Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuunganisha Ulimwengu Ninawashukuru sana kwa makala ya jalada “Je, Kuunganisha Ulimwengu Ni Balaa au Ni Baraka?” (Mei 22, 2002) Nimehudhuria mihadhara mingi inayohusu utandaridhi na nimetambua kuwa haina usawaziko bali hupendelea upande mmoja. Wasemaji walijaribu kupendelea utandaridhi kwa kutoa faida zake tu au kuukashifu bila kutoa njia za badala. Lakini, kama makala yenu inavyosema, Ufalme wa Mungu utaunganisha ulimwengu kwa njia itakayotunufaisha sote. Ninangojea mabadiliko hayo yenye manufaa kwa hamu nyingi!
E. F., Ufilipino
Kwa mara nyingine tena mmeandika makala bora sana itakayovutia watu wengi. Kama umalizio wenu unavyokazia, suluhisho pekee la matatizo ya wanadamu ni utawala wa Ufalme wa Mungu juu ya dunia iliyo paradiso. Ninawashukuru kwa kazi yenu nzuri ya kuandika makala inayofaa siku hizi hatari tunamoishi.
G. B., Ireland
Ningependa kuwashukuru kwa kazi yenu yenye kusifika ya kueneza injili. Nilisoma makala ya jalada “Je, Kuunganisha Ulimwengu Ni Balaa au Ni Baraka?” na niliona ikiwa sahihi kabisa. Makala hizi hutusaidia kutambua udhaifu wetu tukiwa wanadamu. Pia, hutusaidia kudhamini kwamba tusipoishi kupatana na sheria za Yehova, hatuwezi kufanikiwa katika jambo lolote.
J. D., Ubelgiji
Nilifurahia makala zinazohusu utandaridhi. Hizo ni makala nzuri sana na zenye picha za kupendeza. Kabla ya kuzisoma sikujua lolote kuhusu neno utandaridhi, lakini sasa nimefahamu mengi. Mimi hupenda kusoma Amkeni!
E. K., Peru
Kusikia Asanteni sana kwa makala “Linda Uwezo Wako wa Kusikia!” (Mei 22, 2002) Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika mtaala wa kutumia vifaa vya masikio, kwa hiyo kila siku mimi huona jinsi watu wanavyoathiriwa na kelele. Hasa ni muhimu kuwasaidia vijana watambue kelele wanazokabiliana nazo kila siku.
C. K., Ujerumani
Vijana Huuliza Nilijifunza mengi mno kutoka kwenye makala “Vijana Huuliza . . . Ninawezaje Kupata Mtu Mzuri wa Kuishi Naye?” (Mei 22, 2002) Mimi si kijana, lakini hivi majuzi nilitalikiana na mume wangu. Nilishangaa kutambua kwamba kwa sababu ya gharama ya juu ya maisha, singeweza kutosheleza mahitaji yangu. Nililazimika kutafuta mtu ambaye tungeishi pamoja. Nilifikiri hilo lingekuwa jambo gumu sana kwa sababu ya umri wangu. Dada mmoja kijana, aliyekuwa amejiunga na kutaniko letu karibuni, alihitaji mtu wa kuishi naye pia. Tulianza kuishi pamoja. Mpango huo ulikuwa mzuri sana. Punde si punde, tulijikuta katika matatizo ya kifedha, na dada mwingine akaja kuishi nasi. Sina budi kukiri kwamba ni katika tengenezo la Yehova pekee ambapo nyanya wa miaka 60 na wanawake wawili vijana wanaotoka kwenye malezi tofauti wanaweza kuishi pamoja kwa amani na upendo mwingi! Sasa tumekuwa familia ndogo, ambayo imeondoa upweke tuliokuwa nao maishani.
L. G., Marekani
Kuutazama Ulimwengu Asanteni kwa sehemu yenye kichwa “Kuelewa Ugonjwa wa Akili” katika makala ya “Kuutazama Ulimwengu.” (Mei 22, 2002) Nimeugua ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika kwa miaka 18. Licha ya ugonjwa huu, nimetimiza mambo mengi maishani. Nimelea watoto watatu na nimekuwa mke mwema. Pia, nimewasaidia watu fulani kupata ujuzi wa Biblia. Nina familia yenye upendo na marafiki wapendwa kutanikoni. Asanteni sana kwa kuchapisha Amkeni! Linatusaidia kufikia kiwango kilekile cha elimu.
H. B., Afrika Kusini
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.