makundi-makundi.

Tunaondoka kwenye kijia hicho na kusonga karibu ili tumwone panyabuku huyo, lakini amekwisha toweka. Tunasubiri, tukitarajia kwamba mnyama huyo mwenye haya atatokezea tena. Muda mfupi baadaye, mke wangu anatoa ishara kwa uchangamfu. Panyabuku mmoja anatuchungulia huku akijificha nyuma ya jabali! Manyoya yake yenye rangi ya kijivu-kahawia yanafanana na mwamba huo, na kumfanya mnyama huyo asionekane kwa urahisi. Ninapotazama kwa makini, ninatambua kwamba kumbe panyabuku mwingine mchanga anatuchungulia pia. Mbele zaidi tunamwona panyabuku mwingine—na tunakisia kuwa yeye ndiye baba yao. Ijapokuwa hatuna uhakika, tunakisia kwamba tunatazama familia ya panyabuku.

Panyabuku “baba” ana urefu wa karibu sentimeta 45 na ameketi wima kwa miguu yake ya nyuma, kana kwamba analinda boma. Wakati huohuo, panyabuku wale wengine wawili wanasonga kati ya vichaka. Panyabuku huchimba udongo kwa miguu yao ya mbele yenye kucha ngumu ili kupata chakula. Wanapopata mzizi wanaotaka, wao huketi wima, kisha wanatumia miguu yao ya mbele kuweka mzizi huo kinywani na kuutafuna. Panyabuku hula asubuhi na mapema na vilevile jioni, nao hulala kati ya saa hizo za kula. Mbali na kula mimea, wanyama hao hula panzi, mbawakavu, minyoo, na mayai ya ndege, lakini hawahifadhi chakula katika mashimo yao.

Tunafurahia kutazama familia hiyo ya panyabuku, lakini ninapojaribu kuwakaribia ili niwapige picha, panyabuku wote watatu wanasimama ghafula palepale walipo. Ninaposogea karibu zaidi, panyabuku “baba” anapiga mbinja mbili kali zinazovuma katika bonde hilo lenye ukimya. Ghafula bin vuu, panyabuku “mama” na panyabuku “kijana” wanatimua na kuingia katika vijia viwili vyembamba na kutokomea chini ya majabali. Panyabuku “baba” ananitupia jicho kidogo. Kisha, anapiga mbinja mbili tena na kutimua kujiunga na familia yake.

Baada ya kuteremka bonde hilo kidogo, ninafika kwenye jabali jingine ambako ninaweza kuona mandhari vizuri. Ninalala juu ya jabali hilo nikisubiri panyabuku watokeze. Punde baadaye, panyabuku wengine wawili wanajitokeza. Mmoja wao anapanda jabali kubwa na kulala kifudifudi. Yule mwingine anapanda jabali hilohilo kutoka upande mwingine. Wanapokutana, yaonekana panyabuku hao wanabusiana.

Ninaendelea kuwatazama panyabuku hao na kustaajabishwa na jinsi wanavyosonga haraka-haraka na kutua kwa vipindi virefu. Ninaposonga kidogo tu, panyabuku hao wanatua ghafula na kuinua vichwa vyao wakiwa chonjo. Kisha wanalala, bila kujali kwamba nipo hapo.

Ninaona mashimo mengi kwenye nyasi ambayo yamezingirwa na udongo mweupe. Panyabuku hukimbilia mashimo hayo wanapoona hatari wakati wa vipindi vyao vifupi vya kula. Mashimo hayo yana chumba cha katikati ambacho kimeunganishwa na vijia kadhaa. Vijia hivyo vinaweza kuwa na urefu wa meta 1 hadi 6, na panyabuku hutumia masharubu yao meusi yaliyo kandokando ya pua yao ili kutambua njia.

Katika majira ya baridi kali, makundi ya panyabuku 10 hadi 15 hivi huingia katika vyumba vyao vya kulala. Panyabuku wachanga kwa wazee kutoka katika makao mbalimbali hukusanyika katika vyumba hivyo na kujikunja na kulala fofofo kwa muda mrefu. Kabla ya wakati huo, mashimo hayo huwa yamejazwa nyasi kavu. Halijoto ya mwili wao hupungua kufikia chini ya nyuzi 8 Selsiasi, mpigo wa moyo hupungua kufikia mipigo mitatu hadi mitano kila dakika, nao hupumua mara mbili au tatu kwa dakika moja. Mifumo ya mwili wao hutenda kazi ipasavyo kuwawezesha kuishi. Mara moja kwa mwezi, wanyama hao huamka na kwenda haja katika mashimo yaliyochimbwa vizuri katika sehemu nyingine ya makao yao. Kisha wao huziba mashimo hayo kabisa. Vyumba mbalimbali vya kulalia hutenganishwa pia, lakini havifunikwi kabisa. Hivyo, hewa ya kutosha huingia katika vyumba hivyo.

Wanasayansi wamefanya uchunguzi kwa muda mrefu ili kuelewa jinsi ambavyo panyabuku hustahimili baridi kali. Hivi majuzi imebainika kwamba panyabuku wanapolala, tezi fulani za ndani hufanya kazi, hasa tezi ya thirodi. Ama kwa hakika, wanyama hawalali wanapodungwa sindano zenye homoni. Lakini, inashangaza kwamba wanyama wanapowekwa katika baridi kali wakati wa kiangazi, utendaji wa tezi ya thirodi na utendaji wa kemikali mwilini mwao huongezeka ili kudumisha halijoto ya kawaida mwilini. Kwa wazi, wao hutumia silika kutambua kwamba wakati wao wa kulala haujafika.

Tunavutiwa sana na panyabuku hao hivi kwamba hatutambui kuwa muda unayoyoma. Tayari ni alasiri, ni lazima tuache kuwatazama na kurudi tena chini bondeni. Tunafika huko usiku unapoingia. Leo tumeona maajabu mengi ya maumbile, lakini yaelekea jambo ambalo limetufurahisha zaidi ni kukutana uso kwa uso na panyabuku.

[Picha katika ukurasa wa 16]

Panyabuku wanasalimiana

[Picha katika ukurasa wa 17]

Maua ya Milima ya Alps

Ua linaloitwa “bearded bellflower”

Yungiyungi linaloitwa “Turk’s-cap”

Ua linaloitwa “edelweiss”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Marmots: Gerken/Naturfoto-Online.de

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Marmots: Gerken/Naturfoto-Online.de