Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Tatizo la Unene Limeenea Ulimwenguni
Unene miongoni mwa watu wazima na watoto “unaongezeka kwa kiwango cha kusikitisha ulimwenguni pote,” na sasa unaathiri baadhi ya mataifa yaliyo maskini zaidi, laripoti gazeti The Lancet. Kulingana na Barry Popkin, mtaalamu wa uchumi na maradhi yanayosababishwa na ulaji katika Chuo Kikuu cha North Carolina, tatizo hilo linachangiwa na maendeleo ya tekinolojia ambayo yamewezesha mafuta ya mbegu za mahindi, soya na pamba yatumiwe. “Katika nchi za Asia na Afrika, unene unasababishwa hasa na mafuta hayo yanayotiwa kwenye chakula cha kila siku,” lasema gazeti The Lancet. Pia, sera za kilimo na biashara za serikali zinaruhusu sukari iagizwe kutoka nje kwa bei nafuu, hivyo ladha ya vyakula inaweza kuboreshwa kwa gharama ndogo. Tekinolojia mbalimbali zimepunguza utendaji na utumizi wa nishati, na hilo linawanenepesha watu pole kwa pole. Jambo linalowahangaisha wataalamu wa vyakula na afya ni kwamba unene unaweza kusababisha magonjwa ya kudumu kama ugonjwa wa sukari, kupanda kwa shinikizo la damu, na maradhi ya mishipa ya moyo.
Kiumbe Kipya cha Kipekee Chagunduliwa
Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Regensburg, Ujerumani, wamevumbua kiumbe kipya cha kupendeza chini ya bahari yenye volkano kaskazini mwa Iceland. Kiumbe hicho hunawiri katika maji moto sana yasiyo na oksijeni, yenye salfa nyingi, lasema gazeti Der Spiegel. Jina la bakteria hiyo, Nanoarchaeum equitans, linalomaanisha mbilikimo wa kikale mpandaji, linatokana na tabia yake ya kuishi juu ya mnyama mwingine mkubwa aitwaye Ignicoccus, au dude la moto, ambaye yaonekana humtegemea kwa ukuzi. Kiumbe huyo mwenye kipenyo cha nanometa 400 tu, ni mdogo sana hivi kwamba kulingana na ripoti hiyo, “zaidi ya viumbe milioni sita wanaweza kutoshea kwenye ncha ya sindano.” Viumbe hao ni wa pekee pia kwa kuwa chembe zao za DNA zina miunganisho ya ngazi inayopungua 500,000. “Hivyo mbilikimo wa kikale ni kiumbe mwenye chembe chache zaidi za urithi,” lasema gazeti Der Spiegel.
“Kuabudu Watu Mashuhuri”
“Uchunguzi mpya wa akili umegundua kwamba kuabudu watu mashuhuri kumeanza kuchukua mahali pa dini katika maisha za watu wengi,” asema mtaalamu wa akili, Dakt. Raj Persaud. Persaud aliandika katika gazeti la The Sunday Times la London, kwamba kadiri imani ya kidini ya mtu ilivyo dhaifu, ndivyo anavyoelekea “kuabudu” watu mashuhuri. Wale ambao huabudu watu mashuhuri huwa tayari kulipa pesa nyingi ili wapate vitu vinavyomilikiwa au kuguswa na watu mashuhuri. Isitoshe, Persaud anasema, “watu wanaoabudu watu mashuhuri” huiga maadili na maisha ya watu hao, ambao mara nyingi huonwa kana kwamba hawawezi kukosea na “kama wana maadili tofauti ambayo watu wa kawaida hawawezi kuelewa na yanayopaswa kukubaliwa.” Athari za watu mashuhuri hudhihirika pia katika mauzo yaliyoongezeka ya bidhaa wanazotangaza na kuigwa katika uchaguzi wa huduma muhimu za afya, asema Dakt. Persaud. Anaongeza kusema: “Kwa sababu tunawaabudu, wanakuwa watu wenye nguvu zaidi ulimwenguni—wanakuwa miungu yetu.”
Asilimia 25 ya Vipofu Ulimwenguni Wanaishi India
“India inatambuliwa kuwa na idadi yenye kusikitisha ya vipofu milioni 12, ambao hufanyiza asilimia 25 ya vipofu ulimwenguni,” lasema gazeti la India Deccan Herald. Ripoti ya shirika la Youth Vision India, ya mwaka wa 2002, inayotegemea habari kutoka vyuo na shule katika majiji zaidi ya 40 kotekote nchini India, ilisema pia kwamba “zaidi ya asilimia 50 ya vijana wanaohitaji vifaa vya kuwawezesha kuona vizuri hata hawafahamu kwamba wana tatizo la macho.” Kulingana na uchunguzi huo, matatizo mengi yalitokana na jicho kushindwa kuelekeza mwono kwenye retina na ugonjwa wa lenzi, ambayo ni matatizo yanayoweza kurekebishwa. “Kutofahamu kama mtu ana tatizo” na “ukosefu wa wataalamu wa kutosha wa macho” ni mambo yaliyotajwa na gazeti hilo kuwa sababu kuu za matatizo ya macho nchini India. Liliongeza kusema: “India ina wataalamu 5000 tu wa macho, na kiwango kilichopendekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni ni 40,000.”
Biblia ya Inuit Yakamilika
Chama cha Biblia cha Kanada kimekamilisha mradi wa miaka 23 wa kutafsiri Biblia nzima katika lugha ya Inuktitut, ambayo ni lugha ya watu wa kabila la Inuit wa Kanada. Ilikuwa kazi ngumu kutafsiri Biblia hiyo. “Kujaribu kutafsiri kutoka lugha ya watu waliofuga kondoo, ngamia na punda, na kukuza mitende hadi lugha ya watu wanaojua sili, sili wa baharini mwenye pembe, na mimea michache tu ni vigumu,” akasema Hart Wiens, mkurugenzi wa utafsiri wa Maandiko wa Chama cha Biblia cha Kanada. “Kwa mfano, Biblia ina majina mengi ya mitende. Lakini huko Nunavut [eneo la kaskazini zaidi la Kanada], hakuna mti hata mmoja, hivyo ni vigumu kuelezea mitende.” Lugha ya Inuktitut ni lugha asili ya Wakanada 28,000 hivi. Kulingana na gazeti National Post, “Biblia sasa inapatikana katika lugha tofauti-tofauti zaidi ya 2,285.”
Hatari za Internet
Utumizi mbaya wa Internet mara nyingi huleta matatizo katika familia, kulingana na shirika kubwa zaidi linalotoa mwongozo wa ndoa nchini Uingereza, Relate, lasema gazeti The Times la London. “Waume na wanawake wanalalamika kwamba wamelazimika kuwa wajane wa Internet kwa sababu ya kuachwa wapweke huku wenzi wao wakitumia saa nyingi kuwasiliana na watu wasiowajua katika Internet, wakinakili muziki na michezo, au kutazama picha chafu.” Vituo vya Internet vinavyowezesha watu kufufua mahaba ya zamani, na kupata msisimuko wa kingono kwenye Internet, vinaweza kuharibu ndoa. Shirika la Relate huwashauri wenzi wa ndoa 90,000 kila mwaka, na asilimia 10 kati yao wanadai kuwa matatizo yao yalisababishwa na Internet. Tatizo hilo linaongezeka. Msimamizi mkuu wa shirika la Relate, Angela Sibson, anasema: “Washauri wetu wanaripoti kwamba Internet inaendelea kuvunja mahusiano.”
Magumu ya Kuwa na Wazee Wengi
“Kuwa na wazee wengi zaidi ni jambo ambalo limeathiri au litakaloathiri kila mwanamume, mwanamke, na mtoto mahali popote ulimwenguni. . . . Kufikia mwaka wa 2050, idadi ya wazee itazidi ile ya vijana kwa mara ya kwanza katika historia ya wanadamu,” asema Ivan Šimonovic, msimamizi wa Baraza la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, alipohutubia Mkutano wa Pili wa Ulimwengu Kuhusu Wazee, uliofanywa Aprili 2002 huko Madrid, Hispania. Katibu Mkuu wa UM Kofi Annan aliuambia mkutano huo kuwa katika miaka inayopungua 50, idadi ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60 itaongezeka kutoka milioni 600 hadi karibu bilioni 2, na hivyo kuzidi idadi ya wale walio na umri wa chini ya miaka 15. Pia alisema kwamba asilimia 80 ya wazee hao watakuwa katika nchi zinazoendelea. Kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa na kuongezeka kwa urefu wa maisha kumechangia sana badiliko hilo. Baraza la sasa limeomba watunzaji wa afya na watoaji wa huduma za kijamii waongezwe ili kutosheleza mahitaji ya pekee ya wazee ili wazeeke “wakiwa na usalama na heshima.”
Stempu Zenye Kuudhi
“Stempu zilizochorwa watu wa kidini na mambo mengine zinaweza kuudhi wakati mwingine,” lasema gazeti Jerusalem Post la Israel. Mhamiaji mmoja kutoka Afrika Kusini, Alan Silver, alipata moja ya stempu zilizotolewa na shirika la posta kuadhimisha miezi ya Kiyahudi. “Akitumia kioo cha kukuzia, Silver aliona jina la Mungu mara kadhaa katika stempu ya mwezi wa Elul, na kulingana na sheria ya Kiyahudi jina hilo linapaswa kutumiwa tu kwa madhumuni matakatifu,” lasema gazeti la Post. Alimwonyesha kiongozi wake wa dini “ambaye aliamuru kwamba stempu ya mwezi wa Elul haipaswi kutumiwa kulingana na sheria ya Kiyahudi. Alisema kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kuinunua na ikiwa anayo, anapaswa kuiweka kwenye sanduku la maandishi matakatifu yanayopaswa kuzikwa, badala ya kutupwa kwenye pipa la takataka.” Hiyo haikuwa stempu ya kwanza kuleta mzozo. Nyingine ambayo ilitolewa kumkumbuka kiongozi wa Kiyahudi wa madhehebu ya Lubavitcher, Menahem Mendel Schneerson ilipingwa na wafuasi wake waliodai eti “hakuwa amekufa” na wengine “waliosema kwamba stempu hiyo iliyochorwa kiongozi wao haipaswi kurambwa au kupigwa muhuri.” Stempu hiyo haikutolewa.